KAULI
MBIU- ‘AHADI KWA USAWA’
Leo tarehe 8 Machi 2016, wanawake duniani
wanasherekea siku ya yao (Siku ya Wanawake Duniani), kwa kauli mbiu ya ‘Ahadi Ya
Usawa’. Kauli mbiu hii inahamasisha watu wote wake kwa waume kuahidi kuwa
watachangia kufikia mafanikio ya usawa wa jinsia katika jamii. Kauli mbiu hii inasisistiza
watu wote kuchukua hatua mathubuti ilikusaidia kufikia usawa wa jinsia haraka
zaidi; kwa kuwasaidia wanawake na wasichana kufikia matarajia yao katika elimu,
uchumi, uongozi wa siasa, huduma za jamii pamoja na kuwaheshimu na kutambua
tofauti ya kijinsia.
Mwaka 2014, Jukwaa la Uchumi Duniani lilikadiria
kuwa itachukua muda mrefu mpaka mwaka 2095 kufikia usawa wa jinsia duniani.
Mwaka mmoja baadaye, mwaka 2015 walikisia kuwa kutokana na kasi ndogo ya maendeleo
katika kupunguza pengo la usawa wa jinsia litapungua ifikapo mwaka 2133.
Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili katika
kusaidia
kufikia Usawa wa Jinsia ifikapo mwaka 2030
Kaulimbiu ya mwaka 2016 inatoa wito kwa watu wote
kusaidia kufikia usawa wa jinsia duniani, Chama cha Wanasheria Watetezi wa
Mazingira kwa Vitendo (LEAT), wanahamasisha usawa huo kwa kuhakikisha kuwa
wanawake wanashiriki kikamilifu katika Usimamizi wa Mali Asili kupitia mradi wa
‘Ushiriki wa Wananchi katika Kusimamia Maliasili’ unaotekelezwa katika wilaya
za Iringa Vijijini na Mufindi mkoani Iringa, kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo
la Kimataifa la Marekani (USAID).
LEAT inatambua na kupongeza jitihada kubwa
zinazofanywa na wanawake wa Tanzania katika kuchangia maendeleo ya taifa hili.
LEAT inatambua kuwa ushiriki wa wanawake katika usimamizi wa maliasili sio tu
kuwa ni suala la usawa wa jinsia lakini pia kutoshiriki kikamilifu kwa wanawake
kunaathiri ufanisi wa usimamizi wa maliasili.
Kauli mbiu ya mwaka 2016 inatoa wito kwa watu wote kuahidi
kuwa watawawezesha wanawake na wasichana kufikia matarajiao yao, imedhihirika
kuwa upatikanaji wa vitu muhimu kwa maisha ya wananchi wa vijijini kama vile maji,
chakula, nishati-kuni pamoja na dawa, kutawawezesha wasichana kupata muda sawa
na wavulana wa kijisomea wakiwa nyumbani, kwa kuwa wasichana watatumia muda
mfupi kusaidia mama zao kutafuta kuni, maji, dawa na chakula kwaajili ya
matumizi ya familia.
Katika utekelezaji wa mradi wa Ushiriki wa Wananchi
katika Usimamazi wa Maliasili, LEAT inatoa mafunzo ya sheria zinazohusika katika
usimamizi wa maliasili, pamoja na mafunzo ya Uwajibikaji Jamii (Social
Accountability Monitoring) kwa wadau mbalimbali wakiwemo, Madiwani, Kamati za
vijiji na wilaya za Maliasili, Ardhi na Mazingira; Mashirika ya kijamii pamoja na
wawakilishi wa makundi mbalimbali ya kijamii.
Ilikuhakikisha kuwa wanawake wanashiriki katika
kupanga, kuamua na kusimamia maliasili, LEAT inasisitiza kuwepo kwa idadi kubwa
ya wanawake wanakaoshiriki katika mafunzo ya mradi, ilikuleta matokeo chanya
kwakuwa, iwapo maliasili zitatunzwa, zitasimaiwa na kutumika vizuri mwanamke
ndiye mnufaika mkubwa kwa kuwa yeye ndiye mwenyejukumu la kuhakikisha kuwa maliasili
hizo (maji, nishati-kuni) na chakula vinapatikana kwa matumizi ya familia na
jamii.
Pia endapo maliasili hizo hazikutunzwa, kusimamiwa
na kutumiwa vizuri na hatimaye kupungua au kutoweka; mwanamke ndiye anayepata
athari zaidi kwa kuwa atalazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji, kuni na
chakula kwaajili ya familia.
