Monday, July 18, 2016

KUJITATHMINI- LEAT YAFANYA TATHMINI YA UCHECHEMUZI


Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) imefanya tathmini kwa Asasi nne ili kupima kiwango cha uchechemuzi (ushawishi) cha Asasi hizo ambazo ni washirika wa utekelezaji wa mradi wa ‘Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili’ unaotekelezwa katika vijiji 32 vya wilaya za Iringa na Mufindi Mkoani Iringa, kwa ufadhili wa Watu wa Marekani. Tathmini ilifanyika mwishoni mwa mwezi Juni, 2016 kwa Asasi za ASH-TECH na MUVIMA za Wilaya ya Mufindi; na kwa Wilaya ya Iringa ni MBOMIPA na MJUMIKK.
Tathmini hiyo ili lenga kuangalia iwapo agenda za uchechemuzi zimepewa kipaumbele ili kufikia malengo ya mradi, pia kuangalia endapo mipango hiyo imehusisha mambo muhimu ikiwa ni pamoja na kujumuisha wanawake na makundi yenye mahitaji maalum; ili kuyafikia makundi yote katika jamii.
Kutoka kushoto: Afisa Ugani wa LEAT, Hana Lupembe; Mwasibu wa MJUMIKK, Aidan Mkusa; Mratibu-MJUMIKK, Simon Komba; Katibu Mkuu-MJUMIKK, Mashaka Kilanga; Mchungaji Ombeni, Mjumbe wa MJUMIKK na Afisa Mradi wa LEAT, Musa Mnasizu.
Zaidi tathmini hiyo ili lenga kubaini endapo wadau wa utekelezaji uchechemuzi ikiwa ni pamoja na wafanyakazi na bodi za Asasi, wananchi na taasisi washirika wanafahamu na wanashiriki katika uainishaji na utekelezaji wa agenda za uchechemuzi.
Hatua hiyo ni muhimu kwa LEAT na Asasi hizo kwa kuwa mafanikio ya mradi yana changiwa na utekelezaji thabiti wa mipango ya uchechemuzi ambayo hutumika kutatua changamoto zinazo ikabili sekta za misitu na wanyamapori, kwa kutumia njia mbali mbali ikiwa ni pamoja na kushinikiza wafanyamaamuzi kuchukua hatua juu ya changamoto hizo.
Kutoka kulia, Afisa Mradi wa LEAT, Musa Mnasizu; Mjumbe wa MJUMIKK,Mchungaji Ombeni; Ktibu Muu wa MJUMIKK, Mashaka Kilanga an Mratibu wa MJUMIKK, Simon Komba
Kutoka kushoto: Afisa Mradi wa MUVIMA,Winnie Moses; Mkurugenzi Msaidizi wa MUVIMA, Speratus Mbeyela; Mkurugenzi- MUVIMA, Albert Chalamila; na Afisa Mradi wa LEAT- Jamal Juma
Baada ya siku sita za tathmini ya uchechemuzi, LEAT pamoja na Asasi waliainisha mapungufu yaliyoonekana katika mikakati ya uchechemuzi, na walipendekeza njia za kuboresha.
LEAT ili jengewa uwezo na Mtaalamu wa Uchechemuzi Tobias Chelechele kutoka Shirika la Pamoja Twajenga, ambao ni wakala wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID). Mradi wa ‘Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili’ unahusu rasilimali misitu na wanyamapori.
Takriban wananchi 6500 watanufaika na mradi huo. Mradi unatoa mafunzo ya usimamizi wa misitu, wanyamapori na ufuatiliaji uwajibikaji jamii, ili kuzijengea uwezo jamii kusimamia, kulinda na kuhoji viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali misitu na wanyamapori. Ili kufikia wananchi wengi, LEAT inaendelea kutoa elimu kwa njia ya Sanaa kupitia vikundi viwili vya Sanaa, makala za magazeti na programu za vipindi vya redio. Kwa kuwa mradi umelenga kujenga misingi ya utawala bora katika sekta ya misitu na wanyamapori, LEAT inatoa mafunzo kwa viongozi wa Vijiji, Madiwani, Wananchi, Maafisa misitu na wanyamapori.