Sunday, November 27, 2016

LEAT YAIPA SERIKALI CHANGAMOTO YA MAZINGIRA KATIKA MDAHALO NA MKUTANO WA MAREJEO YA SHUGHULI ZA MRADI ULIOFANYIKA WILAYA YA IRINGA.

 Mkurugenzi Mtendaji wa LEAT Dk.Rugemeleza Nshala akifungua Mkutano wa marejeo wa Mradi wa CEGO na mdahalo uliowashirikisha viongozi wa serikali, wananchi na wadau wa maliasili mkoani Iringa.
 Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bi. Amina Masenza akihutubia na kufungua rasmi  Mkutano wa marejeo na Mdahalo uliotekelezwa na LEAT kupitia hisani ya watu wa Marekani -USAID
 Viongozi wa serikali ya wilaya ya Iringa na Mufindi wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa Bi. Amina Masenza na Muwakilishi kutoka USAID Bi. Joan Mayer.
 Timu ya Ufuatiliaji wa Uwajibikaji Jamii (UJJ/SAM) wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa serikali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bi. Amina Masenza (Katikati), Muwakilishi kutoka USAID Bi. Joan Mayer na Mkurugenzi Mtendaji wa LEAT Dk. Rugemeleza Nshala (Wa pili kulia)
 Timu ya utekelezaji wa mradi wa ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili (CEGO) wilaya ya Iringa na Mufindi wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa serikali na Muwakilishi kutoka USAID Bi. Joan baada ya Mgeni Rasmi Bi Amina Masenza kufungua Mdahalo huo.

Mhadhiri Mwandamizi Chuo kikuu cha kilimo Morogoro (SUA) Dk. Gimbage Mbeyale akitoa mada ya kwanza kuhusiana na Chanzo cha kukithiri kwa changamoto mbalimbali katika usimamizi wa misitu na wanyamapori


Ndugu. Leo Mavita akitoa mada ya pili katika mdahalo kuhusiana na ni nini chanzo na athari za kutengwa kwa bajeti ndogo kwenye halmshauri za wilaya kwa ajili ya sekta ya misitu na wanyamapori.

Afisa Mradi Mwandamizi wa mradi wa ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili (CEGO) Bw. Remmy Lema akitoa wasilisho la utukelezaji wa shughuli za mradi katika mkutano wa marejeo kwa wadau wa mradi na viongozi wa serikali mkoani Iringa.

 Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mufindi Mh. Festo Mgina akizungumza katika mkutano wa marejeo na mdahalo uliofanywa na LEAT kwa hisani ya watu wa Marekani USAID



 Bw. Jeremiah Daffa - Mhamasishaji wa mdahalo na mkutano wa marejeo uliofanywa na LEAT kwa hisani ya watu wa Marekani (USAID) 
 Mwenyekiti wa Timu ya SAM wilaya  ya Iringa Bw. Ngole Mwangosi  akisoma ripoti yao katika mkutano wa marejeo ya mradi wa ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili (CEGO)

Mkuu wa wilaya ya Iringa Mheshimiwa Richard Kasesela akihitimisha mdahalo kwa kutoa maoni yake juu ya mada zilizojadiliwa na washiriki kutoka serikalini, wadau wa maliasili na wananchi wa mkoa wa Iringa.
Serikali imepewa changamoto ya kutekeleza kikamilifu sheria za Mazingira, Maliasili na Wanyamapori kwa lengo la kupunguza au kumaliza kabisa matatizo yatokanayo na kutofuatwa kwa sheria hizo.
Changamoto  hiyo imetolewa na Timu ya Wanasheria watetezi wa Mazingira kwa vitendo (LEAT) wakati wa mdahalo maalum wa viongozi wa Serikali, wananchi na wadau wa Mazingira, Maliasili na Wanyapori Mkoa wa Iringa. Mdahalo huo ulifunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bi.Amina Masenza.
Akizungumza katika Mdahalo huo wa marejeo ya Mradi wa Ushiriki wa wananchi katika Usimamizi wa Maliasili (CEGO) wilaya za Iringa na Mufindi, Mkurugenzi Mtendaji wa LEAT, Dkt. Rugemeleza Nshala amesema licha ya mapungufu kidogo ya sheria hizo lakini zinao uwezo wa kulisaidia Taifa kuondokana na kero za matumizi yasiyo endelevu ya maliasili misitu na wanyama pori.
Awali, Mkuu wa wilaya Iringa amesema Mkoa wa Iringa unakabiliwa na changamoto kubwa ya kilimo cha mabondeni maarufu kama vinyungu na ugumu wa kuwaondoa watu hao unakuja pale inapokosekana shughuli mbadala watakayoifanya ili iwaingizie kipato.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, amesema juhudi za LEAT kutoa elimu kwa Wananchi ni nzuri kwa sababu zinasaidia kupunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Mhadhiri Mwandamizi Chuo kikuu cha kilimo Morogoro (SUA) Dk. Gimbage Mbeyale katika mdahalo huo alisema kuwa mabadiliko ya tabia ya nchi ni moja ya changamoto zinazokwamisha kuwepo kwa utunzaji na umuduji dumivu wa rasilimali misitu na wanyamapori.
Dk. Mbeyale alisema kuwa changamoto hizo zinasababishwa na uvunaji usiozingatia mpango wa usimamizi misitu sambamba na ongezeko la watu nchini kwa asilimia 3.2 toka milioni 11 kwa mwaka 1960 hadi milioni 56 kwa mwaka 2016.
“Migogoro kati ya mamlaka za hifadhi na wananchi (wakulima na wafugaji) ni changamoto za kuwepo kwa utunzaji na umuduji dumivu wa rasilimali misitu na wanyamapori nchini Tanzania” alisema Dk. Mbeyale
Naye msimamizi wa sekta ya Uchumi na Uzalishaji kutoka ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Leo Mavita, alisema kuwa kiini cha changamoto katika utunzaji na umuduji wa rasilimali misitu na wanyamapori ni kuwa na uwezo wa kuchanganua na kuelezea mahusiano yake na jamii na uchumi wake.

