Friday, May 6, 2016

Yaliyojiri katika Mkutano wa Tathmini ya nusu mwaka ya Mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili


Wadau wa Mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili Waipongeza LEAT

Wadau wa mradi wa Ushiriki wa wananchi katika Usimamizi wa Maliasili waipongeza Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo, kwa kutekeleza shughuli za mradi kwa kushirikisha wadau wote muhimu.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa alisema haya………

Akiongea wakati wa ufunguzi wa mkutano wa tathmini ya maendeleo ya mradi kwa kipindi cha miezi sita, kuanzia Novemba 2015 hadi Aprili 2016, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mheshimiwa Richard Kasesela, alisema taasisi ya LEAT imefanikiwa katika utekelezaji za mradi wake kwasababu ya utaratibu mzuri waliojiwekea, ikiwemo kushirikisha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Ofisi za Wakuu wa Wilaya, Halmashauri za Wilaya, Serikali za vijiji, Mashirika ya kijamii, wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Kutoka kushoto: Mkurugenzi Mtendaji wa LEAT, Dkt. Rugemeleza Nshala na Mkuu wa wilaya ya Iringa, Mh. Richard Kasesela

Alisema’ LEAT imepokelewa vizuri na wananchi wa Iringa kwasababu walitambua umuhimu wa kushirikisha wadau wote toka kuanza kwa mradi hivyo wananchi wanauthamini mradi na kuona kuwa wao ni sehemu ya mafanikio ya mradi’.

Alifafanua kuwa mafaniko ya mradi wa LEAT ni pamoja na mwitikio mkubwa wa wananchi kushiriki katika usimamizi wa maliasili, kwa kutoa taarifa za uhujumu maliasili unaoendana sambamba na ukamataji wa rasilimali za misitu.

Mkuu wa Wilaya alitolea mfano, wananchi walivyoweza kukamata mbao 298 mwezi Januari 2016, katika kijiji cha Mfyome, na mbao 491 zilizokamatwa katika kijiji cha Tungamalenga wilayani Iringa.

Pia alipendekeza LEAT na waandishi wa habari waanzishe ukurasa katika mitandao ya kijamii kwaajili ya kuwaripoti waharibifu wa mazingira, ikiwa ni Pamoja na kuweka picha zao katika kurasa hizo. Alisema kutokana na kasi kubwa ya uvunaji miti, ipo haja ya wadau wote kuanzisha kampeni ya kutokomeza uvunaji haramu kama inavyofanyika kampeni ya kuzuia mauaji ya tembo.
 

 
Kutoka ushoto: Mwenyekiti wa Halmashauri Mufindi, Ashery Mtono, Mkurugenzi Mtendaji wa LEAT, Dkt. Rugemeleza Nshala na Mkuu wa Wilya ya Iringa, Richard Kasesela

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Iringa Alonga…..

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Hamlashauri ya Iringa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Halmashauri za Iringa, Mheshimiwa Steven Mhapa alisema kuwa miradi mingi iliyotekelezwa mkoani Iringa haikuweza kuendelezwa kwasababu serikali na wananchi hawakushirikishwa kikamilifu kuanzia katika hatua za awali za mradi, hivyo wadau hao huhisi kuwa wao sio muhimu katika kufikia malengo ya mradi.

Aliye simama ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Iringa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Mkoa wa Iringa, Mh. Steven Mhapa

 “Nawapongeza LEAT kwakuwa wanafahamu umuhimu wa wadau wote katika kufikia malengo ya mradi, walishirikisha ofisi ya Wakuu wa Wilaya, Halmashauri na wananchi, ndio maana hata leo hii tumejumuika nao katika mkutano wa tathmini ya mradi, kwa kuwa na sisi ni sehemeu ya mafanikio ya mradi.

Mheshimiwa Mhapa alitoa angalizo kuwa kutokana na umuhimu wa maliasili katika ustawi wa uchumi wa nchi,LEAT iangalie namna itakavyoweza kuongeza wigo wa mradi katika wilaya nyingine za mkoa wa Iringa, ili wananchi waliozungukwa na maliasili wafahamu thamani ya rasilimali misitu hususan mbao. Alisema serilkali za vijiji vinvyozungukwa na rasilimali misitu zinapokea mapato hafifu ambayo hayalingani na thamani ya miti inayovunwa.

