Wednesday, December 23, 2009

MABADILIKO YA TABIA-NCHI NA ATHARI ZAKE TANZANIA

Emmanuel Hayuka - LEAT

Japokuwa kwa wakati huu, kwa kiwango kikubwa kuna muafaka mkubwa duniani kote kuhusu uwepo wa mabadiliko ya tabia nchi katika sayari hii tunayoishi. Lakini lipo kundila watu ambalo pia ni weledi wa fani mbalimbali, kama vile; sayansi, jiografia, mazingira, uchumi, hali ya hewa, bailojia na uhandisi, na kadhalika, wanaotilia mashaka sababu na uwepo wa mabadiliko makubwa ya hali ya hewa.

Mashaka yao juu ya jambo hili inawezekana yamesababishwa na mgongano wa kimaslahi na tofauti za mbinu za kitafiti zinazopelekea kuwepo kwa majawabu yanayokinzana. Kwa mfano, nchi za Marekani, China, Urusi, India, Brazil na Canada zimekuwa katika ubishi wa kiwango gani cha utoaji wa gesi ya ukaa (Carbon dioxide) kinachotakiwa kudhibitiwa ili kupunguza athari za ongezeko la joto duniani. Gesi ukaa (Carbon dioxide) inasemekana inachangia kwa kiwango kikubwa sana mabadiliko ya tabia nchi duniani.

Lakini, ukweli wa mambo ni kwamba, “mabadiliko ya tabia nchi” ni jambo dhahiri, linaloendelea kuikabili dunia, na hasa athari zake zimekuwa zikijidhihirisha katika nchi zinazoendelea, hasa kutoka bara la Asia, Afrika, Carribean na Amerika ya Kusini. Athari hizo ni za mazingira, kiuchumi na kijamii. Hivyo, inatulazimu kutafuta na kutekeleza hatua ambazo zitapelekea kupunguza au kuzuia hali hii.

Ufahamu wa dhana ya Mabadiliko ya Tabia Nchi

Bila shaka dhana ya “mabadiliko ya tabia nchi” ni miongoni wa dhana ambazo zimekuwa vinywani kwa watu wengi duniani katika miongo ya hivi karibuni. Hii inajumuisha wale wote wanaojiusisha na masuala ya mazingira na hata wale ambao hawajihusishi nayo. Lakini wengi wetu, pengine tumekuwa tukifanya hivyo bila kujua maana, japo kwa ufupi wa dhana hii. Kuelezea kikamilifu maana ya dhana ya “mabadiliko ya tabia nchi” katika makala fupi kama hii ni jambo lisilowezekana, kwa kuwa dhana hii ni pana sana na imezungumziwa na wataalamu wengi.

Kwa mujibu wa nyaraka ya Dr.Furaha N. Lugoe wa Dar es Salaam Institute of Land Administration and Policy Studies (DILAPS) yenye kichwa cha habari “Mitazamo na Ukweli wa Mabadiliko ya Tabia Nchi”(Climate Change Perspectives and Realities), alioutoa katika warsha inayohusu “Mabadiliko ya tabia nchi” iliyoandaliwa na Citizen’s Global Platform tarehe 26 Novemba 2009, Dar es Salaam, “Mabadiliko ya tabia nchi yanachangiwa sana na ‘ongezeko la joto duniani’ (global warming). ‘Ongezeko la joto duniani’ husababishwa na kuwepo ziada ya hewa za ukaa angani ambazo zinabadilisha viwango vya nishati ya joto na hivyo kusababisha wastani wa hali ya joto angani kwa msimu kuongezeka.

‘Ongezeko la joto duniani’ni jambo linalosababishwa na mwako wa nishati kama vile; petroli, dizeli, gesi asilia, makaa ya mawe na kuni, na kadhalika; kuoza kwa mboji katika maziwa na mashamba ya mpunga na utoaji wa hewa za ukaa kutoka katika mbolea za viwandani, viwanda na vyombo vya usafiri. Hewa za ukaa vilevile hujulikana kama ‘hewa za nyumba ya kijani’, ambazo zinajumuisha Carbon dioxide (CO2), methane, chlorofluorocarbons (CFC), nitrous oxide na ozone (O3)”.

Dr. Lugoe anafafanua zaidi kuwa, “Kwa kawaida, wakati miali ya jua inapopenya katika angahewa, sehemu mojawapo ya mnururisho wa jua unaakisiwa na kurudishwa tena angani na tabaka la juu la angahewa au ufyonzwa na tabaka la ozoni. Sehemu nyingine inapelekwa juu ya ardhi na kubadilishwa kuwa miali isiyoonekana au joto. Halafu mawingu, mvuke wa maji katika angahewa na ‘hewa za nyumba ya kijani’ zinavyonza na kuhifadhi kiwango kikubwa cha joto kinachozalishwa, hatima yake ni kuongezeka kwa joto duniani.”

