Wananchi wa kijiji cha Ludilo wilayani Mufindi,
mkoani Iringa wamepitisha sheria ndogo ya usimamizi wa maliasili (misitu na
wanyamapori) ilikukabiliana na kasi ya uharibifu wa rasilimali hizo. Hatua hiyo
ilifikiwa tarehe 4 Augusti, 2016 katika mkutano wa hadhara ambapo Diwani wa
kata ya Mdabulo Mheshimiwa Henry Nyeho pamoja na Mwanasheria wa Wilaya ya
Mufindi Leonard Jaka walihudhuria mkutano huo.
Sheria iliyopitishwa na wananchi hao ndio itakayotumika
katika usimamizi wa maliasili. Mchakato wa uboreshaji sheria ulianza mwezi
Juni, 2016 ambapo Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT)
kwa kushirikiana na Mwanasheria wa Wilaya ya Mufidni pamoja na wananchi hao,
kupitia mkutano wa hadhara waliangalia upya sheria iliyokuwa ikitumika kijijini
hapo na kugundua kuwa ilikuwa na mapungufu.
Wananchi wakiongozwa na Wanasheria kutoka LEAT na Mwanasheria
wa Wilaya Mufindi walitoa mapendekezo ya maboresho na kuiruhusu timu ya LEAT
kuchapisha sharia hiyo mpya ambayo iliwasilishwa tarehe 4 August 2016. Mtendaji
wa kijiji cha Ludilo bwana Martin Mwanule alisoma kipengele kimoja baada ya
kingine kupitishwa na wananchi.
Sheria hiyo inaelekeza haki na wajibu wa wananchi,
serikali ya kijiji, kamati ya maliasili pamoja na timu ya Ufuatiliaji
Uwajibikaji Jamii. Pia sharia imefafanua adhabu zitakazotolewa kwa watu watakao
kiuka sharia na kuharibu maliasili. Hii ni awamu ya kwanza ya kuzijengea uwezo
serikali za vijiji wa kuunda sharia ndogo za kusimamia maliasili. Katika awamu
hii vijiji vya Ludilo, Ikangamwani na Kibada kwa wilaya ya Mufindi ndivyo vitakavyo fikiwa, kwa wilaya
ya Iringa ni vijiji vya Mbweleli, Kinyika na Kinyali.
Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo
(LEAT) inatekeleza mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili
katika vijiji 32 vya wilaya za Iringa na Mufindi mkoani Iringa. Mradi huu
umefadhiliwa na Watu wa MArekani kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la
MArekani (USAID). Lengo la mradi ni kuzijengea uwezo jamii zinazoishi karibu na
rasilimali misitu na wanyamapori, iliwaweze kuzisimamia na kunufaika nazo.
Mradi unatoa mafunzo ya sharia, sera miongozo, kanuni na Ufuatiliaji
uwajibikaji jamii kwa kamati za vijiji za maliasili na mazingira, uchumi, maji
na matumizi ya ardhi. Pia mradi umetoa mafunzo kwa wananchi, Madiwani, Maafisa Maliasili wa wilaya na Asasi
za kiraia. Takriban wananchi 6500 watafikiwa na mafunzo hayo.
Mradi pia umetoa mafunzo ya ufugaji nyuki kwa wananchi 704 katika vijiji 32 pamoja na kugawa mizinga ya kufugia nyuki na vifaa vya kujikinga na nyuki wakati wa kurina asali. lengo ni kuwapa wananchi kipato mbadala ili kupunguza utegemezi wa kipato kutokana na ukataji miti.
Katika kutimiza azma ya kutoa elimu ya usimimizi wa
maliasili kwa wananchi wengi, LEAT inatoa mafunzo kwa njia ya redio kupitia
Nuru FM, sambamba na kutoa elimu kwa njia ya Sanaa. LEAT ina vikundi viwili vya sanaa; kikundi cha Sanaa Mashujaa
kwa wilaya ya Iringa na kikundi cha Sanaa Mapogoro kwa wilaya ya Mufindi.
Mwanasheria wa Wilaya ya Mufindi, Leonard Jaka akitoa ufafanuzi kabla ya kupitishwa kwa sharia ndogo ya usimamizi wa maliasili
No comments:
Post a Comment