Majina yetu ni Evelina Sanga na Baraka Saiteu tumekuwa tukifanya kazi za kujitolea katika asasi isiyo ya serikali inayojihusisha na Maswala ya mazingira na haki za binadamuinayojulikana kama . Chama cha wanasheria watetezi wa mazingira (LEAT) chini ya mradi wa YETs unaodhaminiwa na World wide for Funds, katika mradi wa YETs tumeweza kupata ujuzi mbalimbali kama vile kufudisha kuhusu mazingira kwenye ngazi ya jamii,maswala ya utunzaji wa mazingira, kusimamia miradi nk.
Katika kipindi chote tulichokuwa LEAT pia tuliweza kujifunza mambo mbalimbali kuhusiana na mazingira na rasilimali zote ,kupata bahati ya kufanya kazi ya kujitolea na LEAT kumetuongezea ujuzi katika kutoa elimu ya Mazingira, na pia kutoa msaada wa Sheria unao husiana na Mazingira, Ardhi, na mengineyo, pia tumejifunza mambo yanayohusu haki za binadamu kwa ujumla wake.
KAZI TULIZOKUWA TUKIFANYA KATIKA KIPINDI CHA KUJITOLEA
TULIWAJIBIKA KUFANYA KAZI ZIFUATAZO
Kuelimisha / kutoa mafunzo kuhusu maswala ya mazingira
Kutoa msaada wa kisheria kwenye jamii za kitanzania
Kufanya utafiti wa mazingira na rasilimali katika maeneo mbalimbali.
Evelina Sanga (Katikati) na Baraka Saiteu (kushoto) wakiwa kwenye utafiti mdogo kuhusu mazingira maeneo ya Kihonda nje kidogo na Manispaa ya Morogoro
FAIDA TULIZOZIPATA KUTOKANA NA KAZI TULIZO WAJIBIKA KUZIFANYA
Tumeweza kupanua uwigo wetu wa ufahamu kuhusu mazingira, mbali na hapo pia tumeweza kujiongezea ujuzi katika shughuli zinazo husiana kufanya utafiti hasa katika sekta ya mazingira napia kusaidia jamii ya kitanzania katika maswala mbalimbali ya sheria.
Faida nyingine ni kupata fulsa ya kujua matatizo gani yanayowakabili watanzania na njia gani mbadala ya kupunguza matatizo hayo kama sio kutokomeza kabisa.
CHANGAMOTO TULIZO ZIPATA
Ni ukweli kwamba kila penye faida wakati mwingine hakukosi hasara, tulikabiliwa na changamoto japo si kwa ukubwa sana, changamoto hizo zilitokana na kazi tulizokuwa tukifanya mfano mzuri tulipokuwa tunatoa msaada wa sheria baadhi ya jamii tulizowafikia walikuwa wakitaka pesa kitu ambaho kilituwia vigumu sana katika utendaji wa kazi.
Changamoto nyingine tuliyopata ni wakati tunatoa mafunzo kuhusu mazingira baadhi ya jamii tulizowafikia walikuwa wakitaka pesa zaidi ya zile tulizowajibika kuwapa kwa madai haziwatoshi,hicho pia kilikuwa kikwazo kwani ilichangia kupoteza uwepo na umakini katika kusikiliza mafundisho hivyo kukwamisha malengo ya kutoa mafundisho.
HITIMISHO
Tunapenda kutanguliza shukrani zetu za dhati kwa Chama cha wanasheria watetezi wa mazingira (LEAT) kwa Muda wote tulioweza kufanya kazi nao, tumeweza kuongeza ujuzi wetu katika utendaji wa kazi kitu ambacho ni Faida kubwa katika soko la ajira.
Mwisho kabisa tunapenda kuwaambia wananchi kuwa asasi ya LEAT inafanya kazi bila upendeleo hivyo wananchi wenye matatizo yahusuyo mazingira mnakaribishwa.
Article By Joyceline Kobero, Legal Officer Lawyer's Environmental Action Team (LEAT)
ATHARI ZA MAZINGIRA ZILETWAZO NA UPANDAJI MITI KATIKA MASHAMBA
MAKUBWA
UKAME
Mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa yakisababishwa hasa na kuongezeka kwa kiasi kikubwa cha matumizi ya nishati Kaskazini, lakini athari zake zitasikika/onekana zaidi Kusini. Uwiano huu usiolingana utaendelezwa na [gesi ya kaboni dioxide iliyohifadhiwa ambayo ina madhara kwa mazingira] kwasababu kiwango kikubwa cha upandaji wa miti itakuwa inapandwa Kusini ambapo kuna ardhi,nguvu kazi ya gharama nafuu, lakini ambapo jamii za kienyeji wamepewa nafasi finyu kushiriki katika majadiliano ya hali ya hewa.
MAFURIKO
Tatizo la mabadiliko ya tabia nchi ambayo ulimwengu unaukabili linajulikana vizuri na pia suluhisho. Mkusanyiko wa gesi ya janikiwiti katika hewa ni matokeo ya vitendo vya uzalishaji na matumizi yasiyo na tija.
Moja kati ya gesi muhimu ya janikiwiti ni kaboni dioxide. Sehemu kubwa ya utoaji wa gesi hii shina lake ni vyanzo vikuu viwili: matumizi ya mafuta na gesi kutoka chini ya ardhi na mlolongo wa ukataji miti (ambayo inaruhusu kutolewa kwa kaboni iliyohifadhiwa katika ujumla wa viumbe hai-biomass). Kwahiyo tiba/suluhisho ni kuondoa matumizi ya mafuta na gesi kutoka chini ya ardhi na kuzuia ukataji miti.
Swali si kama ufumbuzi wa tatizo utafanikiwa sasa ila kwa vyovyote vile serikali zinaonyesha mapatano ya kufikia kusudi/madhumuni na ufumbuzi unatekelezwa kabla ya mfumo wa ikolojia wa dunia na jamii haujaangamia kabisa. Upandaji miti,unaotangazwa kama moja ya suluhisho muhimu kwa mabadiliko ya tabia nchi, wenyewe uko wazi/hatarini zaidi kwa kufyekwa/kukatwa katika nchi nyingi, ambapo misitu imekuwa mbadala wa kilimo cha aina moja ya shamba kubwa la miti. Wakati huo huo suluhisho hili linasababisha matatizo zaidi kwa mahali pale na mazingira, kwa kuwa wenyeji
wanahamishwa{matokeo yake ni ongezeko la ukataji miti], rasilimali udongo na maji zinapungua sana na makazi ya wanyama na mimea inaondoshwa/futika, kutaja kwa uchache.
UVUNAJI WA MAGOGO
Mashamba makubwa ya miti kwa mtazamo wetu.si misitu; mashamba ya miti ina kitu kimoja tu na misitu: kuna miti. Lakini, kimsingi vinatofautiana. Msitu ni changamani,ina utaratibu/mfumo wa kujiotea wenyewe,inajumuisha udongo,maji,mabadliko kidogo ya tabia nchi,nishati, na aina mbalimbali za mimea na wanyama katika uhusiano wa pamoja. Mashamba ya kibiashara,kwa upande mwingine, ni sehemu inayolimwa ambayo aina ya mimea na muundo vimerahisishwa kuvutia kuzalisha bidhaa chache ,kama magogo, makaa,utomvu, mafuta au matunda. Shamba la miti tofauti na msitu,lina aina ndogo ya mimea na umri, na linahitaji muingiliano wa kila siku kwa sehemu kubwa na binadamu.
