Thursday, August 18, 2016

KAMPENI YA KUPINGA SHERIA KANDAMIZI ZA KIMILA ZINAZO KANDAMIZA HAKI YA MWANAMKE KUMILIKI ARDHI NA MALI


Timu ya Wanansheria Watetezi wa Mazingira kwa vitendo (LEAT) imeshiriki katika kampeni ya kupinga haki kandamizi za kimila zinazo kandamiza haki ya mwanamke kumiliki ardhi na mali ambayo inakinzana na katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu. Kampeni hiyo ili fanyika katika wilaya ya Kilindi mkoani Tanga na kuzinduliwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Mheshimiwa Saida Mtondoo ambaye alikuwa amefuatana na Katibu Tawala wa wilaya, Dkt. Filisi Nyimbi na Afisa Tarafa ya Kwekivu, Mgaya Nyake. Kampeni iliandaliwa na Asasi ya kiraia inayoshughulika na Utunzaji Mazingira na kutetea Haki za Mwanamke (Envirocare) na kushirikikisha Asasi za kiraia zinazo shughulika na utunzaji mazingira na utetezi wa haki za binadamu.

Akiongea wakati wa ufunguzi wa kampeni hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Envirocare, Mama Loyce Lema alisema sharia za kimila zimewanyima wanawake haki ya msingi ya kikatiba ya kumiliki ardhi na mali hivyo kuchangia ongezeko kubwa la wanawake masikini wakati wanawake wanachangia kwa kiasi kikubwa katika uzalishaji mali.

Mama Lema alisema kuwa tangu mwaka 2009 Asasi yake imekuwa ikielimisha wanawake juu ya haki ya kumiliki ardhi pamoja na haki ya kutumia mapato yanayotokana na nguvu zao, kwakuwa aliamini kuwa mwanamke akipewa haki ya kumiliki ardhi atahamasika kutunza mazingira. Mama Lema alisema kuwa wanawake wanapaswa kusimama na kudai haki ya kumiliki ardhi na mali kwa kuwa rasilimali hizo ni muhimu kwa ustawi wa jamii na ikizingatiwa kuwawanawake ndio walezi wakuu wa jamii na wanahitaji ardhi kwaajili ya kilimo, ufugaji na utunzaji mazingira.
Mkurugenzi Mtendaji wa Envirocare, Mama Loyce Lema (mwenye nguo ya bluu bahari)akifafanua jambo wakati wa mkutano wa wadau watetezi wa haki za wanawake. Mkutano ulifanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kilindi-Tanga, tarehe 17 Agosti, 2016.
 
Naye, Mkuu wa wilaya ya Kilindi, Saida Mtondoo alitoa wito kwa wanawake na wanaume waliopata elimu ya haki ya mwanamke kumiliki ardhi kutoa elimu hiyo kwa jamii iliwaachane na mila kandamizi. Mkuu wa wilaya alisema kuwa wanawake wanapaswa kuwa na umoja na utayari wa kuwasaidia wanawake watakao dhulumiwa haki ya kumiliki ardhi na mali ili kuwatia moyo kwakuwa inahitaji ushirikiano katika kuzishinda mila kandamizi na mfumo dume ulioota mizizi katika jamii.
Akielezea kifungu vinavyo tamka usawa kwa wanawake na wanaume katika kumiliki ardhi na mali, Mwanasheria wa Envirocare, Godlisten Maro alisema kuwa sharia za kimila zinakinzana na katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika ibara ya 13 inaeleza kuwa watu wote ni sawa mbele ya sharia. Pia katika ibara ya 27 inaeleza kuwa kila mtu ana haki ya kumiliki ardhi. Godlisten alisema kuwa kwakuwa ibara ya 107 ya katiba ya nchi inaeleza kuwa mahakama ndio chombo cha mwisho juu ya utoaji wa haki, na kwakuwa sharia za serikali zinatambua haki ya mwanamke kumiliki ardhi na mali, inapotokea shauri la kudai haki likitolewa hukumu mahakamani sharia ya serikali ndio itakayo fuatwa hata kama awali shauri hilo lilisuluhishwa kwa sharia ya kimila.
 

