Wednesday, November 9, 2011

UCHANGANUZI YAKINIFU KUHUSU UMUHIMU WA KUWEZESHA SEKTA YA KILIMO TANZANIA


Na, Heri Ayubu

UTANGULIZI

Kwa miaka mingi Sekta ya kilimo nchini Tanzania imekuwa ikizeshwa kibajeti na serikali kama mchangiaji mkubwa kwenye maeneo ya huduma na miundo-mbinu. Zaidi ya serikali kuna mchango kutoka kwa Wadau wa Maendeleo au Wahisani ambao wamekuwa wakichangia sekta hii kupitia mfuko wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP) na miradi mingine inayojitegemea. Pia, kuna rasilimali nyingine zimekuwa zikipitia Asasi za Kiraia, za kitaifa na za kimataifa, ambazo pia mchango wake unatambulika katika sekta ya Kilimo Tanzania. Serikali ya Jamhuri wa Tanzania imefanya mabadiliko kadhaa ya kisefra na kisheria katika juhudi zake za kuhakikisha sekta binafsi inachukua nafasi katika uwekezaji kwa sekta ya kilimo nchini. Hatahivyo matokeo ya juhudi za serikali hayajaleta mabadiliko makubwa katika ustawi wa sekta ya kilimo nchini.

Mpaka kipindi cha hivi karibuni ni kwa kiwango kidogo cha Uwekezaji wa Moja kwa Moja wa Kigeni (FDI) kimewekezwa katika sekta ya kilimo nchini Tanzania kwa maeneo ya ununuzi wa mazao na mengineyo yasiyokuwa na ewekezaji mkubwa. Ni kiasi kidogo sana cha uwekezaji huu kimeelekezwa katika uzalishaji na muindo-mbinu. Kwa upande mwingine wakulima wadogo nchini wamekuwa wakikosa msaada kwa maana ya uwezeshwaji ili kuendesha shughuli za kilimo kama njia ya kuwakomboa kimaisha na kuchangia kwa maendeleo ya Taifa lao. Kuna juhudi mbalimbali zinazoendelea kufanywa na serikali katika kuleta ustawi wa Jamii na maendeleo ya Taifa ikiwemo mchakato wa kuanzishwa kwa Benki ya Kilimo ambayo inapendekezwa na KILIMO KWANZA, na pia imefungua milango ya Benki ya Uwekezaji Tanzania ili kuruhusu mikopo ya Kilimo. Kwa kuwa zaidi ya 80% ya watanzania ni wakulima na wafugaji wadogo ambao pia ni wahitaji wakubwa wa rasilimali ili kuendeleza shughuli zao ni wazi kuwa juhudi hizi za serikali, kwa asili yake, haziwanufaishi wakulima wadogo bali kundi dogo la wakulima wa kati na wale wakubwa wenye vigezo vya kuifikia mikopo hiyo.

Andiko hili linalengakuainisha mapungufu ya kibajeti katika sekta ya kilimo ili kuonyesha uhitaji wa ongezeko la rasilimali sambamba na kampeni inayofanywa na Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira (LEAT) ikiitaka serikali kuzingatia na kutekeleza Maazimio mbalimbali ya Kimataifana kitaifa ambayo Tanzania imeingia kama vile Programu Kabambe ya Kuendeleza Kilimo Afrika (CAADP), Tamko la Maputo, Malengo ya Milenia (MDGs), na Kilimo Kwanza. Maazimio haya yanaitaka serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuongeza bajeti ya kilimo kifikia 10% ya Bajeti ya Taifa na kuelekeza kiasi kikubwa (zaidi ya 50%) kwenye uwekezaji wa miradi ya maendeleo kilimo ukilinganisha na gharama za uendeshaji au za kiofisi.

KUHUSU BAJETI YA SERIKALI KWA SEKTA YA KILIMO TANZANIA

Kwa kuangalia Bajeti za serikali kuanzia miaka ya 2001/2002 mpaka 2010/2011 inaonesha kuwa bajeti ya kilimo imekuwa ikiongezeka. Kwa mfano kwa miaka ya fedha ya 2001/2002 mpaka 2004/2005 jumla ya mgawanyo wa kibajeti kwa sekta ya kilimo ilikuwa Kiasi cha Shilingi za Kitanzania Milioni 52,072/- na Milioni 3,347,539/- ambalo ni sawa na ongezeko la 3% hadi 4.7% ya Bajeti ya Jumla ya serikali. Katika miaka ya fedha ya 2009/2010 na 2010/2011 mgawanyo wa bajeti ya taifa katika sekta ya kilimo ilikuwa kiasi cha shilingi 517,611/- bilioni na 903 bilioni ambayo inaweza kutafsiriwa kama 7.6% na 7.7% ya Bajeti na Matumizi ya jumla ya serikali. Kwa bahati mbaya kabisa msimamo wa serikali juu ya juhudi zake katika kukuza sekta ya kilimo kwa kuipangia bajeti ya kutosha umeshindwa kujidhihirisha kwa Bajeti ya Mwaka 2011/2012 ambapo bajeti yake imeshuka hadi 6.8% ya Bajeti ya Serikali.