Saturday, November 26, 2016

LEAT YATEMEBELEWA NA WATAALAM KUTOKA CHEMONICS INTERNATIONAL - USAID KWAAJILI YA KUREKODI VIDEO YA MAFANIKIO YA SHUGHULI ZA MRADI WA CEGO


 


Kutoka Kulia ni Bi. Karina Keating (Meneja mradi Pamoja Twajenga), Remmy Lema (Afisa Mradi Mwandamizi -LEAT), M/Kiti wa MJUMIKIK na Bw. Hamza Chang'a (Mwanilishi wa kikundi cha utunzaji wa mazingira kijiji cha Kiwere) Musa Mnasizu (Afisa Mradi wa CEGO wilaya ya Iringa), Dk. Rugemeleza Nshala (Mkurugenzi Mtendaji -LEAT) na wawili kushoto ni wajumbe wa kikundi cha Utunzaji wa mazingira-Kiwere wakionyesha kitalu cha miti walichokianzisha baada ya kupata mafunzo ya usimamizi wa maliasili kutoka LEAT


 
 
 
 Bw. Mike Bennett akichukua video ya mazungumzo kati ya Dk. Nshala Mkurugenzi Mtendaji wa LEAT na Bw. Hamza Chang'a akiwa na wajumbe wenzake wa kikundi cha Utunzaji wa mazingira, wakielezea faida ya mafunzo ya usimamizi wa maliasili kutoka LEAT iliyowasukuma kuanzisha kitalu cha miti.


 Bw. Mike Bennett Mwandishi kutoka Chemonics International-USAID akichukua video ya wanakijiji wa Kijiji cha Kiwere waliokuwa wakikata mti ulioanguka baada ya kuungua na moto.


Bwana Mike Bennett Mwandishi kutoka Chemonics International- USAID akipiga picha eneo la kijiji lililopandwa miti kutoka katika kitalu cha miti ya Kikundi cha Utunzanji mazingira cha kijiji cha Kiwere

 
 Afisa Ughani wa Mradi wa Ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili (CEGO) wilaya ya Iringa akiwa na Bi. Karina Keating Meneja Mradi Chemonics International/Pamoja Twajenga katika ziara yao katika eneo lililopandwa miti na kikundi cha utunzaji mazingira katika ardhi ya kijiji cha Kiwere


Timu nzima ya mradi wa CEGO, Timu ya wataalamu kutoka Chemonics International-USAID na wanakikundi cha Utunzaji mazingira wa kijiji cha Kiwere wakizungukia eneo la ardhi ya kijiji lililopandwa miti na wanakikundi waliopatiwa mafunzo ya usimamizi wa maliasili kutoka LEAT kwa ufadhili wa USAID



 Kutoka Kushoto ni Bi. Karina Keating (Meneja-Pamoja Twajenga), Mike Bennett (Mwandishi-Chemonics International-USAID) , Dk. Rugemeleza Nshala (Murugenzi Mtendaji -LEAT) na Bi. Maria (Msimamizi wa miradi ya CEGO-Pamoja Twajenga) wakimrekodi Bw. Hamza Chan'ga aliyekuwa akielezea mafanikio ya elimu ya usimamizi wa maliasili kutoka LEAT Iliyowapelekea wanakijiji kuunda kikundi cha utunzaji wa mazingira na kuanzisha kitalu cha miti.



 
 





 Picha ya pamoja ya timu ya LEAT na wataalamu Kutoka Chemonics International baada ya kumaliza shughuli ya kurekodi simulizi za mafaniko zilizotokana na mradi wa ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili (CEGO) unaotekelezwa na LEAT kupitia ufadhili wa shirika la maendeleo la Kimataifa la Marekani - USAID

 
Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID) linaloifadhili LEAT katika mradi wa ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili (CEGO) walipendezwa na moja ya simulizi za mafaniko katika shughuli za mradi huu. Hivyo kutuma Afisa habari kutoka USAID-Chemonics International Ndugu Mike Bennett kuja kutembelea maeneo ya mradi yenye simulizi za mafanikio hayo. Mike Bennett aliongozana na Meneja Mradi  kutoka Pamoja Twajenga Bi. Karina Keating na Bi. Maria (Msimamizi wa asasi za miradi ya CEGO).