Kwa upande mwingine ‘ongezeko la joto duniani’ linatokea pale chembe ndogo ndogo za chlorofluorocarbons (CFC) zinapobadilisha mtungo wa tabaka la ozoni. Kwanza, mnururisho wa miali isiyoonekana(ultra-violet radiation) inasababisha chembe ndogo ndogo za chlorofluorocarbons(CFC) kutoa chembe ndogo za chlorine(Cl) ambazo baadae zinavunja chembe ndogo za ozoni katika namna ileile ambayo miali isiyoonekana (ultra-violet radiation) ingeweza kufanya.Baadae Chroline inaungana na chembe ndogo za oxygen na kutengeneza Chlorine monoxide (ClO) ambayo inazuia utengenezwaji wa tabaka la ozoni.

Kwa hiyo, chembe huru za oxygen kwa kasi zinaunganika na Chlorine monoxide (ClO), baadae zinatoa chembe huru za Oxygen na Chlorine. Mchanganyiko huu wa kikemikali hauruhusu kutengenezwa kwa ozoni. Matokeo yake ni kwamba unene wa tabaka la ozoni unapunguzwa na hatimaye mnururisho wa miali mikali ya jua isiyoonekana (ultra-violet radiation) inaruhusiwa kufika kwenye uso wa dunia. Hali hii inachangia kuleta “ongezeko la joto duniani” ambayo pia inachangia sana kuwepo kwa “mabadiliko ya tabia nchi”

‘Mabadiliko ya tabia nchi’ ambayo kwa kiwango kikubwa yamesababishwa na ‘ongezeko la joto duniani’ inafanya kubadilika kwa mikondo ya mvua, kubadilika kwa kina cha bahari, kubadilika kwa mwelekeo na kasi ya upepo, kubadilika kwa mwelekeo na kasi ya mikondo ya maji ya bahari, kubadilika kwa misimu na kuongezeka kwa uwezekano wa kutokea kwa maafa ya tabia nchi kama vile; ukame, kimbunga na mafuriko.

Jambo la msingi la kuzingatia hapa ni kwamba maana hii fupi ya “mabadiliko ya tabia nchi” iliyokaririwa humu haina kusudio la kuwa maana mahsusi ya dhana hii duniani kote au miongoni mwa wanasayansi, wahandisi na wanaharakati wa mazingira. Isipokuwa kutoa mwangaza kwa umma kutambua kwa ufupi maana ya dhana yenyewe na hivyo kuwawezesha kufahamu juu ya mabadiliko ya tabia nchi na jinsi yanavyoathiri maisha yetu kwa ujumla.

Ushahidi wa mabadiliko ya tabia nchi

Ni jambo muhimu sana, siyo tu kwa wale wanaopinga au kuwa na mashaka ya kuwepo kwa “mabadiliko ya tabia nchi”, lakini na wale wanaoamini kuwepo kwake kujua hata kama siyo wote, baadhi ya ushahidi wa kuwepo kwa mabadiliko ya tabia nchi.

Ushahidi wa “mabadiliko ya tabia nchi” umepatikana kutoka vyanzo mbalimbali ambavyo vinaweza kutumika kuitengeneza tena tabia nchi ya zamani ili kuweza kufanya ulinganifu. Inasemekana kuwa rekodi zilizokamilika za takwimu zinazohusu joto la uso wa duniani ulianza kuhifadhiwa katikati na mwishoni wa miaka ya 1800.

Kuna ushahidi mwingi sana kuthibitisha uwepo wa “mabadiliko ya tabia nchi”. Miongoni wa ushahidi huo ni kuwepo kwa hali mbaya ya hewa, kama vile: ukame, mvua isiyotabirika, mafuriko, mkondo wa joto kali na kuongezeka kwa vimbunga, ongezeko la joto, kuongezeka kwa kasi ya kuyeyuka kwa barafu na kubadilika kwa uoto na maumbile asilia duniani.

Ukweli wa mambo ni kuwa, uthibitisho wa “mabadiliko ya tabia nchi” ni mwingi sana, kiasi kwamba hauwezi wote kutolewa katika makala hii pekee. Isipokuwa kutokana na umuhimu wa kuelimisha umma wa Tanzania juu ya suala hili, ushahidi ule tu wenye uhusiano wa moja kwa moja na Afrika na hasa Tanzania ndiyo unatakiwa kupewa kipaumbele cha juu.

Uthibitisho wa baadhi ya ushahidi huo wa “mabadiliko ya tabia nchi” ni kutokea kwa mafuriko makubwa ambayo hayajawahi kushuhudiwa kwa kipindi kirefu katika sehemu mbalimbali duniani. Mafuriko ya Mto Rhine (Ulaya magharibi) kati ya mwaka 1996 na 1997, mafuriko ya China ya mwaka 1998, mafuriko ya Ulaya mashariki ya mwaka 1998 na 2002, mafuriko ya Msumbiji na Ulaya ya mwaka 2000 na mafuriko ya Bangladesh yaliyosababishwa na mvua za mansuni mwaka 2004 ambayo yalifanya takribani asilimia sitini (60%) ya nchi kuwa chini ya maji na hata mafuliko makubwa yaliyoikumba Ufilipino mwaka huu (2009) ni mojawapo ya mifano inayothibitisha uwepo wa dhana ya “mabadiliko ya tabia nchi”.

