Katika kufikia malengo ya mradi wa ‘Ushiriki wa
Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili, unaotekelezwa mkoani Iringa; Timu ya
Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) imeanza mchakato wa kuziwezesha
serikali za vijiji kuandaa sheria ndogo zitakazo waongoza katika usimamizi wa maliasili
na mazingira.
Sheria hizo zitasaidia kupunguza uharibifu wa rasilimali
misitu na wanyamapori ambazo zipo katika hatari ya kutoweka kutokana na uvunaji
haramu.
Kutoka kushoto ni Mwanasheria wa Wilaya ya Mufindi bwana Simon, Afisa Mazingira wa LEAT, Edina na Mwenyekiti wa kijiji cha Ludilo
Kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi katika wilaya
za Iringa na Mufindi, mkoani Iringa; LEAT ilifanya utafiti juu ya kiwango cha
ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili, pamoja na mambo mengine
katika utafiti huo LEAT ilibaini kuwa baadhi ya vijiji havikuwa na sheria ndogo
ambazo zingetumika kusimamia maliasili na mazingira. Kutokana na hali hiyo LEAT
imeanza mchakato wa kuziwezesha serikali za vijiji kuandaa sheria hizo.
Vijiji vitakavyo wezeshwa katika awamu ya kwanza ni
vijiji vya Mbweleli, Kinyika na Kinyali kwa wilaya ya Iringa. Vijiji hivi hakiwahi
kuwa na sheria ndogo zinazotumika kusimamia maliasili licha ya kuwa na misitu
ya asili ya vijiji. LEAT iliziongoza serikali za vijiji na wananchi katika
kuunda sheria ndogo za usimamizi wa maliasili.
Wananchi na viongozi wa serikali za vijiji walitoa
mapendekezo ya muundo wa sheria hizo, na wote kwa pamoja walikubaliana kuwa
LEAT ichapishe sheria hizo na zimepangwa kuwasilishwa kuanzia mwezi Julai, 2016
kwenye mikutano mikuu ya vijiji, ili wananchi wengi wapate fursa ya kuzijadili
na kuzipitisha.
Kwa wilaya ya Mufindi, vijiji vitakavyo fikiwa
katika awamu ya kwanza ni Kibada, Ludilo na Ikangamwani. Vijiji hivi vina na
sheria ndogo zinazo waongoza katika usimamizi wa maliasili, lakini sheria hizo
zilikuwa na mapungufu.
LEAT, serikali za vijiji pamoja na wananchi
walipitia sheria hizo na waligundua mapungufu. Wananchi na viongozi wa serikali
walioshiriki katika mchakato huo walitoa mapendekezo ya maboresho ya sheria.
Sheria hizo zitawasilishwa katika mikutano mikuu ya
vijiji kuanzia mwezi Julai, 2016 ili wananchi wengi wapate fursa ya kuzijadili,
kuzifahamu na kuzipitisha.
Malengo ya mradi wa ‘Ushiriki wa Wananchi katika
Usimamizi wa Maliasili, ni kujenga utamaduni wa wananchi kushiriki katika
usimamizi wa maliasili, kuzijengea uwezo jamii za wenyeji katika kuziwajibisha
na kuzisimamia taasisi za serikali zenye majukumu ya kuhifadhi na kusimamia
maliasili. Mradi pia umelenga kukuza ufanisi katika utekelezaji na usimamizi wa
sera na sheria muhimu zinazo husika katika usimamizi wa maliasili, mabadiliko
ya hali ya hewa na tabia nchi.
Kwa kuwa rasilimali zilizolengwa zinapatikana
vijijini, LEAT iliona vyema kuwa lazima vijiji hivyo viwe na sheria ndogo
zitakazo waongoza katika kusimamia kikamilifu maliasili zilizopo katika maeneo
yao.
LEAT imekwisha toa mafunzo ya usimamizi wa maliasili
kwa wananchi, kamati za maliasili, mazingira, ardhi, maendeleo ya jamii na
fedha. Viongozi wa serikali za vijiji, Madiwani na Maafisa maliasili na ardhi,
nao wamepatiwa mafunzo hayo. Makundi hayo yote yamejifunza sera na sheria
zinazotumika katika usimamizi wa maliasili. Pia wamejifunza majukumu ya taasisi
na idara za serikali zinazohusika katika usimamizi wa maliasili.
Mradi wa ‘Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa
Maliasili’ unatekelezwa na LEAT katika vijiji 32 vya wilaya za Iringa na
Mufindi, mkoani Iringa. Mradi umefadhiliwa na Watu wa Marekani kupitia Shirika
la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID).
Mwanasheria wa LEAT, Hadija Mrisho akiongea na wananchi wakati wa kujadili muundo wa sharia za usimamizi wa maliasili
Afisa Mazingira wa LEAT, Edina Tibaijuka (anaye watazama wananchi) akifafanua jambo wakati wa mapitio ya sheriandogo za vijiji zinazosimamia maliasili