Thursday, March 31, 2016

WADAU WANASEMAJE KUHUSU- MRADI WA USHIRIKI WA WANANCHI KATIKA USIMAMIZI WA MALIASILI

Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira (LEAT) inatekeleza mradi miaka minne wa ‘Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili’, kwa ufadhili kutoka kwa watu wa Marekani kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (USAID-Tanzania). Mradi huu unatekelezwa katika wilaya za Mufindi na Iringa vijijini katika mkoa wa Iringa. Mradi unatekelezwa katika vijiji 32, na inatarajiwa kuwa zaidi ya watu 6500 watafaidika na mradi. Mradi ulianza mwaka 2014 unatarajiwa kukamilika mwaka 2017.
Katika utekelezaji wa mradi huu, LEAT kwa kushirikiana na Mashirika ya kijamii wanawajengea uwezo wananchi kuhusu ‘Usimamizi wa Maliasili pamoja na Ufuatiliaji Uwajibikaji Jamii. Ilkufikia watu wengi katika makundi mbalimbali LEAT inatoa mafunzo kwa Madiwani, kamati za vijiji na wilaya za maliasili na ardhi; pamoja na wananchi kutoka makundi mbalimbali ya jamii.
Yafuatayo ni baaadhi ya maoni ya wananchi waliofikiwa na mradi:
 
 
Yahya Kutika
Yahya Kutika, akiwa katika bustani ya kupandia miti, kijijini Kiwere
 
Mafunzo ya mradi yamefungua fikra zangu. Nimeanza kufikiri tofauti na nilivyokuwa nikifikiri hapo awali, sasa ninafahamu madhara ya matumizi yasiyo endelevu ya maliasili hususan misitu. Kabla ya mradi, sikujali kuhusu usimamizi wa misitu, na nilikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wanakata miti kwaajili ya kuchoma mkaa. Nilidhani kuwa mimi si wa kulaumiwa kwa kuwa ilikuwa ilikuwa haki kufurahia maliasili zilizopo. Licha ya kuwa watu wengi kijijini wanategemea kuni kama nishati, na vijana wengi wanategemea uuzaji mkaa kama chanzo cha mapato, nadhani kuna haja ya kuangalia njia bora za uvunaji ilitupunguze hatari ya kutoweka kwa rasilimali misitu.
 
Abdul Chang’a
Abdul Chang'a mmoja wa wanakikundi cha uhifadhi mazingira cha Kiwere

Mimi na wake zangu wawili ni wanufaika wa mradi, tulihudhuria mafunzo na tumeshiriki katika utekelezaji wa mradi kwa kuelimisha wenzetu umuhimu wa kutunza msitu wetu, na kuhamasisha upandaji miti katika maeneo yaliyo athiriwa kwa ukataji miti. Tumekuwa mstari wa mbele kuunga mkono jitihada hizi ambazo zinalenga kuiepusha nchi yetu na athari zitokanazo na uharibifu wa mazingira. Huwa ninasikia katika redio namna ambavyo uaharibifu wa misitu umeathiri maeneo mengine duniani, nisingependa hali hiyo itupate. Mimi ni miongoni mwa watu 17 tunaounda kikundi cha uhifadhi mazingira cha Kiwere.
 
Bruno Mpagama
Bruno Mpagama akionesha miche ya miti iliyopandwa na kikundi chao cha Kiwere Hifadhi Mazingira
 
Changamoto kubwa katika usimamizi wa maliasili ni kuwa watu wengi wahatambui wajibu wao, pia nadhani kutofahamu dhana nzima ya ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili. Haya yalidhihirika wakati wa mafunzo ya mradi, ambapo wengi wetu tulikiri kutofahamu dhana hiyo. Nimejifunza kuwa kuto fahamu umuhimu wa kutunza rasilimali hizi za thamani, kuna athari kubwa kwa viumbe hai, kizazi cha sasa na kijacho.
Kutofahamu thamani ya maliasili zetu ndiko kumechangia wananchi wengi wanaoishi karibu na maliasili hizo kuendelea kuwa masikini. Rasilimali hizi zikitunzwa na kutumiwa kwa utaratibu unaofaa zitatunufaisha.
Kupitia mafunzo yaliyotolewa na LEAT nimejifunza kuwa mimi ndiye mdauwa kwanza wa usimamizi wa maliasili, lakini pia nimejifunza sheria na kanuni zilizowekwa ili kurahisisha utelekezaji wa wajibu wangu. Zaidi ya hayo nimefahamu haki na wajibu wangu katika kusimamia utendaji wa viongozi wangu kupitia mfumo wa Ufuatiliaji Uwajibikaji Jamii. Mafunzo haya yamenijengea ujasiri wa kuhoji viongozi wangu kuhusu mapato na matumizi ya mapato yatokanayo na maliasili za kijiji. Mfumo wa Ufuatiliaji Uwajibikaji Jamii unakwenda zaidi ya usimamizi wa maliasili, mfumo huu tutautumia katika kufuatilia katika huduma za jamii, ikiwemo elimu, afya, maji na miundombinu.
 
Mashaka Kilanga- Katibu MJUMUKK
Mashaka Kilanga, Katibu wa MJUMIKK shirika la kijamii linaloshughulikia mazingira, ambalo pia ni miongoni mwa mashirika manne ya kijamii yanayotekeleza mradi
 
Nadhani mradi wa ushiriki wa wananchi katika kusimamaia maliasili umefika kwa wakati katika kijiji chetu. Hapa kijijini tuna msitu wenye ukubwa wa hekta 4904 ambapo kati ya hizo takribani hekta 50 za msitu zimeharibiwa kwa ukataji miti ovyo.
Nathubutu kusema kuwa mafunzo ya mradi wa ushiriki wa wananchi katika kusimamia maliasili ni muhimu sana ilikunusuru harati inayoweza kutokea katika mazingira na viumbe hai. Kabla ya kufikiwa na mradi huu vitendo vya uharibifu wa maliasili vili kithiri ikiwa ni pamoja na ukataji miti usio zingatia taratibu za misitu endelevu, ukataji miti kwaajili ya kuandaa mashamba pamoja na uchomaji misitu ili kufukuza wanyama wanao haribu mazao.
Baada ya kupatiwa mafunzo ya mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili, wananchi wamefahamu wajibu wao na wameanza kuchuka hatua ya ulinzi shirikishi katika msitu wa kijiji. Pia serikali ya kijiji imesitisha vibali vya uvunaji msituni, pia inahamasisha wananchi kupanda miti katika kaya zao.
Nawashukuru LEAT na shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani kwa kutuletea mradii huu ambao utanusuru hatari iliyoanza kuukumba msitu wetu.
 
