Tuesday, March 1, 2016

KIWANDA CHA NGOZI MOSHI CHA TOZWA FAINI YA SHILINGI MILIONI 20 KWA KUTIRIRISHA MAJI MACHAFU


Chanzo: Gazeti la Nipashe-Jumanne Machi 1, 2016

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Luhanga Mpina, amekitoza faini ya shilingi milioni 20 kiwanda cha ngozi cha moshi kwa kushindwa kuboresha miundo mbinu ya kutiririsha maji machafu.
 
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira, Luhanga Mpina
 

Aliagiza fedha hizo kulipwa ndani ya siku 14, huku akitaka Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), kukagua kama menejimenti ya kiwanda hicho imetii amri ya kurekebisha miundo mbinu yake.

“Hii haikubaliki, mifereji ni michafu na maji yanayotumika kusafisha mifereji hii ni machache kiasi kwamba yanashindwa kusukuma vipande vya nyama na ngozi vilivyopo katika mifereji. “Harufu kali sana hapa tumesimama kwa dakika chache tu, lakini hali ni mbaya”, alisema.

Alisema alichukua hatua hiyo baada ya kutoridhishwa na usafi wa miundo mbinu ya kutirirrisha maji machafu, huku akisema kuwa kiwanda hicho kimekuwa kikilalamikiwa mara kwa mara na wananchi kutokana na harufu mbaya.

Mpina alisema kuwa kiwanda hicho kilikaguliwa na NEMC mwaka 2014 na kilipewa maelekezo ya kufanya maboresho ya miundo mbinu yake kufuatia malalamiko ya wananchi, wakitakiwa kuzuia harufu itokanayo na mabaki ya ngozi na maji taka ilikuepuka athari za kiafya zinazoweza kutokea yakiwemo magonjwa ya mlipuko.

JICHO LA PILI

Utiririshaji wa maji taka kutoka viwandani umekuwa kero kwa wananchi wanaoishi jirani na viwanda hivyo. Inasikitisha kuwa wenye viwanda wanakuwa wazito kuyafanyia kazi malalamiko hayo. Swali la kujiuliza je, wamiliki wa viwanda wanaokaidi malalamiko na maelekezo ya serikali, wana sera ya Uwajibikaji wa Kijamii ‘Corporate Social Responsibility’? Kama wanayo kwanini hawatekelezi sera hiyo? Sera ya Uwajibikaji wa Kijamii ni utaratibu binafsi wa shirika/kampuni ambapo wachunguzi wa biashara huhakikisha kuwa shirika/kiwanda kinaendesha shughuli zake kwa kufuata sheria, viwango vya maadili na kanuni za kitaifa na kimataifa.

 Pia sera ya ‘Uwajibikaji wa Kijamii’ huainisha mambo mbalimbali ambayo shirika/kampuni itaitendea jamii inayo zunguka biashara yake. Ni zaidi ya kufuata sheria, kanuni na kutafuta maslahi ya shirika, sera ya Uwajibikaji wa Kijamii ni Kuwajibika kwa kutenda mambo mema kwa jamii. Lengo ni kuongeza faida ya muda mrefu kupitia mahusiano mazuri ya jamii, kuishi katika viwango vya juu vya maadili ili kupunguza migogoro ya kibiashara na kisheria, na kujenga imani kwa Wabia; kwa shirika kuwajibika kwa vitendo.

Kwamfano, iwapo kuna kiwanda eneo fulani, kiwanda hicho huweza kuwajibika kwa jamii inayofanyia biashara zake kwa kusaidia ujenzi wa miundo mbinu ya maji, au ujenzi wa shule, zahanati na mambo kama hayo. Pamoja na kuhakikisha kuwa shirika/kampuni inatekeleza shughuli zake katika mazingira ambayo haya chochei migongano na jamii. Hii inasaidia kujenga mahusiano mazuri baina ya shirika /kampuni na wananchi, kwakuwa wananchi wataona faida ya shirika hilo kuwepo katika eneo lao.

Ipo haja ya serikali kukagua mashirika/makapuni kuangalia kama wanazo sera za ‘Uwajibikaji wa Kijamii‘ na kuwakumbusha kutekeleza wajibu wao kwa jamii zinazo wazunguka, kwa kuwa  wananchi ndio wadau na wateja wa biashara zao.
 


No comments:

Post a Comment