Elimu zaidi ya usawa wa jinsia inahitajika kutolewa
kwa jamii ili kuongeza kasi ya kufikia usawa wa jinsia ifikapo mwaka 2030. Hii
imedhihirika katika mafunzo ya mradi unaotekelezwa na LEAT mkoani Iringa. Ushiriki
wa wanawake katika baadhi ya vijiji unatia moyo lakini bado kuna changamoto
kubwa, elimu inapaswa kuendelea kutolewa ili wanawake wenyewe watambue wajibu
na umuhimu wao katika kufikia usawa wa jinsia.
Licha ya kuwa na idadi ndogo ya wanawake wa vijijini
katika kushiriki ama kushika nyadhifa mbali mbali za uongozi, wanawake ambao
wamepata nafasi katika kamati mbali mbali za maendeleo za vijiji wamekuwa Mabalozi
wazuri wanao toa elimu kwa wanawake wenzao pamoja na jamii kwa ujumla.
Mafunzo ya Uwajibikaji Jamii yamewawezesha wanawake
kutambua wajibu wao, kuwa na ujasiri wa kuwahoji watendaji wa serikali kuanzia
ngazi ya kijiji, kuhusu mapato na matumizi ya fedha za kijiji, pamoja na ubora
wa upatikanaji wa huduma za jamii. Wanawake pia wamekiri kuwa mafunzo haya
yamewaongezea weledi wa kusimamia ustawi wa familia na jamii zao.
Wanawake
na Chanzo Mbadala cha Mapato
LEAT pia imetoa mafunzo ya ufugaji nyuki pamoja na
kugawa mizinga ya nyuki bure kwa wote waliopatiwa mafunzo. Ilisisitiza kuwepo
kwa uwiano mzuri kati ya wanawake na wanaume wanaoshiriki mafunzo, ili kuondoa
dhana ya kuwa ‘ufugaji nyuki ni mradi ya wanaume tu’, pia ni kutoa fursa ya
wananchi wanaoishi katika maeneo yenye maliasili kuwa na chanzo mbadala cha
mapato, kuliko kutegemea mazao ya maliasili kujipatia kipato.
Wanawake wengi
wanatarajia kunufaika na mradi wa ufugaji nyuki na kuboresha maisha ya familia
zao, kwani kuna baadhi ya wanawake ndio walezi pekee wa familia, hii ni
kutokana na kufiwa na waume zao, kuachika ama kutelekezwa. Mwanamke anapokuwa
na vyanzo vya mapato vya uhakika, anakuwa na amani, ujasiri na ari ya kusimamia
maliasili za kijiji. Pia mwanamke anapokuwa na uchumi mzuri, kuna uwezekano
mkubwa wa familia na jamii yake kufaidika moja kwa moja na uchumi huo.
Changamoto zinazo kwamisha Usawa wa Jinsia
katika Usiamamizi wa Maliasili
Kuna changamoto mbalimbali ambazo zina kwamisha ama
kuchelewesha kufikia kwa usawa wa jinsia ikiwa ni pamoja na uelewa mdogo wa
dhana ya usawa wa jinsia, jamii kutotambua majukumu ya wanawake na wanaume,
mila na desturi kandamizi pamoja na kulega lega katika utekelezaji wa sera na sheria.
Uelewa mdogo wa dhana ya usawa wa jinsia katika
kuleta maendeleo imekuwa ni kikwazo kikubwa katika kufikia adhma hiyo. Watu
wengi wanadhani kuwa usawa wa jinsia ni wanawake kuacha kuheshimu wanaume pamoja
na kuacha mila na desturi zinzazo wataka wanawake kuwa wanyenyekevu mbeley ya
wanaume. Ukweli ni kwamba usawa wa jinsia ni kutoa fursa sawa kwa wanawake na
wanaume katika kumiliki uchumi, kupata elimu, nafasi sawa katika uongozi na
maamuzi pamoja na fursa sawa katika upatikanaji wa haki, huduma za jamii, kuheshimiwa
na kuthaminiwa, kwa kuzingatia kuwa binadamu wote ni sawa, haya yanatekelezwa
bila kuathiri mila na desturi za jamii husika kwa kuzingatia haki za
binadamu.
Kikwazo kingine ni jamii kuto tambua majukumu ya
wanawake na wanaume, kutokana na ukweli kuwa mwanamke ndiye mlezi mkuu wa
familia, mara nyingi inatokea baba anatelekeza famila na kumuachia mama mzigo wa kulea familia. Mama anapokuwa mlezi pekee wa familia anakuwa na majukumu mawili, kutafuta kipato na kutafuta mahitaji muhimu ya familia, kwa wanawake wa vijijini ni changamoto zaidi kwa kuwa wanawake hupoteza mida mwing kutafuta maji na kuni kwa matumizi ya familia.
