Wednesday, June 8, 2016

LEAT YASHIRIKI USAFI WA MAZINGIRA


Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) imeshiriki shuguli za usafi pamoja na wananchi katika kijiji cha Mfyome, wilayani Iringa, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya mazingira duniani.

Timu hiyo pamoja na wananchi walifanya usafi katika Zahanati ya Mfyome na baadaye katika mitaa ya kijiji hicho.

Akiongea wakati wa maadhimisho hayo, Nesi wa zahanati ya Mfyome, bi. Veronica Komba aliishukuru LEAT kwa kushiriki katika maadhimisho hayo ikiwa ni pamoja na kuhamasisha jamii kujenga utamaduni wa kusafisha makazi na mazingira yao.

Bi. Komba alisema kuwa jamii haina budi kujenga tabia ya usafi katika makazi yao ikiwa ni pamoja na kuzingatia kanuni za afya kwa kunawa mikono katika maji churuzi, baada ya kutoka maliwatoni, kuchemsha maji ya kunywa, kuchimba mashimo ya kuhifadhi taka ilikujiepusha na magonjwa ya kuhara na kipindupindu.

“Mtu ni afya, na afya bora inapatikana kwa kuzingatia kanuni bora za afya, kila mmoja asisitize usafi katika kaya yake, ilikuepukana na hatari ya kupata maradhi, kama ilivyotokea ugonjwa wa kipindupindu katika kata ya Pawaga na kugharimu maisha ya watu”, alisisitiza Veronica.

Kwa upande wake Afisa Mawasiliano wa LEAT, Miriam Mshana aliwapongeza wananchi kwa kushiriki katika maadhimisho ya siku ya mazingira, na kutoa wito wa kujenga utamaduni wa kuishi katika mazingira safi.

Kutokana na kaulimbiu ya mwaka 2016 ya siku ya mazingira duniani ‘Shiriki kufanya dunia mahali bora’, Miriam alisisitiza wananchi kutunza mazingira na maliasili, kwa kufanya hivyo tutakuwa tumefanya dunia kuwa mahali bora kwa binadamu, wanyama, mimea na viumbe hai wengine.

Alisema takwimu mbalimbali zinazotolewa na wadau wa mazingira zinaashiria kuwa dunia imechafuliwa na kuharibiwa kwa kiasi kikubwa; hivyo jitihada za dhati zinahitajika ilikudhibiti hali hiyo.

Vyanzo vya maji vimechafuliwa kwa kilimo, taka na kemikali zitokazo viwandani na migodini, shughuli hizo zimepelekea maji hayo kuto kuwa safi na salama kwa matumizi ya binadamu. Ukataji miti na uchomaji misitu umekithiri na kuchangia katika ongezeko la hewa ukaa na joto nchini.

Miriam pia aligusia suala la ujangili wa wanyamapori, na kusema kuwa ujangili umetishia kutoweka kwa baadhi ya wanyamapori hasa tembo. Alisema uvunaji wa kasi wa tembo unaathari kubwa kwa biashara ya utalii ambao una mchango mkubwa katika pato la taifa.

“Ombi langu kwa wananchi na viongozi wa vijiji mliopata mafunzo ya mradi wa ‘Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili’, kuwa muendelee kuwa mabalozi kwa kuhamasisha usimamizi na uhifadhi wa maliasili zetu, na kutoa taarifa za uharibifu wa maliasili katika serikali ya kijiji”, alitoa wito.

Kijiji cha Mfyome ni moja kati ya vijiji 32 vya wilaya za Mufindi na Iringa, vilivyofikiwa na LEAT kupitia mradi wa “Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili’, unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID).

 
 
Afisa Mawasiliano wa wa LEAT Miriam Mshana (wapili kutoka kushoto) na Nesi Veronica Komba (wapili kutoka kulia) pamoja na wananchi wakifanya usafi katika Zahanati ya kijiji cha Mfyome
 
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mfyome wakifanya usafi katika Zahanati ya kijiji cha Mfyome 
Picha baada ya usafi
Baada ya usafi

Mwenyekiti wa kijiji cha Mfyome, Thadei Dunda ( wapili kutoka kulia) akishiriki katika usafi wa mazingira siku ya mazingira duniani.
Wananchi wakisikiliza ujumbe wa utunzaji mazingira uliotolewa na kikundi cha sanaa Mashujaa cha kijiji cha Mfyome
Baadhi ya wanakikundi cha sanaa Mshujaa wakiimba shairi
 
 

No comments:

Post a Comment