Sunday, September 10, 2017

TAMKO LA LEAT KULAANI JARIBIO LA KUMUUA NDUGU TUNDU ANTIPHAS MUGHWAI LISSU


Ndugu. Tundu Antiphas Mughwai Lissu

Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) imepokea kwa mshituko na simanzi kubwa jaribio la kumuua Ndugu Tundu Antiphas Mughwai Lissu huko Dodoma mnamo tarehe 7 Septemba 2017. Jaribio hilo si tu ni la kinyama bali lilitendwa kwa lengo moja tu, kumuua Ndugu Lissu.


Waliotenda jaribio hilo, na wale waliowatuma, walilenga kumnyamazisha milele Tundu Lissu. LEAT inasema kuwa wote hao ni watu waovu ambao hawana hata chembe ya utu kwani dhamira zao zimekufa. Damu ya Lissu waliyoimwaga itaendelea kuwalilia na kuwaandama wao na vizazi vyao. Damu yake, kwa upande mwingine, itawachochea Watanzania na wapenda haki na amani kusema ukweli wakati wote bila woga.


Ndugu Lissu alifanya kazi nasi hapa LEAT kwa kipindi cha miaka 10 (1998-2008) na katika miaka hiyo alishiriki kwa ujasiri na ufahamu mkubwa katika kampeni mbali mbali za kupigania utunzaji bora wa mazingira na maliasili za nchi yetu. Aidha, alishiriki katika kampeni za kufichua jinsi ambavyo madini ya nchi yetu yalikuwa yanaporwa kupitia mikataba mibovu ya madini pamoja na sheria mbovu za madini, kodi, na mauzo. Aliwasemea bila woga wachimbaji wadogo walioporwa migodi yao na kampuni hizo zikisaidiwa na vyombo vya dola vya nchi yetu. LEAT inajivunia na kuienzi kazi aliyoifanya ambayo matokeo yake yanaonekana kwa serikali kuanza kuchukua hatua za kubadilisha sheria za madini na petroli pamoja na kuanza majadiliano na makampuni ya madini.


LEAT inataka kufanya uchunguzi huru kuweza kuwabaini wote waliohusika na jaribio hili la kinyama ambalo ni kinyume cha ibara ya 14 ya Katiba ya nchi yetu ikiwa ni pamoja na wale waliowatuma na kuwafikisha katika vyombo vya sheria. Jaribio hili,  pamoja na matukio mengine kama haya ambayo yamepita bila kuchukuliwa hatua, yamechafua vibaya sana taswira na heshima ya nchi yetu. Ni lazima yakomeshwe kwa kufanywa kwa uchunguzi huru, kuwashika na kuwapeleka mahakamani waliyoyatenda.  Kutokufanywa kwa hayo ni kubariki na kuyachagiza na ni kinyume cha dhana ya utawala wa sheria.


LEAT inatoa pole sana kwa Tundu Lissu, mkewe (Alicia) na wanawe, wanachama wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), wapiga kura wake wa Jimbo la Singida Mashariki, wabunge wenzake, chama chake cha Chadema, Watanzania wote na watu wote wapenda haki, demokrasia ya kweli, amani, na utawala wa sheria.


Tunamuomba Mwenyezi Mungu aendelee kumtendea miuujiza na kumponya Tundu Lissu haraka. Amina.