Mashamba ya miti yanakaribiana kwa karibu na kilimo cha mazao ya viwandani kuliko msitu ambao kama kawaida unaeleweka au shamba la kilimo la asili. Kama kawaida mashamba makubwa ya miti yanategemea maelfu au hata mamilioni ya miti ya aina moja,inayozalishwa kwa ukuaji wa haraka, umoja na mavuno makubwa ya malighafi na inapandwa katika mistari inayolingana,inahitaji maandalizi ya kutosha ya udongo,mbolea,kupanda kwa kuacha nafasi,uchaguzi wa mbegu,kupalilia magugu kwa kutumia mashine au sumu ya mimea,matumizi ya dawa ya kuulia wadudu, embamba, kuvuna kwa mashine na wakati mwingine kupogoa.
ATHARI KWA WANYAMA
Tofauti haikwepeki- mashamba ya miti si msitu na kitu kimoja kinachofanana ni kwamba vote viwil,miti ndo inatawala kwa muonekano wa mara moja. Hapo kufanana kunaisha. Mkataba wa makubaliano Kyoto, wa Disemba 1997 ulikosolewa kwa mtazamo wake wa kisoko, kwa sababu ulilenga kuanzisha mfumo wa kibiashara wa kununua na kuuza utokezaji wa kaboni. Upandaji wa miti umeongeza wajibu mkuu kuhusiana na jambo hili kwa sababu ya dhana yao ya masharti ya uhifadhi wa kaboni (kaboni sinki- ni hazina ambayo inaweza kufyonza au kutenga kaboni dioxide kutoka kwenye angahewa pamoja na misitu,udongo,maji ya bahari na mabaki yenye kaboni katika kina cha bahari).
Katika makubaliano ya Kyoto, Marekani wameweka mkakati wa kudhibiti kuongezeka kwa gesi za janikiwiti kwa kuanzisha soko la kimataifa la uhifadhi wa kiwango cha kaboni. Ili utengenezaji wa kiwango cha utoaji wa kaboni ulete utaratibu wa maana, vipimo vya upunguzaji wa kaboni na uhifadhi vitahitaji kuwa vya wastani/aina moja. Njia ya uvumbuzi wa kaboni inahusisha kiwango cha chini cha kaboni iliyopo sehemu husika, na kuanzisha sehemu za mfano za kudumu za viwanja, na kukagua kila baada ya vipindi Fulani uoto wa mimea wa eneo na maeneo mengine. Utengenezaji wa kaboni, ni utoaji wa kibiashara mahsusi kwa kaboni dioxide. Ni moja ya njia ambazo nchi zinaweza kutimiza wajibu wao chini ya makubaliano ya Kyoto kupunguza utoaji wa kaboni ili kujaribu kupunguza ukali wa mabadiliko ya tabia nchi kwa siku zijazo.
Biashara ya utoaji kaboni hufanya kazi kwa kuuza kiasi fulani cha utoaji wa kaboni inayozalishwa na mtoaji. Utoaji wa gesi za janikiwiti unaathiri ustawi wa watu wanaoishi siku zijazo, na pia kuathiri mazingira halisi. Ulimwengu mzima kumekuwa na majaribio mengi ya kuanzisha miradi ya kupunguza kaboni kwa kutumia upandaji miti wa kiwango kikubwa kama njia ya kufyonza kaboni,kwa madhumuni yaliyoainishwa ya kupunguza hewa ya ukaa,ambayo inafikiriwa kuwa ni sababu kubwa ya kuongezeka kwa joto na mabadiliko ya tabia nchi. Ingawa upandaji miti kwa kiwango kikubwa umejumuishwa kwa pamoja katika utaratibu wa maendeleo safi wa makubaliano ya Kyoto,lakini bado hakuna uwezekano wa kuzalisha uhifadhi wa kaboni kwa njia ya kuanzisha mashamba ya miti kwa sababu mbalimbali. Moja ya kikwazo kikubwa cha wazi/kueleweka ni kwamba mashamba ya miti ni mazao ya muda ya mbao, ambayo kawaida hukatwa kwa ajili ya mbao za karatasi au mbao ndani ya kipindi cha muda mfupi; na ipo katika hatari kubwa ya kushika moto na kwa asili yake pia ipo hatarini kwa kiwango cha juu kuharibiwa na magonjwa,upepo na ukame.
Matokeo yake, miti michache ndo itaweza kufaa kuhifadhi kaboni kwa vipindi virefu zaidi kutosha kupunguza ukali wa mabadiliko ya hali ya hewa has ukiangalia madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa katika mashamba makubwa.
Mashamba makubwa ya miti yenyewe hayana uzuri au ubaya:kama kuna manufaa au madhara/hatari inategemea na ukubwa wake, lengo lililokusudiwa na aina ya miti,pamoja na mazingira ya asili,kijamii na uchumi mahali yanapoanzishwa.
Lakini kwa mazingira ya makubaliano ya Kyoto,mamilioni ya hekari za ardhi zitakuwa zimechukuliwa kwa ajili ya kutwaa kaboni ili kuwa na madhara kidogo katika jumla ya utoaji(kupunguza utoaji). Matokeo ya utafiti yanalenga kuongeza ufahamu miongoni mwa wawakilishi wa serikali kuhusu matatizo ya kijamii na kimazingira ambayo yatatokea kutokana na uanzishwaji wa mashamba makubwa ya miti kuhifadhi kaboni, ili waweze kuchukua uamuzi rasmi kulingana na jambo hili.
Moja ya madhara yaliyo wazi ya upandaji wa miti ni maisha ya mashaka kati ya jamii na bahari ya mashamba ya mbao ambayo yanapunguza fursa ya kutumia ardhi kwa kulima na kufuga, ilhali kuna manufaa kidogo ya moja kwa moja katika ajira na mambo mengine ya kijamii na kiuchumi. Jamii inajisikia kutengwa sana na haya mashamba makubwa ya mbao. Kupotea kwa mimea na
wanyama wa eneo husika kutokana na mashamba hayo kuna hatari kijamii,kitamaduni na kiuchumi kwa jamii kwa ujumla.
Mashamba ya mbao za viwandani mara zote huwa na matokeo hasi kwa jamii za kienyeji,uchumi na viumbe hai. Mabadiliko ya matumizi ya ardhi yanaathiri watu na riziki yao, na kwa upande mwingine zinaathiri utoaji wa gesi ya janikiwiti. Hili ni eneo ambalo lkwa kiasi kikubwa limesahaulika au kudharaulika na linaweza kusababisha utoaji wa gesi ya janikiwiti kwa kiwango ambacho hakijawahi kuandikwa ambayo yanatokana na mashamba ya ya miti yanayozalisha na kuhifadhi kaboni. Wenyeji na jamii husika zinazoishi katika misitu wanateseka kwa kuingiliwa/kutwaliwa kwa ardhi yao na makampuni ya mashamba na wanalazimika kuyaacha,kupoteza ardhi yao na riziki, hii inamaanisha kudharau msingi wa kiini na kiroho wa tamaduni zao . Katika mifano mingi,mashamba makubwa yanahitaji uharibifu wa misitu ya asili ambayo hatimaye huathiri asili ya kazi/riziki.
Ndio,wanatoa ajira kwa jamii husika kama wafanyakakzi wa mashambani(lakini mara zote na kwa vipindi) na baadae wanahamia sehemu zingine kwasababu mashamba yanatoa nafasi chache za ajira kuliko shughuli za kilimo ambazo ni mbadala. Kwa kiasi kikubwa, wanaonekana kama chanzo cha wafanyakazi wa bei rahisi wakayti wa kupanda na baadae , wakati wa kuvuna miti.
Hii inamaanisha kwamba kabla mashamba makubwa ya miti hayajawa hifadhi ya muda ya kaboni, ukweli ni kwamba yana sababisha kutolewa kwa kiasi kikubwa cha kaboni ambayo awali ilihifadhiwa katika misitu na udongo wa msituni unachukua nafasi wakati mashamba makubwa ya miti inapotokea.
Mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa yakisababishwa hasa na kuongezeka kwa kiasi kikubwa cha matumizi ya nishati Kaskazini, lakini athari zake zitasikika/onekana zaidi Kusini. Uwiano huu usiolingana utaendelezwa na [gesi ya kaboni dioxide iliyohifadhiwa ambayo ina madhara kwa mazingira] kwasababu kiwango kikubwa cha upandaji wa miti itakuwa inapandwa Kusini ambapo kuna ardhi,nguvu kazi ya gharama nafuu, lakini ambapo jamii za kienyeji wamepewa nafasi finyu kushiriki katika majadiliano ya hali ya hewa.
Upandaji wa miti una athari katika maeneo mengi ya mazingira ikiwemo maji. Mazao yote yanafanya kazi kama mabomba ya kuvutia maji, ni kwamba virutubisho vya udongo vinafikia majani yaliyoyeyushwa kwenye maji. Jinsi ukuaji unavyokuwa wa haraka,ukubwa wa mmea na ukubwa wa eneo na ndivyo kiwango kikubwa cha maji yanatumika. Inapunguza mtiririko wa maji, utoaji wa maji ya ardhini na ubora; zikiambatana na athari za viumbe asili vya majini.
Udongo pia unaathirika.Mashamba makubwa yanasababisha mabadiliko katika muundo wa udongo na mchanganyiko wa kemikali, ikihusisha na utumiaji wa mashine nzito zinazoweka mmomonyoko wa udongo. Virutubisho muhimu vinatolewa wakati magogo yakiondolewa. Mabadiliko haya kwa kiasi kikubwa hayabadiliki. Athari katika mfumo wa ikolojia ya mahali: kwa kuwa sehemu kubwa ya wanyamapori,mashamba hayatoi chakula wala malazi wala fursa ya kuzalisha. Pia zina athari kubwa katika vitu vinavyohusiana na ikolojia ya mkoa kama ukanda wa mbuga, eneo chepechepe na vyanzo vya maji.
Environmental Lawyer,
Lawyers’ Environmental Action Team (LEAT)
September 2010
VYURA WA KIHANSI?
Hawa ni vyura wa ajabu! Wanapatikana katika maporomoko ya maji yaKihansi na Muhalala, kusini mwa milima ya Udzungwa nchini Tanzania.
Vyura hawa ambao kwa jina la kitaalamu hujulikana kama ‘Nectophrynoides asperginis’ wanatajwa na wanasayansi kuwa miongoni mwa viumbe vilivyo katika hatari ya kutoweka kabisa kutokana na kuishi kweye makazi hatarishi, au kupoteza makazi yao ya asili na kupungua kwa idadi yao.
Vyura wa Kihansi waligunduliwa mnamo mwaka 1996 na timu iliyojumuisha wataalamu cha Elimu ya wanyama na Uhifadhi wa Wanyamapori kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika mchakato wa kufanya Tathmini ya athari za mazingira (Environmental Impact Assessment) kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa bwawa la uzalishaji wa umeme wa Kihansi.Ingawa yalitolewa mapendekezo ya namna ya kuwalinda viumbe hawa, mnamo mwaka 1996 karibu asilimia 90 ya maji ya mto Kihansi yalibadilishwa uelekeo kwa alili ya uzalishaji wa umeme kitu kilichopelekea upungufu mkubwa wa maji katika bonde la Kihansi, ambayo ndio hasa makazi ya vyura hawa. Kwa lugha rahisi kabisa ni kwamba mradi wa umeme uliyaharibu vibaya kama sio kutaka kuyapoteza makazi ya Maliasili hii ya kipekee.
Muathirika wa Kihansi
Mabadiliko haya yalikuwa na athari kubwa! Zaidi ya makazi ya viumbe hawa kuharibiwa, inaaminika kuwa kulikuwa na upungufu mkubwa wa hewa ya oksijeni ambayo ni muhimu sana kwa uhai wa viumbe wote, vilevile inaripotiwa kwamba kulikuwa na mlipuko wa ugonjwa wa ‘fangas’ walioenezwa viatu (mabuti) na Wahifadhi wa Mazigira pamoja na wataalamu katika kipindi cha utafiti. Kikubwa kuliko yote hakukuwa tena na uwiano wa kimazingira katika makazi hayo. Yote haya yalipelekea kupungua kwa vyura wa Kihansi kwa idadi inayokadiriwa kutoka vyura 50,000 hadi 12,000. Zaidi ya hapo ugonjwa wa fangas uliendelea kuua viumbe hawa kwa kasi kubwa.
Bonde la Kihansi kabla ya ujenzi wa mradi wa Umeme.
BWAWA LA UMEME LA KIHANSI
“Kwa wanamazingira na watetezi wa haki za wanyamapori, huu ulikuwa ni msiba mkubwa kushuhudia viumbe hawa wakitoweka kabisa. Kwao Umuhimu wa mradi wa umeme kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania usingetosha kama sababu ya kutokomeza vyura hawa. Kwa thamani ya mazingira mradi wa umeme unapaswa kutekelezwa kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira na viumbe waliomo, hivyo basi endapo mradi kama huu utatishia uhifadhi na usalama wa mazingira na viumbe itakuwa ni sababu ya msingi ya kupinga utekelezwaji wa mradi huo”
UKOMBOZI WA KIMAZINGIRA
Bronx Zoo
Ilikuwa ni mwishoni mwa mwaka 2000 ambapo kilio cha wanamazingira kilisikika kikichagangiwa na msukumo wa taasisi za kimataifa pamoja muitikio chanya wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, donia ilishuhudia serikali ya Tanzania ikishirikiana na Jamii ya Uhifadhi wa Wanyamapori (‘the Wildlife Conservation Society-WCS)ikisafirisha vyura 500 kutoka kwenye bonde la Kihansi,Tanzania kwa ndege maalumu kwenda nchini Marekani katika hifadhi ya Bronx (Bronx Zoo) na baadae kwenye hifadhi ya Taledo (Taledo Zoo) lengo likiwa kuwanusuru vyura hao wasipotee kwa kuwaweka katika mazingira yaliyo na hali karibu sawa na ile ya bonde la Kihansi kabla ya kuharibiwa na utekelezaji wa mradi wa umeme. Gharama iliyotumika kukamilisha zoezi la uhamishwaji wa vyura hawa pamoja na uhafadhi wake huko Marekani, hakika linatoa picha ya thamani ya uwepo wa kila kiumbe hapa duniani, kwani ni jambo lisilothibitika kuwa uwepo wa viumbe, akiwemo binadamu, unategemeana sana.
Baadhi ya Vyura waliorejea Tanzania.
Mwaka 2009 Muungano wa Kimataifa kwa Uhifadhi wa Asili - International Union for the Conservation of Nature (IUCN) ilitangaza rasmi kuwa vyura wa Kihansi kuwa miongoni mwa viumbe vilivyo katika hatari ya kutoweka duniani na hivyo kutoa wito kwa jamii ya kimataifa na wanaharakati wa mazingira duniani kwalinda Vyura hawa ambao ni maliasili adimu duniani. Hata hivyo kumekuwepo na faraja juu ya maisha ya vyura hawa katika kipindi cha maisha yao huko ugeninii. Hii inatokana na repoti kuwa idadi ya vyura hao imeongezeka inayokadiriwa kufikia vyura 7,000 kwa sasa.
Japokuwa kwa wakati huu, kwa kiwango kikubwa kuna muafaka mkubwa duniani kote kuhusu uwepo wa mabadiliko ya tabia nchi katika sayari hii tunayoishi. Lakini lipo kundila watu ambalo pia ni weledi wa fani mbalimbali, kama vile; sayansi, jiografia, mazingira, uchumi, hali ya hewa, bailojia na uhandisi, na kadhalika, wanaotilia mashaka sababu na uwepo wa mabadiliko makubwa ya hali ya hewa.