 
Hamza Chang’a
 
Hamza Chang'a, Kiongozi wa kikundi cha uhifadhi mazingira cha Kiwere, akiwa katika bustani ya kupandia miche ya miti
 
Baada ya kuhudhuria mafunzo ya mradi na kuhamasika, mimi na wenzangu 16 tuliamua kuunda kikundi cha kuhifadhi mazingira na tumefanikiwa kupanda miti 45,000 ambayo itapandwa katika eneo la hekta 50 lililo haribiwa kwa ukataji miti. Miti mingine tutaigawa kwa makundi mbalimbali, pamoja na kuendelea kuhamasisha watu kuwa walinzi wa msitu wetu na waendelee kupanda miti ilikukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Nakiri kuwa mkoa wa Iringa tumebarikiwa kuwa na rasilimali misitu na wanyamapori, vitu ambavyo maeneo mengine ya nchi yetu havipatikani, hivyo tunawajibu wa kutunza maliasili hizi ili zituinue kiuchumi, tuondokane na umasikini uliokithiri.
Nimefaidika na mafunzo ya mradi, nimefahamu wizara na taasisi zinazo husika katika uhifadhi na usimamizi wa maliasili. Pia nimazifamahu sheri, kanuni na miongozo inayotumika kusimamia rasilimali hizi, bila kusahau wajibu wangu wa kisheria na kikatiba.
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 

Tuesday, March 22, 2016

SIKU YA MAJI DUNIANI

KAULI MBIU: MAJI BORA, AJIRA BORA

Leo ni siku ya maji duniani, kaulimbiu ‘Maji bora, Ajira bora’. Kauli mbiu hii inaelezea umuhimu wa maji kwa maendeleo endelevu. Ni kweli iwapo maji yatapatikana katika jamii yanaweza kuleta ajira zenye heshima na  staha ambazo zitabadilisha uchumi na maisha ya watu. Upatikanaji wa maji safi na salama kwa maeneo ya mijini na vijini bado ni changamoto kubwa. Kwa maeneo ya mijini inachangiwa na kutokuwepo na miundo mbinu ya maji ya kutosha, uharibifu wa miundo mbinu iliyopo, gharama kubwa za kuunganishiwa maji kutoka mamlaka za maji pamoja na gharama kubwa za kuchimba visima binafsi.
Moja ya vyanzo vya maji ambavyo vianapaswa kulindwa na kutunzwa

Mtoto akitoka kutafuta maji kwaajili ya matumizi ya familia.

Kwa maeneo ya vijijini, changamoto ni kubwa kwakuwa maeneo mengi hayajafikiwa na huduma kutoka mamlaka za maji, gharama kubwa za uchimbaji visima na uharibifu wa mazingira hasa katika vyanzo vya maji. Wakazi wengi wa vijijini wanategemea vyanzo asilia vya maji kama mito, maziwa na chemchem. Lakini wananchi hao ndio huharibu vyanzo hivyo na kuongeza tatizo la upatiakanaji wa maji.

LEAT kupitia mradi wetu wa ‘Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili’ unaotekelezwa katika wilaya za Iringa vijijini na Mufindi, tunaendelea kuelimisha jamii, umuhimu wa kutunza misitu na vyanzo vya maji kwa maendeleo endelevu. Vyanzo vingi vya maji vinaanzia misituni, hivyo misitu inapotunzwa hutunza vyanzo vya maji.

Moja ya matunda ya mafunzo yanayotolewa kupitia mradi huu katika utunzaji na usimamizi wa maliasili misitu pamoja na rasilimali zinazopatikana humo ikiwemo rasilimali finyu ya maji, ni kuimarika kwa utekelezaji wa sheria za usimamizi wa maliasili na maji, zinazosimamiwa na serikali za vijiji. Kabla ya mradi wananchi walikiri kulegalega kwa utekelezaji wa sharia hizo na kusababisha uharibifu wa vyanzo vya maji na misitu. Pia, serikali kwa kushirikiana na wananchi wameweka vibao kuonesha vyanzo vya maji ili watu wasilime katika vyanzo vya maji.

Elimu zaidi inahitajika ili wananchi waelewe madhara ya uharibifu wa mazingira hususan vyanzo vya maji, ilikupunguza adha ya ukosefu wa maji katika jamii. Ukosefu wa maji katika jamii hupelekea wanawake na watoto kutembea umbali mrefu kila siku ilikutafuta maji kwa matumizi ya familia zao. Kazi ya kutafuta maji ni ngumu, licha ya umuhimu wake, ni kazi isiyokuwa na ujira wala kuthaminiwa.
Iwapo upatikanaji wa maji utakuwa wa uhakika, wanawake hawa wangeweza kupata muda wa kujifunza ujuzi ambao ungewasaidia kupata kazi bora zaidi. Ili kuunga mkono agenda ya siku ya Maji Duniani ya mwaka 2016 kila mmoja katika nafasi yake ashiriki katika kutoa elimu ya usimamizi na utunzaji wa vyanzo vya rasilimali maji, kuhakikisha kuna uhakika wa upatikanaji wa maji safi na salama, na kusaidia upatikanaji wa ajira kutokana na maji.

Maji ni muhimu katika kukua kwa uchumi, ustawi wa jamii na viumbe hai. Tanzania imebarikiwa kwa vyanzo vya maji ikiwa ni pamoja na mito, maziwa, maeneo oevu na bahari. Kwa miaka ya hivi karibuni Tanzania imeona kupungua kwa maji kwa kiasi kikubwa katika vyanzo hiyo, na baadhi ya vyanzo vimekauka kabisa. Katika kusaidia athari zaidi, kila mtanzania anawajibika kulinda vyanzo vya maji. 

Duniani wadau wa maendeleo wanaupa kipaumbele mpango wa maji safi na salama kwa maendeleo ya uchumi wa kijani. Kauli mbiu ya mwaka huu imealenga kuonesha jinsi maji yanavyoweza kuunda ajira za heshima katika kuchangia uchumi wa kijani na maendeleo endelevu.

Shirika la dunia linaloshughulikia programu za mazingira, limefafanua dhana ya Uchumi wa Kijani kuwa ni uchumi unaolenga matokeo ya kuboresha ustawi wa binadamu, usawa wa kijamii na kupunguza kwa kiasi kikubwa hatari za mazingira na uhaba wa viumbe hai. Uchumi wa kijani umelenga zaidi kwa maitafa yanayoendelea kwakuwa ndio waathirika wakubwa wa matokeo ya uharibifu wa mazingira.
 
Wanawake na watoto wakitoka kutafuta maji

Friday, March 18, 2016

JENGA UWEZO KULETA UWAJIBIKAJI- LEAT WASHIRIKI WARSHA YA UANDISHI WA UCHECHEMUZI


Katika kutekeleza lengo la shirika la Pamoja Twajenga la ‘Jenga Uwezo Kuleta Uwajibikaji’ shirika hilo liliandaa warsha elekezi ya siku moja ya uandishi wa mpango makakati wa uchechemuzi (Advocacy Strategy) kwa Asasi zinazo fanyakazi nazo. Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) walishiriki warsha hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Pamoja Twajenga, tarehe 16 Machi, 2016.

Mafunzo hayo yalilenga kuwakutanisha wadau wa Pamoja Twajenga iliwaweze kushirikishana uzoefu wao katika uandishi wa mpango mkakati wa uchechemuzi kwa kila Asasi. Washiriki walipitia mipango mikakati yao kwa kuangalia mpangilio wa uandishi pamoja na maudhui, ili wadau wote waweze kuwa na mfumo mzuri na unaolingana utakao rahisisha katika upimaji wa matokeo ya utekelezaji wa Asasi, pamoja na kukidhi vigezo vya mfadhili (USAID)-Tanzania.

Miongoni mwa vitu muhimu vilivyo angaliwa katika uandishi wa mpango makakati wa uchechemuzi ni pamoja na kuahikisha kuwa wanaweka kipengele cha jinsia na makundi maalum katika jamii, ilikuhakikisha kuwa utekelezaji wa shughuli au miradi wa Asasi unazingatia makundi hayo muhimu.

