Wednesday, March 1, 2017

MAFANIKIO YA MRADI WA CEGO KATIKA KIJIJI CHA MALIZANGA KATA YA MLOWA WILAYA YA IRINGA

Katika picha ni Bw. Lulamso Kadaga,Mwenyekiti wa Kijiji cha Malizanga kilichopo Kata ya Mlowa wilayani Iringa, Akiwa ameshika mashine ya kufyatulia tofali zitumiazo saruji na mchanga iliyonunuliwa na halmashauri ya kijiji hicho ili kuachana na matofali ya kuchoma yanayochochea uharibifu wa misitu.


LEAT inatekeleza mradi wa “Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili” (CEGO-NRM), katika wilaya ya Iringa na Mufindi, kuptia ufadhili wa Shirika la Misaada la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID). Mradi huu unatekelezwa katika vijiji 32 (16 wilaya ya Iringa na 16 Wilaya ya Mufindi).

Moja ya kijiji kilichohusishwa katika utekelezaji wa mradi huu ni kijiji cha Malizanga kilichopo kata ya Mlowa, wilaya ya Iringa vijijini. Mafunzo ya Usimamizi wa maliasili na Ufuatiliaji wa Uwajibikaji wa Jamii (UUJ) yalitolewa kuanzia ngazi ya Halmashauri ya kijiji mpaka ngazi ya mwisho kabisa ya wanakijiji wenyewe.


Baadhi ya wajumbe wa halmashauri ya kijiji hiko wamedai kuwa, hali ya misitu ilikuwa mbaya sana kabla LEAT haijaleta mafunzo ya usimamizi wa maliasili katika kijiji chao. Watu wengi walikuwa wakiharibu misitu kwa kigezo cha uhitaji wa kuni, fito, mbao na mkaa kwaajili ya nishati, ujenzi  na kuuza ili kujipatia kipato.


Mwenyekiti wa Kijiji cha Malizanga Ndugu Lulamso Kadaga alisema, “Uhifadhi wa maliasili katika kijiji chake umeongezeka kwa kiasi kikubwa, kwani wengi wamepata elimu ya uhifadhi wa maliasili kutoka LEAT. Pia kupitia mafunzo ya Ufuatiliaji wa Uwajibikaji Jamii -

UUJ, wanakijiji wamekuwa wakifuatilia vitu vingi hususani shughuli za kimaendeleo kama ujenzi wa majengo ya kitaasisi na kuhoji bila woga pale wanapoona mambo yanaenda tofauti. Hapo mwanzo wananchi hawakuwa wakifuatilia shughuli zozote za kimaendeleo hapa kijijini. Ila kwa sasa hali ya ufuatiliaji inafanya viongozi tuwajibike kwani wananchi wanatusaidia na kutukumbusha wajibu wetu. Hivyo inatusaidia pia kuwawajibisha wale ambao hawatekelezi shughuli za miradi kama zinavyopangwa”


“Tumeweka kalenda ya vikao na mikutano ya halmashauri ya kijiji inayofanyika kila mwezi na mkutano mkuu unaofanyika kila baada ya miezi mitatu. Sisi kama viongozi tunahakikisha kalenda hii inafuatwa. Endapo mikutano ya kijiji haitafanyika kwa wakati, jamii imekuwa ikihoji sababu ya kutofanyika mikuatano hiyo. Hivyo jamii pia imeamka kutokana na kutambua umuhimu wa mikutano ya kijiji baada ya kupata elimu ya UUJ kutoka LEAT”. Aliongezea Ndugu Kadaga.


“Binafsi sikusomea uongozi, hivyo vitu vingi sana nimejifunza na kunufaika kutoka LEAT. Mafunzo waliyotupatia kuhusiana na UUJ hasa muongozo juu ya nguzo tano za UUJ yalininufaisha mimi kama kiongozi lakini pia hata wananchi kwa ujumla. Niliguswa sana na mada ya U3( Ufafanuzi, Uhalalisho na Uthibitisho). Nimenufaika juu ya suala la uongozi kwani kabla ya LEAT pengine nilikuwa ninaenda kinyume kwa kutokujua. LEAT imeniwezesha kutambua umuhimu wa utawala bora kwani nilijifunza kuwa mimi kama kiongozi natakiwa niwajibike, nijitume na niwe muwazi kwa wananchi wangu. Kama sitofanya hivyo nitalazimika kutoa U3 kwa wananchi wangu”. Alisema Ndugu Kadaga

  
"Hivyo basi mimi kama kiongozi nimeonyesha njia bora ya usimamizi wa maliasili katika kijiji changu hasa baada ya kupata mafunzo ya utunzaji Mazingira kutoka LEAT.
Niliita Halmashauri ya kijiji na kuwataka tukubaliane kukomesha suala la uharibifu wa misitu unaosababishwa na ukataji wa miti kwaajili ya kuchomea tofali za ujenzi. Tulianza utekelezaji huu kwa kununua mashine ya kufyatulia tofali zinazotumia Saruji naMchanga.

