Friday, May 13, 2016

WANANCHI WA VIJIJI VYA IFWAGI NA LUDILO WANOLEWA

Wananchi wa vijiji vya Ifwagi na Ludilo katika Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa wahudhuria mafunzo ya siku saba yaliyotolewa na Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo' (LEAT) kwa kushirikiana na Asasi ya Kiraia ya ASH-TECH ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa 'Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili', unaofadhiliwa na Watu wa Marekani kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID).

Kwa mujibu wa Afisa Ugani wa LEAT kwa wilaya ya Mufindi, Franklyn Masikia, takribani wananchi 120 walihudhuria mafunzo hayo, ambayo yalihusu Usimamizi wa Maliasili na Ufuatiliaji Uwajibikaji Jamii.
Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wananchi kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa rasiliami misitu na wanyamapori, ilikuzinusuru na hatari ya kutoweka kutokana na kukithiri kwa uvunaji usio endelevu.

 Pia kupitia mafunzo ya Ufuatiliaji Uwajibikaji Jamii, wananchi watakuwa na uwezo wa kuwa wajibisha viongozi wao kwa kudai uwazi katika kupanga matumizi ya maliasili, sambamba na kuhoji mapato na matumizi yatokanayo na rasilimali zinazopatikana katika vijiji vyao.
Mafunzo hayo yalianza mwanzoni mwa mwezi Mei, katika nyakati tofauti, ambapo kila kijiji kilikuwa na washiriki 60.

Katika mafunzo hayo, wananchi walipata fursa ya kuzifahamu sera, sheria na miongozo katika usimamizi dumivu wa maliasili. Pia, Washiriki waliweza kuona wajibu na umuhimu wa wadau mbalimbali katika sekta ya maliasili, ikiwemo taasisi zinazo simamia, mashirika ya kijamii ya kitaifa na kimataifa, wizara, pamioja na wajibu wa wananchi katika usimamizi wa maliasili.

  Mradi huu unatekelezwa katika vijiji 32 vya wilaya za Iringa vijijini na Mufindi, mkoani Iringa. Takriban wananchi 6500 watafikiwa na mradi huu.

Sehemu ya Washiriki wa mafunzo katika kijiji cha Ludilo wakimsikiliza Mwezeshaji kutoka Asasi ya ASH-TECH, Thomas Mtelega
Katika picha ya pamoja na Washiriki wa mafunzo kijiji cha Ifwagi

No comments:

Post a Comment