Akiwakaribisha washiriki, Mkuu wa Shirika la Pamoja Twajenga, Charles Nonga, alisema kuwa warsha hiyo ya siku moja imelenga kutoa fursa kwa Asasi zinazo fanyakazi na shirika lake kubadilishana uelewa katika uchechemuzi, wakizingatia kuwa mpango kazi wa Pamoja Twajenga unalenga kujenga uwezo miongoni mwa Asasi hizo.

“Badala ya sisi kuendelea kupanga na kufanya kila kitu tuliamua mwaka wa tatu wa mradi, tuwe tunakutana na kuelezana tunafanya nini na tupate fursa ya ufumbuzi wa changamoto tunazo kutananazo. Kwa mtazamo huu shirikishi nategemea mambo yanayoendelea katika miradi yetu yataleta tija”, alisema Nonga.

Picha ya pamoja baada ya warsha,

Kutoka kushoto: Afisa Mradi wa PELUM Tanzania, Angolile Rayson; Mtaalam Uchechemuzi wa Pamoja Twajenga, Tobia Chelechele; Afisa Uchechemuzi wa NACOPHA, Last Mlaki; Afisa Mawasiliano na Nyaraka- NACOPHA, Mensia John; Afisa Ufuatiliaji na Tathmini wa LEAT, Safarani Msuya; Afisa Mawasiliano wa LEAT, Miriam Mshana na Mkurugenzi wa PELUM Tanzania, Donati Senzia.

Naye Afisa Mawasiliano wa LEAT Miriam Mshana alisema kuwa, ushiriki wa Asasi mbalimbali unasiadia kufahamu aina mbalimbali za uandishi wa mapango mkakati wa uchechemuzi, pamoja na kupata njia tofauti za utatuzi wa baadhi ya vipengele ambavyo vilikuwa vikimpa changamoto.

Aliongeza kuwa Asasi zilipata fursa ya kujadili kwa upana umuhimu wa kuweka kipengele cha jinsia na makundi maalum katika jamii.

“Nimefurahi kuona namna ambavyo tumeshirikishana uzoefu katika kuhusisha jinsia na makundi maalum ya jamii ilikuweza kuwafikia watu wengi katika jamii. Ilikuleta tija katika utekelezaji wa programu inatulazimu kuzingatia usawa wa jinsia katika ufikiwaji na ufaidikaji wa jamii”, alisema Miriam.

Alifafanua kuwa, maendeleo yanaletwa na watu wote katika jamii bila ya kujali jinsia, jamii inahitaji kushirikishwa katika kuainisha wajibu na majukumu ya mwanamke na mwanaume ili kila mmoja apate fursa ya kuchangia maendeleo ya jamii yake.
 
Mshiriki mwingine kutoka Asasi ya NACOPHA, Last Mlaki, ambaye ni Afisa Uchechemuzi na Mtandao, alisema kuwa upitiaji wa uandishi wa mpango mkakati wa uchechemuzi utasaidia kwa Asasi kuwa na mfumo mmoja katika utekelezaji wa makakati huo.

“Pia tumeona baadhi ya Asasi hazikuweka kipengele cha jinsia na makundi maalum ya jamii, ambayo inaweza kuwa kikwazo cha kuyafikia makundi yote na kutambua changamoto na fursa wanazokutana nazo, pia inaweza kuta tafsiriwa kuwa kundi fulani halina umuhimu katika jamii, hivyo likashindwa kutoa mchango katika maendeleo”, alisema Mlaki.

Naye Mratibu Uchechemuzi kutoka TACOSODE Abraham Kimuli, alisema kuwa warsha hiyo imempa fursa ya kufanya baadhi ya maboresho ikiwemo uandishi wa malengo ya uchechemuzi na mtiririko mzuri wa mpango mkakati kwa kupata maoni ya washiriki wote, na kuongeza kuwa hiyo inasaidia kutambua maeneo yenye changamoto.

Akifunga warsha hiyo Mtaalamu wa Uchechemuzi wa Pamoja Twajenga, Tobia Chelechele alisema, warsha hiyo ilikuwa wamu ya pili, awamu ya kwanza ilifanyika Desemba 2015, awamu ya tatu itayanyika mwezi Juni na awamu ya mwisho itakuwa mwezi Septemba 2016.

Alisema kuwa awamu ya tatu ya mwezi Juni itahusu uandishi wa jumbe za uchechemuzi, na kuwataka washiriki wote kuandaa jumbe mbalimbali kulingana na miradi wanayofanya ili jumbe hizo ziweze kupimwa na washiriki wote ilikuongeza uelewa zaidi na kurahisisha utekelezaji wake.

Warsha hiyo iliongozwa na Mtaalamu Uchechemuzi wa Pamoja Twajenga, Tobia Chelechele, na kuhudhuriwa na Asasi za LEAT, TACOSODE, NACOPHA, WiLDAF na PELUM Tanzania.

Pamoja Twajenga ni wakala wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (USAID),  wanatekeleza shughuli zake chini ya program za USAID-Tanzania kupitia mpango wa Demokrasia, Haki za Binadamu na Utawala Bora, ilikusaidia uwajibikaji wa wananchi wa Tanzania. Pamoja Twajenga inafanyakazi na mashirika yaliyopata ruzuku kutoka USAID, ili kujenga uwezo wao katika kuboresha uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali za umma kupitia ushiriki wa raia.

 
Kutoka kulia: Afisa Ufuatiliaji an Tathmini wa LEAT, Safarani Msuya, na Mtaalamu Uchechemuzi wa Pamoja Twajenga, Tobias Chelechele akifafanua jambo wakati wa warsha.
Afisa Mradi wa PELUM Tanzania, Angolile Rayson na  Mkurugenzi wa PELUM Tanzania, Donati Senzia, wakifuatilia jambo

 
Mtaalamu wa Uchechemuzi wa Pamoja Twajenga, Tobias Chelechele akifuatilia mpango chechemuzi wa Asasa ya TACOSODE ulioandaliwa na Mratibu Uchechemuzi wa TACOSODE, bwana Abraham Kimuli, (kulia).
Kutoka kushoto ni Afisa Mawasiliano na Nyaraka (NACOPHA) Mensia John, Afisa Uchechemuzi wa NACOPHA, Last Mlaki wakiwasilisha mpango chechemuzi wa Asasi yao kwa Mtaalamu Uchechemuzi wa Pamoja Twajenga, Tobias Chelechele.
 

 

Tuesday, March 15, 2016

LEAT WAHUDHURIA WARSHA ELEKEZI YA UANDISHI WA MPANGO MKAKATI


Wafanyakazi wa Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) wanaotekeleza mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili, walishiriki warsha elekezi ya siku mbili iliyofanyika tarehe 11 na 12 Februari, 2016 katika hoteli ya Regency Park, jijini Dar Es Salaam.
Afisa Mradi wa LEAT Jamal Juma akichangia mada wakati wa semina elekezi ya uandishi wa mpango mkakati kwa Asasi za Kiraia

Baadhi ya washiriki wa warsha elekezi kutoka Asasi ya WILDAF
 
Lengo la warsha hiyo ilikuwa kuzikutanisha Asasi za Kiraia ambazo zinafadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (USAID), ilikuwaelekeza upya namna ya kuandika mpango mkakati wa utekelezaji wa shughuli za mashirika yao.

