Sunday, October 10, 2010

VYURA WA KIHANSI: THAMANI YA MALIASILI DUNIANI


Article by Heri Ayubu ,LL.B (Hons)  
Environmental Lawyer,
Lawyers’ Environmental Action Team (LEAT)
September 2010

 VYURA WA KIHANSI?
Hawa ni vyura wa ajabu! Wanapatikana katika maporomoko ya maji ya Kihansi na Muhalala, kusini mwa milima ya Udzungwa nchini Tanzania.
Vyura hawa ambao kwa jina la kitaalamu hujulikana kama ‘Nectophrynoides asperginis wanatajwa na wanasayansi kuwa miongoni mwa viumbe vilivyo katika hatari ya kutoweka kabisa kutokana na kuishi kweye makazi hatarishi, au kupoteza makazi yao ya asili na kupungua kwa idadi yao.
Vyura wa Kihansi waligunduliwa mnamo mwaka 1996 na timu iliyojumuisha wataalamu cha Elimu ya wanyama na Uhifadhi wa Wanyamapori kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika mchakato wa kufanya Tathmini ya athari za mazingira (Environmental Impact Assessment) kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa bwawa la uzalishaji wa umeme wa Kihansi.Ingawa yalitolewa mapendekezo ya namna ya kuwalinda viumbe hawa, mnamo mwaka 1996 karibu asilimia 90 ya maji ya mto Kihansi yalibadilishwa uelekeo kwa alili ya uzalishaji wa umeme kitu kilichopelekea upungufu mkubwa wa maji katika bonde la Kihansi, ambayo ndio hasa makazi ya vyura hawa. Kwa lugha rahisi kabisa ni kwamba mradi wa umeme uliyaharibu vibaya kama sio kutaka kuyapoteza makazi ya Maliasili hii ya kipekee.
Muathirika wa Kihansi
Mabadiliko haya yalikuwa na athari kubwa! Zaidi ya makazi ya viumbe hawa kuharibiwa, inaaminika kuwa kulikuwa na upungufu mkubwa wa hewa ya oksijeni ambayo ni muhimu sana kwa uhai wa viumbe wote, vilevile inaripotiwa kwamba kulikuwa na mlipuko wa ugonjwa wa ‘fangas’ walioenezwa viatu (mabuti) na Wahifadhi wa Mazigira pamoja na wataalamu katika kipindi cha utafiti. Kikubwa kuliko yote hakukuwa tena na uwiano wa kimazingira katika makazi hayo. Yote haya yalipelekea kupungua kwa vyura wa Kihansi kwa idadi inayokadiriwa kutoka vyura 50,000 hadi 12,000. Zaidi ya hapo ugonjwa wa fangas uliendelea kuua viumbe hawa kwa kasi kubwa.

Bonde la Kihansi kabla ya ujenzi wa mradi wa Umeme.

BWAWA LA UMEME LA KIHANSI
“Kwa wanamazingira na watetezi wa haki za wanyamapori, huu ulikuwa ni msiba mkubwa kushuhudia viumbe hawa wakitoweka kabisa. Kwao Umuhimu wa mradi wa umeme kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania usingetosha kama sababu ya kutokomeza vyura hawa. Kwa thamani ya mazingira mradi wa umeme unapaswa kutekelezwa kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira na viumbe waliomo, hivyo basi endapo mradi kama huu utatishia uhifadhi na usalama wa mazingira na viumbe itakuwa ni sababu ya msingi ya kupinga utekelezwaji wa mradi huo

UKOMBOZI WA KIMAZINGIRA
Bronx Zoo
Ilikuwa ni mwishoni mwa mwaka 2000 ambapo kilio cha wanamazingira kilisikika kikichagangiwa na msukumo wa taasisi za kimataifa pamoja muitikio chanya wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, donia ilishuhudia serikali ya Tanzania ikishirikiana na Jamii ya Uhifadhi wa Wanyamapori (‘the Wildlife Conservation Society-WCS)  ikisafirisha vyura 500 kutoka kwenye bonde la Kihansi,Tanzania kwa ndege maalumu kwenda nchini Marekani katika hifadhi ya Bronx (Bronx Zoo) na baadae kwenye hifadhi ya Taledo (Taledo Zoo) lengo likiwa kuwanusuru vyura hao wasipotee kwa kuwaweka katika mazingira yaliyo na hali karibu sawa na ile ya bonde la Kihansi kabla ya kuharibiwa na utekelezaji wa mradi wa umeme. Gharama iliyotumika kukamilisha zoezi la uhamishwaji wa vyura hawa pamoja na uhafadhi wake huko Marekani, hakika linatoa picha ya thamani ya uwepo wa kila kiumbe hapa duniani, kwani ni jambo lisilothibitika kuwa uwepo wa viumbe, akiwemo binadamu, unategemeana sana.
Baadhi ya Vyura waliorejea Tanzania.
Mwaka 2009 Muungano wa Kimataifa kwa Uhifadhi wa Asili - International Union for the Conservation of Nature (IUCN) ilitangaza rasmi kuwa vyura wa Kihansi kuwa miongoni mwa viumbe vilivyo katika hatari ya kutoweka duniani na hivyo kutoa wito kwa jamii ya kimataifa na wanaharakati wa mazingira duniani kwalinda Vyura hawa ambao ni maliasili adimu duniani. Hata hivyo kumekuwepo na faraja juu ya maisha ya vyura hawa katika kipindi cha maisha yao huko ugeninii. Hii inatokana na repoti kuwa idadi ya vyura hao imeongezeka inayokadiriwa kufikia vyura 7,000 kwa sasa.

KARIBU NYUMBANI VYURA WA KIHANSI.


Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira, Mhe. Batilda Burian
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira.
Mwaka wa 2010 utakumbukwa na dunia kwa mafanikioya kihistoria katika kutetea uhifadhi wa mazingira na uhai wa viumbe walio katika hatari ya kupotea. Dunia ilishudia kundi la kwanza la vyura wa 100 Kihansi wakipanda ndege maalumu kurejea nyumbani Tanzania na kupokelewa kwa heshima zote katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere siku ya Jumatano, tarehe 11 Agosti 2010 majira ya saa nne na nusu usiku. Baada ya mapokezi makubwa walipelekwa katika sehemu maalumu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam chini ya kitengo cha wanyama cha chuo hicho kabla ya majaribio ya kuwarudisha katika makazi yao ya awali, Bonde la Kihansi. Mkabidhiano rasmi yalifanyika tarehe 17 Agosti 2010 na Katibu mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira, Mhe. Ruth Mollel.

2 comments:

  1. We are all living organisms. Protecting wild animals means ensuring ecological balance.
    Thanx n Gig up for such an inspiring article Mr.Heri.

    ReplyDelete
  2. Article yako ni nzuri sana mhe. Mwanasheria wa Mazingira inaonyesha umuhimu wa kila kiumbe hapa duniani. Tushirikiane kutetea haki za mazingira na viumbe vilivyomo.
    By, Lazzaro Njowoka.
    LL.B student,
    University of Dodoma.

    ReplyDelete