Tulikubaliana majengo yote ya taasisi tutayajenga kwa kutumia tofali za kawaida na si za kuchoma. Hivyo tuliweza kufyatua tofali 3800 zilizotumika kujenga madarasa mawili na ofisi moja. Tumetumia tofali 1800 na zimebaki 2000 zitakazotumika katika shughuli zingine za ujenzi. Hivyo tutakaposimama kuzuia suala la ukataji misitu kwa wanajamii, tutasimama kifua mbele kwani tuna mfano wa kuwaambia na kuwaonyesha.

Hapo nyuma ilikuwa ngumu kuwazuia wasikate miti wakati wewe kiongozi unawaita wafanye shughuli za kimaendeleo zilizokuwa zinahusisha suala la ukataji miti kwaajili ya kuni za kuchomea tofali kwa ajili ya shughuli za ujenzi”. Alimalizia Ndugu Kadaga, Mwenyekiti wa kijiji cha Malizanga"

Tuesday, February 21, 2017

VIKUNDI VYA LEAT VYA SANAA KIJIJI CHA MAPOGORO NA MFYOME KATIKA UELIMISHAJI NA UHAMASISHAJI JAMII JUU YA USHIRIKI WA WANANCHI KATIKA USIMAMIZI WA MALIASILI


Katika picha ni kikundi cha sanaa mapogoro kilichowezeshwa na LEAT kutoa elimu ya utunzaji mazingira kupitia sanaa

Afisa Habari wa LEAT Bi. Edina Tibaijuka akihamasisha kikundi cha sanaa Mapogoro kuendelea kutoa elimu ya usimamizi wa maliasili kupitia sanaa.

Picha ya pamoja ya kikundi cha sanaa cha Mapogoro na Afisa habari wa LEAT Bi. Edina Tibaijuka

Katika picha ni baadhi ya wanakikundi cha sanaa Mfyome 


Katika kuhakikisha kuwa jamii kubwa inaelimishwa na kuhamasishwa juu ya Usimamizi wa Maliasili, Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo ( LEAT) inatumia vikundi vya sanaa katika wilaya zinazotekeleza  mradi wa Ushirki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili, wilaya za Iringa na Mufindi.

LEAT ina vikundi viwili vya Sanaa ambavyo ni kikundi cha Sanaa Mapogoro kilichopo wilaya ya Mufindi na kikundi cha Sanaa Mfyome kilichopo wilaya ya Iringa. Kikundi cha Sanaa Mfyome kinaundwa na wasanii kutoka vijiji vya Mfyome na Kiwere.





LEAT YAWEZESHA HALMASHAURI ZA VIJIJI KUPITISHA SHERIA NDOGO YA USIMAMIZI WA MALIASILI



Wananchi wa kijiji cha Kiwere wilaya ya  Iringa wakiwa katika mkutano mkuu wa kijiji wa kupitisha sheria ndogo ya usimamizi wa maliasili katika kijiji chao

Afisa Mtendaji wa kijiji cha Kiwere wilayani Iringa akisomea wananchi mapendekezo ya sheria ndogo na  kutoa nafasi ya kujadili kipengele baada ya kipenge vilivyoainishwa katika  sheria  ndogo hiyo 


Afisa Mtendaji wa kijiji cha Lugoda Lutali wilayani Mufindi, Akisomea wananchi mapendekezo ya sheria ndogo ya usimamizi wa maliasili na kutoa fursa kwa wananchi kujadili kipengele baada ya kipengele kabla ya kuipitisha sheria hiyo

Katika picha ni wananchi wa kijiji cha Lugoda Lutali wilayani Mufindi wakiwa katika mkutano mkuu wa kijiji wa kupitisha sheria ndogo ya usimamizi wa maliasili za kijiji chao.