Mashaka yao juu ya jambo hili inawezekana yamesababishwa na mgongano wa kimaslahi na tofauti za mbinu za kitafiti zinazopelekea kuwepo kwa majawabu yanayokinzana. Kwa mfano, nchi za Marekani, China, Urusi, India, Brazil na Canada zimekuwa katika ubishi wa kiwango gani cha utoaji wa gesi ya ukaa (Carbon dioxide) kinachotakiwa kudhibitiwa ili kupunguza athari za ongezeko la joto duniani. Gesi ukaa (Carbon dioxide) inasemekana inachangia kwa kiwango kikubwa sana mabadiliko ya tabia nchi duniani.
Lakini, ukweli wa mambo ni kwamba, “mabadiliko ya tabia nchi” ni jambo dhahiri, linaloendelea kuikabili dunia, na hasa athari zake zimekuwa zikijidhihirisha katika nchi zinazoendelea, hasa kutoka bara la Asia, Afrika, Carribean na Amerika ya Kusini. Athari hizo ni za mazingira, kiuchumi na kijamii. Hivyo, inatulazimu kutafuta na kutekeleza hatua ambazo zitapelekea kupunguza au kuzuia hali hii.
Ufahamu wa dhana ya Mabadiliko ya Tabia Nchi
Bila shaka dhana ya “mabadiliko ya tabia nchi” ni miongoni wa dhana ambazo zimekuwa vinywani kwa watu wengi duniani katika miongo ya hivi karibuni. Hii inajumuisha wale wote wanaojiusisha na masuala ya mazingira na hata wale ambao hawajihusishi nayo. Lakini wengi wetu, pengine tumekuwa tukifanya hivyo bila kujua maana, japo kwa ufupi wa dhana hii. Kuelezea kikamilifu maana ya dhana ya “mabadiliko ya tabia nchi” katika makala fupi kama hii ni jambo lisilowezekana, kwa kuwa dhana hii ni pana sana na imezungumziwa na wataalamu wengi.
Kwa mujibu wa nyaraka ya Dr.Furaha N. Lugoe wa Dar es Salaam Institute of Land Administration and Policy Studies (DILAPS) yenye kichwa cha habari “Mitazamo na Ukweli wa Mabadiliko ya Tabia Nchi”(Climate Change Perspectives and Realities), alioutoa katika warsha inayohusu“Mabadiliko ya tabia nchi” iliyoandaliwa na Citizen’s Global Platform tarehe 26 Novemba 2009, Dar es Salaam, “Mabadiliko ya tabia nchi yanachangiwa sana na ‘ongezeko la joto duniani’ (global warming). ‘Ongezeko la joto duniani’ husababishwa na kuwepo ziada ya hewa za ukaa angani ambazo zinabadilisha viwango vya nishati ya joto na hivyo kusababisha wastani wa hali ya joto angani kwa msimu kuongezeka.
‘Ongezeko la joto duniani’ni jambo linalosababishwa na mwako wa nishati kama vile;petroli, dizeli, gesi asilia, makaa ya mawe na kuni, na kadhalika; kuoza kwa mboji katika maziwa na mashamba ya mpunga na utoaji wa hewa za ukaa kutoka katika mbolea za viwandani, viwanda na vyombo vya usafiri. Hewa za ukaa vilevile hujulikana kama ‘hewa za nyumba ya kijani’, ambazo zinajumuisha Carbon dioxide (CO2), methane, chlorofluorocarbons (CFC), nitrous oxide na ozone (O3)”.
Dr. Lugoe anafafanua zaidi kuwa, “Kwa kawaida, wakati miali ya jua inapopenya katika angahewa, sehemu mojawapo ya mnururisho wa jua unaakisiwa na kurudishwa tena angani na tabaka la juu la angahewa au ufyonzwa na tabaka la ozoni. Sehemu nyingine inapelekwa juu ya ardhi na kubadilishwa kuwa miali isiyoonekana au joto. Halafu mawingu, mvuke wa maji katika angahewa na ‘hewa za nyumba ya kijani’ zinavyonza na kuhifadhi kiwango kikubwa cha joto kinachozalishwa, hatima yake ni kuongezeka kwa joto duniani.”
Kwa upande mwingine ‘ongezeko la joto duniani’ linatokea pale chembe ndogo ndogo za chlorofluorocarbons (CFC) zinapobadilisha mtungo wa tabaka la ozoni. Kwanza, mnururisho wa miali isiyoonekana(ultra-violet radiation) inasababisha chembe ndogo ndogo za chlorofluorocarbons(CFC) kutoa chembe ndogo za chlorine(Cl) ambazo baadae zinavunja chembe ndogo za ozoni katika namna ileile ambayo miali isiyoonekana (ultra-violet radiation) ingeweza kufanya.Baadae Chroline inaungana na chembe ndogo za oxygen na kutengeneza Chlorine monoxide (ClO) ambayo inazuia utengenezwaji wa tabaka la ozoni.
Kwa hiyo, chembe huru za oxygen kwa kasi zinaunganika na Chlorine monoxide (ClO), baadae zinatoa chembe huru za Oxygen na Chlorine. Mchanganyiko huu wa kikemikali hauruhusu kutengenezwa kwa ozoni. Matokeo yake ni kwamba unene wa tabaka la ozoni unapunguzwa na hatimaye mnururisho wa miali mikali ya jua isiyoonekana (ultra-violet radiation) inaruhusiwa kufika kwenye uso wa dunia. Hali hii inachangia kuleta “ongezeko la joto duniani” ambayo pia inachangia sana kuwepo kwa “mabadiliko ya tabia nchi”
‘Mabadiliko ya tabia nchi’ ambayo kwa kiwango kikubwa yamesababishwa na ‘ongezeko la joto duniani’ inafanya kubadilika kwa mikondo ya mvua, kubadilika kwa kina cha bahari, kubadilika kwa mwelekeo na kasi ya upepo, kubadilika kwa mwelekeo na kasi ya mikondo ya maji ya bahari, kubadilika kwa misimu na kuongezeka kwa uwezekano wa kutokea kwa maafa ya tabia nchi kama vile; ukame, kimbunga na mafuriko.
Jambo la msingi la kuzingatia hapa ni kwamba maana hii fupi ya “mabadiliko ya tabia nchi” iliyokaririwa humu haina kusudio la kuwa maana mahsusi ya dhana hii duniani kote au miongoni mwa wanasayansi, wahandisi na wanaharakati wa mazingira. Isipokuwa kutoa mwangaza kwa umma kutambua kwa ufupi maana ya dhana yenyewe na hivyo kuwawezesha kufahamu juu ya mabadiliko ya tabia nchi na jinsi yanavyoathiri maisha yetu kwa ujumla.
Ushahidi wa mabadiliko ya tabia nchi
Ni jambo muhimu sana, siyo tu kwa wale wanaopinga au kuwa na mashaka ya kuwepo kwa “mabadiliko ya tabia nchi”, lakini na wale wanaoamini kuwepo kwake kujua hata kama siyo wote, baadhi ya ushahidi wa kuwepo kwa mabadiliko ya tabia nchi.
Ushahidi wa “mabadiliko ya tabia nchi” umepatikana kutoka vyanzo mbalimbali ambavyo vinaweza kutumika kuitengeneza tena tabia nchi ya zamani ili kuweza kufanya ulinganifu. Inasemekana kuwa rekodi zilizokamilika za takwimu zinazohusu joto la uso wa duniani ulianza kuhifadhiwa katikati na mwishoni wa miaka ya 1800.
Kuna ushahidi mwingi sana kuthibitisha uwepo wa “mabadiliko ya tabia nchi”. Miongoni wa ushahidi huo ni kuwepo kwa hali mbaya ya hewa, kama vile: ukame, mvua isiyotabirika, mafuriko, mkondo wa joto kali na kuongezeka kwa vimbunga, ongezeko la joto, kuongezeka kwa kasi ya kuyeyuka kwa barafu na kubadilika kwa uoto na maumbile asilia duniani.
