Tuesday, November 22, 2016

LEAT YAIWEZESHA TIMU YA SAM YA WILAYA KUFANYA MREJESHO WA TAARIFA YA UFUATILIAJI WA UWAJIBIKAJI JAMII KWA VIONGOZI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA IRINGA.


 

 
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Richard Kasesela akizungumza baada ya kusikiliza mrejesho wa taarifa ya timu ya Ufuatiliaji wa uwajibikaji jamii (Timu ya SAM) ya wilaya inayowezeshwa na LEAT kupitia hisani ya watu wa Marekani (USAID)
 
 
 Mkuu wa Idara ya maliasili wa Wilaya ya Iringa Ndugu Dornald Mshani akitoa maoni yake baada ya kusikiliza mrejesho wa taarifa ya timu ya Ufuatiliaji wa uwajibikaji jamii (Timu ya SAM) ya wilaya inayowezeshwa na LEAT kupitia hisani ya watu wa Marekani (USAID)

 
Mkuu wa Idara ya Maliasili Ndg. Dornald Mshani (Kulia) na Afisa Misitu wa wilaya ya Iringa Ndg. Njoni (Kushoto) wakisikilza kwa makini na kuchukua taarifa ya mrejesho uliowasilishwa na Mwenyekiti wa timu ya SAM ya wilaya ya Iringa







 Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Richard Kasesela amepiga marufuku uvunaji wa mistu ya asili katika misitu ya hifadhi za vijiji vinavyozunguka wilaya yake bila ya barua kutoka ofisini kwake kama njia ya kukabiliana na vitendo vya uharibifu wa mazingira katika wilaya yake.

 Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa mrejesho wa Timu ya wilaya ya Ufuatiliaji wa uwajibikaji jamii (Timu ya SAM) kutoka wilaya ya Iringa inayoratibiwa na Timu ya  Wanasheria    Watetezi wa Mazingira (LEAT) kupitia hisani ya watu wa Marekani (USAID), Mh. Kasesela alisema hali ya uvunaji wa misitu kwa sasa inatisha kiasi cha kulifanya eneo hilo kuwa jangwa.

“Ninawashukuru sana (LEAT) kwa namna mlivyosaidia kutoa elimu kwa wananchi wangu, kwa sasa wamewezesha kukamatwa kwa magunia ya mkaa na mbao mfano katika kijiji cha Kiwere, na leo ninaagiza kuanzia sasa hakuna mtu atakayeruhusiwa kuvuna miti hadi hapo atakapokuwa na barua kutoka ofisini kwangu”alisema Mh. Kasesela.

 Mh. Kasesela alionya watumishi wa Halmashuari ya Iringa wanaohusika na utoaji vibali kwa ajili ya uvunaji wa misitu kuwa ni muhimu kushirikisha ofisi yake na kama hawatafanya hivyo atachukua hatua kali dhidi yao.

 Mkuu huyo wa wilaya aliagiza wajumbe wa kamati za mazingira wa vijiji kukamata watu wote wanaojihusisha na uharibifu wa mazingira wakiwamo  wenye vibali wasio na barua kutoka ofisini kwake bila kujali vyeo vyao.

 Mwenyekiti wa kamati za usimamizi wa mazingira wilaya ya Iringa Ngole Mwangosi alisema tangu kuanza kutekelezwa kwa mradi wa Ushiriki wa Usimamizi wa maliasili (CEGO) unaotekelezwa na LEAT kwa ufadhili wa USAID kumekuwa na ongezeko la wananchi kutoa taraifa za uharibifu wa maliasili katika maeneo yao.

“Katika kijiji cha Kitisi, baadhi ya wananchi waliokuwa wakijiita Mtajirungu  waliokuwa wakifanya uwindaji haramu kwa kutumia Mbwa na rungu (silaha za jadi) walidhibitiwa baada ya baadhi ya wananchi kutoa taarifa kwa maaskari wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

 Alisema sambamba na hilo bado wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali ikiwamo ya uelewa wa viongozi wa serikali za vijiji juu ya kile kinachodaiwa muingiliano wa majukumu kati ya serikali ya kijiji na  kamati za mazingira.

 Kwa upande wake Afisa miradi wa LEAT Musa Mnasizu, Alisema LEAT iliamua kutekeleza mradi huo kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata elimu na kutambua kuwa rasimali za asili zilizopo kijijini mwao wanawajibu wa kuzilinda na kunufaika nazo.

“Wengi walikuwa hawatambui kuwa rasimali za maliasili zilizopo katika maeneo yao kuwa si mali yao bali ni ya serikali jambo lilichangia wao kutojihusisha na jukumu la kuzilinda rasimali hizo ikiwamo misitu na wanyamapori”alisema Mnasizu.

No comments:

Post a Comment