Mathalani, utafiti wa kisayansi unaonyesha bayana kuwa kiwango cha ujazo wa maji katika maziwa makubwa ya Afrika kama vile Ziwa Niger, Ziwa Chad na Ziwa Victoria kimekuwa kikipungua kati ya asilimia arobaini (40%) na sitini (60%). Sambamba na hilo kumekuwa na kuongezeka kwa jangwa katika maeneo mbalimbali ya kusini, kaskazini, mashariki (Tanzania ikiwemo) na magharibi ya Afrika unaosababishwa na wastani wa chini wa mvua kwa mwaka, mvua kubwa kupita kiasi inayosababisha umwagaji na mtiririko wa maji juu ya ardhi, pamoja na unyevunyevu wenye joto katika udongo.

Mbali ya hayo, kuna uthibitisho mwingine unaodhihirisha kuwepo kwa “mabadiliko ya tabia nchi” duniani na hata Afrika ni kuongezeka kwa kasi ya kuyeyuka barafu. Utafiti wa kisayansi unaonyesha barafu imeyeyuka kwa kiwango kikubwa sana katika karne ya ishirini. Wastani wa joto katika eneo la Arctic ambalo lina barafu na baridi kali limeongezeka takribani mara mbili ya wastani wa dunia kwa kipindi cha miaka mia moja (100) iliyopita. Kiwango cha joto katika tabaka lenye ubaridi kimeongezeka kuanzia miaka ya 1980 kwa sentigredi tatu (3 centigrade).

Jambo kama hili pia linatokea nchini Tanzania. Mojawapo ya kivutio chetu kikubwa cha utalii, Mlima Kilimanjaro ambao vilevile vilele vyake vya Kibo na Mawenzi vimefunikwa na theluji umeathirika kwa kiwango kikubwa na “mabadiliko ya tabia nchi” yanayoendelea kuikabili dunia. Hali hii inatishia theluji hiyo kupotea kabisa na kufanya kizazi kijacho kuiona theluji hiyo kupitia picha za kitalii au vitabu vya hadithi tu.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa hivi karibuni kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro na Bwana Lonnie Thomson, mtaalamu wa Sayansi ya Theluji (Glaciologist) anayefanya kazi zake katika kituo kiitwacho Byrd Polar Research Centre, Columbus (Kituo cha Utafiti wa Theluji cha Byrd) kilichopo katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Ohio (Ohio State University) unaonyesha kwamba kuyeyuka kwa theluji ya Mlima Kilimanjaro unaendelea kwa kasi kubwa.

Utafiti huo umebaini kuwa zaidi ya robo ya kiwango cha theluji kilichoufunika Mlima Kilimanjaro mwaka 2000 kilipotea ilipofika mwisho wa mwaka 2007. Bwana Thompson na washirika wake walitoa ripoti hiyo tarehe 2 Novemba 2009, katika mhadhara uliondaliwa na Chuo cha Kitaifa cha Sayansi cha Marekani (National Academy of Science).

Takwimu zilizopatikana kutokana na utafiti uliofanywa angani umeongezea takwimu zilizokusanywa na timu ya utafiti ya Bwana Thompson na washirika wake. Takwimu hizo zinaonyesha kwamba uyeyukaji wa theluji katika Mlima Kilimanjaro uliongezeka kwa kiasi kikubwa miongo ya hivi karibuni, anasema Bwana Thompson. Inasemekana kuwa kuanzia mwaka 1912 hadi 1953 theluji inayofunika Mlima Kilimanjaro ilipungua kwa kiwango cha 1.1% kwa mwaka. Vivyo hivyo, kati ya mwaka 1953 na 1989 wastani wa kiwango cha kupungua kwa theluji kwa mwaka kiliongezeka na kufikia 1.4%.

Tokea utafiti ulifanywa mwaka 1989 hadi kufikia utafiti uliofanywa hivi karibuni, mnamo mwaka 2007 umeonyesha kupungua kwa kiwango kikubwa cha eneo la Mlima Kilimanjaro lililofunikwa na theluji, kwa wastani mkubwa sana cha 2.4%, wanabainisha watafiti hao.

Bwana Thompson anasema, siyo tu kwamba mapande makubwa ya theluji kwenye kilele cha mlima yamekuwa yakipungua, yanapungua kwa kasi kubwa, mwelekeo huu umegundulika tu kwa kutumia njia ya utazamaji kutokea ardhini iliyoboreshwa miaka ya hivi karibuni.

Sehemu pana zaidi ya kilele ambayo inakadiriwa kuwa na upana wa meta 50 iitwayo “Ukanda wa Theluji wa Kaskazini”, imekuwa ikipungua kwa kiwango cha meta 1.9 kati ya mwaka 2000 na 2007. Kwa kipindi hicho hicho, “Ukanda wa Theluji wa Kusini” wa mlima Kilimanjaro ambao unakadiriwa kuwa na upana wa meta 21 mwaka 2000, umepoteza meta 5.1 ya unene wa theluji mwaka 2007.