Ukweli wa mambo ni kuwa, uthibitisho wa “mabadiliko ya tabia nchi” ni mwingi sana, kiasi kwamba hauwezi wote kutolewa katika makala hii pekee. Isipokuwa kutokana na umuhimu wa kuelimisha umma wa Tanzania juu ya suala hili, ushahidi ule tu wenye uhusiano wa moja kwa moja na Afrika na hasa Tanzania ndiyo unatakiwa kupewa kipaumbele cha juu.
Uthibitisho wa baadhi ya ushahidi huo wa “mabadiliko ya tabia nchi” ni kutokea kwa mafuriko makubwa ambayo hayajawahi kushuhudiwa kwa kipindi kirefu katika sehemu mbalimbali duniani. Mafuriko ya Mto Rhine (Ulaya magharibi) kati ya mwaka 1996 na 1997, mafuriko ya China ya mwaka 1998, mafuriko ya Ulaya mashariki ya mwaka 1998 na 2002, mafuriko ya Msumbiji na Ulaya ya mwaka 2000 na mafuriko ya Bangladesh yaliyosababishwa na mvua za mansuni mwaka 2004 ambayo yalifanya takribani asilimia sitini (60%) ya nchi kuwa chini ya maji na hata mafuliko makubwa yaliyoikumba Ufilipino mwaka huu (2009) ni mojawapo ya mifano inayothibitisha uwepo wa dhana ya “mabadiliko ya tabia nchi”.
Mathalani, utafiti wa kisayansi unaonyesha bayana kuwa kiwango cha ujazo wa maji katika maziwa makubwa ya Afrika kama vile Ziwa Niger, Ziwa Chad na Ziwa Victoria kimekuwa kikipungua kati ya asilimia arobaini (40%) na sitini (60%). Sambamba na hilo kumekuwa na kuongezeka kwa jangwa katika maeneo mbalimbali ya kusini, kaskazini, mashariki (Tanzania ikiwemo) na magharibi ya Afrika unaosababishwa na wastani wa chini wa mvua kwa mwaka, mvua kubwa kupita kiasi inayosababisha umwagaji na mtiririko wa maji juu ya ardhi, pamoja na unyevunyevu wenye joto katika udongo.
Mbali ya hayo, kuna uthibitisho mwingine unaodhihirisha kuwepo kwa “mabadiliko ya tabia nchi” duniani na hata Afrika ni kuongezeka kwa kasi ya kuyeyuka barafu. Utafiti wa kisayansi unaonyesha barafu imeyeyuka kwa kiwango kikubwa sana katika karne ya ishirini. Wastani wa joto katika eneo la Arctic ambalo lina barafu na baridi kali limeongezeka takribani mara mbili ya wastani wa dunia kwa kipindi cha miaka mia moja (100) iliyopita. Kiwango cha joto katika tabaka lenye ubaridi kimeongezeka kuanzia miaka ya 1980 kwa sentigredi tatu (3 centigrade).
Jambo kama hili pia linatokea nchini Tanzania. Mojawapo ya kivutio chetu kikubwa cha utalii, Mlima Kilimanjaro ambao vilevile vilele vyake vya Kibo na Mawenzi vimefunikwa na theluji umeathirika kwa kiwango kikubwa na “mabadiliko ya tabia nchi” yanayoendelea kuikabili dunia. Hali hii inatishia theluji hiyo kupotea kabisa na kufanya kizazi kijacho kuiona theluji hiyo kupitia picha za kitalii au vitabu vya hadithi tu.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa hivi karibuni kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro na Bwana Lonnie Thomson, mtaalamu wa Sayansi ya Theluji (Glaciologist) anayefanya kazi zake katika kituo kiitwacho Byrd Polar Research Centre, Columbus (Kituo cha Utafiti wa Theluji cha Byrd) kilichopo katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Ohio (Ohio State University) unaonyesha kwamba kuyeyuka kwa theluji ya Mlima Kilimanjaro unaendelea kwa kasi kubwa.
Utafiti huo umebaini kuwa zaidi ya robo ya kiwango cha theluji kilichoufunika Mlima Kilimanjaro mwaka 2000 kilipotea ilipofika mwisho wa mwaka 2007. Bwana Thompson na washirika wake walitoa ripoti hiyo tarehe 2 Novemba 2009, katika mhadhara uliondaliwa na Chuo cha Kitaifa cha Sayansi cha Marekani (National Academy of Science).
Takwimu zilizopatikana kutokana na utafiti uliofanywa angani umeongezea takwimu zilizokusanywa na timu ya utafiti ya Bwana Thompson na washirika wake. Takwimu hizo zinaonyesha kwamba uyeyukaji wa theluji katika Mlima Kilimanjaro uliongezeka kwa kiasi kikubwa miongo ya hivi karibuni, anasema Bwana Thompson. Inasemekana kuwa kuanzia mwaka 1912 hadi 1953 theluji inayofunika Mlima Kilimanjaro ilipungua kwa kiwango cha 1.1% kwa mwaka. Vivyo hivyo, kati ya mwaka 1953 na 1989 wastani wa kiwango cha kupungua kwa theluji kwa mwaka kiliongezeka na kufikia 1.4%.
Tokea utafiti ulifanywa mwaka 1989 hadi kufikia utafiti uliofanywa hivi karibuni, mnamo mwaka 2007 umeonyesha kupungua kwa kiwango kikubwa cha eneo la Mlima Kilimanjaro lililofunikwa na theluji, kwa wastani mkubwa sana cha 2.4%, wanabainisha watafiti hao.
Bwana Thompson anasema, siyo tu kwamba mapande makubwa ya theluji kwenye kilele cha mlima yamekuwa yakipungua, yanapungua kwa kasi kubwa, mwelekeo huu umegundulika tu kwa kutumia njia ya utazamaji kutokea ardhini iliyoboreshwa miaka ya hivi karibuni.
Sehemu pana zaidi ya kilele ambayo inakadiriwa kuwa na upana wa meta 50 iitwayo “Ukanda wa Theluji wa Kaskazini”, imekuwa ikipungua kwa kiwango cha meta 1.9 kati ya mwaka 2000 na 2007. Kwa kipindi hicho hicho, “Ukanda wa Theluji wa Kusini” wa mlima Kilimanjaro ambao unakadiriwa kuwa na upana wa meta 21 mwaka 2000, umepoteza meta 5.1 ya unene wa theluji mwaka 2007.
Bwana Thompson anaongeza kuwa, kama theluji ya mlima Kilimanjaro itaendelea kuyeyuka, kuporomoka na kukatika vipande vidogo vidogo, miamba myeusi itakayozunguka theluji itakayo salia, itafyonza miale ya jua mingi zaidi na kuchemka, na hivyo kuongeza zaidi kasi ya kuyeyuka theluji. Watafiti wanakadiria kwamba kwa kiwango cha sasa cha uyeyukaji wa theluji, tabaka la kudumu la theluji katika Mlima Kilimanjaro litatoweka ifikapo mwaka 2022.
Hata Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bwana John Chiligati ameunga mkono ushahidi uliotolewa hapa juu. Katika mahojiano yake na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC (British Broadcasting Corporation), mnamo tarehe 13 Novemba 2009, Waziri Chiligati alisema kuwa “mabadiliko ya tabia nchi” yamesababisha ukame katika sehemu ambazo hapo awali zilikuwa zinapata mvua za kutosha…, hata theluji ya Mlima Kilimanjaro ambayo inajulikana sana kama kofia nyeupe (white caps) imeanza kutoweka kwa kasi kubwa, kitu ambacho kinahatarisha sana uwepo wa kivutio hiki muhimu cha utalii cha nchi yetu”.
Kutokana na uthibitisho huu, sidhani kama kuna mtu yoyote atakayeshindwa kung’amua nini itakuwa hatima yake kwa dunia, na hasa Tanzania, kama hali hii itaachwa bila kudhibitiwa.
