Chanzo: Gazeti la
Nipashe-Jumanne Machi 1, 2016
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na
Mazingira, Luhanga Mpina, amekitoza faini ya shilingi milioni 20 kiwanda cha
ngozi cha moshi kwa kushindwa kuboresha miundo mbinu ya kutiririsha maji
machafu.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira, Luhanga Mpina |
Aliagiza fedha hizo kulipwa ndani ya siku 14, huku akitaka
Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), kukagua kama
menejimenti ya kiwanda hicho imetii amri ya kurekebisha miundo mbinu yake.
“Hii haikubaliki, mifereji ni michafu na maji yanayotumika
kusafisha mifereji hii ni machache kiasi kwamba yanashindwa kusukuma vipande
vya nyama na ngozi vilivyopo katika mifereji. “Harufu kali sana hapa tumesimama
kwa dakika chache tu, lakini hali ni mbaya”, alisema.
Alisema alichukua hatua hiyo baada ya kutoridhishwa na usafi
wa miundo mbinu ya kutirirrisha maji machafu, huku akisema kuwa kiwanda hicho
kimekuwa kikilalamikiwa mara kwa mara na wananchi kutokana na harufu mbaya.
Mpina alisema kuwa kiwanda hicho kilikaguliwa na NEMC mwaka
2014 na kilipewa maelekezo ya kufanya maboresho ya miundo mbinu yake kufuatia
malalamiko ya wananchi, wakitakiwa kuzuia harufu itokanayo na mabaki ya ngozi
na maji taka ilikuepuka athari za kiafya zinazoweza kutokea yakiwemo magonjwa
ya mlipuko.
JICHO LA PILI
Utiririshaji wa maji taka kutoka viwandani umekuwa kero kwa
wananchi wanaoishi jirani na viwanda hivyo. Inasikitisha kuwa wenye viwanda
wanakuwa wazito kuyafanyia kazi malalamiko hayo. Swali la kujiuliza je,
wamiliki wa viwanda wanaokaidi malalamiko na maelekezo ya serikali, wana sera
ya Uwajibikaji wa Kijamii ‘Corporate Social Responsibility’? Kama wanayo kwanini
hawatekelezi sera hiyo? Sera ya Uwajibikaji wa Kijamii ni utaratibu binafsi wa
shirika/kampuni ambapo wachunguzi wa biashara huhakikisha kuwa shirika/kiwanda
kinaendesha shughuli zake kwa kufuata sheria, viwango vya maadili na kanuni za
kitaifa na kimataifa.
Pia sera ya ‘Uwajibikaji
wa Kijamii’ huainisha mambo mbalimbali ambayo shirika/kampuni itaitendea jamii
inayo zunguka biashara yake. Ni zaidi ya kufuata sheria, kanuni na kutafuta
maslahi ya shirika, sera ya Uwajibikaji wa Kijamii ni Kuwajibika kwa kutenda
mambo mema kwa jamii. Lengo ni kuongeza faida ya muda mrefu kupitia mahusiano
mazuri ya jamii, kuishi katika viwango vya juu vya maadili ili kupunguza migogoro
ya kibiashara na kisheria, na kujenga imani kwa Wabia; kwa shirika kuwajibika
kwa vitendo.
Kwamfano, iwapo kuna kiwanda eneo fulani, kiwanda hicho
huweza kuwajibika kwa jamii inayofanyia biashara zake kwa kusaidia ujenzi wa
miundo mbinu ya maji, au ujenzi wa shule, zahanati na mambo kama hayo. Pamoja
na kuhakikisha kuwa shirika/kampuni inatekeleza shughuli zake katika mazingira
ambayo haya chochei migongano na jamii. Hii inasaidia kujenga mahusiano mazuri
baina ya shirika /kampuni na wananchi, kwakuwa wananchi wataona faida ya shirika
hilo kuwepo katika eneo lao.
Ipo haja ya serikali kukagua mashirika/makapuni kuangalia kama
wanazo sera za ‘Uwajibikaji wa Kijamii‘ na kuwakumbusha kutekeleza wajibu wao kwa
jamii zinazo wazunguka, kwa kuwa wananchi
ndio wadau na wateja wa biashara zao.
No comments:
Post a Comment