Katika Meza kuu Kutoka Kulia ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Lugoda Lutali Bw. Clemence Mwepelwa, Mwanasheria wa wilaya ya Mufindi Ndugu Gasper Kalinga, Afisa Mradi wa LEAT  Bw. Jamal Juma na Afisa Mawasiliano wa LEAT Bi. Edina Tibaijuka, wakihamasisha wanakijiji kupitisha sheria ndogo ya usimamizi ma maliasili za kijiji cha Lugada Lutali


Timu ya Wanasheria Watetezi wa mazingira kwa Vitendo (LEAT) Imekiwezesha kijiji cha Kiwere wilayani Iringa na Kijiji cha Lugoda Lutali wilayani Mufindi kukamilisha mchakato wa kupata sheria ndogo ya usimamizi wa maliasili ili kukabiliana na uharibifu wa misitu na ujangili wa wanyapori. 


LEAT imeshirikiana kwa ukaribu na Ofisi ya Halmashauri ya wilaya Iringa na Mufindi, (Idara ya maliasili na Sheria), na Halmashauri ya Kijiji cha Kiwere  na Lugoda Lutali ambao kwa pamoja waliweza kutoa mapendekezo ya sheria hizo. Wanasheria wa LEAT, Afisa Misitu wa Wilaya na Wanasheria wa halmashauri hizo walishiriki katika mikutano ya halmashauri za kijiji hivyo kama washauri ili kuweza kuboresha mapendekezo ya wajumbe wa halmashauri za vijiji hivyo kabla hayajapelekwa katika mikutano mikuu ya vijiji.


Wakiongozwa na Afisa Watendaji wa vijiji hivyo, wananchi wa kijiji cha Kiwere na Lugoda Lutali waliipitisha sheria hizo kwa kupitia kipengele kimoja baada ya kingine katika mkutano mkuu wa kijiji uliofanyika Jumamosi tarehe 17/2/2017 Kijiji cha Kiwere ringa na Jumatatu tarehe 20/2/2017 Kijiji cha Lugoda Lutali Mufindi.


LEAT inafanya mchakato huu wa kuwashahwishi wananchi kutunga na kupitisha sheria ndogo kupitia mradi wa "Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili" unaofadhiliwa na USAID katika vijiji 32 vya wilaya ya Iringa na Mufindi mkoani Iringa. LEAT inatazamia kuwezesha jumla ya halmashauri za  vijiji 26 wilaya ya Iringa na Mufindi kutunga na kupitisha sheria ndogo za usimamizi wa maliasili.


Lengo la utekelezaji wa shughuli hizi katika mradi huu ni kuzijengea uwezo jamii zinazoishi karibu na rasilimali misitu na wanyapori ili waweze kuzisimamia na kunufaika nazo kwa kuwapa mafunzo ya sheria, sera, miongozo, kanuni na ufuatiliaji wa uwajibikaji jamii.


Baada ya kupitisha sheria hizi katika mikutano ya vijiji, LEAT itaendeleza mchakato huu kwa kushirikiana na halmashauri za vijiji husika na halmashauri za wiliya katika kupitisha sheria ndogo hizi, ikiwa ni pamoja na  kuzipeleka katika baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa na Mufindi ambao jukumu lao ni kuidhinisha ili taratibu za kutumika zianze.



Sunday, November 27, 2016

LEAT YAIPA SERIKALI CHANGAMOTO YA MAZINGIRA KATIKA MDAHALO NA MKUTANO WA MAREJEO YA SHUGHULI ZA MRADI ULIOFANYIKA WILAYA YA IRINGA.

 Mkurugenzi Mtendaji wa LEAT Dk.Rugemeleza Nshala akifungua Mkutano wa marejeo wa Mradi wa CEGO na mdahalo uliowashirikisha viongozi wa serikali, wananchi na wadau wa maliasili mkoani Iringa.
 Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bi. Amina Masenza akihutubia na kufungua rasmi  Mkutano wa marejeo na Mdahalo uliotekelezwa na LEAT kupitia hisani ya watu wa Marekani -USAID
 Viongozi wa serikali ya wilaya ya Iringa na Mufindi wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa Bi. Amina Masenza na Muwakilishi kutoka USAID Bi. Joan Mayer.
 Timu ya Ufuatiliaji wa Uwajibikaji Jamii (UJJ/SAM) wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa serikali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bi. Amina Masenza (Katikati), Muwakilishi kutoka USAID Bi. Joan Mayer na Mkurugenzi Mtendaji wa LEAT Dk. Rugemeleza Nshala (Wa pili kulia)
 Timu ya utekelezaji wa mradi wa ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili (CEGO) wilaya ya Iringa na Mufindi wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa serikali na Muwakilishi kutoka USAID Bi. Joan baada ya Mgeni Rasmi Bi Amina Masenza kufungua Mdahalo huo.

