NA George Ngolo
LEAT
LEAT
Tanzania ni nchi iliyobarikiwa maliasili nyingi sana ukilinganisha na nchi nyingine. Tumebarikiwa madini aina mbalimbali kama vile dhahabu(Geita), almasi(Mwadui-Shinyanga), makaa ya mawe(Kiwira), na madini yasiyopatikana sehemu yoyote ile duniani, Tanzanite.Ukiachana na madini, pia Tanzania ina wanyama wengi wa kuvutia kama vile; simba wanaopanda miti,vyura wanaozaa(Kihansi) nk.
Tofauti na nchi nyingine ambazo suala la upatikanaji wa vyanzo vya maji ni tatizo hasa kwa ajili ya shughuli za kiuchumi kama Zambia(land locked country), Tanzania imejaaliwa mito, maziwa na bahari. Kando kando mwa maziwa na bahari kuna fukwe ambazo ni hazina kubwa ya maendeleo ya kiuchumi ya nchi yetu. Baadhi ya fukwe maarufu nchini Tanzania ni pamoja na Kunduchi, Mbezi na Bahari Beach ambazo zinapatikana ukingoni mwa bahari ya Hindi.Lakini pia tuna fukwe zinazopatikana katika maziwa Victoria, Rukwa na Tanganyika.
FUKWE YA BWEJUU TANZANIA |
Vivutio vingi vya fukwe za nchini Tanzania vimekuwa vikitoweka siku hadi siku kutokana na uvamizi wa wageni lakini hasa unaochagizwa na ongezeko la ujenzi wa hoteli ya kifahari pembezoni mwa bahari na maziwa.Wamiliki wengi wa hoteli hizi wamekuwa wakijenga kuta kuzunguka hoteli ili kuwazuia wananchi kufika katika fukwe hizi ambazo ni mali yao ya asili.Kibaya zaidi hoteli nyingi zimekuwa zikitililisha maji taka na kuyaelekezea baharini na ziwani kama njia rahisi ya kumwaga taka. Kitendo hiki ni hatari kwa afya za wananchi pamoja na mazingira. Nia ya makala hii ni kuelezea faida za fukwe, kwa nini fukwe zinavamiwa , madhara ya uvamizi na nini kifanyike ili kuondokana na tatizo hili.
Hakuna asiyejua manufaa ya fukwe hasa kwa nchi inayoendelea kama Tanzania.Sekta ya utalii nchini Tanzania imekuwa ikiongeza pato la Taifa(GDP) kwa kiwango kikubwa. Mojawapo ya vivutio vya utalii nchini Tanzania ni fukwe kama ilivyoainishwa hapo juu. Watu wengi wanapendelea kwenda ufukweni kwa madhumuni tofauti; wapo wanokwenda kubarizi, kucheza michezo mbalimbali, kufanya tafiti na shughuli nyingine za kitamaduni na burudani(recreational activities).Ujenzi hasa wa maeneo ya pwani hutegemea mchanga kutoka ufukweni. Mfano 90% ya ujenzi Dar es Salaam hutegemea mchanga kutoka eneo la KUNDUCHI. Eneo hili hivi sasa limegubikwa na mashimo makubwa(gallies) yaliyopelekea uharibifu mkubwa wa mazingira kutokana na kuchochea mmomonyoko wa udongo. Fukwe ni chanzo cha ajira miongoni mwa wananchi ambao kazi yao kubwa ni kukusanya viumbe wa baharini kama; chasa, magamba ya kasa, nge, konokono ambao hunakshiwa na kutumika kama mapambo.
Wengi watajiuliza nini kinasababisha ongezeko la uvamizi wa fukwe?. Suala la uvamizi wa fukwe nchini Tanzania haliwezi kutenganishwa na ongezeko la rushwa na ufisadi nchini.Maeneo mengi ya wazi na fukwe nchini Tanzania yamevamiwa hasa maeneo ya wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam. Kitendo hiki kinachochewa na vitendo vya rushwa miongoni mwa maofisa wa ardhi, viongozi wa serikali kuu na serikali za mitaa. Ushahidi unaonyesha kuwa watendaji hawa wamekuwa wakipokea rushwa kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa ambao wanayatumia maeneo haya kwa ajili ya ujenzi wa mahoteli ya kitalii(rejea taarifa ya habari iliyorusha siku ya tarehe 19/07/2010 na kituo cha televisheni cha TBC1).Hata hivyo, hili linaweza kuthibitishwa na kitendo cha kupelekwa mahakamani kwa baadhi ya maofisa ardhi wa wilaya ya Kinondoni kwa tuhuma za uuzaji holela wa maeneo ya wazi na fukwe.