Picha ya pamoja ya washiriki wa mkutano uliojadili athari za sharia za kimila kandamizi zinazo kandamiza haki za wanawake kumiliki ardhi na mali. Mkutano huo ulifanyika siku moja kabla ya kampeni tarehe 17 Agosti, 2016, ilikutoa fursa kwa wadau washirikishana changamoto na uzoefu katika utatuzi wa mashauri ya haki za wanawake katika kumiliki ardhi na mali.
 
Aidha, Godlisten alisema kuwa sharia ya ardhi namba 4 ya mwaka 1999 kifungu cha 19 kina eleza kuwa mtu yeyote mwenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea ana haki ya kumiliki ardhi. Pia sharia ya ardhi ya vijiji ya namba 5 ya mwaka 1999 kifungu cha 3 kinaweka bayana kuwa wanawake wanahaki ya kumiliki ardhi. Kuhusu wanandoa kumiliki ardhi, Godlisten alisema kuwa kumekuwa na malalamiko mengi kuwa wanaume wengi waliopo katika ndoa wana miliki ardhi bila ya kushirikisha wake zao ilihali wamenunua pamoja ardhi husika. Sheria ya marekebisho ya ardhi ya mwaka 2004 inaruhusu wanandoa kumiliki ardhi pamoja kwasababu wote wanakuwa wamechangia kwa namna moja au nyingine katika kupatikana kwa ardhi, na ikitokea mwanandoa mmoja anataka kuuza au kuweka rehani lazima amshirikishe mwenzake.
 
Aliongeza kuwa haki ya mwanamke kumiliki mali inatambuliwa katika Mkataba wa Kimataifa wa kuondoa unyanyasaji kwa wanawake wa mwaka 1979, pia Mkataba wa Afrika wa haki za binadamu na haki za watu ibara ya 14 inasema kila mtu anahaki ya kumiliki mali. Tanzania imeridhia mikataba hii hivyo inapaswa kutetea haki za binadamu wote wake kwa waume.
Kuhusu mfumo dume, Godlisten alisema mfumo dume ni tatizo na umekwamisha kufikia malengo ya taifa ya kuhakikisha kuwa katika mabaraza ya ardhi ya vijiji, kata na wilaya yanakuwa na wajumbe wanawake 3 kati ya wajumbe 8 kwa mujibu wa sharia ya utatuzi wa migogoro ya ardhi ya mwaka 2002. Alisema wanaume katika maeneo mengi bado hawakubali kuwa wanawake wanaweza kuongoza, pia hata wanawake wenyewe hawajikubali kuwa wanaweza kuongoza, hii inatokea hasa wanawake wenzao wanapojitokeza kugombea nafasi mbalimbali.
Pia kulikuwa na shuhuda za simanzi kutoka kwa wanawake walio dhulumiwa ardhi na mali zao na waume zao baada ya ndo za kuvunjika na wengine wali dhulumiwa mali na ardhi na ndugu wa waume zao baada ya kufariki.
 
Washiriki walikuwa wamebeba jumbe mbalimbali kama ‘Wanawake washirikishwe katika mabaraza ya utatuzi wa migogoro ya ardhi, Pinga mila potofu mmilikishe mwanamke ardhi, Mwanamke kumiliki ardhi ni haki yake ya kikatiba, Sheria kandamizi za kimila hazizingatii katiba, Ardhi ni mali na Sheria za kimila zitoe fursa sawa.
 
Kampeni hiyo ilihudhuriwa na Asasi za kiraia ikiwemo LEAT, WILAC, LHRC, TAMWA, EFD, Action Aid, Mtandao wa jinsia na taasisi za serikali Tume ya kurekebisha sharia, Chama cha Wanasheria Tanganyika, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Wizara ya Ardhi, Dawati la jinsia la kituo cha polisi Songe, Viongozi wa dini, Wazee wa mila na wananchi.
 
 
 
 
 
 
Maandamano yalianzia ofisi za halmashauri ua Kilindi kelekea viwanja vya stendi ya mabasa ya Songe
 

Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu pamoja na wananchi katika matembezi kutoka ofisi za halmashauri kuelekea viwanjavya stendi ya mabasi Songe
 


Katibu Tawala wa wilaya ya Kilindi Dkt. Filisi Nyimbi(aliyeshika bango kushoto) akionesha wananchi bango lililopinga sharia kandamizi za kimila zinazo kandamiza haki za wanawake katika kumiliki ardhi na mali.


Baadhi ya wananchi katika kampeni

 

No comments:

Post a Comment