Wednesday, May 6, 2015

LEAT KUTUMIA VIKUNDI VYA SANAA KUHAMASISHA USHIRIKI WA WANANCHI KATIKA USIMAMIZI WA MALIASILI

Sanaa kwa maendeleo ni dhana ya kutumia sanaa hasa  za  maonesho ili kumuwezesha mwanajamii kujiletea maendeleo yake mwenyewe.
Mbinu ya sanaa kwa maendeleo imejikita zaidi katika kuamini kuwa ikiwa jamii Fulani ina matatizo ya kimaendeleo, ni wanajamii wenyewe ndio wana uwezo wa kuyajadili na kuyatafutia ufumbuzi matatizo hayo. Ingawa dhana hii sio ngeni sana masikioni mwa wnajamii na wanaharakati mbalimbali wa maendeleo imekuwa ikitumika kama kielelezo kuonesha mchango wa sanaa katika kuleta maendeleo ya mtanzania.
LEAT inaamini kuwa sanaa ni chombo kinachoweza kuionesha jamii jinsi ilivyo kwani sanaa kwa maendeleo ni zao la jamii lenyewe. Kwa kuliona hili LEAT kupitia nradi wa ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili imetoa mafunzo kwa vikundi mbalimbali vya sanaa katika wilaya za Iringa Vijijini na Mufindi. Lengo la mafunzo haya ni kuvijengea uwezo vikundi hivi kutumia fani mbalimbali za sanaa zilizopo katika jamii husika kama vile ngoma, hadithi, maigizo,nyimbo mashairi, viziga na nyinginezo  katika kuamsha ari na kuwawezesha wanajamii kupata fursa ya kujadili na kuhoji mambo mbalimbali hasa yanayohusu usimamizi wa maliasili ambayo yamekuwa kikwazo cha maendeleo.
Sanaa shirikishi inalenga kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika shughuli za kujiletea maendeleo . Kama sanaa ikitumika vizuri inaweza kuwahamasisha wanajamii kuinuka  na kuweza kuwawajibisha viongozi wazembe pale wanaposhindwa kutekeleza majukumu yao.
Mafunzo haya  kwa vikundi vya sanaa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Ushiriki wa  Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili(CEGO-NRM)  wenye lengo ka kuwawezesha wananchi kushiriki katika usimamizi wa maliasili na kuweza kuwajibisha viongozi na mamlaka mbalimbali zenye dhamana ya kusimamia maliasili pale zinaposhindwa kutekeleza majukumu yake. Mafunzo haya yalifanyika katika kata mbili, Kata ya Kiwere iliyopo wilaya ya Iringa Vijijini na kata ya Igombavanu iliyopo wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa, Mafunzo yalianza katika Kata ya Kiwere tarehe 24- 27 Aprili 2015 na Kisha kwenda katika Kata ya Igombavanu tarehe 29 Aprili-1Mei 2015. Baada ya Mafunzo haya LEAT inategemea kuvitumia vikundi hivi vya sanaa katika kufanya maonesho yanayohusu ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa maliasili na ufuatiliaji wa uwajibikaji jamii.
Mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili unafadhiliwa na USAID na  unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mi nne (4) katika wilaya za Iringa Vijijini na Mufindi mkoani Iringa.