Timu hii ilitembelea kijiji cha Kiwere wilayani Iringa ambacho ni miongoni mwa vijiji vilivyopatiwa mafunzo ya Usimamizi wa maliasili, Ufuatiliaji wa uwajibikaji jamii (UJJ-SAM) na ufugaji nyuki yaliyowezeshwa na LEAT, Kijiji hiki kilionyesha matunda ya elimu waliyoipata kutoka LEAT kwa kuanzisha kikundi cha utunzanji wa mazingira huku lengo lao likiwa ni kutunza misitu inayoharibiwa kwa kasi kubwa katika maeneo yao.

 Miongoni mwa wanakijiji waliopatiwa mafunzo hayo katika kijiji cha Kiwere ni Bw. Hamza Hamis Chang’a  ambaye ni mwanzilishi na msimamizi wa shughuli za kikundi hiko. Bw. Hamza akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa LEAT na timu nzima ya mradi iliyotembelea kijiji hicho alisema, “kikundi hiki tulikianzisha baada ya kupata elimu nzuri ya usimamizi wa mazingira kutoka LEAT, tulipata muamko mkubwa wa kurejesha hali ya misitu yetu iliyoharibiwa kwa kiasi kikubwa, hivyo hatukutaka kuyalalia mafunzo hayo bali tulichukua jitihada za kuanzisha kikundi cha utunzanji wa mazingira kwa lengo la kutunza mazingira yaliyoharibiwa”

 Aliendelea “Jitihada zetu zilianza kwa kuanzisha kitalu cha miti. Tuliiomba halmshauri ya kijiji cha Kiwere itupatie eneo la wazi ili tupande miti hiyo. Kijiji kilitupatia eneo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari mbili ambapo ndipo tulipopanda miti hiyo”.

Aliongezea Bwana Hamza kuwa “LEAT imetuhamasisha kwa kiasi kikubwa katika suala la utunzaji wa mazingira, na kupitia kikundi tulichoanzisha chenye takribani ya wajumbe 17 hadi sasa, tunaweza kuhifadhi misitu na kukuza kipato chetu kutokana na miche ya miti tutanayoiuza, kwani mpaka sasa tumeshauza miche kadhaa na kujipatia fedha kidogo iliyotusaidia kununua mbegu na kuotesha miche mingine kisha kiasi kilichobaki tuligawana kama faida kwa wanakikundi wote.

 

Tuesday, November 22, 2016

LEAT YAIWEZESHA TIMU YA SAM YA WILAYA KUFANYA MREJESHO WA TAARIFA YA UFUATILIAJI WA UWAJIBIKAJI JAMII KWA VIONGOZI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA IRINGA.


 

 
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Richard Kasesela akizungumza baada ya kusikiliza mrejesho wa taarifa ya timu ya Ufuatiliaji wa uwajibikaji jamii (Timu ya SAM) ya wilaya inayowezeshwa na LEAT kupitia hisani ya watu wa Marekani (USAID)
 
 
 Mkuu wa Idara ya maliasili wa Wilaya ya Iringa Ndugu Dornald Mshani akitoa maoni yake baada ya kusikiliza mrejesho wa taarifa ya timu ya Ufuatiliaji wa uwajibikaji jamii (Timu ya SAM) ya wilaya inayowezeshwa na LEAT kupitia hisani ya watu wa Marekani (USAID)

 
Mkuu wa Idara ya Maliasili Ndg. Dornald Mshani (Kulia) na Afisa Misitu wa wilaya ya Iringa Ndg. Njoni (Kushoto) wakisikilza kwa makini na kuchukua taarifa ya mrejesho uliowasilishwa na Mwenyekiti wa timu ya SAM ya wilaya ya Iringa







 Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Richard Kasesela amepiga marufuku uvunaji wa mistu ya asili katika misitu ya hifadhi za vijiji vinavyozunguka wilaya yake bila ya barua kutoka ofisini kwake kama njia ya kukabiliana na vitendo vya uharibifu wa mazingira katika wilaya yake.

 Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa mrejesho wa Timu ya wilaya ya Ufuatiliaji wa uwajibikaji jamii (Timu ya SAM) kutoka wilaya ya Iringa inayoratibiwa na Timu ya  Wanasheria    Watetezi wa Mazingira (LEAT) kupitia hisani ya watu wa Marekani (USAID), Mh. Kasesela alisema hali ya uvunaji wa misitu kwa sasa inatisha kiasi cha kulifanya eneo hilo kuwa jangwa.

“Ninawashukuru sana (LEAT) kwa namna mlivyosaidia kutoa elimu kwa wananchi wangu, kwa sasa wamewezesha kukamatwa kwa magunia ya mkaa na mbao mfano katika kijiji cha Kiwere, na leo ninaagiza kuanzia sasa hakuna mtu atakayeruhusiwa kuvuna miti hadi hapo atakapokuwa na barua kutoka ofisini kwangu”alisema Mh. Kasesela.