Pamoja na mambo mengine washiriki walipatafursa ya kufanya kazi kwa makundi pamoja na kupitia mipango mikakati inayokwisha muda wake ya baadhi ya Asasi za Kiraia, ilikuangalia ni kwa kiasi gani waliweza kutengeneza mopango hiyo.

Mkuu wa Shirika la Pamoja Twajenga, Charles Nonga aliyapongeza mashirika kwa kushiriki warsha hiyo, pia alisema kuwa anatarajia kila shirika lililohudhuria watakwenda kuyafanyia kazi mafunzo waliyoyapata na kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akitoa maoni kuhusu warsha hiyo, Afisa Ufuatiliaji na Tathmini wa LEAT, Safarani Msuya, alisema kuwa warsha hiyo ni muhimu kwake kwakuwa imegusia maeneo yanayohusu ufuatiliaji na tathmini ya Asasi kwa ujumla.
“Nimeongeza ujuzi wa namna ya kuandika mpango mkakati wa Asasi pamoja na kuandaa na kutekeleza mpango kazi wa ufuatiliaji na tathmini, natumaini ujuzi huu utaongeza uafanisi katika utekelezaji wa majukumu yangu kama Afisa Ufuatiliaji na Tathmini. Pia mafunzo haya nitayatumia wakati tutakapokuwa tuna tathmini mpango mkakati unaomaliza muda wake ili tuweze kuboresha mapango mkakati mpya”, alisema Safarani.

Kwa upande wake Afisa Mawasiliano wa LEAT, Miriam Mshana alisema kuwa warsha hiyo imemuongezea maarifa ya uandishi wa mpango mkakati wa Asasi. Alieleza kuwa warsha hiyo imetoa mwelekeo wa namna kila mmoja katika Asasi anavyopaswa kutekeleza majukumu yake kulingana na lengo walilojiwekea, pamoja na umuhimu wa kila mmoja kushiriki katika kutathmini mchakato wa utendaji wa Asasi ilikupata matokeo bora zaidi. Afisa Mwandamizi wa Mradi, Remmy Lema an Afisa Mradi Jamal Juma wa LEAT nao walishiriki warsha hiyo.

Hiyo ilikuwa ni sehemu ya kwanza ya mchakato wa warsha elekezi ya uandishi wa mpango mkakati, awamu ya pili itafanyika mwezi Aprili 2016, itakuwa ya vitendo zaidi ambapo wataalamu kutoka Pamoja Twajenga na Change Associate International watatembelea Asasi mojamoja ilikupima ni namna gani washiriki wanaweza kutumia ujuzi walioupata katika kutathmini mpango mkakati unaomaliza muda wake na uandishi wa mpango mkakati mpya.

Mafunzo ya warsha hiyo yalitolewa na shirika la Change Associate International lenye usajili jijini Washington DC, nchini Marekani na Dar Es Salaam, Tanzania. Takriban washiriki 40 kutoka Asasi za Kiraia zizofadhiliwa na USAID kwa Tanzania bara na Visiwani walishiriki warsha hiyo. LEAT inatekeleza mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika Usimamaizi wa Maliasili katika wilaya za Iringa vijijini na Mufindi, mradi huo umefadhiliwa na USAID. Asasi zilizohudhuria warsha ni pamoja na LEAT, NACOPHA, RECLAIM, WILDAF, MAT, WICSA, AAC, PELUM, Zanzibar Legal Service Center.

Warsha hiyo iliandaliwa na shirika la Pamoja Twajenga ambao ni Wakala wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (USAID)- Tanzania. Pamoja Twajenga wanatekeleza shughuli zake chini ya programu za USAID/Tanzania kupitia mpango wa Demokrasia, Haki za Binadamu na Utawala Bora, ilikusaidia uwajibikaji kwa wananchi wa Tanzania. Hasa Pamoja Twajenga inafanyakazi na Asasi za Kiraia zilizopata ruzuku kutoka USAID, ili kujenga uwezo wao katika kuboresha uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali za umma kupitia ushiriki wa raia.
Katika picha ya kikundi ni washiriki wakifanya kazi ya kikundi wakati wa warsha

Tuesday, March 8, 2016

SIKU YA WANAWAKE DUNIANI- WANAWAKE WAIPONGEZA LEAT KWA KUSAIDIA KUINUA UCHUMI WAO

Katika kusherekea Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa kila tarehe 8 mwezi Mchi, 2016, wanawake wanaoishi katika vijiji ambavyo LEAT inatekeleza mradi wa Ushirki wa Wananchi katika Usimamaizi wa Maliasili, wameipongeza LEAT kwa kuwapelekea mradi wa ufugaji nyuki ilikuinua viapato vyao.
Bi. Felista Choga, mkazi wa kijiji cha Lugoda Lutali, wilayani Mufindi, mkoani Iringa alisema kuwa anatarajia kunufaika na mradi wa ufugaji nyuki kwakuwa utaongeza kipato na kuboresha maisha ya familia yake.
Bi. FelistaChoga mmoja wa wanufaika wa mradi wa ufugaji nyuki
 
Bi. Felista alisema kuwa mwanamke anawajibu mkubwa kwa familia na jamii kwa ujumla kwasababu ndiye mlezi na anatarajiwa kuwajibika kwa ustawi wa familia, hivyo endapo mwanamke atakuwa na vyanzo zaidi ya kimoja vya mapato ataboresha kipato cha familia pia atakuwa na muda wa kujitolea kusimamia maliasili.
 
"Matumizi ya asali yameongezeka katika jamii, hii ni kutokana na umuhimu wake kwani asali inatumika kama chakula, kwamfano baadhi ya watu hutumia asali badala ya sukari ya viwandani, pia asali ni dawa, huwa tunatumia katika kutibu, magonjwa ya tumbo, na kifua, ikichanganywa na amdalasini iliyo twangwa, pia ni dawa ya kutibu majeraha yatokanayo na kuungua na moto, hivyo natumaini ni biashara nzuri kutokana na umuhimu wake", alisema Felista.
 
Mimi ni mkulima na nimekuwa nikitegemea kilimo kupata mapato, sasa hivi nimepata chanzo kingine cha mapato, natarajia maisha yangu yataimarika, aliongeza.
Akiongelea nafasi ya mwanamke katika Usimamizi wa Maliasili, alisema kuwa, mwanamke ndiye mtumiaji mkuu wa maliasili hizi, hivyo alipaswa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa usimamizi na kufanya maamuzi ya matumizi ya mazao yatokanayo na maliasili hizi hasa misitu.
 
Alisema kuwa mwanawake pamoja na kuwa ndiye mtafutaji mkubwa na mtumiaji wa mazao yatoka nayo na misitu, bado hajashiriki kikamilifu katika usimamizi wa maliasili, hiyo inatokana na kutotambua wajibu wake katika jamii.
 
"Kwa nafasi yangu kama Mjumbe wa kamati ya maji ya kijiji, huwa nina hamasisha wanawake wenzangu katika vikundi vyetu kuwa wanahaki na wajibu wa kushiriki katika ngazi za maamuzi katika usimamizi wa maliasili za kijiji, pia nitashirikiana na wanawake wenzangu kueneza ujumbe huu katika mikutano ya hadhara ya kijiji, ili hata vijana na wanaume watambue majukumu na umuhimu wa wanawake katika kuharakisha maendeleo ya kijiji chetu", alisema.
 
