Friday, June 10, 2011

MABADILIKO YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA



Imeandaliwa na,
EMMANUEL MASSAWE na HERI AYUBU
CHAMA CHA WANASHERIA WATETEZI WA MAZINGIRA (LEAT)
© Juni 2011

Utangulizi
Katiba ni mwongozo wa jinsi ya kufanya mambo katika jamii ya kisiasa, katika nchi. Mwongozo huu ni mali ya wale waliokubali kuwa nao. Kila jammi au hata taasisi ina miongozo midogomidogo inayosema nini kifanyike litokeapo jambo fulani. Kwa nchi ambayo ina mambo mengi na watu wengi mwongozo huo ni wa muhimu zaidi. Ni muhimu kwa wanajamii iliyokubaliana kuishi pamoja kama jumuiya kuwekeana misingi au mfumo ya uongozi na usimamizi wa jamii hiyo katika maeneo muhimu kama vile; stahili za wanajamii, wigo wa madaraka, mgawanyo wa rasilimali miongoni mwa makundi mbalimbali, na kujibu maswali mbalimbali miongoni mwa wanajamii, kama vile;
1.   Nani atastahili kuwa kiongozi? Na je, atapatikana kwa mfumo upi? Kwa kipindi gani cha uongozi? Na upi utakuwa mfumo wa kudabilisha uongozi? NANI watahusika?
2.   Nini malengo ya kuwa na Uongozi? Ni mamlaka gani watu wanaweza kuwapa viongozi kukamilisha malengo hayo? Je, watu waupe uongozi mamlaka yote, au baadha ya mamlaka wabaki mayo?
3.   Kama sehemu ya MAMLAKA itabaki kwa wananchi, Je, ni mfumo upi utahakikisha kuwa viongozi kamwe hawavuki mipaka ya madaraka waliyopewa?
4.   Kama watu hawaridhiki na uongozi uliopo madarakani, Ni namna gani watahakikisha wanawaondoa madarakani?
5.   Iwapo mtu au kikundi cha watu kimevinja MAKUBALIANO yaliyowekwa na Jamii hiyo, Wafanywe nini, na kwa Taratibu zipi?
6.   Ni nani atakuwa na jukumu la kutatua migogoro inayoibuka kwenye Jamii? Kati ya mtu na mtu, watu na serikali yao? Je ni chombo huru? Uhuru kiasi gani?
7.   Kwa mikakati ipi, jamii italishughulikia kundi la wasiojiweza? Je hili ni jukumu la familia, au jamii nzima?
8.   Ni namna gani GHARAMA zitokanazo na maisha ya viongozi zinachukuliwa? Nani anawajibika, wanajamii wote au kundi Fulani la watu?  
9.   Ni nani anaamua kuhusu RASILIMALI za jamii? Na ni mfumo upi utaamua UGAWAJI wa rasilimali hizo? Ipi ni MIPAKA na VIKOMO vya Utumiaji wa RASILIMALI za jamii.
10.               Je, KATIBA hii inaweza KUBADILISHWA? Kama ndiyo, Ni nani au ni CHOMBO gani kitakuwa na mamlaka ya kufanya mabadiliko hayo? Viongozi? WATU?
Aina za Katiba
Kuna aina mbili za katiba:
1.   Zilizoandikwa au katiba andishi (mf. Tanzania katiba ya sasa,Marekani, Kenya, n.k.).
2.   Ambazo hazijaandikwa au Katiba Mapokeo (mf. Uingereza)
Tangu tupate uhuru tumepata kuwa na katiba zifuatazo:
1.   Katiba ya Uhuru (1961)
2.   Katiba ya Jamhuri (1962)
3.   Katiba ya Mpito ya Tanganyika na Zanzibar (1964) 
4.   Katiba ya mpito ya mwaka (1965)
5.   Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977)
Katiba mpya ya jamii yoyote iwayo  inaweza kuundwa kwa kutumia njia zifuatazo: 
1.   Njia ya viraka
Hapa wahusika wakuu wa nia hii ni wawili – serikali na Bunge. Serikali 