Bwana Thompson anaongeza kuwa, kama theluji ya mlima Kilimanjaro itaendelea kuyeyuka, kuporomoka na kukatika vipande vidogo vidogo, miamba myeusi itakayozunguka theluji itakayo salia, itafyonza miale ya jua mingi zaidi na kuchemka, na hivyo kuongeza zaidi kasi ya kuyeyuka theluji. Watafiti wanakadiria kwamba kwa kiwango cha sasa cha uyeyukaji wa theluji, tabaka la kudumu la theluji katika Mlima Kilimanjaro litatoweka ifikapo mwaka 2022.

Hata Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bwana John Chiligati ameunga mkono ushahidi uliotolewa hapa juu. Katika mahojiano yake na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC (British Broadcasting Corporation), mnamo tarehe 13 Novemba 2009, Waziri Chiligati alisema kuwa “mabadiliko ya tabia nchi” yamesababisha ukame katika sehemu ambazo hapo awali zilikuwa zinapata mvua za kutosha…, hata theluji ya Mlima Kilimanjaro ambayo inajulikana sana kama kofia nyeupe (white caps) imeanza kutoweka kwa kasi kubwa, kitu ambacho kinahatarisha sana uwepo wa kivutio hiki muhimu cha utalii cha nchi yetu”.

Kutokana na uthibitisho huu, sidhani kama kuna mtu yoyote atakayeshindwa kung’amua nini itakuwa hatima yake kwa dunia, na hasa Tanzania, kama hali hii itaachwa bila kudhibitiwa.

Nini kisababishacho

Kuna nadharia kadha wa kadha zinazojaribu kuelezea sababu zinazosababisha mabadiliko makubwa ya tabia nchi yanayoendelea kushuhudiwa sasa ulimwenguni kote. Miongoni wa sababu zinazotajwa kuwa ndizo zimepelekea kuwepo kwa “mabadiliko ya tabia nchi” ni; mabadiliko ya mnururisho wa jua, mchepuko wa sayari ya dunia katika mzunguko wake, mtengenezeko wa milima na mwelekeo wa mabara, kubadilika kwa mkusanyiko wa pamoja wa gesi inayoathiri hali ya hewa kutokana na shughuli za binadamu.

Kitaaluma sababu zote hizo na nyingine ambazo hazija orodheshwa humu ni muhimu sana. Lakini katika makala hii sababu ya mabadiliko ya tabia nchi yanayotokana na uzalishaji wa “hewa ya ukaa” (carbon dioxide) na gesijoto unaosababishwa na shughuli za binadamu, ndiyo ukaopewa kipaumbele.

Kwa sasa kuna muafaka wa kisayansi kuhusiana na mabadiliko ya tabia nchi, kwamba shughuli za binadamu inawezekana zikawa ni sababu kubwa ya kuongezeka kwa kasi kubwa sana ya wastani wa joto duniani kwa kipindi cha miongo kadhaa iliyopita. Shughuli za kila siku za binadamu zinasababisha utoaji na ongezeko la hewa ya ukaa na gesijoto angani, ambazo usababishwa na uunguzaji wa nishati inayotokana na mabaki ya viumbe hai, kama vile: petroli, dizeli, makaa ya mawe na gesi asilia. Mchakato huu ndio unaleta ongezeko la joto duniani na hivyo kubadilisha tabia nchi iliyokuwepo awali.

Vivyo hivyo, mchakato huo wa kuongezeka kwa hewa ya ukaa (carbon dioxide) na gesijoto angani unachangia uharibifu wa “tabaka la ozoni” (ozone layer) ambalo limekuwa likiikinga dunia na kunururishiwa miale mikali ya jua. Jambo hili pia husababisha ongezeko la joto duniani na hatimaye “mabadiliko ya tabia nchi”.

Sababu nyingine ya “mabadiliko ya tabia nchi” ni ukataji mkubwa usio endelevu wa misitu (deforestation). Hali hii pia inachangia sana kuongezeka kwa joto duniani, kwa kuwa mchakato wa ufyonzaji gesi ya ukaa unaofanywa na misitu na mimea unaathirika sana. Hii hupelekea kuwepo kwa mlundikano wa kiwango cha juu cha hewa ukaa na ongezeko la joto hutokea.

Shughuli za binadamu zinazochangia ongezeko la joto duniani na hatimaye “mabadiliko ya tabia nchi” ni nyingi mno, mbali na hizi zilizotajwa, zingine ni kama vile: kilimo cha umwagiliaji, uchomaji wa misitu pamoja na mabaki ya mazao na ufugaji wanyama kwa kiwango kikubwa.

Namna za kutatua

Ni ukweli usiopingika kwamba ulimwengu unakabiliwa na mabadiliko makubwa ya tabia nchi. Kama tulivyoona hapo juu, mbali na sababu za kiasili, vilevile shughuli za binadamu zimekuwa ni sababu kubwa sana zinazosababisha “mabadiliko ya tabia nchi” kama ilivyoelezwa awali katika makala hii.