Nini kisababishacho
Kuna nadharia kadha wa kadha zinazojaribu kuelezea sababu zinazosababisha mabadiliko makubwa ya tabia nchi yanayoendelea kushuhudiwa sasa ulimwenguni kote. Miongoni wa sababu zinazotajwa kuwa ndizo zimepelekea kuwepo kwa “mabadiliko ya tabia nchi” ni; mabadiliko ya mnururisho wa jua, mchepuko wa sayari ya dunia katika mzunguko wake, mtengenezeko wa milima na mwelekeo wa mabara, kubadilika kwa mkusanyiko wa pamoja wa gesi inayoathiri hali ya hewa kutokana na shughuli za binadamu.
Kitaaluma sababu zote hizo na nyingine ambazo hazija orodheshwa humu ni muhimu sana. Lakini katika makala hii sababu ya mabadiliko ya tabia nchi yanayotokana na uzalishaji wa “hewa ya ukaa” (carbon dioxide) na gesijoto unaosababishwa na shughuli za binadamu, ndiyo ukaopewa kipaumbele.
Kwa sasa kuna muafaka wa kisayansi kuhusiana na mabadiliko ya tabia nchi, kwamba shughuli za binadamu inawezekana zikawa ni sababu kubwa ya kuongezeka kwa kasi kubwa sana ya wastani wa joto duniani kwa kipindi cha miongo kadhaa iliyopita. Shughuli za kila siku za binadamu zinasababisha utoaji na ongezeko la hewa ya ukaa na gesijoto angani, ambazo usababishwa na uunguzaji wa nishati inayotokana na mabaki ya viumbe hai, kama vile: petroli, dizeli, makaa ya mawe na gesi asilia. Mchakato huu ndio unaleta ongezeko la joto duniani na hivyo kubadilisha tabia nchi iliyokuwepo awali.
Vivyo hivyo, mchakato huo wa kuongezeka kwa hewa ya ukaa (carbon dioxide) na gesijoto angani unachangia uharibifu wa “tabaka la ozoni” (ozone layer) ambalo limekuwa likiikinga dunia na kunururishiwa miale mikali ya jua. Jambo hili pia husababisha ongezeko la joto duniani na hatimaye “mabadiliko ya tabia nchi”.
Sababu nyingine ya “mabadiliko ya tabia nchi” ni ukataji mkubwa usio endelevu wa misitu (deforestation). Hali hii pia inachangia sana kuongezeka kwa joto duniani, kwa kuwa mchakato wa ufyonzaji gesi ya ukaa unaofanywa na misitu na mimea unaathirika sana. Hii hupelekea kuwepo kwa mlundikano wa kiwango cha juu cha hewa ukaa na ongezeko la joto hutokea.
Shughuli za binadamu zinazochangia ongezeko la joto duniani na hatimaye “mabadiliko ya tabia nchi” ni nyingi mno, mbali na hizi zilizotajwa, zingine ni kama vile: kilimo cha umwagiliaji, uchomaji wa misitu pamoja na mabaki ya mazao na ufugaji wanyama kwa kiwango kikubwa.
Namna za kutatua
Ni ukweli usiopingika kwamba ulimwengu unakabiliwa na mabadiliko makubwa ya tabia nchi. Kama tulivyoona hapo juu, mbali na sababu za kiasili, vilevile shughuli za binadamu zimekuwa ni sababu kubwa sana zinazosababisha “mabadiliko ya tabia nchi” kama ilivyoelezwa awali katika makala hii.
Kutokana na ukweli huu hata utatuzi wa jambo hili pia unategemea namna ya kuikabili sababu hii kubwa inayochangia kuwepo kwake. Ndiyo maana, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. Jakaya Mrisho Kikwete aliwahi kukaririwa akisema kwamba, “Kwa mazingira masafi na sayari salama kwa sisi kuishi, ni lazima tuondoe gesijoto kwenye anga, tusimamishe na tupunguze kiwango cha sasa cha utoaji hewa ya ukaa na tupunguze mlundikano wake angani”.
Ni dhahiri kwamba kauli hii ya Rais Kikwete imelenga kwenye kitovu cha chanzo cha tatizo la “mabadiliko ya tabia nchi”. Kwa hali hii ni jambo la msingi kujua namna ambavyo gesijoto hasa hewa ukaa ambazo husababisha ongezeko la joto dunia na hatimaye “mabadiliko ya tabia nchi”, zinavyoweza kupunguzwa.
Bwana Emmanuel Massawe, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira (Lawyers’ Environmental Action Team, LEAT) ametoa kauli inayoshahabiana kwa kiwango kikubwa na ile ya Mheshimiwa Rais Kikwete, kwamba, “Mabadiliko ya tabia nchi yanayoshuhudiwa duniani kwa sasa, inawezekana kuepukwa kwa kuhakikisha kwamba ongezeko la joto duniani linapunguzwa na kudhibitiwa. Jambo hili linawezekana tu, kwa kupunguzwa kiwango cha utoaji wa hewa ukaa na gesijoto angani ambazo zinachangia sana kuleta ongezeko la joto duniani na swahiba wake mabadiliko ya tabia nchi”.
Bwana Massawe, anaongeza kuwa jambo ili litawezekana kama tutapunguza kwa kiwango kikubwa matumizi ya makaa ya mawe, dizeli, petroli au kudhibiti shughuli zinazotumia nishati hizo kwa kiwango kikubwa kwa kutumia nishati mbadala.
“Nadhani utekelezaji wa Mpango wa Kupunguza Uzalishaji wa Hewa ya Ukaa kutokana na ukataji miti hovyo na uharibifu wa Misitu (MKUHUMI) utasaidia sana kupunguza kasi ya “mabadiliko ya tabia nchi”, Bwana Massawe, aliongeza.
Mpango huu (MKUHUMI) unatokana na Jumuia ya Kimataifa kutambua kwamba, kama misitu itajumuishwa katika utatuzi wa “mabadiliko ya tabia nchi”, hivyo nchi zinazoendelea lazima zifidiwe kwa kuhifadhi na kupunguza ukataji wa misitu unaotokea pale misitu inavyokatwa kwa matumizi mengine ya ardhi hiyo, pamoja na uharibifu wa misitu unaotokea pale maliasili za misitu zinavyoharibiwa. Kwa kuwa, ardhi yenye misitu inaweza kuwa na thamani kutokana na uuzaji wa mbao uletao fedha za kigeni kwa taifa au uwezekano wa kutumika kwa kilimo cha mazao ya biashara na chakula kwa ajili ya kulisha idadi ya watu inayoongezeka kila siku. Hivyo ni muhimu kutoa tuzo ya fedha ili kuhakikisha kuwepo misitu hiyo kwa kuwapa wananchi hamasa ya kuihifadhi, kuitunza na kuitumia kiuendelevu.
Mchango wa misitu katika kutatua tatizo la “mabadiliko ya tabia nchi” ni kutokana na ukweli kwamba misitu hufyonza hewa ukaa na hivyo kupunguza mlundikano wake angani. Inakadiriwa kuwa asilimia ishirini (20%) ya utoaji wa hewa ukaa angani unaweza kupunguzwa kwa kutokata na kuharibu misitu. Vilevile misitu inaweza kuchangia katika kukabiliana na “mabadiliko ya tabia nchi” kwa kuipatia dunia huduma ya ikolojia.
Hivyo, Bwana Massawe anafafanua zaidi kuwa, “Sisi LEAT tunauona MKUHUMI kuwa wenye manufaa sana, kwa kuwa ni utaratibu uliobuniwa kutoa zawadi au motisha kwa nchi zile zitakazotunza misitu kama vile Tanzania. Chini ya mfumo huu nchi zitapima na kuratibu kiasi cha misitu kilichoko na kutathmini kiasi cha hewa ukaa kinachopunguzwa angani kwa kufyonzwa na misitu iliyohifadhiwa na kutunzwa vizuri ndani ya mipaka ya nchi husika. Hii itawezesha kutathmini kiasi cha uondoaji wa hewa ukaa angani na kutambua kiasi cha mlundikano wa gesijoto angani kilichopunguzwa ili kujua kiasi cha karadha (credits) za hewa ukaa kinachoweza kuuzika kilichotokana na kupunguzwa kwa mlundikano wa hewa ukaa angani. Halafu karadha hizi zitaweza kuuzwa katika soko la dunia la hewa ukaa na kupata kipato kizuri”.