inapendekeza hayo mabadiliko na Bunge linayajadili na kuyapitisha (au 
kuyakataa). Hadi sasa kumekwishakuwa na marekebisho 14.
2.   Njia ya waraka maalum wa Serikali (White Paper)
Njia hii ilipendekezwa na Serikali katika mabadiliko ya Katiba ya 13 hapo 2000. Waraka wenyewe ulikuwa wa 1999. Wahusika wakuu katika njia hii ni Serikali inayochagua nini kingie kwenye mapendekezo hayo. Wananchi hutoa maoni yao kuhusu kilichopendekezwa na Serikali. Bunge ndilo hupitisha mapendekezo hayo.
  1. Njia ya wataalamu na Bunge la Katiba 
Njia hii ilipendekezwa na Tume ya Jaji Nyalali. Wahusika wake wakuu ni wawili Tume ya Wataalamu watakaotengeneza rasimu ya Katiba mpya na Bunge la Katiba (yaani lililochaguliwa maalumu kwa ajili ya kupitisha Katiba). Njia hii inajaribu kuleta urari kati ya nafasi ya wataalim katika Tume ya Katiba nay a wananchi kwa kupitia kwa wawakilishi wao katika Bunge la Katiba. Tume ya Katiba inatakiwa iwe na uwakilishi mpana ili vyama na vikundi mbalimbali viweze kuwakilishwa, au viridhike na kazi yake.
4. Njia ya kutafuta ridhaa ya wananchi i.e Referendum
Njia hii imependekezwa na viongozi wa vyama ya upinzani na wataalamu mbalimbali. Njia hii inawapa nafasi wananchi kutengeneza Katiba. Kwa hiyo kunakuwa na hatua nne:
Kwanza Mkutano wa Taifa; pili Tume ya Katiba; Tatu Bunge la Katiba; na mwisho, Kura ya Maoni. Katika njia hii wana wajibu ufuatao:-
  1. Wanaonekana katika mkutano mkuu wa taifa.
  2. Wanachagua watakaoingia katika bunge la katiba.
  3. Wanapiga kura ya maoni ili kuridhia yale yaliyopitishwa na Bunge la Katiba.
HISTORIA YA MABADILIKO YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA 1977
Ndugu wanazuoni yafuatayo ni mabadiliko ya katiba yetu tangu mwaka 1977 ambayo wengine wanaita viraka, Katiba iliyopo imeweza kubadilishwa bila kuunda nyingine mpya. Katiba tuliyonayo Tanzania imebadilishwa ili ikidhi matakwa ya viongozi wetu wakati husika huko nyuma. Mpaka sasa katiba ya sasa ya Tanzania (1977) imeshafanyiwa marekebisho kumi na nne kama ifuatanvyo: - 
Mabadiliko ya Kwanza: 1979: yaliyounda Mahakama ya Rufani ya Tanzania.Mabadiliko ya Pili, 1980: yalihusu kuiingiza Katiba ya Zanzibar katika Katiba ya Muungano. Mabadiliko ya Tatu, 1980: yalizungumzia uchaguzi wa Rais wa Zanzibar (kazi zake, muundo wake), na Baraza la wawakilishi (muundo, mamlaka, na utungaji sharia zisizohusu mambo ya muungano).
Mabadiliko ya Nne, 1982: yalihusu utaratibu mpya wa kuteua wakuu wa mikoa.  Mabadiliko ya Tano: 1984: yalihusu kuongezwa sehemu III – Haki za Binadamu – katika  Katiba; kuimarisha Muungano, mgombea urais Zanzibar kupata Baraka za Kamati Kuu ya CCM. Mabadiliko ya Sita, 1990: yalihusu muundo mpya wa Tume ya Uchaguzi na mamlaka yake.
Mabadiliko ya Saba, 1990: yalihusu masharti ya mgombea mmoja tu kwa urais wa Zanzibar.