Kutokana na ukweli huu hata utatuzi wa jambo hili pia unategemea namna ya kuikabili sababu hii kubwa inayochangia kuwepo kwake. Ndiyo maana, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. Jakaya Mrisho Kikwete aliwahi kukaririwa akisema kwamba, “Kwa mazingira masafi na sayari salama kwa sisi kuishi, ni lazima tuondoe gesijoto kwenye anga, tusimamishe na tupunguze kiwango cha sasa cha utoaji hewa ya ukaa na tupunguze mlundikano wake angani”.

Ni dhahiri kwamba kauli hii ya Rais Kikwete imelenga kwenye kitovu cha chanzo cha tatizo la “mabadiliko ya tabia nchi”. Kwa hali hii ni jambo la msingi kujua namna ambavyo gesijoto hasa hewa ukaa ambazo husababisha ongezeko la joto dunia na hatimaye “mabadiliko ya tabia nchi”, zinavyoweza kupunguzwa.

Bwana Emmanuel Massawe, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira (Lawyers’ Environmental Action Team, LEAT) ametoa kauli inayoshahabiana kwa kiwango kikubwa na ile ya Mheshimiwa Rais Kikwete, kwamba, “Mabadiliko ya tabia nchi yanayoshuhudiwa duniani kwa sasa, inawezekana kuepukwa kwa kuhakikisha kwamba ongezeko la joto duniani linapunguzwa na kudhibitiwa. Jambo hili linawezekana tu, kwa kupunguzwa kiwango cha utoaji wa hewa ukaa na gesijoto angani ambazo zinachangia sana kuleta ongezeko la joto duniani na swahiba wake mabadiliko ya tabia nchi”.

Bwana Massawe, anaongeza kuwa jambo ili litawezekana kama tutapunguza kwa kiwango kikubwa matumizi ya makaa ya mawe, dizeli, petroli au kudhibiti shughuli zinazotumia nishati hizo kwa kiwango kikubwa kwa kutumia nishati mbadala.

“Nadhani utekelezaji wa Mpango wa Kupunguza Uzalishaji wa Hewa ya Ukaa kutokana na ukataji miti hovyo na uharibifu wa Misitu (MKUHUMI) utasaidia sana kupunguza kasi ya “mabadiliko ya tabia nchi”, Bwana Massawe, aliongeza.

Mpango huu (MKUHUMI) unatokana na Jumuia ya Kimataifa kutambua kwamba, kama misitu itajumuishwa katika utatuzi wa “mabadiliko ya tabia nchi”, hivyo nchi zinazoendelea lazima zifidiwe kwa kuhifadhi na kupunguza ukataji wa misitu unaotokea pale misitu inavyokatwa kwa matumizi mengine ya ardhi hiyo, pamoja na uharibifu wa misitu unaotokea pale maliasili za misitu zinavyoharibiwa. Kwa kuwa, ardhi yenye misitu inaweza kuwa na thamani kutokana na uuzaji wa mbao uletao fedha za kigeni kwa taifa au uwezekano wa kutumika kwa kilimo cha mazao ya biashara na chakula kwa ajili ya kulisha idadi ya watu inayoongezeka kila siku. Hivyo ni muhimu kutoa tuzo ya fedha ili kuhakikisha kuwepo misitu hiyo kwa kuwapa wananchi hamasa ya kuihifadhi, kuitunza na kuitumia kiuendelevu.

Mchango wa misitu katika kutatua tatizo la “mabadiliko ya tabia nchi” ni kutokana na ukweli kwamba misitu hufyonza hewa ukaa na hivyo kupunguza mlundikano wake angani. Inakadiriwa kuwa asilimia ishirini (20%) ya utoaji wa hewa ukaa angani unaweza kupunguzwa kwa kutokata na kuharibu misitu. Vilevile misitu inaweza kuchangia katika kukabiliana na “mabadiliko ya tabia nchi” kwa kuipatia dunia huduma ya ikolojia.

Hivyo, Bwana Massawe anafafanua zaidi kuwa, “Sisi LEAT tunauona MKUHUMI kuwa wenye manufaa sana, kwa kuwa ni utaratibu uliobuniwa kutoa zawadi au motisha kwa nchi zile zitakazotunza misitu kama vile Tanzania. Chini ya mfumo huu nchi zitapima na kuratibu kiasi cha misitu kilichoko na kutathmini kiasi cha hewa ukaa kinachopunguzwa angani kwa kufyonzwa na misitu iliyohifadhiwa na kutunzwa vizuri ndani ya mipaka ya nchi husika. Hii itawezesha kutathmini kiasi cha uondoaji wa hewa ukaa angani na kutambua kiasi cha mlundikano wa gesijoto angani kilichopunguzwa ili kujua kiasi cha karadha (credits) za hewa ukaa kinachoweza kuuzika kilichotokana na kupunguzwa kwa mlundikano wa hewa ukaa angani. Halafu karadha hizi zitaweza kuuzwa katika soko la dunia la hewa ukaa na kupata kipato kizuri”.

