Wananchi wa kijiji cha Mfyome kata ya Kiwere, katika
halmashauri ya Iringa Vijijini wamekamata mzigo wa mbao 298 zilizo vunwa isivyo
halali katika msitu wa asili wa Gangalamtumba, hivyo kusababisha uharibifu wa
mazingira.
Ukamatwaji wa mbao hizo ni matokeo ya mafunzo ya mradi
wa Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili, maradi unaotekelezwa na
Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) kwa ufadhili wa
Watu wa Marekani kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID).
Mwishoni mwa mwezi Januari wananchi wa kijiji hicho
walikamata mbao hizo, mtuhumiwa alikimbia na kutelekeza mzigo huo. Viongozi wa
kijiji waliamua kutaifisha mbao hizo na kuelekeza kuwa zitatumika kutengeneza
madawati ilikukabiliana na changamoto ya upungufu wa madawati inayoikabili
jamii hiyo.
Kwa upande wake Mjumbe wa Timu ya Ufuatiliaji
Uwajibikaji katika Jamii kwa ngazi ya Wilaya, ambaye ni mkazi wa kijiji hicho
bwana Chuki Mduda alisema kuwa mafunzo ya Ushiriki wa Wananchi katika
Usimamaizi wa Maliasili yameleta hamasa na mwamko mkubwa katika jamii kwakuwa
wananchi sasa wananshiriki kikamilifu na matokeo ya kukamatwa kwa mbao hizo ni
kielelezo cha ari ya uwajibikaji.
Alisema mbao hizo zilivunwa kutoka katika msitu wa
asili wa Gangalamtumba, alidai kuwa tayari eneo kubwa la msitu huo limeathiriwa
vibaya.
“Tangu tulipohudhuria mafunzo haya kumekuwa na mabadiliko
makubwa, tume hamasika kulinda maliasili zetu, na tumejipanga
kupambana na wote watakao vuna rasilimali misitu bila ya kibali, tutawachukulia hatua za
kisheria, ikiwa ni pamoja na kuwanyang’anya rasilimali watakazo kamatwa nazo na
watalipa faini kulingana na sheria za kijiji”, alisema Mduda.
No comments:
Post a Comment