Tuesday, March 8, 2016

SIKU YA WANAWAKE DUNIANI- WANAWAKE WAIPONGEZA LEAT KWA KUSAIDIA KUINUA UCHUMI WAO

Katika kusherekea Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa kila tarehe 8 mwezi Mchi, 2016, wanawake wanaoishi katika vijiji ambavyo LEAT inatekeleza mradi wa Ushirki wa Wananchi katika Usimamaizi wa Maliasili, wameipongeza LEAT kwa kuwapelekea mradi wa ufugaji nyuki ilikuinua viapato vyao.
Bi. Felista Choga, mkazi wa kijiji cha Lugoda Lutali, wilayani Mufindi, mkoani Iringa alisema kuwa anatarajia kunufaika na mradi wa ufugaji nyuki kwakuwa utaongeza kipato na kuboresha maisha ya familia yake.
Bi. FelistaChoga mmoja wa wanufaika wa mradi wa ufugaji nyuki
 
Bi. Felista alisema kuwa mwanamke anawajibu mkubwa kwa familia na jamii kwa ujumla kwasababu ndiye mlezi na anatarajiwa kuwajibika kwa ustawi wa familia, hivyo endapo mwanamke atakuwa na vyanzo zaidi ya kimoja vya mapato ataboresha kipato cha familia pia atakuwa na muda wa kujitolea kusimamia maliasili.
 
"Matumizi ya asali yameongezeka katika jamii, hii ni kutokana na umuhimu wake kwani asali inatumika kama chakula, kwamfano baadhi ya watu hutumia asali badala ya sukari ya viwandani, pia asali ni dawa, huwa tunatumia katika kutibu, magonjwa ya tumbo, na kifua, ikichanganywa na amdalasini iliyo twangwa, pia ni dawa ya kutibu majeraha yatokanayo na kuungua na moto, hivyo natumaini ni biashara nzuri kutokana na umuhimu wake", alisema Felista.
 
Mimi ni mkulima na nimekuwa nikitegemea kilimo kupata mapato, sasa hivi nimepata chanzo kingine cha mapato, natarajia maisha yangu yataimarika, aliongeza.
Akiongelea nafasi ya mwanamke katika Usimamizi wa Maliasili, alisema kuwa, mwanamke ndiye mtumiaji mkuu wa maliasili hizi, hivyo alipaswa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa usimamizi na kufanya maamuzi ya matumizi ya mazao yatokanayo na maliasili hizi hasa misitu.
 
Alisema kuwa mwanawake pamoja na kuwa ndiye mtafutaji mkubwa na mtumiaji wa mazao yatoka nayo na misitu, bado hajashiriki kikamilifu katika usimamizi wa maliasili, hiyo inatokana na kutotambua wajibu wake katika jamii.
 
"Kwa nafasi yangu kama Mjumbe wa kamati ya maji ya kijiji, huwa nina hamasisha wanawake wenzangu katika vikundi vyetu kuwa wanahaki na wajibu wa kushiriki katika ngazi za maamuzi katika usimamizi wa maliasili za kijiji, pia nitashirikiana na wanawake wenzangu kueneza ujumbe huu katika mikutano ya hadhara ya kijiji, ili hata vijana na wanaume watambue majukumu na umuhimu wa wanawake katika kuharakisha maendeleo ya kijiji chetu", alisema.
 
Aliendelea mbele kusema kuwa Mafunzo ya Uwajibikaji Jamii yanayotolewa na LEAT katika mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili, yamemjengea ujasiri wa kuwakilisha maoni ya wanawake wenzake katika kamati ya maji ya kijiji chao.
 
Akiongelea kuhusu kauli mbiu ya siku ya wamawake kwa mwaka 2016, ya 'Ahadi kwa Usawa', alisema kuwa usawa utapatikana iwapo wanawake watajengewa uwezo wa kutambua wajibu wao na fursa zinazopatikana katika jamii, iliwaweze kushiriki katika masuala ya maendeleo.
 
Alifafanua kuwa kumuwezesha mwanamke kiuchumi pamoja na kushiriki katika fursa zinazopatikana katika jamii, kutachochea kasi ya kufikia malengo ya usawa wa jinsia. Alifafanua kuwa jitihada zaidi zinahitajika katika kusaidia wanawake wanaoishi vijijini kupata fursa sawa na wanawake wanaoishi mijini ilikupunguza tofauti ya maendeleo ya wanawake waishi mijini na wale waishio vijijini.
Alisema kuwa wanawake wa vijjini wanakosa fursa muhimu kama vile fursa ya mikopo ya fedha kwaajili ya shughuli za kilimo na biashara. 'Mwanamke mwenye uchumi bora ana heshimika na kuthaminiwa katika jamii, na atashirikishwa katika kufanya maamuzi. Serikali na mashirika ya maendeleo yaongeze nguvu katika kupunguza tofauti kubwa kati ya walionachi na wasionacho, ambapo wengi wa wasionacho ni wanawake wa vijijini', alisema.
Natoa shukran za dhati kwa Shirika la Maendeleo la Marekani, USAID kwa kufadhili mradi huu ambao utanusuru misitu yetu pamoja na kutuletea chanzo mbadala cha mapato, Serikali na Mashirika mengine ya maendeleo yangesaidia katika kutoa elimu ya biashara na mikopo kwaajili ya wanawake.
 
LEAT inatekeleza mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili, katika wilaya za Iringa vijijini na Mufindi, mkoani Iringa. Mradi umefadhiliwa na Watu wa Marekani, kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID), ni mradi wa miaka minne, ulianza mwaka 2014 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2017. Mradi huu unatekelezwa katika vijiji 32, na unatarajiwa kuwa zaidi ya watu 6500 watafikiwa na mradi huu.
Katika utekelezaji wa mradi huu, LEAT ilijengewa uawezo na PAMOJA TWAJENGA ambao ni wakala wa USAID Tanzania, na LEAT ikawajengea uwezo Mashirika ya kijamii, Kamati za wilaya na Vijiji za maliasili, Ardhi, Maofisa wa serikali kutoka idara za Maliasili na Ardhi, Madiwani na Wananchi wanao wakilisha makundi mbalimbali ya jamii.
Mafunzo yanayotolewa ni pamoja na sheria zote zinazohusu usimamizi wa maliasili zikiwemo, Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999, Sheria ya Serikali za mitaa ya mwaka 1982, Sheria ya Mazingira ya 2004, Sheria ya Misitu ya 2002, Sheria ya Hifadhi za Taifa ya 1959 na  Sheria ya Uhifdhi Wanyamapori ya mwaka 2007. Pia LEAT inafundisha Kanuni, Miongozo na Adhabu zinazo husiana na usimamizi wa maliasili.
 
 



No comments:

Post a Comment