Wednesday, December 2, 2009

MCHANGO WA SERA KATIKA KUSABABISHA MABADILIKO YA TABIA-NCHI TANZANIA

Emmanuel S. Massawe

Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira - LEAT



Utangulizi

Mabadiliko ya tabia-nchi ni maafa yaliyo dhahiri kisayansi kwa sasa. Imethibitishwa na wanasayansi mbalimbali duniani kuwa maafa haya (mabadiliko ya tabia-nchi) yanahatarisha maisha ya wanadamu na viumbe hai wengine. Jambo muhimu la kutilia maanani ni kuwa mabadiliko ya tabia-nchi yamesababishwa na mwanadamu kwa kutekeleza mipango ilokusudiwa kuchagiza maendeleo ya kiuchumi.

Nchi zote za ulimwenguni zimekuwa zikitekeleza na kuweka kipaumbele shughuli zinazoleta maendeleo bila kutilia maanani mazingira na vizazi vijavyo. Mabadiliko ya tabia-nchi yanasababishwa kwa kiasi kikubwa na vitendo vya kuchoma nishati asilia, kubadilisha eneo la misitu kuwa jangwa na kufanya shughuli zinazozalisha gesijoto kwa wingi. Nishati asilia inapochomwa huzalisha gesijoto ambayo huenda angani na kutuama/kuelea katika sehemu ya anga.

Hii husababisha kuongezeka kwa joto duniani. Uzalishaji wa gesijoto kwa wingi na kasi ya kugeuza misitu kuwa jangwa hupunguza uwezo wa misitu kunyonya hewa ukaa na gesi nyingine, hivyo kuharibu uwiano wa asili angani na kupelekea kuwepo kwa mlundikano wa gesijoto angani. Kwa sasa mlundikano wa hewa ukaa angani inaaminika umefikia kiwango cha juu kabisa. Hivyo kuna uhitaji mkubwa wa kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na gesijoto duniani.

Nchi zenye maendeleo ya viwanda (kwa mfano, nchi za Ulaya, China, India na Marekani) zimechangia/zinachangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya tabia-nchi kutokana na gesijoto zinazozalishwa kutoka viwandani na katika sekta ya usafiri. Nchi zinazoendelea zimechangia kwa kiasi kidogo sana. Ni asilimia 17 tu ndio inazalishwa na nchi zinazoendelea kutokana na kupotea kwa misitu kunakotokana na uvunaji holela.

Bara lote la Afrika linachangia asilimia 3 tu ya gesijoto inayozalishwa duniani. Ijapokuwa nchi zinazoendelea zinachangia kidogo sana mabadiliko ya tabia-nchi (hasa zile za Afrika), ndizo zinazoathrika sana kutokana na athari za mabadiliko ya tabia-nchi. Nchi tajiri duniani haziathiriki sana ukilinganisha na nchi maskini.

Mabadiliko ya tabia-nchi ni maafa yaliyo bayana kabisa na yenye kuviza maendeleo ya mwanadamu. Mathalani, maafa haya yameathiri kwa kiasi fulani jitihada za jumuiya za kimataifa kupunguza umaskini duniani na kutimiza Malengo ya Milenia. Ni dhahiri kuwa kwa sasa, mabadiliko ya tabia-nchi yanaathiri misingi ya maisha duniani. Yanaathiri rasilimali na mifumo-hai ambayo wanadamu tunategemea kwa chakula na maji, uzalishaji wa misitu yetu na maeneo ya kilimo.

Athari ziletwazo na mabadiliko ya tabia-nchi

Kutokana na Ripoti ya Nne ya Jopo la Wataalamu la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Mabadiliko ya Tabia-nchi (IPCC) iliyotolewa mwishoni mwa 2007, wastani wa joto duniani umeongezeka kwa digrii za sentigredi 0.74 toka mapinduzi ya viwanda kuanzishwa.

Ripoti hii imeonesha kuwa kati ya 1970 na 2004, mlundikano wa gesijoto angani umeongezeka kwa asilimia 70, ambapo mlundikano wa hewa ukaa umeongezeka kwa asilimia 80 kwa kipindi hicho. Ni dhahiri kuwa kadiri mlundikano wa hewa ukaa na gesijoto angani unavyoongezeka, ndivyo maafa na athari za mabadiliko ya tabia-nchi yanavyoongezeka kwa nchi maskini.

Kutokana na haya, tafiti zimethibitisha kuwa:-

· Kumetokea maafa ya ukame duniani ambayo yameathiri upatikanaji wa chakula kwa binadamu na wanyama. Pia yatapelekea kushuka kwa uzalishaji wa mazao kwa kilimo kinachotegemea mvua kwa asilimia 50. Hii itaathiri upatikanaji wa chakula na kuwepo kwa baa la njaa.

· Kuongezeka kwa matukio ya mafuriko makubwa ambayo yameathiri mifumo-hai na kusababisha vifo vya watu na wanyama na kuharibu miundo-mbinu.

· Kumetokea vipindi virefu vya joto kali na ukame vilivyopunguza upatikanaji wa maji safi kwa kunywa na kilimo.

· Kumetokea mioto hatari iliyoteketeza misitu ambayo mwanadamu anaitegemea kwa nishati kuni, hewa safi (oksijeni) na uoto wa asili.

· Kumekuwepo ongezeko la joto duniani linaliathiri maisha ya kawaida ya mwanadamu.

