LEAT YAWAASA WANANCHI
KUSHIRIKI KIKAMILIFU KATIKA UHIFADHI WA MAZINGIRA NA MALIASILI
Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT)
imewaasa wananchi kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa mazingira na
maliasili kwa ustawi wa taifa. Nasihi hizo ilitolewa na Afisa Mawasiliano wa
LEAT, Miriam Mshana wakati wa maadhimisho ya siku ya mazingira duniani
yaliyofanyika kijijini Lugoda Lutali katika ngazi ya wilaya ya Mufindi, mkoani
Iringa.
Katika utunzaji wa mazingira, Miriam alisema kuwa uharibifu wa
mazingira umechangiwa kwa sehemu kubwa na shughuli za binadamu ikiwa ni pamoja
na ukataji miti ovyo, utupaji taka ngumu na zenye sumu ambao umeathiri mandhari ya miji yetu na kuchangia ongezeko la magonjwa ya njia ya hewa, kuhara na kipindupindu.
Miriam alisema, utupaji taka ngumu na zenye sumu karibu na
makazi ya watu na vyanzo vya maji, umeleta athari kubwa kiafya kwakuwa kemikali
hizo hupenya ardhini na kudhuru ardhi na vyanzo vya maji, hasa kwa wananchi
wanoishi karibu na viwanda na sehemu za uchimbaji madini.
“Inasikitisha kuwa
wamiliki wa viwanda vingi na machimbo ya madini wanakiuka sheria ya mazingira
lakini pia wameshindwa kuwajibika kwa jamii zinazo wazunguka ambazo ndio wadau
wakubwa wa biashara zao, kwa kaidi kuchukua hatua za kuzuia uharibifu wa
mazingira hata baada ya athari kutokea”, alisema Miriam. Aliongeza kuwa shirika
la LEAT limekuwa mstari wa mbele kwa zaidi ya miaka 20, katika kusimamia
mazingira nchini katika sekta ya madini, viwanda, na mazingira kwa ujumla.
Aliongeza kuwa mamlaka zilizopewa jukumu la kusimamia mazingira zimekuwa na uzito katika utekelezaji wa majukumu yake hali hiyo inatoa mwanya kwa watu kukiuka sharia za uhifadhi wa mazingira.
Kumekuwa na malalamiko mengi na hata madhara yaliyowapata wananchi yanayotokana na uzembe makusudi wa utiririshaji wa maji yenye sumu katika makazi ya watu, lakini matukio mengi yanafumbiwa macho.
Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO)
iliyotolewa mwezi Aprili, 2016 inaonesha takribani watu milioni 2 hufa kila
mwaka duniani na zaidi ya watu bilioni moja hupatwa na magonjwa yanayo
sababishwa na uchafuzi wa mazingira, alisema Miriam.
Iwapo serikali, wananchi na wamiliki wa viwanda na machimbo
ya madini, kila mmoja akitimiza wajibu wa kutunza mazingira tutakuwa natekeleza
haki ya kuishi, haki ya afya bora na ustawi, kama ambavyo serikali ilivyo
ridhia katika mikataba mbalimbali ya kimataifa ikiwemo mkataba wa Stockholm
nchini Sweden na Rio De janeiro nchini
Brazil.
LEAT kama taasisi kubwa ya Wanansheria Watetezi wa Mazingira
nchini inatoa wito kwa mamlaka za usimamizi wa mazingira na maliasili kutimiza
wajibu wao kwakuwa serikali imewaamini na kuwapa jukumu hilo. Kwakufanya hivyo
tutakuwa tunaitikia wito wa kaulimbiu ya mwaka 2016 ya siku ya mazingira
duniani-‘Shiriki kufanya dunia mahali pazuri’.
Kuhusu usimamizi wa maliasili, Miriam alisema Alisema,
uvunaji wa kasi hasa wa misitu umeathiri na kuchangia mabadiliko ya tabia nchi,
kuiweka nchi katika hatari ya kuwa jangwa. Uvunaji haramu wa wanyamapori
hususan tembo umeipa hasara taifa.
Aliongeza kuwa kwa
mujibu wa ripoti ya Mtaalam Mashuhuri wa tafiti za tembo duniani, Ian Douglas
Hamilton, kwa mara ya kwanza mwaka 1976 alifanya utafiti wa angani, Tanzania
kwa ujumla ilikuwa na tembo 316,000, ambayo ilikuwa idadi kubwa sana
ikilinganishwa na maeneo mengine duniani.
Mwaka 1976, mbuga ya Selou pamoja na maeneo jirani ilikuwa
na idadi ya tembo109,000. Utafiti uliofanywa mwaka 2013, ulibaini kuwa mbuga ya
Selou ilikuwa na tembo 13,084 pekee.
Takwimu hizo zinaashiria hatari ya kutoweka kabisa kwa tembo
katika nchi yetu na itaathiri biashara ya utalii ambayo ilikuwa ikitoa mchango
mkubwa katika pato la taifa.
Sherehe za siku ya mazingira duniani zilizofanyika wilayani
Mufindi tarehe 3 Juni 2016 na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jowika
Kasugo, Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Asumpta Mshama, Mkuu wa Wilaya ya
Mbarali, ; pamoja na mashirika ya TANAPA, WCS, WWF, SPANEST, LEAT na wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Wanging'ombe, Mh. Asumpta Mshama akiongea na wananchi wakati wa maadhimisho ya siku ya mazingira duniani.
Mwananchi akitia saini baada ya kupokea kitabu cha utunzaji wa misitu, kilicho tolewa na LEAT
No comments:
Post a Comment