Friday, March 18, 2016

JENGA UWEZO KULETA UWAJIBIKAJI- LEAT WASHIRIKI WARSHA YA UANDISHI WA UCHECHEMUZI


Katika kutekeleza lengo la shirika la Pamoja Twajenga la ‘Jenga Uwezo Kuleta Uwajibikaji’ shirika hilo liliandaa warsha elekezi ya siku moja ya uandishi wa mpango makakati wa uchechemuzi (Advocacy Strategy) kwa Asasi zinazo fanyakazi nazo. Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) walishiriki warsha hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Pamoja Twajenga, tarehe 16 Machi, 2016.

Mafunzo hayo yalilenga kuwakutanisha wadau wa Pamoja Twajenga iliwaweze kushirikishana uzoefu wao katika uandishi wa mpango mkakati wa uchechemuzi kwa kila Asasi. Washiriki walipitia mipango mikakati yao kwa kuangalia mpangilio wa uandishi pamoja na maudhui, ili wadau wote waweze kuwa na mfumo mzuri na unaolingana utakao rahisisha katika upimaji wa matokeo ya utekelezaji wa Asasi, pamoja na kukidhi vigezo vya mfadhili (USAID)-Tanzania.

Miongoni mwa vitu muhimu vilivyo angaliwa katika uandishi wa mpango makakati wa uchechemuzi ni pamoja na kuahikisha kuwa wanaweka kipengele cha jinsia na makundi maalum katika jamii, ilikuhakikisha kuwa utekelezaji wa shughuli au miradi wa Asasi unazingatia makundi hayo muhimu.

Akiwakaribisha washiriki, Mkuu wa Shirika la Pamoja Twajenga, Charles Nonga, alisema kuwa warsha hiyo ya siku moja imelenga kutoa fursa kwa Asasi zinazo fanyakazi na shirika lake kubadilishana uelewa katika uchechemuzi, wakizingatia kuwa mpango kazi wa Pamoja Twajenga unalenga kujenga uwezo miongoni mwa Asasi hizo.

“Badala ya sisi kuendelea kupanga na kufanya kila kitu tuliamua mwaka wa tatu wa mradi, tuwe tunakutana na kuelezana tunafanya nini na tupate fursa ya ufumbuzi wa changamoto tunazo kutananazo. Kwa mtazamo huu shirikishi nategemea mambo yanayoendelea katika miradi yetu yataleta tija”, alisema Nonga.

Picha ya pamoja baada ya warsha,

Kutoka kushoto: Afisa Mradi wa PELUM Tanzania, Angolile Rayson; Mtaalam Uchechemuzi wa Pamoja Twajenga, Tobia Chelechele; Afisa Uchechemuzi wa NACOPHA, Last Mlaki; Afisa Mawasiliano na Nyaraka- NACOPHA, Mensia John; Afisa Ufuatiliaji na Tathmini wa LEAT, Safarani Msuya; Afisa Mawasiliano wa LEAT, Miriam Mshana na Mkurugenzi wa PELUM Tanzania, Donati Senzia.

Naye Afisa Mawasiliano wa LEAT Miriam Mshana alisema kuwa, ushiriki wa Asasi mbalimbali unasiadia kufahamu aina mbalimbali za uandishi wa mapango mkakati wa uchechemuzi, pamoja na kupata njia tofauti za utatuzi wa baadhi ya vipengele ambavyo vilikuwa vikimpa changamoto.

Aliongeza kuwa Asasi zilipata fursa ya kujadili kwa upana umuhimu wa kuweka kipengele cha jinsia na makundi maalum katika jamii.

“Nimefurahi kuona namna ambavyo tumeshirikishana uzoefu katika kuhusisha jinsia na makundi maalum ya jamii ilikuweza kuwafikia watu wengi katika jamii. Ilikuleta tija katika utekelezaji wa programu inatulazimu kuzingatia usawa wa jinsia katika ufikiwaji na ufaidikaji wa jamii”, alisema Miriam.