· Kumekuwa na ongezeko la magonjwa ya kitropiki, mathalani, malaria ambayo yamechagizwa na kuongezeka kwa mazalio ya mbu kutokana na kuongezeka kwa joto.

· Kuyeyuka kwa theluji kwenye safu za milima mirefu na maeneo yaliyo katika ncha za dunia kunakosababisha kupanda kwa kina cha bahari.

· Kina cha bahari kuongezeka kwa baadhi ya maeneo duniani na kupelekea eneo fulani la visiwa au nchi kavu kufunikwa na maji. Hii inahatarisha maisha ya watu waishio visiwani kwani kama hali ikiendelea visiwa vyote vyaweza kufunikwa na maji ya bahari. Pia kuongezeka kwa kina cha bahari kutapunguza kuwepo kwa maji baridi kwa ajili ya matumizi ya binadamu kunakotokana na kuongezeka kwa maji ya chumvi katika nchi kavu (Salt water intrusion).

Athari na maafa haya yamethibitishwa kutokea na kuhusiana na mabadiliko ya tabia-nchi. Yanaendelea kutokea na kuathiri baadhi ya maeneo ya dunia kwa sasa. Jitihada mahsusi na za haraka zinahitaji kuchukuliwa ili kuwakinga watu na athari na kupunguza visababishi vya mabadiliko ya tabia-nchi.


Sera mbali mbali na mchango wake katika kusababisha Mabadiliko ya Tabia-Nchi

Sera ni chombo cha utekelezaji wa Sheria, mipango ya maendeleo, na mikakati mbalimbali. Sera hazina nguvu ya kisheria lakini zinaweka msingi wa kutunga au kurekebisha Sheria. Sera hutoa maelekezo na hatua za kuchukua katika utekelezaji wake. Serikali hutumia Sera mbalimbali kutekeleza mipango na mikakati ya maendeleo.

Utekelezaji wa Sera kadha wa kadha unatakiwa kuleta matunda bora kwa jamii kwa kuchagiza maendeleo na kupunguza umaskini. Utekelezaji wa Sera unaweza kuwa wa manufaa kwa jamii au ukaiathiri jamii kwa namna moja au nyingine. Malengo na maudhui ya Sera mbalimbali hayatakiwi kugongana kwani zitaleta madhara kwa jamii.

Sera zinazoratibu sekta moja zinatakiwa zishirikiane kimaudhui na kiutekelezaji ili kuratibu vyema shughuli za utekelezaji wa mipango na mikakati ya maendeleo. Sera zinatakiwa zilete maendeleo endelevu bila kuathiri mahitaji na maslahi ya vizazi vijavyo. Utekelezaji wa Sera mbalimbali huchangia kwa namna moja au nyingine kuleta mabadiliko ya tabia-nchi. Sera hizi na jinsi zinavyochangia kuwepo kwa mabadiliko ya tabia-nchi zinaelezewa hapa chini kinagaubaga.

Sera ya Taifa ya Misitu, 1998

Sera ya Taifa ya Misitu nchini Tanzania ilitangazwa mwaka 1953. Sera hii imekuwa inarekebishwa mara kadhaa pale uhitaji wa kuirekebisha ulipotokea. Lengo la kuwa na Sera hii ni kuainisha na kuratibu namna ambavyo rasilimali ya misitu na miti inaweza kutumika kwa misingi endelevu ili kukidhi mahitaji na matakwa ya jamii na taifa.

Moja ya madhumuni ya sekta ya misitu ni kupanua ajira na kuongeza pato la fedha za kigeni kutokana na maendeleo endelevu katika viwanda vinavyojikita kwenye misitu na biashara. Ili kufikia dhumuni hili serikali inabudi kufungua milango na kuruhusu uwekezaji katika sekta ya misitu.

Ili uwekezaji katika sekta ya misitu ulete na kuongeza fedha za kigeni ni lazima uvunaji wa rasilimali misitu na miti ufanyike kwa kiwango kikubwa ili kuleta manufaa ya kibiashara. Uvunaji wa misitu unatakiwa kuwa endelevu kwa kutilia maanani rasilimali misitu na miti zilizoko nchini. Hili linachangia kuwepo kwa mabadiliko ya tabia-nchi kwani miti huvunwa kwa wingi sana ili kuongeza pato la fedha za kigeni.


Tutambue kuwa miti hufyonza hewa ukaa kwa ajili ya kutengenezea chakula. Lakini uvunaji wa kiwango kikubwa wa misitu na rasilimali miti huacha eneo kubwa la nchi kuwa jangwa. Hii inamaanisha kuwa hewa ukaa na gesijoto zinalundikana angani na kusababisha mabadiliko ya tabia-nchi.

Sera ya Taifa ya Mazingira, 1997

Sera hii ilipitishwa na serikali kwa madhumuni ya kutoa ufafanuzi na maelekezo ya namna ya kuratibu shughuli za kuhifadhi na kuyalinda mazingira. Baadhi ya malengo ya Sera ya Taifa ya Mazingira ni kuhakikisha upatikanaji, ulinzi na matumizi sawa ya rasilimali kwa ajili ya mahitaji muhimu ya vizazi vya sasa na vijavyo bila ya kuharibu mazingira au kuhatarisha afya au usalama wa binadamu.