 Mh. Kasesela alionya watumishi wa Halmashuari ya Iringa wanaohusika na utoaji vibali kwa ajili ya uvunaji wa misitu kuwa ni muhimu kushirikisha ofisi yake na kama hawatafanya hivyo atachukua hatua kali dhidi yao.

 Mkuu huyo wa wilaya aliagiza wajumbe wa kamati za mazingira wa vijiji kukamata watu wote wanaojihusisha na uharibifu wa mazingira wakiwamo  wenye vibali wasio na barua kutoka ofisini kwake bila kujali vyeo vyao.

 Mwenyekiti wa kamati za usimamizi wa mazingira wilaya ya Iringa Ngole Mwangosi alisema tangu kuanza kutekelezwa kwa mradi wa Ushiriki wa Usimamizi wa maliasili (CEGO) unaotekelezwa na LEAT kwa ufadhili wa USAID kumekuwa na ongezeko la wananchi kutoa taraifa za uharibifu wa maliasili katika maeneo yao.

“Katika kijiji cha Kitisi, baadhi ya wananchi waliokuwa wakijiita Mtajirungu  waliokuwa wakifanya uwindaji haramu kwa kutumia Mbwa na rungu (silaha za jadi) walidhibitiwa baada ya baadhi ya wananchi kutoa taarifa kwa maaskari wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

 Alisema sambamba na hilo bado wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali ikiwamo ya uelewa wa viongozi wa serikali za vijiji juu ya kile kinachodaiwa muingiliano wa majukumu kati ya serikali ya kijiji na  kamati za mazingira.

 Kwa upande wake Afisa miradi wa LEAT Musa Mnasizu, Alisema LEAT iliamua kutekeleza mradi huo kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata elimu na kutambua kuwa rasimali za asili zilizopo kijijini mwao wanawajibu wa kuzilinda na kunufaika nazo.

“Wengi walikuwa hawatambui kuwa rasimali za maliasili zilizopo katika maeneo yao kuwa si mali yao bali ni ya serikali jambo lilichangia wao kutojihusisha na jukumu la kuzilinda rasimali hizo ikiwamo misitu na wanyamapori”alisema Mnasizu.

Tuesday, November 8, 2016

Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imeidhinisha kuanza kutumika kwa sheria ndogo ya usimamizi wa maliasili

  Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa Bw. Stephen Mhapa, Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa na katibu tawala wa wilaya ya Iringa Bw. Joseph Chitika wakiongoza majadiliano katika mkutano wa baraza la wadiwani 
 
Mwanasheria mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Iringa Bi. Kissah Mbilla akifuatilia majadiliano ya baraza la madiwani wakati wa kupitisha sheria ndogo za vijiji 
 
 
Baadhi ya wajumbe na waandishi wa habari waliohudhuria mkutano wa baraza la madiwani wakifuatilia kwa makini kuidhinishwa kwa sheria ndogo za vijiji vya Mbweleli, Kinyali na Kinyika.
 
Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa Bw. Donald Mshani akihojiwa na waandishi wa habari baada ya baraza ya madiwani kuidhinisha sheria ndogo za vijiji husika   
 
 
Mwanasheria mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa Bi. Kissah Mbilla akihojiwa na waandishi wa habari baada ya baraza ya madiwani kuidhinisha sheria ndogo za vijiji husika 


Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imeidhinisha kuanza kutumika kwa sheria ndogo  za usimamizi wa maliasili ili kukabiliana na kasi ya uharibifu wa rasilimali za misitu na wanyamapori katika vijiji vitatu miongoni mwa vijiji ambavyo LEAT inatekeleza mradi wa ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili.

Sheria zilizoidhinishwa na halmashauri hiyo zimetungwa na halmashauri za vijiji vya Mbweleli, Kinyika na Kinyali chini ya msaada wa Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT),  lengo likiwa ni kudhibiti uharibifu wa mazingira unaokuwa kwa kasi katika vijiji hivyo.

Mara baada ya baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kuidhinisha kuanza kutumika kwa sheria hizo katika kikao cha baraza la madiwani  kilichoketi  tarehe 29/10/2016, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Stephen  Mhapa alisema sheria hizo zitasaidia kuongeza kasi ya utunzaji wa mazingira na wanyamapori katika vijiji husika.

Alisema Halmashauri za vijiji zina mamlaka kamili ya kutunga sheria ndogo zinazohusu usimamizi wa maeneo yao na kwamba sheria hizo zisipingane na sheria mama za nchi na Halmashauri husika.

“Kitendo cha halmashauri za vijiji kutunga sheria ndogo za kusimamia na kudhibiti uharibifu wa maliasili katika maeneo yao kimenifurahisha na kwamba kuanzia sasa misitu na wanyamapori waliokuwa katika hatari ya kutoweka kutokana na ujangili na uchomaji moto watakuwa salama”alisema Mhapa:

“Hiyo ni kutokana na wananchi wa eneo husika wao wenyewe kwa hiyari yao kujitungia sheria wanazoweza kuzisimamia, katika hili ninawashukuru Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa vitendo (LEAT) ambao wamewapatia elimu na msaada wa kufikia hatua hiyo ya kutunga sheria ndogo watakazoweza kuzisimamia wao wenyewe” alisema Mhapa.

