Tuesday, June 7, 2016

SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI



LEAT YAWAASA WANANCHI KUSHIRIKI KIKAMILIFU KATIKA UHIFADHI WA MAZINGIRA NA MALIASILI
Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) imewaasa wananchi kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa mazingira na maliasili kwa ustawi wa taifa. Nasihi hizo ilitolewa na Afisa Mawasiliano wa LEAT, Miriam Mshana wakati wa maadhimisho ya siku ya mazingira duniani yaliyofanyika kijijini Lugoda Lutali katika ngazi ya wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa.
Katika utunzaji wa mazingira, Miriam alisema kuwa uharibifu wa mazingira umechangiwa kwa sehemu kubwa na shughuli za binadamu ikiwa ni pamoja na ukataji miti ovyo, utupaji taka ngumu na zenye sumu ambao umeathiri mandhari ya miji yetu na kuchangia ongezeko la magonjwa ya njia ya hewa, kuhara na kipindupindu.
Miriam alisema, utupaji taka ngumu na zenye sumu karibu na makazi ya watu na vyanzo vya maji, umeleta athari kubwa kiafya kwakuwa kemikali hizo hupenya ardhini na kudhuru ardhi na vyanzo vya maji, hasa kwa wananchi wanoishi karibu na viwanda na sehemu za uchimbaji madini.
 “Inasikitisha kuwa wamiliki wa viwanda vingi na machimbo ya madini wanakiuka sheria ya mazingira lakini pia wameshindwa kuwajibika kwa jamii zinazo wazunguka ambazo ndio wadau wakubwa wa biashara zao, kwa kaidi kuchukua hatua za kuzuia uharibifu wa mazingira hata baada ya athari kutokea”, alisema Miriam. Aliongeza kuwa shirika la LEAT limekuwa mstari wa mbele kwa zaidi ya miaka 20, katika kusimamia mazingira nchini katika sekta ya madini, viwanda, na mazingira kwa ujumla.
Aliongeza kuwa mamlaka zilizopewa jukumu la kusimamia mazingira zimekuwa na uzito katika utekelezaji wa majukumu yake hali hiyo inatoa mwanya kwa watu kukiuka sharia za uhifadhi wa mazingira.
Kumekuwa na malalamiko mengi na hata madhara yaliyowapata wananchi yanayotokana na uzembe makusudi wa utiririshaji wa maji yenye sumu katika makazi ya watu, lakini matukio mengi yanafumbiwa macho.
Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyotolewa mwezi Aprili, 2016 inaonesha takribani watu milioni 2 hufa kila mwaka duniani na zaidi ya watu bilioni moja hupatwa na magonjwa yanayo sababishwa na uchafuzi wa mazingira, alisema Miriam.
Iwapo serikali, wananchi na wamiliki wa viwanda na machimbo ya madini, kila mmoja akitimiza wajibu wa kutunza mazingira tutakuwa natekeleza haki ya kuishi, haki ya afya bora na ustawi, kama ambavyo serikali ilivyo ridhia katika mikataba mbalimbali ya kimataifa ikiwemo mkataba wa Stockholm nchini Sweden  na Rio De janeiro nchini Brazil.
LEAT kama taasisi kubwa ya Wanansheria Watetezi wa Mazingira nchini inatoa wito kwa mamlaka za usimamizi wa mazingira na maliasili kutimiza wajibu wao kwakuwa serikali imewaamini na kuwapa jukumu hilo. Kwakufanya hivyo tutakuwa tunaitikia wito wa kaulimbiu ya mwaka 2016 ya siku ya mazingira duniani-‘Shiriki kufanya dunia mahali pazuri’.
Kuhusu usimamizi wa maliasili, Miriam alisema Alisema, uvunaji wa kasi hasa wa misitu umeathiri na kuchangia mabadiliko ya tabia nchi, kuiweka nchi katika hatari ya kuwa jangwa. Uvunaji haramu wa wanyamapori hususan tembo umeipa hasara taifa.
 Aliongeza kuwa kwa mujibu wa ripoti ya Mtaalam Mashuhuri wa tafiti za tembo duniani, Ian Douglas Hamilton, kwa mara ya kwanza mwaka 1976 alifanya utafiti wa angani, Tanzania kwa ujumla ilikuwa na tembo 316,000, ambayo ilikuwa idadi kubwa sana ikilinganishwa na maeneo mengine duniani.
Mwaka 1976, mbuga ya Selou pamoja na maeneo jirani ilikuwa na idadi ya tembo109,000. Utafiti uliofanywa mwaka 2013, ulibaini kuwa mbuga ya Selou ilikuwa  na tembo 13,084 pekee.
 
Takwimu hizo zinaashiria hatari ya kutoweka kabisa kwa tembo katika nchi yetu na itaathiri biashara ya utalii ambayo ilikuwa ikitoa mchango mkubwa katika pato la taifa.
Sherehe za siku ya mazingira duniani zilizofanyika wilayani Mufindi tarehe 3 Juni 2016 na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jowika Kasugo, Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Asumpta Mshama, Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, ; pamoja na mashirika ya TANAPA, WCS, WWF, SPANEST, LEAT na wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Wanging'ombe, Mh. Asumpta Mshama akiongea na wananchi wakati wa maadhimisho ya siku ya mazingira duniani.
 
Kikundi cha sanaa Mapogoro wakihamasisha utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa maliasili
LEAT pia iligawa vitabu na vipeperushi kwaajili ya kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa maliasili
 
 

Mwananchi akitia saini baada ya kupokea kitabu cha utunzaji wa misitu, kilicho tolewa na LEAT
 
 
 
 
 
 

No comments:

Post a Comment