Aliendelea mbele kusema kuwa Mafunzo ya Uwajibikaji Jamii yanayotolewa na LEAT katika mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili, yamemjengea ujasiri wa kuwakilisha maoni ya wanawake wenzake katika kamati ya maji ya kijiji chao.
 
Akiongelea kuhusu kauli mbiu ya siku ya wamawake kwa mwaka 2016, ya 'Ahadi kwa Usawa', alisema kuwa usawa utapatikana iwapo wanawake watajengewa uwezo wa kutambua wajibu wao na fursa zinazopatikana katika jamii, iliwaweze kushiriki katika masuala ya maendeleo.
 
Alifafanua kuwa kumuwezesha mwanamke kiuchumi pamoja na kushiriki katika fursa zinazopatikana katika jamii, kutachochea kasi ya kufikia malengo ya usawa wa jinsia. Alifafanua kuwa jitihada zaidi zinahitajika katika kusaidia wanawake wanaoishi vijijini kupata fursa sawa na wanawake wanaoishi mijini ilikupunguza tofauti ya maendeleo ya wanawake waishi mijini na wale waishio vijijini.
Alisema kuwa wanawake wa vijjini wanakosa fursa muhimu kama vile fursa ya mikopo ya fedha kwaajili ya shughuli za kilimo na biashara. 'Mwanamke mwenye uchumi bora ana heshimika na kuthaminiwa katika jamii, na atashirikishwa katika kufanya maamuzi. Serikali na mashirika ya maendeleo yaongeze nguvu katika kupunguza tofauti kubwa kati ya walionachi na wasionacho, ambapo wengi wa wasionacho ni wanawake wa vijijini', alisema.
Natoa shukran za dhati kwa Shirika la Maendeleo la Marekani, USAID kwa kufadhili mradi huu ambao utanusuru misitu yetu pamoja na kutuletea chanzo mbadala cha mapato, Serikali na Mashirika mengine ya maendeleo yangesaidia katika kutoa elimu ya biashara na mikopo kwaajili ya wanawake.
 
LEAT inatekeleza mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili, katika wilaya za Iringa vijijini na Mufindi, mkoani Iringa. Mradi umefadhiliwa na Watu wa Marekani, kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID), ni mradi wa miaka minne, ulianza mwaka 2014 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2017. Mradi huu unatekelezwa katika vijiji 32, na unatarajiwa kuwa zaidi ya watu 6500 watafikiwa na mradi huu.
Katika utekelezaji wa mradi huu, LEAT ilijengewa uawezo na PAMOJA TWAJENGA ambao ni wakala wa USAID Tanzania, na LEAT ikawajengea uwezo Mashirika ya kijamii, Kamati za wilaya na Vijiji za maliasili, Ardhi, Maofisa wa serikali kutoka idara za Maliasili na Ardhi, Madiwani na Wananchi wanao wakilisha makundi mbalimbali ya jamii.
Mafunzo yanayotolewa ni pamoja na sheria zote zinazohusu usimamizi wa maliasili zikiwemo, Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999, Sheria ya Serikali za mitaa ya mwaka 1982, Sheria ya Mazingira ya 2004, Sheria ya Misitu ya 2002, Sheria ya Hifadhi za Taifa ya 1959 na  Sheria ya Uhifdhi Wanyamapori ya mwaka 2007. Pia LEAT inafundisha Kanuni, Miongozo na Adhabu zinazo husiana na usimamizi wa maliasili.
 
 



SIKU YA WANAWAKE DUNIANI-MACHI 8, 2016


KAULI MBIU- ‘AHADI KWA USAWA’

Leo tarehe 8 Machi 2016, wanawake duniani wanasherekea siku ya yao (Siku ya Wanawake Duniani), kwa kauli mbiu ya ‘Ahadi Ya Usawa’. Kauli mbiu hii inahamasisha watu wote wake kwa waume kuahidi kuwa watachangia kufikia mafanikio ya usawa wa jinsia katika jamii. Kauli mbiu hii inasisistiza watu wote kuchukua hatua mathubuti ilikusaidia kufikia usawa wa jinsia haraka zaidi; kwa kuwasaidia wanawake na wasichana kufikia matarajia yao katika elimu, uchumi, uongozi wa siasa, huduma za jamii pamoja na kuwaheshimu na kutambua tofauti ya kijinsia.

Mwaka 2014, Jukwaa la Uchumi Duniani lilikadiria kuwa itachukua muda mrefu mpaka mwaka 2095 kufikia usawa wa jinsia duniani. Mwaka mmoja baadaye, mwaka 2015 walikisia kuwa kutokana na kasi ndogo ya maendeleo katika kupunguza pengo la usawa wa jinsia litapungua ifikapo mwaka 2133.


Wanawake wa Afrika

Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili katika
kusaidia kufikia Usawa wa Jinsia ifikapo mwaka 2030

Kaulimbiu ya mwaka 2016 inatoa wito kwa watu wote kusaidia kufikia usawa wa jinsia duniani, Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT), wanahamasisha usawa huo kwa kuhakikisha kuwa wanawake wanashiriki kikamilifu katika Usimamizi wa Mali Asili kupitia mradi wa ‘Ushiriki wa Wananchi katika Kusimamia Maliasili’ unaotekelezwa katika wilaya za Iringa Vijijini na Mufindi mkoani Iringa, kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID).

LEAT inatambua na kupongeza jitihada kubwa zinazofanywa na wanawake wa Tanzania katika kuchangia maendeleo ya taifa hili. LEAT inatambua kuwa ushiriki wa wanawake katika usimamizi wa maliasili sio tu kuwa ni suala la usawa wa jinsia lakini pia kutoshiriki kikamilifu kwa wanawake kunaathiri ufanisi wa usimamizi wa maliasili.

Kauli mbiu ya mwaka 2016 inatoa wito kwa watu wote kuahidi kuwa watawawezesha wanawake na wasichana kufikia matarajiao yao, imedhihirika kuwa upatikanaji wa vitu muhimu kwa maisha ya wananchi wa vijijini kama vile maji, chakula, nishati-kuni pamoja na dawa, kutawawezesha wasichana kupata muda sawa na wavulana wa kijisomea wakiwa nyumbani, kwa kuwa wasichana watatumia muda mfupi kusaidia mama zao kutafuta kuni, maji, dawa na chakula kwaajili ya matumizi ya familia.

Katika utekelezaji wa mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika Usimamazi wa Maliasili, LEAT inatoa mafunzo ya sheria zinazohusika katika usimamizi wa maliasili, pamoja na mafunzo ya Uwajibikaji Jamii (Social Accountability Monitoring) kwa wadau mbalimbali wakiwemo, Madiwani, Kamati za vijiji na wilaya za Maliasili, Ardhi na Mazingira; Mashirika ya kijamii pamoja na wawakilishi wa makundi mbalimbali ya kijamii.

Ilikuhakikisha kuwa wanawake wanashiriki katika kupanga, kuamua na kusimamia maliasili, LEAT inasisitiza kuwepo kwa idadi kubwa ya wanawake wanakaoshiriki katika mafunzo ya mradi, ilikuleta matokeo chanya kwakuwa, iwapo maliasili zitatunzwa, zitasimaiwa na kutumika vizuri mwanamke ndiye mnufaika mkubwa kwa kuwa yeye ndiye mwenyejukumu la kuhakikisha kuwa maliasili hizo (maji, nishati-kuni) na chakula vinapatikana kwa matumizi ya familia na jamii.