Mwanasheria mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa Kissah Mbilla alisema jukumu la ofisi yake katika mchakato huo pamoja na kushirikiana na wanasheria wa LEAT ilikuwa kuhakikisha sheria hizo ndogo hazipingani na sheria mama ambayo ni ile ya Halmashauri na ya Nchi.

“Halmashauri ya kijiji inayo mamlaka ya kutunga sheria ndogo na ofisi yetu inachofanya ni kuangalia kama taratibu zimefuatwa, adhabu zinazotolewa katika sheria ndogo za kijiji hazizidi Tsh 50,000 na kwakuwa wamepitisha na baraza la madiwani limeidhinisha sheria hizi, sasa ni sheria kamili na zinaweza kuanza kutumika” alisema Mbilla.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili wa Halmashauri hiyo Donald Mshani alisema kuidhinishwa kwa sheria hizo kutasaidia idara yake kupambana na uharibifu wa mazingira ambao kwa sasa umekuwa ukishika kasi.

Alisema hatua hiyo inaweza kuwa ya mafanikio kutokana na sheria hizo tangu mchakato wa kutunga hadi kuidhinishwa na baraza la madiwani umeshirikisha wananchi katika kufikia malengo hayo.

Afisa habari wa Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) alisema hatua ya baraza la madiwani kuidhinisha kutumika kwa sheria hizo kumewafariji kwa kuwa jukumu lao la kuelimisha wananchi na kuwahamasisha kutunga sheria hizo linakuwa limetimia.

Edina Tibaijuka alisema LEAT kupitia mradi wa Ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili unaofadhiliwa na shirika la Kimataifa la watu wa Marekani (USAID) ilihamasisha halmashauri za vijiji vya Kinyali na Kinyika kutunga sheria ndogo hizo kwani awali hawakuwa nazo kabisa na kwa upande wa kijiji cha Mbweleli LEAT iliwawezesha Halmashauri ya kijiji hiko kufanya marekebisho ya sheria yao baada ya kuipitia na kuona sheria waliyokuwa wakiitumia awali ina mapungufu.


“Baada ya mikutano  mikuu ya vijiji hivyo kuridhia na kupitisha sheria hizo kuhusiana na maliasili ziliwasilishwa katika ofisi ya mwanasheria wa wilaya, kisha zilijadiliwa na kupitishwa na kamati husika za wilaya na kufikishwa katika baraza la madiwani ambao waliridhia kuanza kutumika kwa sheria hizo na kunatoa fursa kwa serikali za vijiji kuanza kuzitumia ili kudhibiti vitendo vya uharibifu wa mazingira” alisema. Tibaijuka.

Thursday, August 18, 2016

KAMPENI YA KUPINGA SHERIA KANDAMIZI ZA KIMILA ZINAZO KANDAMIZA HAKI YA MWANAMKE KUMILIKI ARDHI NA MALI


Timu ya Wanansheria Watetezi wa Mazingira kwa vitendo (LEAT) imeshiriki katika kampeni ya kupinga haki kandamizi za kimila zinazo kandamiza haki ya mwanamke kumiliki ardhi na mali ambayo inakinzana na katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu. Kampeni hiyo ili fanyika katika wilaya ya Kilindi mkoani Tanga na kuzinduliwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Mheshimiwa Saida Mtondoo ambaye alikuwa amefuatana na Katibu Tawala wa wilaya, Dkt. Filisi Nyimbi na Afisa Tarafa ya Kwekivu, Mgaya Nyake. Kampeni iliandaliwa na Asasi ya kiraia inayoshughulika na Utunzaji Mazingira na kutetea Haki za Mwanamke (Envirocare) na kushirikikisha Asasi za kiraia zinazo shughulika na utunzaji mazingira na utetezi wa haki za binadamu.

Akiongea wakati wa ufunguzi wa kampeni hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Envirocare, Mama Loyce Lema alisema sharia za kimila zimewanyima wanawake haki ya msingi ya kikatiba ya kumiliki ardhi na mali hivyo kuchangia ongezeko kubwa la wanawake masikini wakati wanawake wanachangia kwa kiasi kikubwa katika uzalishaji mali.

Mama Lema alisema kuwa tangu mwaka 2009 Asasi yake imekuwa ikielimisha wanawake juu ya haki ya kumiliki ardhi pamoja na haki ya kutumia mapato yanayotokana na nguvu zao, kwakuwa aliamini kuwa mwanamke akipewa haki ya kumiliki ardhi atahamasika kutunza mazingira. Mama Lema alisema kuwa wanawake wanapaswa kusimama na kudai haki ya kumiliki ardhi na mali kwa kuwa rasilimali hizo ni muhimu kwa ustawi wa jamii na ikizingatiwa kuwawanawake ndio walezi wakuu wa jamii na wanahitaji ardhi kwaajili ya kilimo, ufugaji na utunzaji mazingira.
Mkurugenzi Mtendaji wa Envirocare, Mama Loyce Lema (mwenye nguo ya bluu bahari)akifafanua jambo wakati wa mkutano wa wadau watetezi wa haki za wanawake. Mkutano ulifanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kilindi-Tanga, tarehe 17 Agosti, 2016.
 