Ongezeko la watu linasemekana pia kuwa chanzo cha uvamizi wa fukwe. Hili linadhibitishwa na taarifa ya UMOJA WA MATAIFA KUHUSU MAENDELEO ENDELEVU (United Nations Sustainable Development [Agenda no.21]).Taarifa ina sema kuwa zaidi ya nusu ya wakazi duni duniani wanaishi katika maeneo ya pwani. Hivyo kufikia mwaka 2020 hali ya ukanda wa pwani itakuwa mbaya mara tatu ya hali ilivyo sasa.Kauli hii inaweza kudhibitishwa na hali ilivyo katika nchi za Indonesea, Bangladesh na Nepal.Watu wanapoongezeka kunakuwa na ushindani mkubwa wa mahitaji muhimu hasa makazi hivyo kupelekea uvamizi wa maeneo ya wazi pamoja na ukataji wa miti hasa miti adimu ya mikoko inayopatikana kwa wingi maeneo ya pwani.Sheria za mazingira hazizingatiwi nchini Tanzania. Mfano sheria inamtaka mjenzi kuanzisha mradi wake umbali wa mita 60 kutoka baharini au ziwani. Kipengele hiki hakizingatiwi na wajenzi walio wengi kutokana na ufuatiliji mdogo .Mfano wa wazi wa ukiukwaji wa sharti hili ni ujenzi maeneo ya MSASANI, MASAKI, na KUNDUCHI(Dar es Salaam). Lakini mfano ulio hai zaidi ni ujenzi wa KUNDUCHI beach ambayo ilijengwa umbali wa mita 2 kutoka baharini kabla ya kufanyiwa land recramation mwaka 1998 (Dubi na Nyandwi-1999).
Uchimbaji holela wa mchanga,mawe na kokoto kwa ajili ya ujenzi nao ni kichocheo tosha katika ongezeko la uvamizi wa fukwe. Serikali za mitaa zimeruhusu uchimbaji wa mchanga katika baadhi ya maeneo ya fukwe. Mchanga huu hutumika kwa ajili ya kujengea majumba mengi ya kifahari Dar es Salaam hasa mahoteli ya kitalii. Uchimbaji wa mchanga husababisha mmomonyoko mkubwa wa udongo kutokana na kutengeneza mahandaki na pia ukataji wa miti aina ya mikoko.Miti hii hutumika kama vikinga upepo wakati wa upepo na mawimbi makali.
Ongezeko la ukuaji wa sekta ya utalii nchini Tanzania umechangia sana uvamizi wa maeneo ya fukwe. Wafanyabiashara wengi wamejikita katika ujenzi wa hoteli za kitalii kutokana na faida wanayoipata kuwa ni kubwa. Kutokana na mahitaji kuwa makubwa ukilinganisha na maeneo kumesababisha baadhi ya wafanyabiashara kuwashawishi viongozi wa serikali kuuza maeneo ambayo hayaruhusiwi mathalani fukwe na maeneo ya wazi.
Uvamizi wa fukwe una athari nyingi kwa binadamu na mazingira.Uchafuzi wa vyanzo vya maji hasa ya bahari na mito unachangiwa na utililishaji wa maji taka kutoka mahotelini. Mathara ya kutumia maji haya ni pamoja na mtumiaji kuugua magonjwa ya ngozi (scabies) pamoja na allergy(mzio).Wale wanaotumia maji ya ziwa kama Victoria kwa ajili ya matimizi ya nyumbani kama kunywa wanahatari ya kupata magonjwa ya kuhara na kuhara damu.Ikumbukwe kuwa ujenzi wa mahoteli huambatana na ukataji wa miti mfano mikoko ambayo ni adimu(endangered species). Kitendo hiki huchochea mmomonyoko wa udongo kwani kama ilivyoelezwa hapo juu mikoko hutumika kama kikinga upepo.Zaidi ya athari kwa binadamu na mimea, pia maji yanayomwagwa na mahoteli baadhi huwa naviwatilifu( kemikali) vya sumu ambazo huwauwa samaki na viumbe wengine na hivyo wavuvi wanaotegemea kazi hii kukosa kipato. Athari ya wazi inayosababishwa na ujenzi holela wa mahoteli maeneo ya fukwe ni kitendo cha wamiliki wa mahoteli kujenga kuta nene zinazozunguka hoteli na kuwalipisha watu wanaotaka kuingia ufukweni. Kitendo hiki ni kinyume na sheria inayowataka wakazi kufurahia mali asili ya nchi, kuta hizi pia huwazuia watu wanaotegemea kazi ya uokotaji wa viumbe kama kasa, konokono na magamba ya kobe kwa ajili ya biashara ya mapambo.
Tatizo kubwa linalolikabili taifa hili ni ukosefu wa sheria makini kwa ajili ya ulinzi wa fukwe zetu. Tunazo sheria anuai zinazogusia kuhusu fukwe kama Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004(Environmental Management Act), Sheria ya Ardhi na Sheria ya ardhi ya Kijiji ya Mwaka 1999 na Sheria ya Mipango miji ya mwaka 1962.SHeria hizi na nyingine zimejaribu kuzungumzia kuhusu fukwe, haki ya jamii kupita eneo Fulani n.k.
Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 inamtaka mjenzi kujenga mradi wowote umbali wa mita 60 kutoka ziwani au baharini. Kipengele hiki kimewekwa makusudi ili kuwalinda wananchi kuwa na uwezo wa kuzifikia fukwe.Lakini hali halisi ni kwamba majengo mengi hasa hoteli za kitalii zimekuwa zikijengwa umbali wa takribani mita 2 kutoka baharini mfano hoteli ya KUNDUCHI hapo juu. Hii ni kutokana matumizi ya rushwa na ukosefu wa sheria yenye ‘meno’.Sheria hii inakwenda mbali zaidi kwa kusisitiza kuwa kila Mtazania ana haki ya kuishi katika mazingira safi na salama yaani pamoja na wananchi kuwa na uwezo wa kufikia maeneo mbalimbali kwa ajili ya burudani, dini, afya n.k. Tofauti na sheria inavyosema, watu wamekuwa wakizuiwa kuingia katika fukwe mpaka watoe kiingilio. Ikumbukwe kuwa wananchi wengi wa Tanzania ni masikini hivyo hawawezi kulipia gharama za kuingilia ufukweni ambazo ni kubwa.Sheria inamtaka mtu anayetaka kuanzisha mradi furani (ikiwamo ya karibu na fukwe) kufanya tathmini ya athari za mazingira (Environmental Impact Assessment[EIA]). Ili kujiridhisha kama mradi tajwa una madhara ya kibinadamu, kimazingira, kiuchumi , kijamii na kiuchumi. Uzoefu unaonyesha kuwa tathmini nyingi huwa zinafanywa kuhusiana na athari za mazingira(kidogo), za kiuchumi lakini sio za kiutamaduni na kijamii.
Serikali za mitaa nazo zimepewa nguvu ya kisheria chini ya Sheria hii na Sheri ya Serikali za mitaa ya mwaka 1982.Mojawapo ya kazi za serikali za mitaa ni pamoja na kusimamia mazingira na uendelezaji na upangaji wa mji. Uzoefu unaonyesha serikali nyingi za mitaa(mfano Manispaa ya Kinondoni) zimekuwa zikishiriki katika uporaji na uvamizi wa fukwe na maeneo ya wazi.
Sheria ya ardhi na ile ya Kijiji ya mwaka 1999 inatoa haki kwa mwananchi ya kupita kitika eneo fulani. Wananchi wana haki ya msingi ya kisheria kupeleka lalamiko lao mahali popote ambapo wanafikiri haki yao ya njia ya kupita imekiukwa. Lakini pia waziri aliyepewa mamlaka ya kusimamia masuala ya ardhi ana uwezo wa kushughulikia suala la haki ya msingi ya wananchi kufurahia maliasili ya nchi ikiwa ni pamoja na njia ya kwenda fukweni.Serikali za mitaa, jumuia ya watu au kikundi fulani cha watu wamepewa mamlaka katika kulinda ardhi na mazingira. Watu hawa wamepewa haki ya kupeleka laamiko lao kwa kamishna wa ardhi, au kupeleka lalamiko mahakamani kama lalamiko ni la jumla (public interest case). Ushahidi unaonyesha mara nyingi malalamiko ya wananchi hutupiliwa mbali na mahakama, waziri au kamishna wa ardhi kutokana na kukosa ushahidi au kutokujua sheria au kutokuwa na maslahi na kesi( locus stand).
Rushwa ni chanzo cha matatizo mengi hapa nchini. Tatizo la kutoa na kupokea rushwa likidhibitiwa suala la uvamizi wa fukwe litapungua kama si kuisha kabisa. Rushwa inaweza kutokomezwa kwa kuhakikisha watu wote wanaotoa na kupokea rushwa wanaadhibiwa kwa kutumikia vifungo gerezani wakipatikana na hatia pamoja na kulipa faini. Sheria za Usimamizi wa Mazingira zisimamiwe ipasavyo kwa kuwatoza faini wavunjaji pamoja na vifungo kwa wale wanopatikana na hatia. Pia tatizo sugu la uvamizi wa viwanja linaweza kudhibitiwa kwa kutunga sheria kali ya usimamizi wa fukwe na mwisho uchimbaji wa mchanga katika maeneo ya fukwe upigwe marufuku kisheria na wavunjaji wa sheria wapewe adhabu kali.
UCHAFU ENEO LA FUKWE TANZANIA |
Kama suala la uzuiaji wa uvamizi wa fukwe usipozingatiwa, vizazi vijavyo vitakuwa vikisimuliwa na kuangalia tu kumbukumku kwenye vitabu na mikanda ya video kuwa Tanzania iikuwa na fukwe za kuvutia!.
No comments:
Post a Comment