Mila na desturi kandamizi ni pale ambapo wanaume
wanapoona kuwa mwanamke ni mtu dhaifu asiye stahili kupewa madaraka makubwa, na
kuwa ni mtu anayepaswa kuongozwa tu. Licha ya kuwa kumekuwa na mwamko kwa
wanawake waishio mijini, changamoto bado ipo kwa wanawake waishio vijijini
ambao inadaiwa kuwa ni wengi kuliko waishio mijini.
Pia wanawake wenyewe
kutojiamini kuwa wanaweza kutenda mambo makubwa katika jamii, hii inatokana na
mila na desturi kandamizi, kuwa mtoto wa kike tangu akiwa mdogo anafundishwa
kuwa yeye ni mlezi wa familia lakini si mzalishaji mali.
Kulega lega kwa utekelezaji wa sera na sheria kumechangia
kupunguza kasi ya kufikia usawa wa jinsia. Sera na sheria zinaeleza vizuri
mipango ya serikali kufikia usawa wa jinsia lakini utekelezaji wake ni hafifu.
Kwamfano, sera na sheria ya ardhi inaeleza wazi kuwa kila mtu anahaki ya
kumiliki ardhi, lakini cha kushangaza serikali haijafanya jitihada za kutosha
kuhakikisha kuwa wanawake wanapewa kipaumbele kwa kuwezeshwa kumiliki ardhi kwa
kuwa umiliki wa ardhi unahitaji pesa nyingi, na wanawake wengi ni masikini.
Serikali ilipaswa iwawezeshe wanawake hawa kumiliki ardhi kwa kuitoa kwa mikopo
nafuu. Ilikufikia usawa wa 50/50 katika ngazi za maamuzi tunapaswa ku hakikisha
kuwa kuna usawa katika kumiliki uchumi.
Matumaini
ya Kufikia Usawa wa Jinsia
Baada ya mkutano wa Wanawake uliofanyika Jijini
Beijing, nchini China mwaka 1995, Tanzania imesaini mikataba mbali mbali ya
kimataifa ya kuzuia ukatili wa kijinsia na kukubali kusaidia wanawake kupata
fursa sawa na wanaume ilikuharakisha maendeleo.
Serikali pia imetoa fursa mbalimbali ilikusaidia
wanawake kushiriki katika ngazi mbali mbali za uongozi na siasa, kwamfano
Tanzania kwa mara ya kwanza ina Makamu wa Rais mwanamke, Mh. Samia Suluhu, pia
ilikuwa na mwanamke Spika wa Bunge, Anna Makinda, Mama Asha Rose Migiro alikuwa
Waziri wa Mambo ya Nje wa kwanza mwanamke; na alishika wadhifa wa juu kimataifa
alipokuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Wapo wanawake wengi katika nchi hii waliopata nafasi
za juu za uongozi katika siasa kwa upande wa vijijini kuna wanawake wamepata
Udiwani na Ubunge kwa viti maalum. Kwa upande wa ajira tumeona mashirika mengi
yakitangaza nafasi za kazi wanatoa kipaumbele kwa wanawake, kuwa iwapo mwanamke
na mwanaume wote wakiwa na viwango vinavyolingana mwanamke ndiye atakaye pewa
nafasi hiyo.
Kauli mbiu ya mwaka huu inatoa wito kwa watu wote
kutoa ahidi kuchukua hatua mathubuti za kufikia usawa wa jinsia ifikapo mwaka
2030. Mashirika ya maendeleo kitaifa na kimataifa yanaendeleza harakati za
kuhamasisha usawa wa jinsia kwa kutekeleza miradi mbali mbali. LEAT pia huwa
inashiriki katika mijadala mbali mbali inayotoa elimu kwa jamii kuhusu usawa wa
jinsia katika utoaji wa haki pamoja na kutekeleza miradi ya kuzuia ukatili wa
jinsia.
Wewe
Je?, unachukua hatua gani kuhakikisha kuwa dunia inafikai asilimia 50/50 katika
elimu, uchumi, ajira, uongozi wa siasa na upatikanaji wa huduma za jamii?
Usawa
wa Jinsia Unaanzia Nyumbani Kwako!
Chakua
Hatua, Ahidi Usawa, Wewe ni Chanzo cha Mafanikio.
No comments:
Post a Comment