Naye, Mkuu wa wilaya ya Kilindi, Saida Mtondoo alitoa wito kwa wanawake na wanaume waliopata elimu ya haki ya mwanamke kumiliki ardhi kutoa elimu hiyo kwa jamii iliwaachane na mila kandamizi. Mkuu wa wilaya alisema kuwa wanawake wanapaswa kuwa na umoja na utayari wa kuwasaidia wanawake watakao dhulumiwa haki ya kumiliki ardhi na mali ili kuwatia moyo kwakuwa inahitaji ushirikiano katika kuzishinda mila kandamizi na mfumo dume ulioota mizizi katika jamii.
Akielezea kifungu vinavyo tamka usawa kwa wanawake na wanaume katika kumiliki ardhi na mali, Mwanasheria wa Envirocare, Godlisten Maro alisema kuwa sharia za kimila zinakinzana na katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika ibara ya 13 inaeleza kuwa watu wote ni sawa mbele ya sharia. Pia katika ibara ya 27 inaeleza kuwa kila mtu ana haki ya kumiliki ardhi. Godlisten alisema kuwa kwakuwa ibara ya 107 ya katiba ya nchi inaeleza kuwa mahakama ndio chombo cha mwisho juu ya utoaji wa haki, na kwakuwa sharia za serikali zinatambua haki ya mwanamke kumiliki ardhi na mali, inapotokea shauri la kudai haki likitolewa hukumu mahakamani sharia ya serikali ndio itakayo fuatwa hata kama awali shauri hilo lilisuluhishwa kwa sharia ya kimila.
 

Picha ya pamoja ya washiriki wa mkutano uliojadili athari za sharia za kimila kandamizi zinazo kandamiza haki za wanawake kumiliki ardhi na mali. Mkutano huo ulifanyika siku moja kabla ya kampeni tarehe 17 Agosti, 2016, ilikutoa fursa kwa wadau washirikishana changamoto na uzoefu katika utatuzi wa mashauri ya haki za wanawake katika kumiliki ardhi na mali.
 
Aidha, Godlisten alisema kuwa sharia ya ardhi namba 4 ya mwaka 1999 kifungu cha 19 kina eleza kuwa mtu yeyote mwenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea ana haki ya kumiliki ardhi. Pia sharia ya ardhi ya vijiji ya namba 5 ya mwaka 1999 kifungu cha 3 kinaweka bayana kuwa wanawake wanahaki ya kumiliki ardhi. Kuhusu wanandoa kumiliki ardhi, Godlisten alisema kuwa kumekuwa na malalamiko mengi kuwa wanaume wengi waliopo katika ndoa wana miliki ardhi bila ya kushirikisha wake zao ilihali wamenunua pamoja ardhi husika. Sheria ya marekebisho ya ardhi ya mwaka 2004 inaruhusu wanandoa kumiliki ardhi pamoja kwasababu wote wanakuwa wamechangia kwa namna moja au nyingine katika kupatikana kwa ardhi, na ikitokea mwanandoa mmoja anataka kuuza au kuweka rehani lazima amshirikishe mwenzake.
 
Aliongeza kuwa haki ya mwanamke kumiliki mali inatambuliwa katika Mkataba wa Kimataifa wa kuondoa unyanyasaji kwa wanawake wa mwaka 1979, pia Mkataba wa Afrika wa haki za binadamu na haki za watu ibara ya 14 inasema kila mtu anahaki ya kumiliki mali. Tanzania imeridhia mikataba hii hivyo inapaswa kutetea haki za binadamu wote wake kwa waume.
Kuhusu mfumo dume, Godlisten alisema mfumo dume ni tatizo na umekwamisha kufikia malengo ya taifa ya kuhakikisha kuwa katika mabaraza ya ardhi ya vijiji, kata na wilaya yanakuwa na wajumbe wanawake 3 kati ya wajumbe 8 kwa mujibu wa sharia ya utatuzi wa migogoro ya ardhi ya mwaka 2002. Alisema wanaume katika maeneo mengi bado hawakubali kuwa wanawake wanaweza kuongoza, pia hata wanawake wenyewe hawajikubali kuwa wanaweza kuongoza, hii inatokea hasa wanawake wenzao wanapojitokeza kugombea nafasi mbalimbali.
Pia kulikuwa na shuhuda za simanzi kutoka kwa wanawake walio dhulumiwa ardhi na mali zao na waume zao baada ya ndo za kuvunjika na wengine wali dhulumiwa mali na ardhi na ndugu wa waume zao baada ya kufariki.
 
