Ndugu. Tundu Antiphas Mughwai Lissu
Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT)
imepokea kwa mshituko na simanzi kubwa jaribio la kumuua Ndugu Tundu Antiphas
Mughwai Lissu huko Dodoma mnamo tarehe 7 Septemba 2017. Jaribio hilo si tu ni
la kinyama bali lilitendwa kwa lengo moja tu, kumuua Ndugu Lissu.
Waliotenda jaribio hilo, na wale waliowatuma, walilenga
kumnyamazisha milele Tundu Lissu. LEAT inasema kuwa wote hao ni watu waovu
ambao hawana hata chembe ya utu kwani dhamira zao zimekufa. Damu ya Lissu
waliyoimwaga itaendelea kuwalilia na kuwaandama wao na vizazi vyao. Damu yake,
kwa upande mwingine, itawachochea Watanzania na wapenda haki na amani kusema
ukweli wakati wote bila woga.
Ndugu Lissu alifanya kazi nasi hapa LEAT kwa kipindi cha
miaka 10 (1998-2008) na katika miaka hiyo alishiriki kwa ujasiri na ufahamu
mkubwa katika kampeni mbali mbali za kupigania utunzaji bora wa mazingira na
maliasili za nchi yetu. Aidha, alishiriki katika kampeni za kufichua jinsi
ambavyo madini ya nchi yetu yalikuwa yanaporwa kupitia mikataba mibovu ya
madini pamoja na sheria mbovu za madini, kodi, na mauzo. Aliwasemea bila woga
wachimbaji wadogo walioporwa migodi yao na kampuni hizo zikisaidiwa na vyombo
vya dola vya nchi yetu. LEAT inajivunia na kuienzi kazi aliyoifanya ambayo
matokeo yake yanaonekana kwa serikali kuanza kuchukua hatua za kubadilisha
sheria za madini na petroli pamoja na kuanza majadiliano na makampuni ya
madini.
LEAT inataka kufanya uchunguzi huru kuweza kuwabaini wote
waliohusika na jaribio hili la kinyama ambalo ni kinyume cha ibara ya 14 ya
Katiba ya nchi yetu ikiwa ni pamoja na wale waliowatuma na kuwafikisha katika
vyombo vya sheria. Jaribio hili, pamoja
na matukio mengine kama haya ambayo yamepita bila kuchukuliwa hatua, yamechafua
vibaya sana taswira na heshima ya nchi yetu. Ni lazima yakomeshwe kwa kufanywa
kwa uchunguzi huru, kuwashika na kuwapeleka mahakamani waliyoyatenda. Kutokufanywa kwa hayo ni kubariki na
kuyachagiza na ni kinyume cha dhana ya utawala wa sheria.
LEAT inatoa pole sana kwa Tundu Lissu, mkewe (Alicia) na
wanawe, wanachama wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), wapiga kura wake
wa Jimbo la Singida Mashariki, wabunge wenzake, chama chake cha Chadema,
Watanzania wote na watu wote wapenda haki, demokrasia ya kweli, amani, na
utawala wa sheria.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu aendelee kumtendea miuujiza na
kumponya Tundu Lissu haraka. Amina.