Tuesday, February 21, 2017

LEAT YAWEZESHA HALMASHAURI ZA VIJIJI KUPITISHA SHERIA NDOGO YA USIMAMIZI WA MALIASILI



Wananchi wa kijiji cha Kiwere wilaya ya  Iringa wakiwa katika mkutano mkuu wa kijiji wa kupitisha sheria ndogo ya usimamizi wa maliasili katika kijiji chao

Afisa Mtendaji wa kijiji cha Kiwere wilayani Iringa akisomea wananchi mapendekezo ya sheria ndogo na  kutoa nafasi ya kujadili kipengele baada ya kipenge vilivyoainishwa katika  sheria  ndogo hiyo 


Afisa Mtendaji wa kijiji cha Lugoda Lutali wilayani Mufindi, Akisomea wananchi mapendekezo ya sheria ndogo ya usimamizi wa maliasili na kutoa fursa kwa wananchi kujadili kipengele baada ya kipengele kabla ya kuipitisha sheria hiyo

Katika picha ni wananchi wa kijiji cha Lugoda Lutali wilayani Mufindi wakiwa katika mkutano mkuu wa kijiji wa kupitisha sheria ndogo ya usimamizi wa maliasili za kijiji chao.

Katika Meza kuu Kutoka Kulia ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Lugoda Lutali Bw. Clemence Mwepelwa, Mwanasheria wa wilaya ya Mufindi Ndugu Gasper Kalinga, Afisa Mradi wa LEAT  Bw. Jamal Juma na Afisa Mawasiliano wa LEAT Bi. Edina Tibaijuka, wakihamasisha wanakijiji kupitisha sheria ndogo ya usimamizi ma maliasili za kijiji cha Lugada Lutali


Timu ya Wanasheria Watetezi wa mazingira kwa Vitendo (LEAT) Imekiwezesha kijiji cha Kiwere wilayani Iringa na Kijiji cha Lugoda Lutali wilayani Mufindi kukamilisha mchakato wa kupata sheria ndogo ya usimamizi wa maliasili ili kukabiliana na uharibifu wa misitu na ujangili wa wanyapori. 


LEAT imeshirikiana kwa ukaribu na Ofisi ya Halmashauri ya wilaya Iringa na Mufindi, (Idara ya maliasili na Sheria), na Halmashauri ya Kijiji cha Kiwere  na Lugoda Lutali ambao kwa pamoja waliweza kutoa mapendekezo ya sheria hizo. Wanasheria wa LEAT, Afisa Misitu wa Wilaya na Wanasheria wa halmashauri hizo walishiriki katika mikutano ya halmashauri za kijiji hivyo kama washauri ili kuweza kuboresha mapendekezo ya wajumbe wa halmashauri za vijiji hivyo kabla hayajapelekwa katika mikutano mikuu ya vijiji.


Wakiongozwa na Afisa Watendaji wa vijiji hivyo, wananchi wa kijiji cha Kiwere na Lugoda Lutali waliipitisha sheria hizo kwa kupitia kipengele kimoja baada ya kingine katika mkutano mkuu wa kijiji uliofanyika Jumamosi tarehe 17/2/2017 Kijiji cha Kiwere ringa na Jumatatu tarehe 20/2/2017 Kijiji cha Lugoda Lutali Mufindi.


LEAT inafanya mchakato huu wa kuwashahwishi wananchi kutunga na kupitisha sheria ndogo kupitia mradi wa "Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili" unaofadhiliwa na USAID katika vijiji 32 vya wilaya ya Iringa na Mufindi mkoani Iringa. LEAT inatazamia kuwezesha jumla ya halmashauri za  vijiji 26 wilaya ya Iringa na Mufindi kutunga na kupitisha sheria ndogo za usimamizi wa maliasili.


Lengo la utekelezaji wa shughuli hizi katika mradi huu ni kuzijengea uwezo jamii zinazoishi karibu na rasilimali misitu na wanyapori ili waweze kuzisimamia na kunufaika nazo kwa kuwapa mafunzo ya sheria, sera, miongozo, kanuni na ufuatiliaji wa uwajibikaji jamii.


Baada ya kupitisha sheria hizi katika mikutano ya vijiji, LEAT itaendeleza mchakato huu kwa kushirikiana na halmashauri za vijiji husika na halmashauri za wiliya katika kupitisha sheria ndogo hizi, ikiwa ni pamoja na  kuzipeleka katika baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa na Mufindi ambao jukumu lao ni kuidhinisha ili taratibu za kutumika zianze.



No comments:

Post a Comment