Mabadiliko ya tabia-nchi ni maafa yaliyo dhahiri kisayansi kwa sasa. Imethibitishwa na wanasayansi mbalimbali duniani kuwa maafa haya (mabadiliko ya tabia-nchi) yanahatarisha maisha ya wanadamu na viumbe hai wengine. Jambo muhimu la kutilia maanani ni kuwa mabadiliko ya tabia-nchi yamesababishwa na mwanadamu kwa kutekeleza mipango ilokusudiwa kuchagiza maendeleo ya kiuchumi.
Nchi zote za ulimwenguni zimekuwa zikitekeleza na kuweka kipaumbele shughuli zinazoleta maendeleo bila kutilia maanani mazingira na vizazi vijavyo. Mabadiliko ya tabia-nchi yanasababishwa kwa kiasi kikubwa na vitendo vya kuchoma nishati asilia, kubadilisha eneo la misitu kuwa jangwa na kufanya shughuli zinazozalisha gesijoto kwa wingi. Nishati asilia inapochomwa huzalisha gesijoto ambayo huenda angani na kutuama/kuelea katika sehemu ya anga.
Hii husababisha kuongezeka kwa joto duniani. Uzalishaji wa gesijoto kwa wingi na kasi ya kugeuza misitu kuwa jangwa hupunguza uwezo wa misitu kunyonya hewa ukaa na gesi nyingine, hivyo kuharibu uwiano wa asili angani na kupelekea kuwepo kwa mlundikano wa gesijoto angani.Kwa sasa mlundikano wa hewa ukaa angani inaaminika umefikia kiwango cha juu kabisa. Hivyo kuna uhitaji mkubwa wa kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na gesijoto duniani.
Nchi zenye maendeleo ya viwanda (kwa mfano, nchi za Ulaya, China, India na Marekani) zimechangia/zinachangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya tabia-nchi kutokana na gesijoto zinazozalishwa kutoka viwandani na katika sekta ya usafiri. Nchi zinazoendelea zimechangia kwa kiasi kidogo sana. Ni asilimia 17 tu ndio inazalishwa na nchi zinazoendelea kutokana na kupotea kwa misitu kunakotokana na uvunaji holela.
Bara lote la Afrika linachangia asilimia 3 tu ya gesijoto inayozalishwa duniani. Ijapokuwa nchi zinazoendelea zinachangia kidogo sana mabadiliko ya tabia-nchi (hasa zile za Afrika), ndizo zinazoathrika sana kutokana na athari za mabadiliko ya tabia-nchi. Nchi tajiri duniani haziathiriki sana ukilinganisha na nchi maskini.
Mabadiliko ya tabia-nchi ni maafa yaliyo bayana kabisa na yenye kuviza maendeleo ya mwanadamu. Mathalani, maafa haya yameathiri kwa kiasi fulani jitihada za jumuiya za kimataifa kupunguza umaskini duniani na kutimiza Malengo ya Milenia. Ni dhahiri kuwa kwa sasa, mabadiliko ya tabia-nchi yanaathiri misingi ya maisha duniani. Yanaathiri rasilimali na mifumo-hai ambayo wanadamu tunategemea kwa chakula na maji, uzalishaji wa misitu yetu na maeneo ya kilimo.
Athari ziletwazo na mabadiliko ya tabia-nchi
Kutokana na Ripoti ya Nne ya Jopo la Wataalamu la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Mabadiliko ya Tabia-nchi (IPCC) iliyotolewa mwishoni mwa 2007, wastani wa joto duniani umeongezeka kwa digrii za sentigredi 0.74 toka mapinduzi ya viwanda kuanzishwa.
Ripoti hii imeonesha kuwa kati ya 1970 na 2004, mlundikano wa gesijoto angani umeongezeka kwa asilimia 70, ambapo mlundikano wa hewa ukaa umeongezeka kwa asilimia 80 kwa kipindi hicho. Ni dhahiri kuwa kadiri mlundikano wa hewa ukaa na gesijoto angani unavyoongezeka, ndivyo maafa na athari za mabadiliko ya tabia-nchi yanavyoongezeka kwa nchi maskini.
Kutokana na haya, tafiti zimethibitisha kuwa:-
·Kumetokea maafa ya ukame duniani ambayo yameathiri upatikanaji wa chakula kwa binadamu na wanyama. Pia yatapelekea kushuka kwa uzalishaji wa mazao kwa kilimo kinachotegemea mvua kwa asilimia 50. Hii itaathiri upatikanaji wa chakula na kuwepo kwa baa la njaa.
·Kuongezeka kwa matukio ya mafuriko makubwa ambayo yameathiri mifumo-hai na kusababisha vifo vya watu na wanyama na kuharibu miundo-mbinu.
·Kumetokea vipindi virefu vya joto kali na ukame vilivyopunguza upatikanaji wa maji safi kwa kunywa na kilimo.
·Kumetokea mioto hatari iliyoteketeza misitu ambayo mwanadamu anaitegemea kwa nishati kuni, hewa safi (oksijeni) na uoto wa asili.
·Kumekuwepo ongezeko la joto duniani linaliathiri maisha ya kawaida ya mwanadamu.
·Kumekuwa na ongezeko la magonjwa ya kitropiki, mathalani, malaria ambayo yamechagizwa na kuongezeka kwa mazalio ya mbu kutokana na kuongezeka kwa joto.
·Kuyeyuka kwa theluji kwenye safu za milima mirefu na maeneo yaliyo katika ncha za dunia kunakosababisha kupanda kwa kina cha bahari.
·Kina cha bahari kuongezeka kwa baadhi ya maeneo duniani na kupelekea eneo fulani la visiwa au nchi kavu kufunikwa na maji. Hii inahatarisha maisha ya watu waishio visiwani kwani kama hali ikiendelea visiwa vyote vyaweza kufunikwa na maji ya bahari. Pia kuongezeka kwa kina cha bahari kutapunguza kuwepo kwa maji baridi kwa ajili ya matumizi ya binadamu kunakotokana na kuongezeka kwa maji ya chumvi katika nchi kavu (Salt water intrusion).
Athari na maafa haya yamethibitishwa kutokea na kuhusiana na mabadiliko ya tabia-nchi. Yanaendelea kutokea na kuathiri baadhi ya maeneo ya dunia kwa sasa. Jitihada mahsusi na za haraka zinahitaji kuchukuliwa ili kuwakinga watu na athari na kupunguza visababishi vya mabadiliko ya tabia-nchi.
Sera mbali mbali na mchango wake katika kusababisha Mabadiliko ya Tabia-Nchi
Sera ni chombo cha utekelezaji wa Sheria, mipango ya maendeleo, na mikakati mbalimbali. Sera hazina nguvu ya kisheria lakini zinaweka msingi wa kutunga au kurekebisha Sheria. Sera hutoa maelekezo na hatua za kuchukua katika utekelezaji wake. Serikali hutumia Sera mbalimbali kutekeleza mipango na mikakati ya maendeleo.
Utekelezaji wa Sera kadha wa kadha unatakiwa kuleta matunda bora kwa jamii kwa kuchagiza maendeleo na kupunguza umaskini. Utekelezaji wa Sera unaweza kuwa wa manufaa kwa jamii au ukaiathiri jamii kwa namna moja au nyingine. Malengo na maudhui ya Sera mbalimbali hayatakiwi kugongana kwani zitaleta madhara kwa jamii.
