TAARIFA KWA UMMA
Warsha ya Kitaifa ya Wadau wa Kilimo
Jumanne, Tarehe 24 Julai 2012
UTANGULIZI
Wadau mbalimbali wa kilimo kutoka Taasisi zisizo Kiserikali, vikundi vya wakulima, wanataaluma, wakulima na wawakilishi wa serikali za mitaa, kutoka mikoa ya Morogoro, Shinyanga, Iringa, Dar es Salaam, Mbeya, Pwani,Singida, Tabora, Kilimanjaro, Arusha na Dodoma, wamekutana mkoani Morogoro kwa siku mbili ili kujadili mwenendo wa mgawanyo wa rasilimali za Taifa (Bajeti) kwa sekta ya kilimo na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hii nchini.
Mkutano huu umeandaliwa na Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira (LEAT) kwa ushirikiano na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA).
Mkutano huu, pamoja na mambo mengine, umeibua masuala yafuatayo ambayo ingefaa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na jamii kuyafahamu na kuyafanyia kazi;
Moja, Bajeti ya serikali haioneshi Dhamira ya kweli ya kuendeleza sekta ya kilimo.
Hii inaoneshwa dhahiri na kupungua kwa bajeti ya kilimo kutoka Billioni bilioni 258.35 mwaka 2011/2012 hadi shilingi bilioni 237.624 mwaka 2012/2013 (Bajeti zote hizi ni Chini ya 7% ya Bajeti ya Jumla)
Mgawanyo wa bajeti katika Matumizi ya Maendeleo haujapewa kipaumbele ukilinganisha na Matumizi ya Kawaida.
-Mwaka 2011/2012 – kati ya 258.35 zilizoidhinishwa Billioni 152 Matumizi ya Kawaida na Billioni 105 tu Maendeleo (40%).
-Pamoja na kupungua kwa jumla kwa bajeti, matumizi ya kawaida yameongezeka kutoka shilingi bilioni 152.41 mwaka 2011/2012 hadi kufikia shilingi bilioni 170.364 mwaka huu wa 2012/2013
-Bajeti ya maendeleo katika wizara hii imepungua kutoka shilingi bilioni 105.94 mwaka 2011/2012 hadi kufikia shilingi bilioni 67.260 mwaka 2012/2013
-Bajeti ya kilimo kutegemea fedha za wahisani ikiwa ni moja ya vikwazo vinavyokwamisha kupelekwa kwa fedha zilizoidhinishwa kwa shughuli zilizokusudiwa.
-Hadi tarehe 31 Mei, 2012 fedha za matumizi zilizopelekwa wizarani kutoka hazina ni shilingi bilioni 103.06 sawa na asimia 67.62 ya kiasi kilichoidhinishwa (Billioni 152)
-Kwa upande wa fedha za maendeleo hadi kufikia tarehe 31 Mei, 2012 fedha zilizokuwa zimepelekwa wizarani kutoka hazina ni shilingi bilioni 72.63 sawa na asilimia 68.56 ya fedha zilizoidhinishwa (Billioni 105)
Wadau TUNAHOJI je huu ni mwenendo wa kuendeleza kilimo nchini ambayo zaidi ya 80% ya wananchi wanategemea KILIMO?
Pili, Kutokana na mwenendo huu wadau tunasikitika namwenendo wa serikali kupuuzia maazimio iliyoingia yenyewe kimataifa yenye lengo la kuendeleza sekta ya kilimo kama vile Program Kabambe ya Kuendeleza Kilimo Afrika (CAADP) na Azimio la Maputo la mwaka 2003 ambayo, pamoja na mambo mengine yanaitaka serikali Kuongeza bajeti ya kilimo angalau kufikia asilimia 10 ya Bajeti ya Jumla, na kuzingaatia mgawanyo wa angalau 50%/50% kwa bajeti ya Matumizi ya kawaida na shughuli za Maendeleo. Hii ni dhahiri kuwa lengo la ukuaji wa sekta angalau kwa 6% kwa mwaka, haliwezi kufikiwa na Malengo ya kuboresha hali ya umaskini wa wananchi wa kawaida wanaotegemea kilimo hayatafikiwa.
Tatu, Kwa kuwa mchakato wa uandaaji wa bajeti ni shirikishi kupitia mfumo wa FURSA na VIKWAZO, wadau tumebaini kuwa mfumo huu hautekelezwi kama ulivyokusudiwa hivyo bajeti hizi kimsingi hazitoki kwa wananchi. Hivyo basi,
-Tunaitaka serikali kuchukua jitihada za makusudi kutoa elimu au kuziwesha Taasisi zisizo za Kiserikali kutoa elimu kwa umma wa watanzania, hasa wakulima wadogo Kuhusu namna ya kutumia fursa ya ushiriki katika mchakato wa bajeti.
-Serikali iwajibike kupanga bajeti kulingana na vipaumbele vilivyoainishwa na wananchi.
Nne, Tunaona Umuhimu mkubwa kwa wakulima wote, wadau wa kilimo na wananchi kwa ujumla kutumia fursa ya kushiriki katika mchakato wa KATIBA MPYA ili kuweka mfumo utakaotetea masilahi na kulinda haki za mkulima. Vile vile tunaitaka serikali kuzingatia maoni yatakayotolewa na wakulima na kuyajumuisha katika katiba mpya.
Tano, Serikali ihakikishe pembejeo zinawafikia wakulima kwa wakati muafaka, zikizingatia mahitaji yao. Pia gharama za uchangiaji zizingatie hali halisi ya kipato cha mkulima mwenye kipato cha chini.
Sita, Wakulima wahahakishiwe soko, linalozingatia gharama za uzalishaji na kwamba mkulima apewe uhuru wa kutafuta soko popote linapopatikana kwa kuzingatia utaratibu mzuri wenye maslahi kwa umma. Aidha tunazitaka halmashauri ziondoe au kupinguza ushuru wa mazao kwa wakulima wadogo.
Saba, Serikali iachane na sera na matamko yasiyo na tija kwa mkulima. Wadau wamebaini kuwa bajeti ya serikali inalenga kutekeleza tamko la Kilimo kwanza Tamko ambalo wakulima wadogo wa nchi hii hawana umiliki na kimsingi Tamko hili halilengi kutatua matatizo ya kundi hili.
Nane, Tunaitaka serikali ifanye juhudi za makusudi kufanya Mpango wa Matumizi ya Ardhi kwa vijiji na Taifa, na kwamba ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa kigeni isitolewe katika ardhi ya vijiji ili Kuondoa migogoro inayoibuka kati ya wawekezaji na vijiji. Pamoja na hayo, suala la umiliki wa ardhi liwe ni moja na masuala muhimu katika Katiba mpya ili kuhakikisha umiliki wa ardhi unakuwa na ulinzi wa kikatiba kwa wakulima.
Hitimisho
Wadau tunaomba wakulima wote watambue hali inayoendelea kwa sekta ya kilimo na tuungane pamoja ketetea haki na kuweka mfumo utakaoleta tija kwa wakulima. Muda umefika kwa wakulima kuanza kudai haki zao, na serikali kutekeleza madai ya wakulima.
Heri Ayubu
Mratibu wa Mradi
No comments:
Post a Comment