LEAT inatekeleza mradi wa “Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili” (CEGO-NRM), katika wilaya ya Iringa na Mufindi, kuptia ufadhili wa Shirika la Misaada la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID). Mradi huu unatekelezwa katika vijiji 32 (16 wilaya ya Iringa na 16 Wilaya ya Mufindi).
Moja ya kijiji kilichohusishwa
katika utekelezaji wa mradi huu ni kijiji cha Malizanga kilichopo kata ya
Mlowa, wilaya ya Iringa vijijini. Mafunzo ya Usimamizi wa maliasili na Ufuatiliaji
wa Uwajibikaji wa Jamii (UUJ) yalitolewa kuanzia ngazi ya Halmashauri ya kijiji
mpaka ngazi ya mwisho kabisa ya wanakijiji wenyewe.
Baadhi ya wajumbe wa halmashauri
ya kijiji hiko wamedai kuwa, hali ya misitu ilikuwa mbaya sana kabla LEAT haijaleta
mafunzo ya usimamizi wa maliasili katika kijiji chao. Watu wengi walikuwa
wakiharibu misitu kwa kigezo cha uhitaji wa kuni, fito, mbao na mkaa kwaajili
ya nishati, ujenzi na kuuza ili kujipatia kipato.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Malizanga
Ndugu Lulamso Kadaga alisema, “Uhifadhi wa maliasili katika kijiji chake
umeongezeka kwa kiasi kikubwa, kwani wengi wamepata elimu ya uhifadhi wa
maliasili kutoka LEAT. Pia kupitia mafunzo ya Ufuatiliaji wa Uwajibikaji Jamii -
UUJ,
wanakijiji wamekuwa wakifuatilia vitu vingi hususani shughuli za kimaendeleo
kama ujenzi wa majengo ya kitaasisi na kuhoji bila woga pale wanapoona mambo
yanaenda tofauti. Hapo mwanzo wananchi hawakuwa wakifuatilia shughuli zozote za
kimaendeleo hapa kijijini. Ila kwa sasa hali ya ufuatiliaji inafanya viongozi
tuwajibike kwani wananchi wanatusaidia na kutukumbusha wajibu wetu. Hivyo
inatusaidia pia kuwawajibisha wale ambao hawatekelezi shughuli za miradi kama
zinavyopangwa”
“Tumeweka kalenda ya vikao na
mikutano ya halmashauri ya kijiji inayofanyika kila mwezi na mkutano mkuu unaofanyika
kila baada ya miezi mitatu. Sisi kama viongozi tunahakikisha kalenda hii inafuatwa.
Endapo mikutano ya kijiji haitafanyika kwa wakati, jamii imekuwa ikihoji sababu
ya kutofanyika mikuatano hiyo. Hivyo jamii pia imeamka kutokana na kutambua
umuhimu wa mikutano ya kijiji baada ya kupata elimu ya UUJ kutoka LEAT”.
Aliongezea Ndugu Kadaga.
“Binafsi sikusomea uongozi, hivyo
vitu vingi sana nimejifunza na kunufaika kutoka LEAT. Mafunzo waliyotupatia
kuhusiana na UUJ hasa muongozo juu ya nguzo tano za UUJ yalininufaisha mimi
kama kiongozi lakini pia hata wananchi kwa ujumla. Niliguswa sana na mada ya
U3( Ufafanuzi, Uhalalisho na Uthibitisho). Nimenufaika juu ya suala la uongozi kwani
kabla ya LEAT pengine nilikuwa ninaenda kinyume kwa kutokujua. LEAT imeniwezesha
kutambua umuhimu wa utawala bora kwani nilijifunza kuwa mimi kama kiongozi
natakiwa niwajibike, nijitume na niwe muwazi kwa wananchi wangu. Kama sitofanya
hivyo nitalazimika kutoa U3 kwa wananchi wangu”. Alisema Ndugu Kadaga
"Hivyo basi mimi kama kiongozi
nimeonyesha njia bora ya usimamizi wa maliasili katika kijiji changu hasa baada
ya kupata mafunzo ya utunzaji Mazingira kutoka LEAT.
Niliita Halmashauri ya kijiji na kuwataka
tukubaliane kukomesha suala la uharibifu wa misitu unaosababishwa na ukataji wa
miti kwaajili ya kuchomea tofali za ujenzi. Tulianza utekelezaji huu kwa
kununua mashine ya kufyatulia tofali zinazotumia Saruji naMchanga.
Tulikubaliana majengo yote ya taasisi
tutayajenga kwa kutumia tofali za kawaida na si za kuchoma. Hivyo tuliweza
kufyatua tofali 3800 zilizotumika kujenga madarasa mawili na ofisi moja.
Tumetumia tofali 1800 na zimebaki 2000 zitakazotumika katika shughuli zingine
za ujenzi. Hivyo tutakaposimama kuzuia suala la ukataji misitu kwa wanajamii,
tutasimama kifua mbele kwani tuna mfano wa kuwaambia na kuwaonyesha.
Hapo nyuma ilikuwa ngumu kuwazuia wasikate
miti wakati wewe kiongozi unawaita wafanye shughuli za kimaendeleo zilizokuwa
zinahusisha suala la ukataji miti kwaajili ya kuni za kuchomea tofali kwa ajili
ya shughuli za ujenzi”. Alimalizia Ndugu Kadaga, Mwenyekiti wa kijiji cha
Malizanga"
No comments:
Post a Comment