Washiriki walikuwa wamebeba jumbe mbalimbali kama ‘Wanawake washirikishwe katika mabaraza ya utatuzi wa migogoro ya ardhi, Pinga mila potofu mmilikishe mwanamke ardhi, Mwanamke kumiliki ardhi ni haki yake ya kikatiba, Sheria kandamizi za kimila hazizingatii katiba, Ardhi ni mali na Sheria za kimila zitoe fursa sawa.
 
Kampeni hiyo ilihudhuriwa na Asasi za kiraia ikiwemo LEAT, WILAC, LHRC, TAMWA, EFD, Action Aid, Mtandao wa jinsia na taasisi za serikali Tume ya kurekebisha sharia, Chama cha Wanasheria Tanganyika, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Wizara ya Ardhi, Dawati la jinsia la kituo cha polisi Songe, Viongozi wa dini, Wazee wa mila na wananchi.
 
 
 
 
 
 
Maandamano yalianzia ofisi za halmashauri ua Kilindi kelekea viwanja vya stendi ya mabasa ya Songe
 

Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu pamoja na wananchi katika matembezi kutoka ofisi za halmashauri kuelekea viwanjavya stendi ya mabasi Songe
 


Katibu Tawala wa wilaya ya Kilindi Dkt. Filisi Nyimbi(aliyeshika bango kushoto) akionesha wananchi bango lililopinga sharia kandamizi za kimila zinazo kandamiza haki za wanawake katika kumiliki ardhi na mali.


Baadhi ya wananchi katika kampeni

 

Saturday, August 6, 2016

WANANCHI WA KIJIJI CHA LUDILO WAPITISHA SHERIA NDOGO YA USIMAMIZI WA MALIASILI

Ludilo, Mufindi-Iringa

Wananchi wa kijiji cha Ludilo wilayani Mufindi, mkoani Iringa wamepitisha sheria ndogo ya usimamizi wa maliasili (misitu na wanyamapori) ilikukabiliana na kasi ya uharibifu wa rasilimali hizo. Hatua hiyo ilifikiwa tarehe 4 Augusti, 2016 katika mkutano wa hadhara ambapo Diwani wa kata ya Mdabulo Mheshimiwa Henry Nyeho pamoja na Mwanasheria wa Wilaya ya Mufindi Leonard Jaka walihudhuria mkutano huo.

Sheria iliyopitishwa na wananchi hao ndio itakayotumika katika usimamizi wa maliasili. Mchakato wa uboreshaji sheria ulianza mwezi Juni, 2016 ambapo Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) kwa kushirikiana na Mwanasheria wa Wilaya ya Mufidni pamoja na wananchi hao, kupitia mkutano wa hadhara waliangalia upya sheria iliyokuwa ikitumika kijijini hapo na kugundua kuwa ilikuwa na mapungufu.

 

 
 

Wananchi wakiongozwa na Wanasheria kutoka LEAT na Mwanasheria wa Wilaya Mufindi walitoa mapendekezo ya maboresho na kuiruhusu timu ya LEAT kuchapisha sharia hiyo mpya ambayo iliwasilishwa tarehe 4 August 2016. Mtendaji wa kijiji cha Ludilo bwana Martin Mwanule alisoma kipengele kimoja baada ya kingine kupitishwa na wananchi.

Sheria hiyo inaelekeza haki na wajibu wa wananchi, serikali ya kijiji, kamati ya maliasili pamoja na timu ya Ufuatiliaji Uwajibikaji Jamii. Pia sharia imefafanua adhabu zitakazotolewa kwa watu watakao kiuka sharia na kuharibu maliasili. Hii ni awamu ya kwanza ya kuzijengea uwezo serikali za vijiji wa kuunda sharia ndogo za kusimamia maliasili. Katika awamu hii vijiji vya Ludilo, Ikangamwani na Kibada kwa wilaya ya Mufindi ndivyo vitakavyo fikiwa, kwa wilaya ya Iringa ni vijiji vya Mbweleli, Kinyika na Kinyali.

Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) inatekeleza mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili katika vijiji 32 vya wilaya za Iringa na Mufindi mkoani Iringa. Mradi huu umefadhiliwa na Watu wa MArekani kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la MArekani (USAID). Lengo la mradi ni kuzijengea uwezo jamii zinazoishi karibu na rasilimali misitu na wanyamapori, iliwaweze kuzisimamia na kunufaika nazo. Mradi unatoa mafunzo ya sharia, sera miongozo, kanuni na Ufuatiliaji uwajibikaji jamii kwa kamati za vijiji za maliasili na mazingira, uchumi, maji na matumizi ya ardhi. Pia mradi umetoa mafunzo kwa wananchi, Madiwani, Maafisa Maliasili wa wilaya na Asasi za kiraia. Takriban wananchi 6500 watafikiwa na mafunzo hayo.
Mradi pia umetoa mafunzo ya ufugaji nyuki kwa wananchi 704 katika vijiji 32 pamoja na kugawa mizinga ya kufugia nyuki na vifaa vya kujikinga na nyuki wakati wa kurina asali. lengo ni kuwapa wananchi kipato mbadala ili kupunguza utegemezi wa kipato kutokana na ukataji miti.