Sera zinazoratibu sekta moja zinatakiwa zishirikiane kimaudhui na kiutekelezaji ili kuratibu vyema shughuli za utekelezaji wa mipango na mikakati ya maendeleo. Sera zinatakiwa zilete maendeleo endelevu bila kuathiri mahitaji na maslahi ya vizazi vijavyo. Utekelezaji wa Sera mbalimbali huchangia kwa namna moja au nyingine kuleta mabadiliko ya tabia-nchi. Sera hizi na jinsi zinavyochangia kuwepo kwa mabadiliko ya tabia-nchi zinaelezewa hapa chini kinagaubaga.
Sera ya Taifa ya Misitu, 1998
Sera ya Taifa ya Misitu nchini Tanzania ilitangazwa mwaka 1953. Sera hii imekuwa inarekebishwa mara kadhaa pale uhitaji wa kuirekebisha ulipotokea. Lengo la kuwa na Sera hii ni kuainisha na kuratibu namna ambavyo rasilimali ya misitu na miti inaweza kutumika kwa misingi endelevu ili kukidhi mahitaji na matakwa ya jamii na taifa.
Moja ya madhumuni ya sekta ya misitu ni kupanua ajira na kuongeza pato la fedha za kigeni kutokana na maendeleo endelevu katika viwanda vinavyojikita kwenye misitu na biashara. Ili kufikia dhumuni hili serikali inabudi kufungua milango na kuruhusu uwekezaji katika sekta ya misitu.
Ili uwekezaji katika sekta ya misitu ulete na kuongeza fedha za kigeni ni lazima uvunaji wa rasilimali misitu na miti ufanyike kwa kiwango kikubwa ili kuleta manufaa ya kibiashara. Uvunaji wa misitu unatakiwa kuwa endelevu kwa kutilia maanani rasilimali misitu na miti zilizoko nchini. Hili linachangia kuwepo kwa mabadiliko ya tabia-nchi kwani miti huvunwa kwa wingi sana ili kuongeza pato la fedha za kigeni.
Tutambue kuwa miti hufyonza hewa ukaa kwa ajili ya kutengenezea chakula. Lakini uvunaji wa kiwango kikubwa wa misitu na rasilimali miti huacha eneo kubwa la nchi kuwa jangwa. Hii inamaanisha kuwa hewa ukaa na gesijoto zinalundikana angani na kusababisha mabadiliko ya tabia-nchi.
Sera ya Taifa ya Mazingira, 1997
Sera hii ilipitishwa na serikali kwa madhumuni ya kutoa ufafanuzi na maelekezo ya namna ya kuratibu shughuli za kuhifadhi na kuyalinda mazingira. Baadhi ya malengo ya Sera ya Taifa ya Mazingira ni kuhakikisha upatikanaji, ulinzi na matumizi sawa ya rasilimali kwa ajili ya mahitaji muhimu ya vizazi vya sasa na vijavyo bila ya kuharibu mazingira au kuhatarisha afya au usalama wa binadamu.
Pia, kuzuia kudhibiti na uharibifu wa ardhi, maji, mimea na hewa ambavyo ndivyo vinashikilia mifumo ya maisha yetu. Malengo haya yanatakiwa yatekelezwe kikamilifu na yasimamiwe na watendaji makini. Mapungufu au uzembe katika kuratibu na kutekeleza malengo ya Sera ya Mazingira yatapelekea uharibifu wa mazingira na uzalishaji wa hewa ukaa na gesijoto kwa wingi.
Ili kuyalinda na kuyatunza mazingira, hatuna budi kukusanya na kutupa taka ngumu na taka-kimiminika tunazozalisha kila siku kwa uangalifu bila kuathiri mazingira na afya za wanadamu. Kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Mazingira, taka ngumu na taka-kimiminika hutupwa katika dampo lililofunguliwa na kusimamiwa kitaalamu.
Taka zinapotupwa katika dampo hulundikaka na kuoza. Taka hizi huzalisha gesijoto aina ya Methane ambayo husababisha mabadiliko ya tabia-nchi. Ni kwa minajili hii utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mazingira inachangia kuwepo kwa mabadiliko ya tabia-nchi.
Sera ya Wanyamapori, 2007
Sera hii iliundwa kwa lengo la kuhifadhi, kulinda na kuratibu matumizi endelevu ya wanyamapori na maeneo ya ardhi-oevu. Utekelezaji wa Sera hii hauna mchango wa moja kwa moja kwa mabadiliko ya tabia-nchi. Ila uhifadhi wa wanyamapori huchangia kwa namna moja au nyingine kuwepo kwa mabadiliko ya tabia-nchi. Vinyesi vya wanyamapori na uwindaji haramu wa kuwaua hovyo wanyamapori kwa kusaka ngozi au pembe za ndovu huzalisha hewa ukaa na gesijoto ambavyo huchangia mabadiliko ya tabia-nchi.
Sera ya Taifa ya Nishati, 2003
Sera hii inanuia kuhakikisha kuwepo na upatikanaji wa nishati ya kudumu na ya bei nafuu na kuwepo kwa matumizi endelevu ya nishati ili kuchagiza maendeleo ya kiuchumi. Upatikanaji wa nishati ya uhakika na ya kudumu unahitaji kutekelezwa kwa shughuli za ufuaji au uzalishaji wa nishati kwa njia tanzu tofauti. Nishati huzalishwa kwa kutumia maji, mionzi ya jua, upepo, petroli, nuklia na mimea (kwa mfano, bayo-dizeli). Uzalishaji nishati kwa kutumia njia hizi kunaweza kukasababisha mabadiliko ya tabia-nchi.
Mfano hai ni kuzalisha nishati ya bayo-dizeli kwa kutumia mibono. Uzalishaji wa nishati kwa njia hii hutumia maeneo makubwa ya mashamba ambayo huanzishwa kwa kukata miti ili kupata eneo la wazi la kulima mibono. Kwa kukata miti uoto wa asili unaofyonza hewa ukaa utaondolewa na kupelekea kuwepo kwa mlundikano mkubwa wa hewa ukaa na gesijoto angani.
Pia, ufuaji umeme kwa kutumia petroli kunapelekea kupata nishati bora kwa matumizi ya uzalishaji na kuleta maendeleo. Ila matumizi ya petroli kwa kuzalisha umeme kunachangia kwa kiwango kikubwa kuongezeka kwa hewa ukaa duniani. Kwa kutekeleza Sera ya Taifa ya nishati kuzalisha nishati kusipotilia maanani athari za mazingira zinazoletwa na matumizi ya njia husika ya uzalishaji umeme/nishati kunachangia mabadiliko ya tabia-nchi.
Sera ya Taifa ya Kilimo kwanza
Baadhi ya mazao ya nafaka hasa yale yalimwayo katika maji mengi yanachangia kuongezeka kwa gesi joto iitwayo methane. Hii inatokana na kupungua kwa hewa ya oksijeni kwenye udongo kadri maji yanavyokuwa mengi na kusababisha kuoza kwa masalia ya mimea na wanyama. Mimea kama ya mpunga haiwezi kushikilia kabon kwenye udongo kukiwa hakuna oksijen, na hii husababisha bakteria walioko ardhini kutengeneza methane. Hii gesi joto inayotengenezwa huachiliwa angani kwa njia ya upumuaji unaofanywa na mimea ya mpunga. Hivyo husababisha kuongezeka kwa gesi joto angani.
Hitimisho
Utekelezaji wa Sera mbalimbali za Taifa unalenga kuchagiza maendeleo ya kiuchumi na kupunguza umaskini. Ni dhahiri kuwa Sera huchangia kuwepo kwa mabadiliko ya tabia-nchi. Hivyo, utekelezaji wa Sera hizi unatakiwa ufanyike kwa umakini wa hali ya juu ukizingatia masuala ya mazingira na athari za utekelezaji wake.