Wednesday, March 2, 2016

WALIOVAMIA MABONDENI HAWATAPATA STAHIKI YOYOTE-MAKAMBA

Chanzo: Gazeti la Mwananchi, Machi 1, 2016
·        Tangu mwaka 1949 Bonde la Msimbazi lilitangazwa kuwa eneo hatarishi

·        Zoezi la ubomoaji liataendeshwa kwa utaratibu mzuri

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira, January Makamba
 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira, January Makamba alisema kuwa waliovamia mabondeni wataondolewa na hawatalipwa stahiki yoyote kwa kuwa wamevunja sheria. Makamba alisema kuwa utaratibu huo ulikuwepo katika awamu nne za Marais waliotangulia, tatizo utekelezaji wa sharia haukufuatwa kikamilifu.

Alisema kuwa bonde la Msimbazi lilitangazwa kuwa eneo hatarishi kwa maisha ya watu tangu mwaka 1949 na baadaye mwaka 1979. “Kumekuwa na taratibu za kuondoa watu ilikurejesha maeneo hayo katika hali yake ya asili”, alisema.

Aliongeza kuwa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi iliwahi kutangaza Bonde la Msimbazi kuwa eneo maalum na mipango miji, ilikutimiza suala hilo ilikuwa lazima watu waondolewe.

Alisema kazi ya kuwaondoa wananchi wanaoishi kwenye bonde hilo ilikumbwa na changamoto kadhaa na kukajengeka dhana kuwa wanaonewa.

“Serikali tulieleza kama mtu alipewa kibali na serikali akajenga nyumba, basi serikali ilifanyamakosa na itamtafutia mahali pengine. Ila kama mtu alikuja tu na kujenga nyumba eneo hilo, lazima aondoke”, alisema Makamba.

Alifafanua kuwa waliovamia na kujenga mabondeni serikali haiwezi kuweka utaratibu wa kuwapatia maeneo mengine kwa sababu kufanya hivyo ni sawasawa na kuwapa zawadi wanaovunja sheria. Aliongeza kuwa licha ya watu kujenga nyumba na kufikia kiwango cha kuishi, haiwezi kuwa kipimo cha kujipambanua kuwa hawana makossa.

“Unapofanya makossa ukamilifu wa kosa siyo msamaha wa kutorekebishwa. Ukisema kwasababu mtu hakukamatwa wakati akijenga msingi basi asikamatwe kwasababu nyumba imeisha si kweli”, alisema.

Alisema kazi ya kubomoa nyumba zilizo mabondeni iliingiliwa na wanasiasa na akasisitiza kuwa maisha wanayoishi wananchi katika maeneo hayo, si ya kuridhisha na ukiwa kiongozi huwezi kukubali kuona wakiendelea kuishi humo.

“Sisi ambacho tumekubali lazima tuendeleze zoezi lile kwa utaratibu mzuri zaidi. Lazima watu wapate taarifa na waliovamia kuelezwa wazi kuwa hawatapata stahiki yoyote na waliopewa vibali na serikali wapewe maeneo mengine”, alisema Makamba.

“Kuna utamaduni ulijengeka muda mrefu wa watu kutoheshimu na kutii sharia. Sasa tukiendelea hivyo hivyo si sawa maana bila sharia hakuna serikali. Nchi hii mtu hawezi kuamua ajenge kibanda mahali popote na akiondolewa serikali ndiyo ioenkane ina dhambi. Hatuwezi kuendesha nchi kwa utaratibu huu”.



JICHO LA PILI

Zoezi la ubomoaji wa nyumba zilizo jengwa mabondeni limeonekana kuwa ni uonevu mkubwa kwa wananchi waliojenga katika maeneo hayo. Watu mbalimbali wakiwemo wanasiasa waliliongelea kwa hisia kali na kuelekeza lawama kwa serikali.   Wakidai kuwa serikali ilikuwa wapi wakati wananchi hao walipoanza ujenzi katika huko mabondeni.

Inawezekana serikali haikuliona hilo ama kwa namna yoyote ambayo watu wanaweza kutafsiri, lakini linapojadiliwa suala la sheria tunaambiwa Kutojua Sheria Si sababu ya Kuvunja Sheria. Kwa uhalisia ukiangalia masiha ya watu wanaoishi mabondeni ni magumu na hatari mno, kimazingira na kiafya.

Mabondeni hakuna mfumo mzuri wa uhifadhi taka pamoja na miundombinu ya kupitisha maji taka, hii ni kutokana na eneo jografia ya eneo ilivyo, wakazi wa Dar es Salaam wanaelewa hilo. Ingawa kuna watakao hoji mbona hata watu ambao hawaishi mabondeni wanatatizo la miundo mbinu ya kuhifadhi taka na mirefeji ya kupitisha maji.

Ni kweli kwa Jiji la Dar Es Salaam kuna tatizo la miundo mbinu, lakini hali huwa mbaya zaidi kwa wakazi wa mabondeni. Kwa mfano wakazi wa bonde la Msimbazi wakati wa mvua bonde hujaa maji kiasi kwamba wakazi hao hulazimika kuhama makazi yao katika kipindi chote cha mvua.

Katika kipindi cha mvua mafuriko ya bonde la Msimbazi yamegharimu maisha ya wengi na kusababisha hasara za mali za watu. Zaidi ya hayo, wakati wa mvua watu wengi hutirirsha maji taka kutoka katika majumba yao na kuelekeza sehemu za mabondeni, hivyo kuhatarisha afya za watu waishio mabondeni.

Ni heri kuchukua tahadhari kuliko kusubiri hatari.

 
 
 

 

No comments:

Post a Comment