Wakazi wa kijiji cha Kiwere wilaya ya Iringa vijijini
wametoa shukrani zao za dhati kwa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani
(USAID) na kwa Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT)
kwa kuendesha mradi wa ‘Ushiriki wa wananchi katika Kusimamia Maliasili’.
Akiongea wakati wa tathimini ya mafunzo ya mradi,
kiongozi wa kikundi cha kuhifadhi mazingira (Kiwere Hifadhi Mazingira), Hamza
Chang’a alisema, kabla ya mradi alikuwa na uelewa wa kawaida kuwa ukataji miti
hauruhusiwi kwa kuwa unaharibu mazingira, hakuelewa kuwa wananchi wanao wajibu
wa kulinda mazingira na maliasili kwa maendeleo endelevu na kuwa jambo hilo
limeelezwa katika katiba ya nchi.
“Nilipoona watu wakikata miti, niliona ni jambo la
kawaida, sikufahamu athari ya muda mrefu itokanayo na vitendo hivyo, namna vianavyo
athiri ubora wa maisha ya sasa na vizazi vijavyo. Nilidhani ni wajibu wa kamati
ya maliasili ya kijiji na viongozi wa kijiji kulinda maliasili, aliongeza.
Alisema mafunzo yamemwongeza ufahamu, yamebadilisha
mtazamo kuhusu usimamizi wa maliasili, na ameanza kutumia ujuzi wake kwa
vitendo kama mwananchi muwajibikaji.
Aliendelea kusema kuwa amepata dhana kamili ya
ushiriki katika michakato wa maendeleo hivyo atajitolea kushawishi, kufanya
kampeni na kufuatilia utekelezaji wa huduma za jamii.
Baada ya mafunzo, Chang’a na wenzake 16 waliunda
kikundi cha kuhifadhi mazingira na katika kipindi cha miezi minne wamepanda
zaidi ya miti 45,000 aina ya Mijoholo na Mikaratusi. Miti hiyo itapandwa katika
eneo la msitu wa Msuni lilio haribiwa kutokana na ukataji miti hovyo na
uchomaji mkaa.
Kwa upande wake Devotha Mihayo alisema, amejifunza
kuwa uharibifu wa mazingira una athari kubwa kwa jamii hususan kwa wanawake.
Unaathiri vyanzo vya maji, unasababisha ukame na njaa katika jamii. ‘Iwapo
vyanzo vya maji vita haribiwa tutalazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji,
ambapo utatupotezea muda na kuweka maisha na afya zetu hatarini’ alisisitiza.
Alisema kuwa katika jamii yake hawaja wahi
kushuhudia ukame kwa kuwa mvua inanyesha kwa wakati, lakini mafunzo yame
watahadharisha kuhusu ukataji miti ambao unaweza kusababisha mabadiliko ya hali
ya hewa hivyo kuleta mazalia ya mbu na kusababisha ugonjwa wa malaria. “Kila
mmoja katika jamii yetu anahamasishwa kushiriki katika utunzaji wa mazingira
wakati huo huo tukitunza afya zetu, zaidi ya hapo tuna hamasisha watoto kutoa
taarifa za shughuli za uharibifu wa mazingira ilituchukue hatua za kuzuia haraka
iwezekanavyo, alisema.
Naye Mashaka Kalinga Katibu Mtendaji wa asasi ya
kiraia ya MJUMIKK, alithibitisha kuwa kijiji kimefanya jitihada nyingi za
kuanzaisha uvunaji endelevu ili kuongeza mapato na kuhakikisha kuwa mapato
yanayopatikana yananufaisha jamii. Zaidi ya hayo, serikali ya kijiji imezuia
uchomaji mkaa, uvunaji miti usio endelevu, wameimarisha ulinzi na wanahamasisha
wananchi kushiriki jitihada hizo.
Jumla ya wananchi 75 kutoka katika kamati za vijiji
zikiwemo, kamati ya ardhi, kamati za mazingira na maliasili, baraza la ardhi,
kamati ya maliasili ya wilaya na wawakilishi wa wananchi kutoka makundi
mbalimbali, walihudhuria mafunzo ya Mradi wa Ushiriki wa wananchi katika Kusimamia Maliasili.
Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira
kinatekeleza mradi wa miaka minne unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la
Kimataifa la Marekani, mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika Kusimamia
Maliasili, katika wilaya za Iringa na Mufindi, mkoani Iringa. Mradi ulianza
mwaka 2014 na unatarajiwa kumalizika mwaka 2017.
Kiongozi
wa ‘Kiwere Hifadhi Mazingira’, Hamza Chang’a na mwanakikundi Bruno Mpagama wakionesha
sehemu ya miti 45,000, waliyo otesha katika bustani kijijini Kiwere
Katika picha ya pamoja ni baadhi ya washiriki wa mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika Kusimamia Maliasili, Kijijini Kiwere
No comments:
Post a Comment