Thursday, February 11, 2016

MAPAMBANO DHIDI YA UJANGILI-Hifadhi, Mbuga Kulindwa Kijeshi


Chanzo: Gazeti la Mwananchi, 10 Februari, 2016

Waziri wa Maliasili an Utalii, Profesa Jumanne Maghembe
 
Wizara ya Maliasili na Utalii imesema inatathmini mbinu za kukabiliana na majangili na itaanzisha jeshi Usu litakalokuwa na jukumu la kupambana na ujangili kwenye mbuga na hifadhi zote nchini.
Mpango huo umetangazwa siku moja baada ya Jeshi la Polisi kukamata watu tisa wanao tuhumiwa kuhusika na utunguaji wa helikopta iliyokuwa ikifanya doria kwenye Pori la Akiba la Maswi na ranchi ya wanyamapori ya Mwiba.

Katika shambulio hilo la Januari 29, Rubani wa helikopta hiyo Rodgers Gower aliuawa na Rubani Msaidizi kujeruhiwa. Mbali na tukio hilo kumekuwa na idadi kubwa ya wanyamapori wanao uawa na majangili, hasa tembo ambao kasi ya kutoweka kwake imestua dunia.

Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alisema wizara yake imejipanga kuimarisha pambano dhidi ya ujangili na usafirishaji haramu wa mazao ya wanyamapori na misitu.

Kuhusu waliokamatwa kwa tuhuma za kuangusha helikopta hiyo, alisema watu hao walikamatwa na silaha mbili aina ya riffle pamoja na risasi tano, pikipiki moja na kilo 31 za pembe za ndovu alizodai kuwa walimuua siku ya tukio. Katika wiki hiyo ya msako walikamata majangili wanne katika hifadhi ya Selous wakiwa na silaha 20 na Wilayani Tunduru walipata silaha 400.
Waziri, aliwapongeza wananchi na kuwataka waendelee kushirikiana na mamlaka husika.

No comments:

Post a Comment