Mhadhiri Mwandamizi Chuo kikuu cha kilimo Morogoro (SUA) Dk. Gimbage Mbeyale akitoa mada ya kwanza kuhusiana na Chanzo cha kukithiri kwa changamoto mbalimbali katika usimamizi wa misitu na wanyamapori


Ndugu. Leo Mavita akitoa mada ya pili katika mdahalo kuhusiana na ni nini chanzo na athari za kutengwa kwa bajeti ndogo kwenye halmshauri za wilaya kwa ajili ya sekta ya misitu na wanyamapori.

Afisa Mradi Mwandamizi wa mradi wa ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili (CEGO) Bw. Remmy Lema akitoa wasilisho la utukelezaji wa shughuli za mradi katika mkutano wa marejeo kwa wadau wa mradi na viongozi wa serikali mkoani Iringa.

 Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mufindi Mh. Festo Mgina akizungumza katika mkutano wa marejeo na mdahalo uliofanywa na LEAT kwa hisani ya watu wa Marekani USAID



 Bw. Jeremiah Daffa - Mhamasishaji wa mdahalo na mkutano wa marejeo uliofanywa na LEAT kwa hisani ya watu wa Marekani (USAID) 
 Mwenyekiti wa Timu ya SAM wilaya  ya Iringa Bw. Ngole Mwangosi  akisoma ripoti yao katika mkutano wa marejeo ya mradi wa ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili (CEGO)

Mkuu wa wilaya ya Iringa Mheshimiwa Richard Kasesela akihitimisha mdahalo kwa kutoa maoni yake juu ya mada zilizojadiliwa na washiriki kutoka serikalini, wadau wa maliasili na wananchi wa mkoa wa Iringa.
Serikali imepewa changamoto ya kutekeleza kikamilifu sheria za Mazingira, Maliasili na Wanyamapori kwa lengo la kupunguza au kumaliza kabisa matatizo yatokanayo na kutofuatwa kwa sheria hizo.
Changamoto  hiyo imetolewa na Timu ya Wanasheria watetezi wa Mazingira kwa vitendo (LEAT) wakati wa mdahalo maalum wa viongozi wa Serikali, wananchi na wadau wa Mazingira, Maliasili na Wanyapori Mkoa wa Iringa. Mdahalo huo ulifunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bi.Amina Masenza.
Akizungumza katika Mdahalo huo wa marejeo ya Mradi wa Ushiriki wa wananchi katika Usimamizi wa Maliasili (CEGO) wilaya za Iringa na Mufindi, Mkurugenzi Mtendaji wa LEAT, Dkt. Rugemeleza Nshala amesema licha ya mapungufu kidogo ya sheria hizo lakini zinao uwezo wa kulisaidia Taifa kuondokana na kero za matumizi yasiyo endelevu ya maliasili misitu na wanyama pori.
Awali, Mkuu wa wilaya Iringa amesema Mkoa wa Iringa unakabiliwa na changamoto kubwa ya kilimo cha mabondeni maarufu kama vinyungu na ugumu wa kuwaondoa watu hao unakuja pale inapokosekana shughuli mbadala watakayoifanya ili iwaingizie kipato.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, amesema juhudi za LEAT kutoa elimu kwa Wananchi ni nzuri kwa sababu zinasaidia kupunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Mhadhiri Mwandamizi Chuo kikuu cha kilimo Morogoro (SUA) Dk. Gimbage Mbeyale katika mdahalo huo alisema kuwa mabadiliko ya tabia ya nchi ni moja ya changamoto zinazokwamisha kuwepo kwa utunzaji na umuduji dumivu wa rasilimali misitu na wanyamapori.
Dk. Mbeyale alisema kuwa changamoto hizo zinasababishwa na uvunaji usiozingatia mpango wa usimamizi misitu sambamba na ongezeko la watu nchini kwa asilimia 3.2 toka milioni 11 kwa mwaka 1960 hadi milioni 56 kwa mwaka 2016.
“Migogoro kati ya mamlaka za hifadhi na wananchi (wakulima na wafugaji) ni changamoto za kuwepo kwa utunzaji na umuduji dumivu wa rasilimali misitu na wanyamapori nchini Tanzania” alisema Dk. Mbeyale
Naye msimamizi wa sekta ya Uchumi na Uzalishaji kutoka ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Leo Mavita, alisema kuwa kiini cha changamoto katika utunzaji na umuduji wa rasilimali misitu na wanyamapori ni kuwa na uwezo wa kuchanganua na kuelezea mahusiano yake na jamii na uchumi wake.