Alifafanua kuwa, maendeleo yanaletwa na watu wote katika jamii bila ya kujali jinsia, jamii inahitaji kushirikishwa katika kuainisha wajibu na majukumu ya mwanamke na mwanaume ili kila mmoja apate fursa ya kuchangia maendeleo ya jamii yake.
 
Mshiriki mwingine kutoka Asasi ya NACOPHA, Last Mlaki, ambaye ni Afisa Uchechemuzi na Mtandao, alisema kuwa upitiaji wa uandishi wa mpango mkakati wa uchechemuzi utasaidia kwa Asasi kuwa na mfumo mmoja katika utekelezaji wa makakati huo.

“Pia tumeona baadhi ya Asasi hazikuweka kipengele cha jinsia na makundi maalum ya jamii, ambayo inaweza kuwa kikwazo cha kuyafikia makundi yote na kutambua changamoto na fursa wanazokutana nazo, pia inaweza kuta tafsiriwa kuwa kundi fulani halina umuhimu katika jamii, hivyo likashindwa kutoa mchango katika maendeleo”, alisema Mlaki.

Naye Mratibu Uchechemuzi kutoka TACOSODE Abraham Kimuli, alisema kuwa warsha hiyo imempa fursa ya kufanya baadhi ya maboresho ikiwemo uandishi wa malengo ya uchechemuzi na mtiririko mzuri wa mpango mkakati kwa kupata maoni ya washiriki wote, na kuongeza kuwa hiyo inasaidia kutambua maeneo yenye changamoto.

Akifunga warsha hiyo Mtaalamu wa Uchechemuzi wa Pamoja Twajenga, Tobia Chelechele alisema, warsha hiyo ilikuwa wamu ya pili, awamu ya kwanza ilifanyika Desemba 2015, awamu ya tatu itayanyika mwezi Juni na awamu ya mwisho itakuwa mwezi Septemba 2016.

Alisema kuwa awamu ya tatu ya mwezi Juni itahusu uandishi wa jumbe za uchechemuzi, na kuwataka washiriki wote kuandaa jumbe mbalimbali kulingana na miradi wanayofanya ili jumbe hizo ziweze kupimwa na washiriki wote ilikuongeza uelewa zaidi na kurahisisha utekelezaji wake.

Warsha hiyo iliongozwa na Mtaalamu Uchechemuzi wa Pamoja Twajenga, Tobia Chelechele, na kuhudhuriwa na Asasi za LEAT, TACOSODE, NACOPHA, WiLDAF na PELUM Tanzania.

Pamoja Twajenga ni wakala wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (USAID),  wanatekeleza shughuli zake chini ya program za USAID-Tanzania kupitia mpango wa Demokrasia, Haki za Binadamu na Utawala Bora, ilikusaidia uwajibikaji wa wananchi wa Tanzania. Pamoja Twajenga inafanyakazi na mashirika yaliyopata ruzuku kutoka USAID, ili kujenga uwezo wao katika kuboresha uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali za umma kupitia ushiriki wa raia.

 
Kutoka kulia: Afisa Ufuatiliaji an Tathmini wa LEAT, Safarani Msuya, na Mtaalamu Uchechemuzi wa Pamoja Twajenga, Tobias Chelechele akifafanua jambo wakati wa warsha.
Afisa Mradi wa PELUM Tanzania, Angolile Rayson na  Mkurugenzi wa PELUM Tanzania, Donati Senzia, wakifuatilia jambo

 
Mtaalamu wa Uchechemuzi wa Pamoja Twajenga, Tobias Chelechele akifuatilia mpango chechemuzi wa Asasa ya TACOSODE ulioandaliwa na Mratibu Uchechemuzi wa TACOSODE, bwana Abraham Kimuli, (kulia).
Kutoka kushoto ni Afisa Mawasiliano na Nyaraka (NACOPHA) Mensia John, Afisa Uchechemuzi wa NACOPHA, Last Mlaki wakiwasilisha mpango chechemuzi wa Asasi yao kwa Mtaalamu Uchechemuzi wa Pamoja Twajenga, Tobias Chelechele.
 

 

No comments:

Post a Comment