Pia endapo maliasili hizo hazikutunzwa, kusimamiwa na kutumiwa vizuri na hatimaye kupungua au kutoweka; mwanamke ndiye anayepata athari zaidi kwa kuwa atalazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji, kuni na chakula kwaajili ya familia.

Elimu zaidi ya usawa wa jinsia inahitajika kutolewa kwa jamii ili kuongeza kasi ya kufikia usawa wa jinsia ifikapo mwaka 2030. Hii imedhihirika katika mafunzo ya mradi unaotekelezwa na LEAT mkoani Iringa. Ushiriki wa wanawake katika baadhi ya vijiji unatia moyo lakini bado kuna changamoto kubwa, elimu inapaswa kuendelea kutolewa ili wanawake wenyewe watambue wajibu na umuhimu wao katika kufikia usawa wa jinsia.

Licha ya kuwa na idadi ndogo ya wanawake wa vijijini katika kushiriki ama kushika nyadhifa mbali mbali za uongozi, wanawake ambao wamepata nafasi katika kamati mbali mbali za maendeleo za vijiji wamekuwa Mabalozi wazuri wanao toa elimu kwa wanawake wenzao pamoja na jamii kwa ujumla.

Mafunzo ya Uwajibikaji Jamii yamewawezesha wanawake kutambua wajibu wao, kuwa na ujasiri wa kuwahoji watendaji wa serikali kuanzia ngazi ya kijiji, kuhusu mapato na matumizi ya fedha za kijiji, pamoja na ubora wa upatikanaji wa huduma za jamii. Wanawake pia wamekiri kuwa mafunzo haya yamewaongezea weledi wa kusimamia ustawi wa familia na jamii zao.

Wanawake na Chanzo Mbadala cha Mapato

LEAT pia imetoa mafunzo ya ufugaji nyuki pamoja na kugawa mizinga ya nyuki bure kwa wote waliopatiwa mafunzo. Ilisisitiza kuwepo kwa uwiano mzuri kati ya wanawake na wanaume wanaoshiriki mafunzo, ili kuondoa dhana ya kuwa ‘ufugaji nyuki ni mradi ya wanaume tu’, pia ni kutoa fursa ya wananchi wanaoishi katika maeneo yenye maliasili kuwa na chanzo mbadala cha mapato, kuliko kutegemea mazao ya maliasili kujipatia kipato.
Wanawake wengi wanatarajia kunufaika na mradi wa ufugaji nyuki na kuboresha maisha ya familia zao, kwani kuna baadhi ya wanawake ndio walezi pekee wa familia, hii ni kutokana na kufiwa na waume zao, kuachika ama kutelekezwa. Mwanamke anapokuwa na vyanzo vya mapato vya uhakika, anakuwa na amani, ujasiri na ari ya kusimamia maliasili za kijiji. Pia mwanamke anapokuwa na uchumi mzuri, kuna uwezekano mkubwa wa familia na jamii yake kufaidika moja kwa moja na uchumi huo.

 Changamoto zinazo kwamisha Usawa wa Jinsia katika Usiamamizi wa Maliasili

Kuna changamoto mbalimbali ambazo zina kwamisha ama kuchelewesha kufikia kwa usawa wa jinsia ikiwa ni pamoja na uelewa mdogo wa dhana ya usawa wa jinsia, jamii kutotambua majukumu ya wanawake na wanaume, mila na desturi kandamizi pamoja na kulega lega katika utekelezaji wa sera na sheria.

Uelewa mdogo wa dhana ya usawa wa jinsia katika kuleta maendeleo imekuwa ni kikwazo kikubwa katika kufikia adhma hiyo. Watu wengi wanadhani kuwa usawa wa jinsia ni wanawake kuacha kuheshimu wanaume pamoja na kuacha mila na desturi zinzazo wataka wanawake kuwa wanyenyekevu mbeley ya wanaume. Ukweli ni kwamba usawa wa jinsia ni kutoa fursa sawa kwa wanawake na wanaume katika kumiliki uchumi, kupata elimu, nafasi sawa katika uongozi na maamuzi pamoja na fursa sawa katika upatikanaji wa haki, huduma za jamii, kuheshimiwa na kuthaminiwa, kwa kuzingatia kuwa binadamu wote ni sawa, haya yanatekelezwa bila kuathiri mila na desturi za jamii husika kwa kuzingatia haki za binadamu.

Kikwazo kingine ni jamii kuto tambua majukumu ya wanawake na wanaume, kutokana na ukweli kuwa mwanamke ndiye mlezi mkuu wa familia, mara nyingi inatokea baba anatelekeza famila na kumuachia mama mzigo wa kulea familia. Mama anapokuwa mlezi pekee wa familia anakuwa na majukumu mawili, kutafuta kipato na kutafuta mahitaji muhimu ya familia, kwa wanawake wa vijijini ni changamoto zaidi kwa kuwa wanawake hupoteza mida mwing kutafuta maji na kuni kwa matumizi ya familia.
Mila na desturi kandamizi ni pale ambapo wanaume wanapoona kuwa mwanamke ni mtu dhaifu asiye stahili kupewa madaraka makubwa, na kuwa ni mtu anayepaswa kuongozwa tu. Licha ya kuwa kumekuwa na mwamko kwa wanawake waishio mijini, changamoto bado ipo kwa wanawake waishio vijijini ambao inadaiwa kuwa ni wengi kuliko waishio mijini.
Pia wanawake wenyewe kutojiamini kuwa wanaweza kutenda mambo makubwa katika jamii, hii inatokana na mila na desturi kandamizi, kuwa mtoto wa kike tangu akiwa mdogo anafundishwa kuwa yeye ni mlezi wa familia lakini si mzalishaji mali.

Kulega lega kwa utekelezaji wa sera na sheria kumechangia kupunguza kasi ya kufikia usawa wa jinsia. Sera na sheria zinaeleza vizuri mipango ya serikali kufikia usawa wa jinsia lakini utekelezaji wake ni hafifu. Kwamfano, sera na sheria ya ardhi inaeleza wazi kuwa kila mtu anahaki ya kumiliki ardhi, lakini cha kushangaza serikali haijafanya jitihada za kutosha kuhakikisha kuwa wanawake wanapewa kipaumbele kwa kuwezeshwa kumiliki ardhi kwa kuwa umiliki wa ardhi unahitaji pesa nyingi, na wanawake wengi ni masikini. Serikali ilipaswa iwawezeshe wanawake hawa kumiliki ardhi kwa kuitoa kwa mikopo nafuu. Ilikufikia usawa wa 50/50 katika ngazi za maamuzi tunapaswa ku hakikisha kuwa kuna usawa katika kumiliki uchumi.

Matumaini ya Kufikia Usawa wa Jinsia

Baada ya mkutano wa Wanawake uliofanyika Jijini Beijing, nchini China mwaka 1995, Tanzania imesaini mikataba mbali mbali ya kimataifa ya kuzuia ukatili wa kijinsia na kukubali kusaidia wanawake kupata fursa sawa na wanaume ilikuharakisha maendeleo.  