Tutaendelea kushirikiana na LEAT-Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mufindi                                                                                                            

Mheshimiwa Ashery Mtono, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mufindi alisema kuwa halmashauri yake itaendelea kushirikiana na LEAT kwakuwa wameona mafanikio ya mradi katika halmashauri yake. Alisema wananchi wamepata mwamko mkubwa kuhusu ushiriki waa katika usimamizi wa maliasili, kuwa matukio ya ukamataji wahujumu maliasili yameongezeka, pia wananchi wamepata ujasiri wa kuhoji viongozi wao juu ya mapato na matumizi ya maliasili. Pia wananchi wana ujasiri wa kudai uwazi na uwajibikaji kutoka kwa viongozi wao, hivyo kuboresha utoaji wa huduma za jamii.
Aliyesimama: Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mufindi, Mh. Ashery Mtono

Mkurugenzi Mtendaji wa LEAT aelezea lengo la mkutano wa tathmini ya mradi                                                                                                  

Akizungumza katika mkutano wa tathmini ya mradi kwa kipindi cha miezi sita, Novemba 2015 hadi Aprili 2016, Mkurugenzi Mtendaji wa Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT), Dkt. Rugemeleza Nshala alisema kuwa lengo la mkutano ilikuwa kupima utekelezaji wa mradi, kwa kuangalia mafanikio, changamoto na mipango ijayo ilikuhakikisha kuwa wadau wote kila mmoja kwa nafasi yake anashiriki kikamilifu ilikufikia malengo ya mradi.

Mkurugenzi Mtendaji wa LEAT, Dkt. Rugemeleza Nshala akiwasilisha taarifa ya jumla ya maendeleo ya mradi
Afisa Mradi Mwandamizi, Remmy Lema, akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya mradi
Timu ya LEAT: Kutoka kushoto: Hadija Mrisho, Glory Kilawe, Edina Tibaijuka na Glory Ephraem
 
Pia aliwashukuru viongozi wa Wilaya na Halmashauri za Iringa na Mufindi kwa kushiriki bila kuchoka tangu kuanza kwa mradi mwaka 2014 mpaka sasa.Pia aliwajulisha wadau kuwa milango ya LEAT ipo wazi ilikutoa fursa kwa wadau wote kutoa mchango ya kuboresha utekelezaji wa mradi.

LEAT imeboresha utendaji wake -Mwakilishi kutoka Chemonics         

Mwakilishi kutoka shirika la Chemonics, Thobias Chelechele, ambao ni Wakala wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID-Wafadhili wa mradi), aliipongeza LEAT kwa kuboresha utendaji wake, na kuwa hiyo ni kiashiria cha kufanikiwa kwa mradi.
Kutoka kushoto: Afisa Mradi Mwandamizi wa LEAT, Remmy Lema na Mwakilishi wa Chemonics Tanzania, Thobias Chelechele

Bwana Thobia,pia alizishauri Asasi za kiraia kuhakikisha kuwa wanafuata miongozo ya uendeshaji shirika ikiwemo masuala ya utawala, fedha, utunzaji kumbukumbu na utekelezaji mradi kwa ujumla, iliwaweze kukua na kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata fedha baada ya mradi huu kwisha.                                                   

Mkutano huo ulihudhuriwa na wadau kutoka wilaya za Iringa na Mufindi, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Wenyeviti wa halmashauri, Wakuu wa idara za maliasili, Waruzuku wa mradi, asasi za kiraia na wananchi.

Mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili unatekelezwa katika wilaya za Iringa na Mufindi, mkoani Iringa. Mradi huu umefadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID), na unatekelezwa na Timua ya Wanansheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) kwa kushirikiana na Asasi za Kiraia.

Asasi za Kiraia wapatiwa Vitendea Kazi

Asasi za Kiraia ambazo pia ni watekelezaji wa mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili, wapatiwa kompyuta mpakato (laptop) ilikurahisisha utendaji wa shuguli zao. Asasi za Kiraia zilizopokea kompyuta mpakato ni MBOMIPA, MUVIMA, ASH-TECH na MJUMIKK.

 

 

 
 
 
Mkurugenzi wa Asasi ya kiraia ya ASH-TECH, Erasto Mazera akipokea kopmyuta mpakato kwaajili ya kurahisisha utekelezaji wa mradi
 
 

Mwenyekiti wa MBOMIP akipokea kompyuta mpakato
Mwenyekiti wa Asasi ya MJUMIKK, Mashaka Kilanga akipokea kompyuta mpakato


Mkurugenzi wa MUVIMA akipoke kompyuta mpakato
 
Bwana Komba akiwasilisha sehemu ya utekelezaji ya asasi yake ya MJUMIKK
Sehemu ya Wadau wakifuatilia mawasilisho kutoka kwa watekelezaji mbalimbali wa mradi
 
Wadau wa mradi wakifuatilia mawasilisho ya maendeleo ya maradi
 
 
 

No comments:

Post a Comment