Saturday, November 26, 2016

LEAT YATEMEBELEWA NA WATAALAM KUTOKA CHEMONICS INTERNATIONAL - USAID KWAAJILI YA KUREKODI VIDEO YA MAFANIKIO YA SHUGHULI ZA MRADI WA CEGO


 


Kutoka Kulia ni Bi. Karina Keating (Meneja mradi Pamoja Twajenga), Remmy Lema (Afisa Mradi Mwandamizi -LEAT), M/Kiti wa MJUMIKIK na Bw. Hamza Chang'a (Mwanilishi wa kikundi cha utunzaji wa mazingira kijiji cha Kiwere) Musa Mnasizu (Afisa Mradi wa CEGO wilaya ya Iringa), Dk. Rugemeleza Nshala (Mkurugenzi Mtendaji -LEAT) na wawili kushoto ni wajumbe wa kikundi cha Utunzaji wa mazingira-Kiwere wakionyesha kitalu cha miti walichokianzisha baada ya kupata mafunzo ya usimamizi wa maliasili kutoka LEAT


 
 
 
 Bw. Mike Bennett akichukua video ya mazungumzo kati ya Dk. Nshala Mkurugenzi Mtendaji wa LEAT na Bw. Hamza Chang'a akiwa na wajumbe wenzake wa kikundi cha Utunzaji wa mazingira, wakielezea faida ya mafunzo ya usimamizi wa maliasili kutoka LEAT iliyowasukuma kuanzisha kitalu cha miti.


 Bw. Mike Bennett Mwandishi kutoka Chemonics International-USAID akichukua video ya wanakijiji wa Kijiji cha Kiwere waliokuwa wakikata mti ulioanguka baada ya kuungua na moto.


Bwana Mike Bennett Mwandishi kutoka Chemonics International- USAID akipiga picha eneo la kijiji lililopandwa miti kutoka katika kitalu cha miti ya Kikundi cha Utunzanji mazingira cha kijiji cha Kiwere

 
 Afisa Ughani wa Mradi wa Ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili (CEGO) wilaya ya Iringa akiwa na Bi. Karina Keating Meneja Mradi Chemonics International/Pamoja Twajenga katika ziara yao katika eneo lililopandwa miti na kikundi cha utunzaji mazingira katika ardhi ya kijiji cha Kiwere


Timu nzima ya mradi wa CEGO, Timu ya wataalamu kutoka Chemonics International-USAID na wanakikundi cha Utunzaji mazingira wa kijiji cha Kiwere wakizungukia eneo la ardhi ya kijiji lililopandwa miti na wanakikundi waliopatiwa mafunzo ya usimamizi wa maliasili kutoka LEAT kwa ufadhili wa USAID



 Kutoka Kushoto ni Bi. Karina Keating (Meneja-Pamoja Twajenga), Mike Bennett (Mwandishi-Chemonics International-USAID) , Dk. Rugemeleza Nshala (Murugenzi Mtendaji -LEAT) na Bi. Maria (Msimamizi wa miradi ya CEGO-Pamoja Twajenga) wakimrekodi Bw. Hamza Chan'ga aliyekuwa akielezea mafanikio ya elimu ya usimamizi wa maliasili kutoka LEAT Iliyowapelekea wanakijiji kuunda kikundi cha utunzaji wa mazingira na kuanzisha kitalu cha miti.



 
 





 Picha ya pamoja ya timu ya LEAT na wataalamu Kutoka Chemonics International baada ya kumaliza shughuli ya kurekodi simulizi za mafaniko zilizotokana na mradi wa ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili (CEGO) unaotekelezwa na LEAT kupitia ufadhili wa shirika la maendeleo la Kimataifa la Marekani - USAID

 
Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID) linaloifadhili LEAT katika mradi wa ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili (CEGO) walipendezwa na moja ya simulizi za mafaniko katika shughuli za mradi huu. Hivyo kutuma Afisa habari kutoka USAID-Chemonics International Ndugu Mike Bennett kuja kutembelea maeneo ya mradi yenye simulizi za mafanikio hayo. Mike Bennett aliongozana na Meneja Mradi  kutoka Pamoja Twajenga Bi. Karina Keating na Bi. Maria (Msimamizi wa asasi za miradi ya CEGO).