Serikali pia imetoa fursa mbalimbali ilikusaidia wanawake kushiriki katika ngazi mbali mbali za uongozi na siasa, kwamfano Tanzania kwa mara ya kwanza ina Makamu wa Rais mwanamke, Mh. Samia Suluhu, pia ilikuwa na mwanamke Spika wa Bunge, Anna Makinda, Mama Asha Rose Migiro alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa kwanza mwanamke; na alishika wadhifa wa juu kimataifa alipokuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Wapo wanawake wengi katika nchi hii waliopata nafasi za juu za uongozi katika siasa kwa upande wa vijijini kuna wanawake wamepata Udiwani na Ubunge kwa viti maalum. Kwa upande wa ajira tumeona mashirika mengi yakitangaza nafasi za kazi wanatoa kipaumbele kwa wanawake, kuwa iwapo mwanamke na mwanaume wote wakiwa na viwango vinavyolingana mwanamke ndiye atakaye pewa nafasi hiyo.

Kauli mbiu ya mwaka huu inatoa wito kwa watu wote kutoa ahidi kuchukua hatua mathubuti za kufikia usawa wa jinsia ifikapo mwaka 2030. Mashirika ya maendeleo kitaifa na kimataifa yanaendeleza harakati za kuhamasisha usawa wa jinsia kwa kutekeleza miradi mbali mbali. LEAT pia huwa inashiriki katika mijadala mbali mbali inayotoa elimu kwa jamii kuhusu usawa wa jinsia katika utoaji wa haki pamoja na kutekeleza miradi ya kuzuia ukatili wa jinsia.

Wewe Je?, unachukua hatua gani kuhakikisha kuwa dunia inafikai asilimia 50/50 katika elimu, uchumi, ajira, uongozi wa siasa na upatikanaji wa huduma za jamii?

Usawa wa Jinsia Unaanzia Nyumbani Kwako!

Chakua Hatua, Ahidi Usawa, Wewe ni Chanzo cha Mafanikio.

 

Wednesday, March 2, 2016

AFUNGWA JELA MIAKA 20 KWA UJANGILI



Chanzo: Gazeti la Raia Tanzania, Machi 1, 2016

Kibaha: Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Pwani imemuhukumu mfanyabiashara Anania Betela (30) amehukumiwa kwenda jela miaka 20 na kulipa faini ya Sh.1.9 bilioni baada ya kupatikana na hatia katika kesi ya kukutwana vipande 28 vya meno ya tembo bila kibali.
Picha ya Tembo wakiwa katika moja ya mbuga za wanyama za Tanzania
 
Mshtakiwa huyo alihukumiwa terehe 29 Februari 2016, mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Herieth Mwailolo, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo huku upande wa mashtaka ukiwakilisha na Wakili wa Serikali, Salim Msemo.
Akitoa adhabu hiyo Hakimu alisema, mshtakiwa alikuwa akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba moja ya mwaka 2014.

Katika kesi hiyo mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa mwaka 2014 eneo la Vigwaza, wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani ambapo alikutwa na vipande hivyo vya meno ya tembo vyenye thamani ya shilingi milioni 198.
Upande wa mashtaka ulikuwa na jumla ya mashahidi watano Pamoja na vielelezo mbalimbali ikiwemo men ohayo, begi lililobeba meno hayo katika kuthibitisha kesi dhidi ya mshtakiwa.
Baadhi ya meno ya Tembo yaliyo wahi kukamatwa kutokana na ujangili


JICHO LA PILI

Ujangili unapaswa kupigwa vita, wananchi tunawajibu wa kuhakikisha kuwa tunasimamia na kulinda rasilimali za Taifa kwa ajili ya maendeleo yetu na vizazi vijavyo. Vitendo hivi vimekithiri na vinalisababishia taifa hasara kubwa, ni biashara inayo nufauisha watu wachache. Hebu tujiulize uvunaji huu wa kasi wa tembo, usipo pingwa, baada ya miaka kumi hali itakuwaje?

Je, kutakuwa na tembo hata mmoja? Vipi kuhusu biashara ya utalii, itakuwepo?
Ripoti ya Taasisi ya Kulinda Tembo (TEPS) ya mwaka 2015 inaonesha kuwa asilimia 60 ya Tembo waliuawa kuanzaia mwaka 2009 mpaka mwaka 2014. Mwaka 2009 kulikuwa na Tembo 109,051 na ni Tembo 43,330 ndio waliokuwa wamesalia hadi mwaka 2014. Pia ripoti inaonesha kuwa tembo 61,720 waluiawa kwa miaka mitano mfululizo ikiwa ni wastani wa Tembo 30 kwa siku.

Ukweli ni kwamba Tembo hao wakiwa hai wanaliongezea taifa mapato makubwa kupitia biashara ya utalii kuliko wanapo uawa na kuuza meno yao.

Idadi ya Watalii imekuwa ikiongezeka kila mwaka hii inaonesha kuwa sekta ya utalii inakua na kukuza uchumi wanchi hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kupinga ujangili wa wanyamapori wetu.

Pinga Ujangili, Okoa Tembo wa Tanzania!

WALIOVAMIA MABONDENI HAWATAPATA STAHIKI YOYOTE-MAKAMBA

Chanzo: Gazeti la Mwananchi, Machi 1, 2016
·        Tangu mwaka 1949 Bonde la Msimbazi lilitangazwa kuwa eneo hatarishi

·        Zoezi la ubomoaji liataendeshwa kwa utaratibu mzuri

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira, January Makamba
 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira, January Makamba alisema kuwa waliovamia mabondeni wataondolewa na hawatalipwa stahiki yoyote kwa kuwa wamevunja sheria. Makamba alisema kuwa utaratibu huo ulikuwepo katika awamu nne za Marais waliotangulia, tatizo utekelezaji wa sharia haukufuatwa kikamilifu.

Alisema kuwa bonde la Msimbazi lilitangazwa kuwa eneo hatarishi kwa maisha ya watu tangu mwaka 1949 na baadaye mwaka 1979. “Kumekuwa na taratibu za kuondoa watu ilikurejesha maeneo hayo katika hali yake ya asili”, alisema.

Aliongeza kuwa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi iliwahi kutangaza Bonde la Msimbazi kuwa eneo maalum na mipango miji, ilikutimiza suala hilo ilikuwa lazima watu waondolewe.

Alisema kazi ya kuwaondoa wananchi wanaoishi kwenye bonde hilo ilikumbwa na changamoto kadhaa na kukajengeka dhana kuwa wanaonewa.

“Serikali tulieleza kama mtu alipewa kibali na serikali akajenga nyumba, basi serikali ilifanyamakosa na itamtafutia mahali pengine. Ila kama mtu alikuja tu na kujenga nyumba eneo hilo, lazima aondoke”, alisema Makamba.

Alifafanua kuwa waliovamia na kujenga mabondeni serikali haiwezi kuweka utaratibu wa kuwapatia maeneo mengine kwa sababu kufanya hivyo ni sawasawa na kuwapa zawadi wanaovunja sheria. Aliongeza kuwa licha ya watu kujenga nyumba na kufikia kiwango cha kuishi, haiwezi kuwa kipimo cha kujipambanua kuwa hawana makossa.

“Unapofanya makossa ukamilifu wa kosa siyo msamaha wa kutorekebishwa. Ukisema kwasababu mtu hakukamatwa wakati akijenga msingi basi asikamatwe kwasababu nyumba imeisha si kweli”, alisema.