Pia, kuzuia kudhibiti na uharibifu wa ardhi, maji, mimea na hewa ambavyo ndivyo vinashikilia mifumo ya maisha yetu. Malengo haya yanatakiwa yatekelezwe kikamilifu na yasimamiwe na watendaji makini. Mapungufu au uzembe katika kuratibu na kutekeleza malengo ya Sera ya Mazingira yatapelekea uharibifu wa mazingira na uzalishaji wa hewa ukaa na gesijoto kwa wingi.

Ili kuyalinda na kuyatunza mazingira, hatuna budi kukusanya na kutupa taka ngumu na taka-kimiminika tunazozalisha kila siku kwa uangalifu bila kuathiri mazingira na afya za wanadamu. Kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Mazingira, taka ngumu na taka-kimiminika hutupwa katika dampo lililofunguliwa na kusimamiwa kitaalamu.

Taka zinapotupwa katika dampo hulundikaka na kuoza. Taka hizi huzalisha gesijoto aina ya Methane ambayo husababisha mabadiliko ya tabia-nchi. Ni kwa minajili hii utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mazingira inachangia kuwepo kwa mabadiliko ya tabia-nchi.

Sera ya Wanyamapori, 2007

Sera hii iliundwa kwa lengo la kuhifadhi, kulinda na kuratibu matumizi endelevu ya wanyamapori na maeneo ya ardhi-oevu. Utekelezaji wa Sera hii hauna mchango wa moja kwa moja kwa mabadiliko ya tabia-nchi. Ila uhifadhi wa wanyamapori huchangia kwa namna moja au nyingine kuwepo kwa mabadiliko ya tabia-nchi. Vinyesi vya wanyamapori na uwindaji haramu wa kuwaua hovyo wanyamapori kwa kusaka ngozi au pembe za ndovu huzalisha hewa ukaa na gesijoto ambavyo huchangia mabadiliko ya tabia-nchi.

Sera ya Taifa ya Nishati, 2003

Sera hii inanuia kuhakikisha kuwepo na upatikanaji wa nishati ya kudumu na ya bei nafuu na kuwepo kwa matumizi endelevu ya nishati ili kuchagiza maendeleo ya kiuchumi. Upatikanaji wa nishati ya uhakika na ya kudumu unahitaji kutekelezwa kwa shughuli za ufuaji au uzalishaji wa nishati kwa njia tanzu tofauti. Nishati huzalishwa kwa kutumia maji, mionzi ya jua, upepo, petroli, nuklia na mimea (kwa mfano, bayo-dizeli). Uzalishaji nishati kwa kutumia njia hizi kunaweza kukasababisha mabadiliko ya tabia-nchi.

Mfano hai ni kuzalisha nishati ya bayo-dizeli kwa kutumia mibono. Uzalishaji wa nishati kwa njia hii hutumia maeneo makubwa ya mashamba ambayo huanzishwa kwa kukata miti ili kupata eneo la wazi la kulima mibono. Kwa kukata miti uoto wa asili unaofyonza hewa ukaa utaondolewa na kupelekea kuwepo kwa mlundikano mkubwa wa hewa ukaa na gesijoto angani.

Pia, ufuaji umeme kwa kutumia petroli kunapelekea kupata nishati bora kwa matumizi ya uzalishaji na kuleta maendeleo. Ila matumizi ya petroli kwa kuzalisha umeme kunachangia kwa kiwango kikubwa kuongezeka kwa hewa ukaa duniani. Kwa kutekeleza Sera ya Taifa ya nishati kuzalisha nishati kusipotilia maanani athari za mazingira zinazoletwa na matumizi ya njia husika ya uzalishaji umeme/nishati kunachangia mabadiliko ya tabia-nchi.

Sera ya Taifa ya Kilimo kwanza

Baadhi ya mazao ya nafaka hasa yale yalimwayo katika maji mengi yanachangia kuongezeka kwa gesi joto iitwayo methane. Hii inatokana na kupungua kwa hewa ya oksijeni kwenye udongo kadri maji yanavyokuwa mengi na kusababisha kuoza kwa masalia ya mimea na wanyama. Mimea kama ya mpunga haiwezi kushikilia kabon kwenye udongo kukiwa hakuna oksijen, na hii husababisha bakteria walioko ardhini kutengeneza methane. Hii gesi joto inayotengenezwa huachiliwa angani kwa njia ya upumuaji unaofanywa na mimea ya mpunga. Hivyo husababisha kuongezeka kwa gesi joto angani.

Hitimisho

Utekelezaji wa Sera mbalimbali za Taifa unalenga kuchagiza maendeleo ya kiuchumi na kupunguza umaskini. Ni dhahiri kuwa Sera huchangia kuwepo kwa mabadiliko ya tabia-nchi. Hivyo, utekelezaji wa Sera hizi unatakiwa ufanyike kwa umakini wa hali ya juu ukizingatia masuala ya mazingira na athari za utekelezaji wake.