Timu hii ilitembelea kijiji cha Kiwere wilayani Iringa ambacho ni miongoni mwa vijiji vilivyopatiwa mafunzo ya Usimamizi wa maliasili, Ufuatiliaji wa uwajibikaji jamii (UJJ-SAM) na ufugaji nyuki yaliyowezeshwa na LEAT, Kijiji hiki kilionyesha matunda ya elimu waliyoipata kutoka LEAT kwa kuanzisha kikundi cha utunzanji wa mazingira huku lengo lao likiwa ni kutunza misitu inayoharibiwa kwa kasi kubwa katika maeneo yao.

 Miongoni mwa wanakijiji waliopatiwa mafunzo hayo katika kijiji cha Kiwere ni Bw. Hamza Hamis Chang’a  ambaye ni mwanzilishi na msimamizi wa shughuli za kikundi hiko. Bw. Hamza akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa LEAT na timu nzima ya mradi iliyotembelea kijiji hicho alisema, “kikundi hiki tulikianzisha baada ya kupata elimu nzuri ya usimamizi wa mazingira kutoka LEAT, tulipata muamko mkubwa wa kurejesha hali ya misitu yetu iliyoharibiwa kwa kiasi kikubwa, hivyo hatukutaka kuyalalia mafunzo hayo bali tulichukua jitihada za kuanzisha kikundi cha utunzanji wa mazingira kwa lengo la kutunza mazingira yaliyoharibiwa”

 Aliendelea “Jitihada zetu zilianza kwa kuanzisha kitalu cha miti. Tuliiomba halmshauri ya kijiji cha Kiwere itupatie eneo la wazi ili tupande miti hiyo. Kijiji kilitupatia eneo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari mbili ambapo ndipo tulipopanda miti hiyo”.

Aliongezea Bwana Hamza kuwa “LEAT imetuhamasisha kwa kiasi kikubwa katika suala la utunzaji wa mazingira, na kupitia kikundi tulichoanzisha chenye takribani ya wajumbe 17 hadi sasa, tunaweza kuhifadhi misitu na kukuza kipato chetu kutokana na miche ya miti tutanayoiuza, kwani mpaka sasa tumeshauza miche kadhaa na kujipatia fedha kidogo iliyotusaidia kununua mbegu na kuotesha miche mingine kisha kiasi kilichobaki tuligawana kama faida kwa wanakikundi wote.

 

Tuesday, November 22, 2016

LEAT YAIWEZESHA TIMU YA SAM YA WILAYA KUFANYA MREJESHO WA TAARIFA YA UFUATILIAJI WA UWAJIBIKAJI JAMII KWA VIONGOZI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA IRINGA.


 

 
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Richard Kasesela akizungumza baada ya kusikiliza mrejesho wa taarifa ya timu ya Ufuatiliaji wa uwajibikaji jamii (Timu ya SAM) ya wilaya inayowezeshwa na LEAT kupitia hisani ya watu wa Marekani (USAID)
 
 
 Mkuu wa Idara ya maliasili wa Wilaya ya Iringa Ndugu Dornald Mshani akitoa maoni yake baada ya kusikiliza mrejesho wa taarifa ya timu ya Ufuatiliaji wa uwajibikaji jamii (Timu ya SAM) ya wilaya inayowezeshwa na LEAT kupitia hisani ya watu wa Marekani (USAID)

 
Mkuu wa Idara ya Maliasili Ndg. Dornald Mshani (Kulia) na Afisa Misitu wa wilaya ya Iringa Ndg. Njoni (Kushoto) wakisikilza kwa makini na kuchukua taarifa ya mrejesho uliowasilishwa na Mwenyekiti wa timu ya SAM ya wilaya ya Iringa







 Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Richard Kasesela amepiga marufuku uvunaji wa mistu ya asili katika misitu ya hifadhi za vijiji vinavyozunguka wilaya yake bila ya barua kutoka ofisini kwake kama njia ya kukabiliana na vitendo vya uharibifu wa mazingira katika wilaya yake.

 Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa mrejesho wa Timu ya wilaya ya Ufuatiliaji wa uwajibikaji jamii (Timu ya SAM) kutoka wilaya ya Iringa inayoratibiwa na Timu ya  Wanasheria    Watetezi wa Mazingira (LEAT) kupitia hisani ya watu wa Marekani (USAID), Mh. Kasesela alisema hali ya uvunaji wa misitu kwa sasa inatisha kiasi cha kulifanya eneo hilo kuwa jangwa.

“Ninawashukuru sana (LEAT) kwa namna mlivyosaidia kutoa elimu kwa wananchi wangu, kwa sasa wamewezesha kukamatwa kwa magunia ya mkaa na mbao mfano katika kijiji cha Kiwere, na leo ninaagiza kuanzia sasa hakuna mtu atakayeruhusiwa kuvuna miti hadi hapo atakapokuwa na barua kutoka ofisini kwangu”alisema Mh. Kasesela.

 Mh. Kasesela alionya watumishi wa Halmashuari ya Iringa wanaohusika na utoaji vibali kwa ajili ya uvunaji wa misitu kuwa ni muhimu kushirikisha ofisi yake na kama hawatafanya hivyo atachukua hatua kali dhidi yao.

 Mkuu huyo wa wilaya aliagiza wajumbe wa kamati za mazingira wa vijiji kukamata watu wote wanaojihusisha na uharibifu wa mazingira wakiwamo  wenye vibali wasio na barua kutoka ofisini kwake bila kujali vyeo vyao.

 Mwenyekiti wa kamati za usimamizi wa mazingira wilaya ya Iringa Ngole Mwangosi alisema tangu kuanza kutekelezwa kwa mradi wa Ushiriki wa Usimamizi wa maliasili (CEGO) unaotekelezwa na LEAT kwa ufadhili wa USAID kumekuwa na ongezeko la wananchi kutoa taraifa za uharibifu wa maliasili katika maeneo yao.

“Katika kijiji cha Kitisi, baadhi ya wananchi waliokuwa wakijiita Mtajirungu  waliokuwa wakifanya uwindaji haramu kwa kutumia Mbwa na rungu (silaha za jadi) walidhibitiwa baada ya baadhi ya wananchi kutoa taarifa kwa maaskari wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

 Alisema sambamba na hilo bado wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali ikiwamo ya uelewa wa viongozi wa serikali za vijiji juu ya kile kinachodaiwa muingiliano wa majukumu kati ya serikali ya kijiji na  kamati za mazingira.

 Kwa upande wake Afisa miradi wa LEAT Musa Mnasizu, Alisema LEAT iliamua kutekeleza mradi huo kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata elimu na kutambua kuwa rasimali za asili zilizopo kijijini mwao wanawajibu wa kuzilinda na kunufaika nazo.

“Wengi walikuwa hawatambui kuwa rasimali za maliasili zilizopo katika maeneo yao kuwa si mali yao bali ni ya serikali jambo lilichangia wao kutojihusisha na jukumu la kuzilinda rasimali hizo ikiwamo misitu na wanyamapori”alisema Mnasizu.

Tuesday, November 8, 2016

Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imeidhinisha kuanza kutumika kwa sheria ndogo ya usimamizi wa maliasili

  Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa Bw. Stephen Mhapa, Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa na katibu tawala wa wilaya ya Iringa Bw. Joseph Chitika wakiongoza majadiliano katika mkutano wa baraza la wadiwani 
 
Mwanasheria mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Iringa Bi. Kissah Mbilla akifuatilia majadiliano ya baraza la madiwani wakati wa kupitisha sheria ndogo za vijiji 
 
 
Baadhi ya wajumbe na waandishi wa habari waliohudhuria mkutano wa baraza la madiwani wakifuatilia kwa makini kuidhinishwa kwa sheria ndogo za vijiji vya Mbweleli, Kinyali na Kinyika.
 
Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa Bw. Donald Mshani akihojiwa na waandishi wa habari baada ya baraza ya madiwani kuidhinisha sheria ndogo za vijiji husika   
 
 
Mwanasheria mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa Bi. Kissah Mbilla akihojiwa na waandishi wa habari baada ya baraza ya madiwani kuidhinisha sheria ndogo za vijiji husika 


Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imeidhinisha kuanza kutumika kwa sheria ndogo  za usimamizi wa maliasili ili kukabiliana na kasi ya uharibifu wa rasilimali za misitu na wanyamapori katika vijiji vitatu miongoni mwa vijiji ambavyo LEAT inatekeleza mradi wa ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili.