Alisema kazi ya kubomoa nyumba zilizo mabondeni iliingiliwa na wanasiasa na akasisitiza kuwa maisha wanayoishi wananchi katika maeneo hayo, si ya kuridhisha na ukiwa kiongozi huwezi kukubali kuona wakiendelea kuishi humo.

“Sisi ambacho tumekubali lazima tuendeleze zoezi lile kwa utaratibu mzuri zaidi. Lazima watu wapate taarifa na waliovamia kuelezwa wazi kuwa hawatapata stahiki yoyote na waliopewa vibali na serikali wapewe maeneo mengine”, alisema Makamba.

“Kuna utamaduni ulijengeka muda mrefu wa watu kutoheshimu na kutii sharia. Sasa tukiendelea hivyo hivyo si sawa maana bila sharia hakuna serikali. Nchi hii mtu hawezi kuamua ajenge kibanda mahali popote na akiondolewa serikali ndiyo ioenkane ina dhambi. Hatuwezi kuendesha nchi kwa utaratibu huu”.



JICHO LA PILI

Zoezi la ubomoaji wa nyumba zilizo jengwa mabondeni limeonekana kuwa ni uonevu mkubwa kwa wananchi waliojenga katika maeneo hayo. Watu mbalimbali wakiwemo wanasiasa waliliongelea kwa hisia kali na kuelekeza lawama kwa serikali.   Wakidai kuwa serikali ilikuwa wapi wakati wananchi hao walipoanza ujenzi katika huko mabondeni.

Inawezekana serikali haikuliona hilo ama kwa namna yoyote ambayo watu wanaweza kutafsiri, lakini linapojadiliwa suala la sheria tunaambiwa Kutojua Sheria Si sababu ya Kuvunja Sheria. Kwa uhalisia ukiangalia masiha ya watu wanaoishi mabondeni ni magumu na hatari mno, kimazingira na kiafya.

Mabondeni hakuna mfumo mzuri wa uhifadhi taka pamoja na miundombinu ya kupitisha maji taka, hii ni kutokana na eneo jografia ya eneo ilivyo, wakazi wa Dar es Salaam wanaelewa hilo. Ingawa kuna watakao hoji mbona hata watu ambao hawaishi mabondeni wanatatizo la miundo mbinu ya kuhifadhi taka na mirefeji ya kupitisha maji.

Ni kweli kwa Jiji la Dar Es Salaam kuna tatizo la miundo mbinu, lakini hali huwa mbaya zaidi kwa wakazi wa mabondeni. Kwa mfano wakazi wa bonde la Msimbazi wakati wa mvua bonde hujaa maji kiasi kwamba wakazi hao hulazimika kuhama makazi yao katika kipindi chote cha mvua.

Katika kipindi cha mvua mafuriko ya bonde la Msimbazi yamegharimu maisha ya wengi na kusababisha hasara za mali za watu. Zaidi ya hayo, wakati wa mvua watu wengi hutirirsha maji taka kutoka katika majumba yao na kuelekeza sehemu za mabondeni, hivyo kuhatarisha afya za watu waishio mabondeni.

Ni heri kuchukua tahadhari kuliko kusubiri hatari.

 
 
 

 

Tuesday, March 1, 2016

KIWANDA CHA NGOZI MOSHI CHA TOZWA FAINI YA SHILINGI MILIONI 20 KWA KUTIRIRISHA MAJI MACHAFU


Chanzo: Gazeti la Nipashe-Jumanne Machi 1, 2016

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Luhanga Mpina, amekitoza faini ya shilingi milioni 20 kiwanda cha ngozi cha moshi kwa kushindwa kuboresha miundo mbinu ya kutiririsha maji machafu.
 
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira, Luhanga Mpina
 

Aliagiza fedha hizo kulipwa ndani ya siku 14, huku akitaka Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), kukagua kama menejimenti ya kiwanda hicho imetii amri ya kurekebisha miundo mbinu yake.

“Hii haikubaliki, mifereji ni michafu na maji yanayotumika kusafisha mifereji hii ni machache kiasi kwamba yanashindwa kusukuma vipande vya nyama na ngozi vilivyopo katika mifereji. “Harufu kali sana hapa tumesimama kwa dakika chache tu, lakini hali ni mbaya”, alisema.

Alisema alichukua hatua hiyo baada ya kutoridhishwa na usafi wa miundo mbinu ya kutirirrisha maji machafu, huku akisema kuwa kiwanda hicho kimekuwa kikilalamikiwa mara kwa mara na wananchi kutokana na harufu mbaya.

Mpina alisema kuwa kiwanda hicho kilikaguliwa na NEMC mwaka 2014 na kilipewa maelekezo ya kufanya maboresho ya miundo mbinu yake kufuatia malalamiko ya wananchi, wakitakiwa kuzuia harufu itokanayo na mabaki ya ngozi na maji taka ilikuepuka athari za kiafya zinazoweza kutokea yakiwemo magonjwa ya mlipuko.

JICHO LA PILI

Utiririshaji wa maji taka kutoka viwandani umekuwa kero kwa wananchi wanaoishi jirani na viwanda hivyo. Inasikitisha kuwa wenye viwanda wanakuwa wazito kuyafanyia kazi malalamiko hayo. Swali la kujiuliza je, wamiliki wa viwanda wanaokaidi malalamiko na maelekezo ya serikali, wana sera ya Uwajibikaji wa Kijamii ‘Corporate Social Responsibility’? Kama wanayo kwanini hawatekelezi sera hiyo? Sera ya Uwajibikaji wa Kijamii ni utaratibu binafsi wa shirika/kampuni ambapo wachunguzi wa biashara huhakikisha kuwa shirika/kiwanda kinaendesha shughuli zake kwa kufuata sheria, viwango vya maadili na kanuni za kitaifa na kimataifa.

 Pia sera ya ‘Uwajibikaji wa Kijamii’ huainisha mambo mbalimbali ambayo shirika/kampuni itaitendea jamii inayo zunguka biashara yake. Ni zaidi ya kufuata sheria, kanuni na kutafuta maslahi ya shirika, sera ya Uwajibikaji wa Kijamii ni Kuwajibika kwa kutenda mambo mema kwa jamii. Lengo ni kuongeza faida ya muda mrefu kupitia mahusiano mazuri ya jamii, kuishi katika viwango vya juu vya maadili ili kupunguza migogoro ya kibiashara na kisheria, na kujenga imani kwa Wabia; kwa shirika kuwajibika kwa vitendo.

Kwamfano, iwapo kuna kiwanda eneo fulani, kiwanda hicho huweza kuwajibika kwa jamii inayofanyia biashara zake kwa kusaidia ujenzi wa miundo mbinu ya maji, au ujenzi wa shule, zahanati na mambo kama hayo. Pamoja na kuhakikisha kuwa shirika/kampuni inatekeleza shughuli zake katika mazingira ambayo haya chochei migongano na jamii. Hii inasaidia kujenga mahusiano mazuri baina ya shirika /kampuni na wananchi, kwakuwa wananchi wataona faida ya shirika hilo kuwepo katika eneo lao.

Ipo haja ya serikali kukagua mashirika/makapuni kuangalia kama wanazo sera za ‘Uwajibikaji wa Kijamii‘ na kuwakumbusha kutekeleza wajibu wao kwa jamii zinazo wazunguka, kwa kuwa  wananchi ndio wadau na wateja wa biashara zao.