Thursday, February 25, 2016

MAREKANI YATANGAZA VIVUTIO NGORONGORO

Chanzo: Gazeti la Mwananchi, Alhamis, Februari 25,2016

Ngorongoro: Kituo cha Televisheni cha Marekani cha ABC juzi jumanne kilirusha matangazo ya moja kwa moja kwa saa tatu kuonesha vivutio vya utalii katika Hifadhi ya Ngorongoro iliyopo katika mkoa wa Arusha.
Matangazo hayo ambayo yalionekana katika kituo cha Good morning America, yalirushwa kuanzia saa moja asubuhi hadi saa tatu asubuhi, kwa muda wa Marekani wakati Tanzania ilikuwa saa tisa alasiri hadi saa kumi na moja jioni.
Meneja Mwandamizi Mwendeshaji wa vipindi katika kituo cha ABC, Faruna Sanoon, alisema kituo hicho kimejitolea kuandaa kipindi hicho nchini na baadaye watakwenda Afrika Kusini ilikuonesha utajiri wa vivutio vya barani Afrika.
Alisema kituo hicho kitafanya marudio ya kipindi hicho mara 14 kama walivyoombwa na serikali ya Tanzania.
Akizungumza na Waandishi wa habari mjini Arusha, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii nchini, Devota Mdachi, alisema matangazo hayo yanatarajiwa kuongeza idadi ya Watalii nchini.
Mdachi alisema matangazo hayo ni jitihada ya serikali kupitia ubalozi wa Tanzania Marekani, ilikuhakikisha Watalii wanaongezeka nchini na kuinua pato la taifa.

Kaimu Mkurugenzi wa Wanyamapori, Herman Kerariyo ambaye alimwakilisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alisema matangazo hayo yanatarajiwa kuongeza Watalii katika Hifadhi ya Ngorongoro kutoka 600,000 kwa mwaka hadi kufikia 1,000,000.
"Kama mnavyoona maeneo mengi duniani kupitia kituo cah ABC na vingine wanaona matangazo ya Ngorongoro, serikali inaamini Tanzania itanufaika sana", alisema.
Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dk. Fred Manongi, alisema matangazo hayo yametolewa bure na kama Tanzania ingelipa ingepaswa kutoa dola milioni 250 za Marekani.
Alisema licha ya kuonesha wanyamapori pia wameonesha, utalii na utamaduni unaopatikana katika hifadhi hiyo.
"Eneo hili ni la pekee duniani kwani wanyamapori na binadamu wanaishi sehemu moja, bila ya matatizo, hatua inayofanya hifadhi hiyo kuwa moja ya maajabu saba ya asili barani Afrika, na eneo maalum la uhifadhi duniani, alisema.
Pundmilia katika Hifadhi ya Ngorongoro
 
Boma la Wamasai lililopo ndani ya hifadhi ya Ngorongoro
 
 
Pundamilia na Simba katika hifadhi ya Ngorongoro

No comments:

Post a Comment