Mabadiliko ya Nane: 1992: yalihusu kuufuta mfumo wa chama kimoja na kurejesha mfumo wa vyama vingi. Mabadiliko ya Tisa, 1992: yalihusu namna ya kuchagua rais na mamlaka yake. Yalileta pia uwezokano wa ku-impeach rais, na kupunguza uwezo wa rais kulivunja bunge bunge kirahisirahisi.
Mabadiliko ya Kumi: 1993: yalihusu kuwezeshwa kwa Tume ya Uchaguzi kusimamia uchaguzi wa madiwani. Mabadiliko ya Kumi na Moja, 1994: yalihusu nafasi ya Makamu wa Rais, na kuongeza aina ya   wabunge. Mabadiliko ya Kumi na Mbili, 1995: Mabadiliko yalihusu:-
  1. Kipindi cha kushika madaraka kwa Makamu wa Rais.
  2. Kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu.
    Nafasi ya mawaziri na manaibu waziri zinavyoweza kuwa wazi.
  3. Kuongeza aina za wabunge.
  4. Sifa za kuwa mbunge wa kuchaguliwa au wa kuteuliwa.
  5. Kuhusu maadili ya uongozi ya wabunge.
  6. Wabunge kutangaza mali walizo nazo.
  7. Kuhusu Spika na Naibu Spika.
  8. Mamlaka ya kuunda kamati mbalimbali za Bunge.
Mabadiliko ya Kumi na Tatu, 2000:Mabadiliko hayo yalihusu:-
  1. Kupunguza idadi ya wanaoweza kuteuliwa na rais (kif. 33-37)
  2. Rais kuteua wabunge 10.
  3. Uhuru wa Mahakama (Kif. 107A na 107B).
  4. Kuongeza asilimia ya wabunge wanawake toka 15% hadi 20%.
  5. Ubaguzi wa kijinsia {Kif. 13 (5)}.
  6. Kuanzisha tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
  7. Rais kuchaguliwa kwa wingi wowote wa kura na sio 50% na zaidi kama awali.
Mabadiliko ya Kumi na Nne, 2005: Mabadiliko hayo yalihusu:-
  1. Mgawanyo wa mamlaka baina ya matawi matatu umeimarishwa.
  2. Kuifanya Katiba isiwajibike kwa sharia nyingine kwa kutoa maneno “Bila kuathiri sheria……..” katika vifungu vya Katiba.
  3. Haki za Binadamu zimeimarishwa ndani ya Katiba.
  4. Mahakama kama chombo chenye mamlaka ya mwisho ya kutoa haki katika Tanzania; uteuzi wa Majaji, kusimamishwa kazi Majaji n.k.
  5. Idadi ya wabunge wanawake wa Viti Maalumu na wale watokanao na wanaoteuliwa na Baraza la wawakilishi Zanzibar.
  6. Kukaimu urais: Kuwaondoa waliokuwa wanaweza kukaimu urais wanaotoka katika matawi ya Mahakama na Bunge na kuweka wanaotoka katika tawi la utendaji (Waziri Mkuu na Mahakimu wa Rais)
  7. Wagombea kupita bila kupingwa na kura ambazo chama kitapata kwa ajili ya mgao wa viti Maalumu.
Msingi wa USTAWI wa jamii ni MWONGOZO na DIRA wa jamii hiyo. Jamii isiyokuwa na Mwongozo mzuri kamwe haiwezi kupata maendeleo, kuwa na misingi ya Usawa, Itakosa Uadilifu na Kukosa Mwelekeo. Jibu la VIKWAZO hivi pamoja na MASWALI yote yaliyoainishwa hapo juu, ni KATIBA. Tanzania ipo katika mchakato wa kupata KATIBA MPYA na ni matumaini kuwa wananchi wote watakuwa MSTARI wa MBELE kuhakikisha wanajibi maswali na matatizo yanayowasumbua WATANZANIA kwa kupitia katiba.

2 comments:

  1. Article yenu ina ujazo wazee, ni zaidi ya elimu. Endeleeni kuelimisha.

    ReplyDelete
  2. LEAT inasemaje kuhusu katiba mpya na mazingira? maana watu wanazungumzia nafasi ya Rais, uchaguzi, ardhi na haki za binadamu. Wapeni uzoefu wa sekta ya mazingira kwani ni muhimu sana

    ReplyDelete