Katika kutimiza azma ya kutoa elimu ya usimimizi wa maliasili kwa wananchi wengi, LEAT inatoa mafunzo kwa njia ya redio kupitia Nuru FM, sambamba na kutoa elimu kwa njia ya Sanaa. LEAT ina vikundi viwili vya sanaa; kikundi cha Sanaa Mashujaa kwa wilaya ya Iringa na kikundi cha Sanaa Mapogoro kwa wilaya ya Mufindi.
Wananchi wa Ludilo katika mkutano wa kupitisha sharia za usimamizi wa maliasili
Mwanasheria wa Wilaya ya Mufindi, Leonard Jaka akitoa ufafanuzi kabla ya kupitishwa kwa sharia ndogo ya usimamizi wa maliasili
 

 

Monday, July 18, 2016

KUJITATHMINI- LEAT YAFANYA TATHMINI YA UCHECHEMUZI


Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) imefanya tathmini kwa Asasi nne ili kupima kiwango cha uchechemuzi (ushawishi) cha Asasi hizo ambazo ni washirika wa utekelezaji wa mradi wa ‘Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili’ unaotekelezwa katika vijiji 32 vya wilaya za Iringa na Mufindi Mkoani Iringa, kwa ufadhili wa Watu wa Marekani. Tathmini ilifanyika mwishoni mwa mwezi Juni, 2016 kwa Asasi za ASH-TECH na MUVIMA za Wilaya ya Mufindi; na kwa Wilaya ya Iringa ni MBOMIPA na MJUMIKK.
Tathmini hiyo ili lenga kuangalia iwapo agenda za uchechemuzi zimepewa kipaumbele ili kufikia malengo ya mradi, pia kuangalia endapo mipango hiyo imehusisha mambo muhimu ikiwa ni pamoja na kujumuisha wanawake na makundi yenye mahitaji maalum; ili kuyafikia makundi yote katika jamii.
Kutoka kushoto: Afisa Ugani wa LEAT, Hana Lupembe; Mwasibu wa MJUMIKK, Aidan Mkusa; Mratibu-MJUMIKK, Simon Komba; Katibu Mkuu-MJUMIKK, Mashaka Kilanga; Mchungaji Ombeni, Mjumbe wa MJUMIKK na Afisa Mradi wa LEAT, Musa Mnasizu.
Zaidi tathmini hiyo ili lenga kubaini endapo wadau wa utekelezaji uchechemuzi ikiwa ni pamoja na wafanyakazi na bodi za Asasi, wananchi na taasisi washirika wanafahamu na wanashiriki katika uainishaji na utekelezaji wa agenda za uchechemuzi.
Hatua hiyo ni muhimu kwa LEAT na Asasi hizo kwa kuwa mafanikio ya mradi yana changiwa na utekelezaji thabiti wa mipango ya uchechemuzi ambayo hutumika kutatua changamoto zinazo ikabili sekta za misitu na wanyamapori, kwa kutumia njia mbali mbali ikiwa ni pamoja na kushinikiza wafanyamaamuzi kuchukua hatua juu ya changamoto hizo.
Kutoka kulia, Afisa Mradi wa LEAT, Musa Mnasizu; Mjumbe wa MJUMIKK,Mchungaji Ombeni; Ktibu Muu wa MJUMIKK, Mashaka Kilanga an Mratibu wa MJUMIKK, Simon Komba
Kutoka kushoto: Afisa Mradi wa MUVIMA,Winnie Moses; Mkurugenzi Msaidizi wa MUVIMA, Speratus Mbeyela; Mkurugenzi- MUVIMA, Albert Chalamila; na Afisa Mradi wa LEAT- Jamal Juma
Baada ya siku sita za tathmini ya uchechemuzi, LEAT pamoja na Asasi waliainisha mapungufu yaliyoonekana katika mikakati ya uchechemuzi, na walipendekeza njia za kuboresha.
LEAT ili jengewa uwezo na Mtaalamu wa Uchechemuzi Tobias Chelechele kutoka Shirika la Pamoja Twajenga, ambao ni wakala wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID). Mradi wa ‘Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili’ unahusu rasilimali misitu na wanyamapori.
Takriban wananchi 6500 watanufaika na mradi huo. Mradi unatoa mafunzo ya usimamizi wa misitu, wanyamapori na ufuatiliaji uwajibikaji jamii, ili kuzijengea uwezo jamii kusimamia, kulinda na kuhoji viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali misitu na wanyamapori. Ili kufikia wananchi wengi, LEAT inaendelea kutoa elimu kwa njia ya Sanaa kupitia vikundi viwili vya Sanaa, makala za magazeti na programu za vipindi vya redio. Kwa kuwa mradi umelenga kujenga misingi ya utawala bora katika sekta ya misitu na wanyamapori, LEAT inatoa mafunzo kwa viongozi wa Vijiji, Madiwani, Wananchi, Maafisa misitu na wanyamapori.