Vikundi 32 vya ufugaji nyuki vya wilaya za Iringa na
Mufindi vyapatiwa elimu ya ujasiriamali wa mazao ya nyuki ili kuwawezesha
kufanya ujasiriamali bora na kuleta tija katika soko shindani la bidhaa za
nyuki (asali na nta).
Vikundi hivyo vilipatiwa mafunzo ya siku tatu na
Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) kwa kushirikiana na
Mtaalamu wa kujitegemea wa Ujasiriamali, Rogasian Mtana. Wanavikundi hao
walipatiwa mafunzo kwa nyakati tofauti ambapo walijengewa uwezo wa kutambua
asali iliyoiva, urinaji bora (uvunaji wa asali) unaofuata njia za kitaalam na
rafiki kwa mazingira pamoja na njia bora za uchakataji asali ilikukidhi viwango
bora vya asali na nta.
Katika kuhakikisha kuwa vikundi hivyo vinapata
masoko ya asali na nta, ndani na nje ya Tanzania, vikundi vilielekezwa njia
sahihi za kufuata ilikupata vibali vya usindikaji ikiwa ni pamoja na kupata
kibali kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Chakula na Dawa (TFDA).
Pia walifundishwa namna bora ya uhifadhi, usindikaji
na ubinifu wa lebo na alama ambazo hutoa taarifa juu ya viambato, viwango vya
ubora, uzito wa asali, tarehe ya uchakataji na ufungashaji na mahali ilipotoka.
Katika kuhakikisha kuwa asali na nta zinaendelea
kuwa katika viwango vya juu vya ubora, vikundi vilifundisha njia sahihi za
usafirishaji wa bidhaa zao. Pia walijifunza namna ya kutafuta masoko ikiwa ni
pamoja na utoaji huduma bora kwa mteja, pia walipewa orodha ya makampuni
yanayofanya biashara ya asali na nta.
Ilikuwasaidia wanavikundi kuwa na biashara endelevu
na zenye tija, wawezeshaji wa mafunzo walitoa mafunzo ya utunzaji wa fedha na
kumbukumbu. Wanavikundi pia walielekezwa namna ya kuandika katiba za vikundi
vyao iliwaweze kuvisajili kisheria na kufungua akaunti za benki kwaajili ya
kutunza fedha zao.
Mafunzo hayo ya ujasiriamali katika mazao ya nyuki
ndio yamekamilisha programu ya mafunzo ya ufugaji nyuki. Awali vikundi hivyo
vilipatiwa mafunzo ya ufugaji nyuki pamoja na kupewa mizinga ya kufugia nyuki
na vifaa vya kujikinga na nyuki. Kila wilaya ina vikundi 16 ambapo kila kikundi
kina watu 22.
Kukamilika kwa mafunzo ya ufugaji nyuki kutasaidia
kufika malengo ya mradi ya kupunguza utegemezi wa rasilimali misitu na
wanyamapori kwa jamii zinazoishi karibu na rasilimali hizo; kwa kuwapatia
vyanzo mbadala vya mapato.
LEAT inatekeleza mradi wa ‘Ushiriki wa Wananchi
katika Usimamizi wa Maliasili’, kwa kushirikiana na Asasi za kiraia za MUVIMA
na ASH-TECH kwa wilaya ya Mufindi; na Asasi za MJUMIKK na MBOMIPA kwa wilaya ya
Iringa. Mradi unatekelezwa katika vijiji 32 kwa ufadhili wa Watu wa Marekani
kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID).
Wanawake walioamua kufanya ujasiriamali wa mazao ya nyuki -wakiwa katika kazi za kikundi wakati wa mafunzo
Wanakikundi wakijadili jinsi ya kutafuta masoko na mbinu bora za utoaji huduma kwa mteja
Tutatoka tu: Wanakikundi wakijadili usanifu wa lebo nzuri kwaajili ya asali
Mwanakikundi akiangalia chujio ya asali wakati wa mafunzo
Ubunifu: Mmoja wa wanakikundi akisaniu lebo ya asali wakati wa kazi za kikundi za majaribio
Mwanakikundi akichora lebo kwaajili ya vifungashio vya asali
Washiriki wa mafunzo ya ujasiriamali wa mazao ya nyuki wilayani Mufindi
Mshiriki wa mafunzo akiangalia chujio ya asali
Katika picha ya pamoja ni Wanavikundi vya ufugaji nyuki walio hudhuria mafunzo ya ujasiriamali wa mazao ya nyuki wilayani Iringa
No comments:
Post a Comment