Tuesday, March 15, 2016

LEAT WAHUDHURIA WARSHA ELEKEZI YA UANDISHI WA MPANGO MKAKATI


Wafanyakazi wa Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) wanaotekeleza mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili, walishiriki warsha elekezi ya siku mbili iliyofanyika tarehe 11 na 12 Februari, 2016 katika hoteli ya Regency Park, jijini Dar Es Salaam.
Afisa Mradi wa LEAT Jamal Juma akichangia mada wakati wa semina elekezi ya uandishi wa mpango mkakati kwa Asasi za Kiraia

Baadhi ya washiriki wa warsha elekezi kutoka Asasi ya WILDAF
 
Lengo la warsha hiyo ilikuwa kuzikutanisha Asasi za Kiraia ambazo zinafadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (USAID), ilikuwaelekeza upya namna ya kuandika mpango mkakati wa utekelezaji wa shughuli za mashirika yao.

Pamoja na mambo mengine washiriki walipatafursa ya kufanya kazi kwa makundi pamoja na kupitia mipango mikakati inayokwisha muda wake ya baadhi ya Asasi za Kiraia, ilikuangalia ni kwa kiasi gani waliweza kutengeneza mopango hiyo.

Mkuu wa Shirika la Pamoja Twajenga, Charles Nonga aliyapongeza mashirika kwa kushiriki warsha hiyo, pia alisema kuwa anatarajia kila shirika lililohudhuria watakwenda kuyafanyia kazi mafunzo waliyoyapata na kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akitoa maoni kuhusu warsha hiyo, Afisa Ufuatiliaji na Tathmini wa LEAT, Safarani Msuya, alisema kuwa warsha hiyo ni muhimu kwake kwakuwa imegusia maeneo yanayohusu ufuatiliaji na tathmini ya Asasi kwa ujumla.
“Nimeongeza ujuzi wa namna ya kuandika mpango mkakati wa Asasi pamoja na kuandaa na kutekeleza mpango kazi wa ufuatiliaji na tathmini, natumaini ujuzi huu utaongeza uafanisi katika utekelezaji wa majukumu yangu kama Afisa Ufuatiliaji na Tathmini. Pia mafunzo haya nitayatumia wakati tutakapokuwa tuna tathmini mpango mkakati unaomaliza muda wake ili tuweze kuboresha mapango mkakati mpya”, alisema Safarani.

Kwa upande wake Afisa Mawasiliano wa LEAT, Miriam Mshana alisema kuwa warsha hiyo imemuongezea maarifa ya uandishi wa mpango mkakati wa Asasi. Alieleza kuwa warsha hiyo imetoa mwelekeo wa namna kila mmoja katika Asasi anavyopaswa kutekeleza majukumu yake kulingana na lengo walilojiwekea, pamoja na umuhimu wa kila mmoja kushiriki katika kutathmini mchakato wa utendaji wa Asasi ilikupata matokeo bora zaidi. Afisa Mwandamizi wa Mradi, Remmy Lema an Afisa Mradi Jamal Juma wa LEAT nao walishiriki warsha hiyo.

Hiyo ilikuwa ni sehemu ya kwanza ya mchakato wa warsha elekezi ya uandishi wa mpango mkakati, awamu ya pili itafanyika mwezi Aprili 2016, itakuwa ya vitendo zaidi ambapo wataalamu kutoka Pamoja Twajenga na Change Associate International watatembelea Asasi mojamoja ilikupima ni namna gani washiriki wanaweza kutumia ujuzi walioupata katika kutathmini mpango mkakati unaomaliza muda wake na uandishi wa mpango mkakati mpya.

Mafunzo ya warsha hiyo yalitolewa na shirika la Change Associate International lenye usajili jijini Washington DC, nchini Marekani na Dar Es Salaam, Tanzania. Takriban washiriki 40 kutoka Asasi za Kiraia zizofadhiliwa na USAID kwa Tanzania bara na Visiwani walishiriki warsha hiyo. LEAT inatekeleza mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika Usimamaizi wa Maliasili katika wilaya za Iringa vijijini na Mufindi, mradi huo umefadhiliwa na USAID. Asasi zilizohudhuria warsha ni pamoja na LEAT, NACOPHA, RECLAIM, WILDAF, MAT, WICSA, AAC, PELUM, Zanzibar Legal Service Center.

Warsha hiyo iliandaliwa na shirika la Pamoja Twajenga ambao ni Wakala wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (USAID)- Tanzania. Pamoja Twajenga wanatekeleza shughuli zake chini ya programu za USAID/Tanzania kupitia mpango wa Demokrasia, Haki za Binadamu na Utawala Bora, ilikusaidia uwajibikaji kwa wananchi wa Tanzania. Hasa Pamoja Twajenga inafanyakazi na Asasi za Kiraia zilizopata ruzuku kutoka USAID, ili kujenga uwezo wao katika kuboresha uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali za umma kupitia ushiriki wa raia.
Katika picha ya kikundi ni washiriki wakifanya kazi ya kikundi wakati wa warsha

No comments:

Post a Comment