Sheria zilizoidhinishwa na halmashauri hiyo zimetungwa na halmashauri za vijiji vya Mbweleli, Kinyika na Kinyali chini ya msaada wa Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT),  lengo likiwa ni kudhibiti uharibifu wa mazingira unaokuwa kwa kasi katika vijiji hivyo.

Mara baada ya baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kuidhinisha kuanza kutumika kwa sheria hizo katika kikao cha baraza la madiwani  kilichoketi  tarehe 29/10/2016, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Stephen  Mhapa alisema sheria hizo zitasaidia kuongeza kasi ya utunzaji wa mazingira na wanyamapori katika vijiji husika.

Alisema Halmashauri za vijiji zina mamlaka kamili ya kutunga sheria ndogo zinazohusu usimamizi wa maeneo yao na kwamba sheria hizo zisipingane na sheria mama za nchi na Halmashauri husika.

“Kitendo cha halmashauri za vijiji kutunga sheria ndogo za kusimamia na kudhibiti uharibifu wa maliasili katika maeneo yao kimenifurahisha na kwamba kuanzia sasa misitu na wanyamapori waliokuwa katika hatari ya kutoweka kutokana na ujangili na uchomaji moto watakuwa salama”alisema Mhapa:

“Hiyo ni kutokana na wananchi wa eneo husika wao wenyewe kwa hiyari yao kujitungia sheria wanazoweza kuzisimamia, katika hili ninawashukuru Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa vitendo (LEAT) ambao wamewapatia elimu na msaada wa kufikia hatua hiyo ya kutunga sheria ndogo watakazoweza kuzisimamia wao wenyewe” alisema Mhapa.

Mwanasheria mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa Kissah Mbilla alisema jukumu la ofisi yake katika mchakato huo pamoja na kushirikiana na wanasheria wa LEAT ilikuwa kuhakikisha sheria hizo ndogo hazipingani na sheria mama ambayo ni ile ya Halmashauri na ya Nchi.

“Halmashauri ya kijiji inayo mamlaka ya kutunga sheria ndogo na ofisi yetu inachofanya ni kuangalia kama taratibu zimefuatwa, adhabu zinazotolewa katika sheria ndogo za kijiji hazizidi Tsh 50,000 na kwakuwa wamepitisha na baraza la madiwani limeidhinisha sheria hizi, sasa ni sheria kamili na zinaweza kuanza kutumika” alisema Mbilla.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili wa Halmashauri hiyo Donald Mshani alisema kuidhinishwa kwa sheria hizo kutasaidia idara yake kupambana na uharibifu wa mazingira ambao kwa sasa umekuwa ukishika kasi.

Alisema hatua hiyo inaweza kuwa ya mafanikio kutokana na sheria hizo tangu mchakato wa kutunga hadi kuidhinishwa na baraza la madiwani umeshirikisha wananchi katika kufikia malengo hayo.

Afisa habari wa Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) alisema hatua ya baraza la madiwani kuidhinisha kutumika kwa sheria hizo kumewafariji kwa kuwa jukumu lao la kuelimisha wananchi na kuwahamasisha kutunga sheria hizo linakuwa limetimia.

Edina Tibaijuka alisema LEAT kupitia mradi wa Ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili unaofadhiliwa na shirika la Kimataifa la watu wa Marekani (USAID) ilihamasisha halmashauri za vijiji vya Kinyali na Kinyika kutunga sheria ndogo hizo kwani awali hawakuwa nazo kabisa na kwa upande wa kijiji cha Mbweleli LEAT iliwawezesha Halmashauri ya kijiji hiko kufanya marekebisho ya sheria yao baada ya kuipitia na kuona sheria waliyokuwa wakiitumia awali ina mapungufu.


“Baada ya mikutano  mikuu ya vijiji hivyo kuridhia na kupitisha sheria hizo kuhusiana na maliasili ziliwasilishwa katika ofisi ya mwanasheria wa wilaya, kisha zilijadiliwa na kupitishwa na kamati husika za wilaya na kufikishwa katika baraza la madiwani ambao waliridhia kuanza kutumika kwa sheria hizo na kunatoa fursa kwa serikali za vijiji kuanza kuzitumia ili kudhibiti vitendo vya uharibifu wa mazingira” alisema. Tibaijuka.