Tuesday, November 8, 2016

Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imeidhinisha kuanza kutumika kwa sheria ndogo ya usimamizi wa maliasili

  Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa Bw. Stephen Mhapa, Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa na katibu tawala wa wilaya ya Iringa Bw. Joseph Chitika wakiongoza majadiliano katika mkutano wa baraza la wadiwani 
 
Mwanasheria mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Iringa Bi. Kissah Mbilla akifuatilia majadiliano ya baraza la madiwani wakati wa kupitisha sheria ndogo za vijiji 
 
 
Baadhi ya wajumbe na waandishi wa habari waliohudhuria mkutano wa baraza la madiwani wakifuatilia kwa makini kuidhinishwa kwa sheria ndogo za vijiji vya Mbweleli, Kinyali na Kinyika.
 
Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa Bw. Donald Mshani akihojiwa na waandishi wa habari baada ya baraza ya madiwani kuidhinisha sheria ndogo za vijiji husika   
 
 
Mwanasheria mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa Bi. Kissah Mbilla akihojiwa na waandishi wa habari baada ya baraza ya madiwani kuidhinisha sheria ndogo za vijiji husika 


Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imeidhinisha kuanza kutumika kwa sheria ndogo  za usimamizi wa maliasili ili kukabiliana na kasi ya uharibifu wa rasilimali za misitu na wanyamapori katika vijiji vitatu miongoni mwa vijiji ambavyo LEAT inatekeleza mradi wa ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili.

Sheria zilizoidhinishwa na halmashauri hiyo zimetungwa na halmashauri za vijiji vya Mbweleli, Kinyika na Kinyali chini ya msaada wa Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT),  lengo likiwa ni kudhibiti uharibifu wa mazingira unaokuwa kwa kasi katika vijiji hivyo.

Mara baada ya baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kuidhinisha kuanza kutumika kwa sheria hizo katika kikao cha baraza la madiwani  kilichoketi  tarehe 29/10/2016, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Stephen  Mhapa alisema sheria hizo zitasaidia kuongeza kasi ya utunzaji wa mazingira na wanyamapori katika vijiji husika.

Alisema Halmashauri za vijiji zina mamlaka kamili ya kutunga sheria ndogo zinazohusu usimamizi wa maeneo yao na kwamba sheria hizo zisipingane na sheria mama za nchi na Halmashauri husika.

“Kitendo cha halmashauri za vijiji kutunga sheria ndogo za kusimamia na kudhibiti uharibifu wa maliasili katika maeneo yao kimenifurahisha na kwamba kuanzia sasa misitu na wanyamapori waliokuwa katika hatari ya kutoweka kutokana na ujangili na uchomaji moto watakuwa salama”alisema Mhapa:

“Hiyo ni kutokana na wananchi wa eneo husika wao wenyewe kwa hiyari yao kujitungia sheria wanazoweza kuzisimamia, katika hili ninawashukuru Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa vitendo (LEAT) ambao wamewapatia elimu na msaada wa kufikia hatua hiyo ya kutunga sheria ndogo watakazoweza kuzisimamia wao wenyewe” alisema Mhapa.

Mwanasheria mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa Kissah Mbilla alisema jukumu la ofisi yake katika mchakato huo pamoja na kushirikiana na wanasheria wa LEAT ilikuwa kuhakikisha sheria hizo ndogo hazipingani na sheria mama ambayo ni ile ya Halmashauri na ya Nchi.

“Halmashauri ya kijiji inayo mamlaka ya kutunga sheria ndogo na ofisi yetu inachofanya ni kuangalia kama taratibu zimefuatwa, adhabu zinazotolewa katika sheria ndogo za kijiji hazizidi Tsh 50,000 na kwakuwa wamepitisha na baraza la madiwani limeidhinisha sheria hizi, sasa ni sheria kamili na zinaweza kuanza kutumika” alisema Mbilla.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili wa Halmashauri hiyo Donald Mshani alisema kuidhinishwa kwa sheria hizo kutasaidia idara yake kupambana na uharibifu wa mazingira ambao kwa sasa umekuwa ukishika kasi.

Alisema hatua hiyo inaweza kuwa ya mafanikio kutokana na sheria hizo tangu mchakato wa kutunga hadi kuidhinishwa na baraza la madiwani umeshirikisha wananchi katika kufikia malengo hayo.

Afisa habari wa Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) alisema hatua ya baraza la madiwani kuidhinisha kutumika kwa sheria hizo kumewafariji kwa kuwa jukumu lao la kuelimisha wananchi na kuwahamasisha kutunga sheria hizo linakuwa limetimia.

Edina Tibaijuka alisema LEAT kupitia mradi wa Ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili unaofadhiliwa na shirika la Kimataifa la watu wa Marekani (USAID) ilihamasisha halmashauri za vijiji vya Kinyali na Kinyika kutunga sheria ndogo hizo kwani awali hawakuwa nazo kabisa na kwa upande wa kijiji cha Mbweleli LEAT iliwawezesha Halmashauri ya kijiji hiko kufanya marekebisho ya sheria yao baada ya kuipitia na kuona sheria waliyokuwa wakiitumia awali ina mapungufu.


“Baada ya mikutano  mikuu ya vijiji hivyo kuridhia na kupitisha sheria hizo kuhusiana na maliasili ziliwasilishwa katika ofisi ya mwanasheria wa wilaya, kisha zilijadiliwa na kupitishwa na kamati husika za wilaya na kufikishwa katika baraza la madiwani ambao waliridhia kuanza kutumika kwa sheria hizo na kunatoa fursa kwa serikali za vijiji kuanza kuzitumia ili kudhibiti vitendo vya uharibifu wa mazingira” alisema. Tibaijuka.

No comments:

Post a Comment