Wednesday, March 1, 2017

MAFANIKIO YA MRADI WA CEGO KATIKA KIJIJI CHA MALIZANGA KATA YA MLOWA WILAYA YA IRINGA

Katika picha ni Bw. Lulamso Kadaga,Mwenyekiti wa Kijiji cha Malizanga kilichopo Kata ya Mlowa wilayani Iringa, Akiwa ameshika mashine ya kufyatulia tofali zitumiazo saruji na mchanga iliyonunuliwa na halmashauri ya kijiji hicho ili kuachana na matofali ya kuchoma yanayochochea uharibifu wa misitu.


LEAT inatekeleza mradi wa “Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili” (CEGO-NRM), katika wilaya ya Iringa na Mufindi, kuptia ufadhili wa Shirika la Misaada la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID). Mradi huu unatekelezwa katika vijiji 32 (16 wilaya ya Iringa na 16 Wilaya ya Mufindi).

Moja ya kijiji kilichohusishwa katika utekelezaji wa mradi huu ni kijiji cha Malizanga kilichopo kata ya Mlowa, wilaya ya Iringa vijijini. Mafunzo ya Usimamizi wa maliasili na Ufuatiliaji wa Uwajibikaji wa Jamii (UUJ) yalitolewa kuanzia ngazi ya Halmashauri ya kijiji mpaka ngazi ya mwisho kabisa ya wanakijiji wenyewe.


Baadhi ya wajumbe wa halmashauri ya kijiji hiko wamedai kuwa, hali ya misitu ilikuwa mbaya sana kabla LEAT haijaleta mafunzo ya usimamizi wa maliasili katika kijiji chao. Watu wengi walikuwa wakiharibu misitu kwa kigezo cha uhitaji wa kuni, fito, mbao na mkaa kwaajili ya nishati, ujenzi  na kuuza ili kujipatia kipato.


Mwenyekiti wa Kijiji cha Malizanga Ndugu Lulamso Kadaga alisema, “Uhifadhi wa maliasili katika kijiji chake umeongezeka kwa kiasi kikubwa, kwani wengi wamepata elimu ya uhifadhi wa maliasili kutoka LEAT. Pia kupitia mafunzo ya Ufuatiliaji wa Uwajibikaji Jamii -

UUJ, wanakijiji wamekuwa wakifuatilia vitu vingi hususani shughuli za kimaendeleo kama ujenzi wa majengo ya kitaasisi na kuhoji bila woga pale wanapoona mambo yanaenda tofauti. Hapo mwanzo wananchi hawakuwa wakifuatilia shughuli zozote za kimaendeleo hapa kijijini. Ila kwa sasa hali ya ufuatiliaji inafanya viongozi tuwajibike kwani wananchi wanatusaidia na kutukumbusha wajibu wetu. Hivyo inatusaidia pia kuwawajibisha wale ambao hawatekelezi shughuli za miradi kama zinavyopangwa”


“Tumeweka kalenda ya vikao na mikutano ya halmashauri ya kijiji inayofanyika kila mwezi na mkutano mkuu unaofanyika kila baada ya miezi mitatu. Sisi kama viongozi tunahakikisha kalenda hii inafuatwa. Endapo mikutano ya kijiji haitafanyika kwa wakati, jamii imekuwa ikihoji sababu ya kutofanyika mikuatano hiyo. Hivyo jamii pia imeamka kutokana na kutambua umuhimu wa mikutano ya kijiji baada ya kupata elimu ya UUJ kutoka LEAT”. Aliongezea Ndugu Kadaga.


“Binafsi sikusomea uongozi, hivyo vitu vingi sana nimejifunza na kunufaika kutoka LEAT. Mafunzo waliyotupatia kuhusiana na UUJ hasa muongozo juu ya nguzo tano za UUJ yalininufaisha mimi kama kiongozi lakini pia hata wananchi kwa ujumla. Niliguswa sana na mada ya U3( Ufafanuzi, Uhalalisho na Uthibitisho). Nimenufaika juu ya suala la uongozi kwani kabla ya LEAT pengine nilikuwa ninaenda kinyume kwa kutokujua. LEAT imeniwezesha kutambua umuhimu wa utawala bora kwani nilijifunza kuwa mimi kama kiongozi natakiwa niwajibike, nijitume na niwe muwazi kwa wananchi wangu. Kama sitofanya hivyo nitalazimika kutoa U3 kwa wananchi wangu”. Alisema Ndugu Kadaga

  
"Hivyo basi mimi kama kiongozi nimeonyesha njia bora ya usimamizi wa maliasili katika kijiji changu hasa baada ya kupata mafunzo ya utunzaji Mazingira kutoka LEAT.
Niliita Halmashauri ya kijiji na kuwataka tukubaliane kukomesha suala la uharibifu wa misitu unaosababishwa na ukataji wa miti kwaajili ya kuchomea tofali za ujenzi. Tulianza utekelezaji huu kwa kununua mashine ya kufyatulia tofali zinazotumia Saruji naMchanga.

Tulikubaliana majengo yote ya taasisi tutayajenga kwa kutumia tofali za kawaida na si za kuchoma. Hivyo tuliweza kufyatua tofali 3800 zilizotumika kujenga madarasa mawili na ofisi moja. Tumetumia tofali 1800 na zimebaki 2000 zitakazotumika katika shughuli zingine za ujenzi. Hivyo tutakaposimama kuzuia suala la ukataji misitu kwa wanajamii, tutasimama kifua mbele kwani tuna mfano wa kuwaambia na kuwaonyesha.

Hapo nyuma ilikuwa ngumu kuwazuia wasikate miti wakati wewe kiongozi unawaita wafanye shughuli za kimaendeleo zilizokuwa zinahusisha suala la ukataji miti kwaajili ya kuni za kuchomea tofali kwa ajili ya shughuli za ujenzi”. Alimalizia Ndugu Kadaga, Mwenyekiti wa kijiji cha Malizanga"

No comments:

Post a Comment