Thursday, April 7, 2016

MADIWANI NA WABUNGE WA HALMASHAURI YA MUFINDI WAHUDHURIA WARSHA YA USHIRIKI WA WANANCHI KATIKA USIMAMIZI WA MALIASILI


Madiwani 37 na Wabunge 2 wa Mufindi Kaskazini na Kusini walihudhuria warsha ya siku mbili, Febrauri 16 na 17, 2016 iliyoendeshwa na Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT), chini ya mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili, unaotekelezwa katika wilaya za Iringa vijijini na Mufindi mkoani Iringa.

Afisa Mradi wa LEAT Jmal Juma akifafanua jambo kwa Madiwani na Wabunge walio hudhuria warsha ya Ushiriki wa Wananch katika Usimamizi wa Maliasili
Sehemu ya Madiwani wakimsikiliza mwezeshaji wa warsha
Lengo la warsha hiyo ilikuwa kutoa elimu kwa madiwani na wabunge wanaounda halmashauri ya wilaya ya Mufindi juu ya Usimamizi wa Maliasili na mfumo wa Ufuatiliaji Uwajibikaji Jamii. Pamoja na mambo mengine, mafunzo yaliainisha mamlaka na madaraka ya kisisa ya Madiwani katika usimamizi wa rasilimali zinazopatikana wilayani Mufindi na Tanzania kwa ujumla.

Mmoja wa washiriki wa warsha hiyo, Mheshimiwa Zubeda Mbogela, Diwani wa kata ya Makungu  alipongeza mafunzo kwa kuwa yanatolewa wakati ambapo nchi yetu na dunia kwaujumla zinakumbwa na changamoto ya uhifadhi na usimamizi wa maliasili.

Alisema, kabla ya mafunzo alizifahamu athari za uharibifu wa rasilimali misitu ikiwa ni pamoja na ukame na mabadiliko ya tabia nchi, lakini alikiri kuwa baada ya kujifunza sera, sheria na mamlaka aliyonayo kisiasa katika usimamizi wa maliasili, amepata hamasa ya kuendelea kutoa elimu kwa jamii ya uhifadhi wa maliasili hususan wananchi kuacha kulima katika vyanzo vya maji na kukata miti kwaajili ya shughuli mbalimbali.

“Nimejifunza sheria, sera na kanuni za
usimamizi wa maliasili, pia majukumu na nguvu yangu kisiasa katika kuhamasisha, kushawishi na kusimamia rasilimali zetu na miradi ya maendeleo ilikujenga dhana ya uwazi na uwajibikaji katika jamii yetu”, alisema diwani Mbogela.

Akizungumzia umuhimu wa warsha hiyo kwa Madiwani na Wabunge, Afisa Ugani, Franklyn Masika alisema kuwa Madiwani wanamajukumu sawa na Wabunge katika kutumikia jamii. Alisema, Madiwani wanajukumu la usimamaizi katika masuala yanayohusiana na mipango, mgawanyo wa rasilimali pamoja na kufuatilia kwa karibu rasilimali za umma ndani ya mipaka ya kata husika.

Aidha, Madiwani wana uwezo wa kuikataa ama kupitisha bajeti yoyote ya baraza na wanaweza kuwawajibisha Maafisa wa serikali ndani ya halmashauri ya wilaya kutokana na matumizi mabaya ya fedha na rasilimali za umma, kutokana na umuhimu huo, LEAT iliamua kuandaa warsha hiyo kwa Madiwani ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake, Afisa Mradi, Jamal Juma, alisema kuwa, kwa ujumla Madiwani wanamamlaka ya kupitia na kupitisha sheria ndogondogo za kijiji, kata na wilaya, hivyo mafunzo ni muhimu kwao kwakuwa wamefahamu njia sahihi za usimamizi wa maliasili, na kuuelewa mfumo wa Ufuatiliaji wa Uwajibikaji Jamii ili kujenga dhana ya uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma kwa jamii.

Aliongeza kuwa, utayari na nguvu yao ya kisiasa ni muhimu katika kusiamamia na kuongoza wengine katika usimamizi wa rasilimali za misitu na wanyamapori.Zaidi ya hayo, madiwani walikumbushwa kukemea vitendo vya ujangili vinavyofanywa katika maeneo yenye rasilimali za misitu na wanyamapori,kwa kuwa ni rahisi kwao kuhamasisha na kuhimiza wananchi kwenye vijiji na kata, kufuata njia sahihi za usimamizi wa maliasili.

Warsha iliwakutanisha Madiwani wote wa wilaya ya Mufindi pamoja na Wabunge wa Mufindi Kaskazini na Kusini. Washiriki walipata fursa ya kushirikishana uzoefu wao katika usimamizi wa maliasili, pia walijadili changamoto wanazo kumbana nazo na kufanya maamuzi ya pamoja na jinsi ya kukabiliana na changamoto hizo.

Madiwani na Wabunge, pia waliunga mkono jitihada za LEAT katika usimamizi wa mazingira na maliasili na kuahidi kufanyakazi na LEAT ilikunusuru maliasili za taifa.

Warsha hii ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Ushiriki wa Wananachi katika Usimamaizi wa Maliasili, unaotekelezwa katika wilaya za Iringa vijijini na Mufindi kwa ufadhili wa Watu wa Marekani kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani(USAID) Tanzania. Mradi ulianza Novemba 2013 na unatarajiwa kukamilika Novemba 2017. Mradi unatekelezwa katika vijiji 32 na inatarajiwa kuwa takriban watu 6500 watafikiwa na mafunzo ya maradi huu.

No comments:

Post a Comment