Marehemu Vincent Shauri Enzi ya uhai wake.
Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) waadhimisha miaka Kumi ya kifo cha Vincent Shauri, aliye fariki kwa saratani mapafu, tarehe 9 Februari 2006.
Vincent Shauri alikuwa mmoja wa waanzilishi wa LEAT, na aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa LEAT kuanzia Octoba 2003 hadi Februari 2006, alipofikwa na mauti.
Katika kuadhimisha miaka kumi ya kifo cha Vincent Shauri, Mkurugenzi Mtendaji wa LEAT Dr. Rugemeleza Nshala pamoja na wafanyakazi walisimama kwa dakika moja ilikutoa heshima kwa mchango wa Shauri katika asasi hiyo.
Marehemu Shauri alitambulika na kuheshimika kwa mchango mkubwa alio utoa kwa taifa na hata katika jumuiya ya kimataifa. Marehemu Shauri alishiriki katika harakati mbalimbali za utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa maliasili, mchango wake utakumbukwa daima na kuenziwa.
Moja ya harakati alizoweza kuanzisha na kusimamia ni pamoja na kuitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina katika mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu (kwa sasa unaitwa Bulyanhulu Acacia mine), kutokana na madai ya baadhi ya wafanyakazi wa mgodi huo pamoja na wananchi waliokuwa wakiishi karibu na mgodi kudai kuwa kulikuwa na watu takriban 52 waliozikwa wakiwa hai katika mgodi huo.
Pia alishiriki katika uandishi wa sheria ya mazingira ya mwaka 2004 sheria ambayo inatumika hapa nchi mpaka leo hii. Zaidi ya hayo, mchango wake katika uandishi wa Sheria ya Misitu ya mwaka 2002 utakumbukwa daima.
Kutokana na weledi na mchango wake, Shauri alipata fursa ya kusimamia miradi iliyokuwa ikiendeshwa na mashirika ya kimataifa, kwa mfano, mwaka 1999-2002 ali iwakilisha nchi kama Mshauri na Kiongozi wa Mradi uliokuwa ukiandaa namna ambavyo sheria ya kimataifa itatekelezwa katika kusimamia matumizi ya maji ya ukanda wa Ziwa Nyasa, mradi huo ulitekelezwa na Shirika la Chakula Duniani (FAO).
Mwaka 1998 aliungana na Wataalamu wengine jijini Roma, Italia na kushiriki katika mjadala wa Wataalamu uliokuwa ukitathimini Sheria na Sera ya maji, mradi huo uliendeshwa na Shirika la Chakula Duniani.
Mnamo mwezi Agosti, 1997 alipata fursa ya kufanyakazi kama Mshauri wa Sheria katika kutathimini uwiano kati ya ushiriki wa usimamizi wa maliasili na maendeleo ya uchumi wa jamii, za wananchi waishio katika meneo mbalimbali ya hifadhi za taifa.
Shauri aliteuliwa kuwa Mshauri wa Sheria katika mpango wa udhibiti na utekelezaji wa hifadhi ya mazingira nchini Tanzania, mwaka 1997.
Katika misitu, Shauri alishiriki katika kikosi kazi kilichokuwa kikifanya marekebisho ya sharia ya misitu na nyuki ya Tanzania, kuanzia mwaka 1998 hadi 1999. Mradi huo ulikuwa sehemu ya uasndishi wa muswada wa misitu, mazingira na viumbe hai, ambao uliwasilishwa mwaka 1999.
Hii ni baadhi ya michango yake ambayo itakumbukwa na kuenziwa daima.
Mwenyezi Mungu amrehemu, apumzike kwa amani.
No comments:
Post a Comment