UMUHIMU /SABABU ZA KUTHIBITISHA ULAZIMA WA SERIKALI NA BUNGE KUONGEZA BAJETI YA KILIMO

Pamoja na kuwa Serikali ya Jamhuri ya Tanzania imeingia Maazimio mbalimbali yanayoitaka kutimiza adhima hii muhimu na hivyo serikali inao wajibu kimsingi wa kutekeleza Maazimio haya, kuna sababu nyingi katika sekta ya kilimo nchini zinazotthibitisha uhitaji wa Ongezeko la Bajeti ya kilimo hata kama kusingekuwa na Maazimio hayo. Sehemu hii itajadili kwa ufupi juu ya sababu hizi zinazoonyesha umuhimu wa serikali kuwekeza katika kilimo hasa ikilenga WAKULIMA NA WAFUGAJI WADOGO ambao ni 80% ya idadi ya Watanzania wote wanaotegemea sekta hii kwa kazi, chakula na kipato kwa ustawi wa maisha yao binafsi na Taifa kwa ujumla.

Kwa ujumla uhitaji wa ongezeko la Bajeti ya kilimo unategemewa kuleta maendeleo ya teknolojia ya kilimo (kama vile upatikanaji wa mbegu bora, mbinu za kisasa za kukabiliana na magonjwa ya wanyama na mimea, na utaalamu wa kupunguza hasara katika uzalishaji), miundo mbinu vijijini, mafunzo kwa wakulima na wafugaji, pamoja na uboreshwaji wa mfumo wa umwagiliaji. Kwa haya na megine mengi ongezeko la Bajeti ya kilimo mpaka kufikia 10% au zaidi ya Bajetiya jumla ya Serikali ni MUHIMU sana kwa ustawi wa wananchi na Taifa.

Ikiwa serikali inatambua kilimo kama UTI WA MGONGO wa taifa la Tanzania, ipo haja ya serikali kuitambua sekta hii kwa vitendo ambayo kwa miaka iliyopita imekuwa ikipewa isiyokidhi na kuipangia bajeti toshelezi kama ambavyo nchi nyingine duniani ambapo kilimo ni kipaumbele wameonyesha kwa vitendo na kupata mafanikio makubwa. Kwa mfano nchi ya India ilitumia wastani wa 10% mpaka 20% ya Bajeti yake katika miaka ya 1970, vilevile nchi ya Malaysia ilitumia wastani wa 20% ya Bajeti yake kuwekeza katika sekta ya kilimo kati ya miaka ya 1960 na 1983. Nchi hizi mbili katika miaka tajwa zilikuwa karibu sawa kimaendeleo na Tanzania lakini sasa zimepiga hatua kubwa kimaendeleo na kuwa miongoni mwa Mataifa yenye uchumi mkubwa duniani.Izingatiwe kuwa uwekezaji wa nchi hizi ulielekezwa kwa WAKULIMA WADOGO. Hii inadhihirisha umuhimu wa Tanzania kuongeza uwekezaji katika sekta ya kilimo hasa kwa kulenga kundi la wakulima na wafugaji wadogo.

MAPUNGUFU YALIYOPO KATIKA SEKTA YA KILIMO TANZANIA

Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP) inapata fedha kupitia Msaada wa Kiujumla wa Bajeti (General Budget Support – GBS), Mfuko wa Pamoja (Busket Fund), miradi inayojitegemea sekta binafsi. Mpaka sasa kuna Wadau wa Maendeleo au Wafadhili watano katika Mfuko wa Pamoja (Busket Fund) ambao ni Benki ya Dunia (WB), Serikali ya Japan, Msaada kutoka Irish, Ffuko wa Kiamtaifa kwa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Katika ngazi ya Kitaifa fedha hutoka mfumo wa Medium Term Expenditure Fund (MTEF) kulingana na Mwongozo wa Bajeti. Miradi inayojitegemea inajumuisha miradi ya PADEP, DASIP na ASP kwa upande wa Zanzibar.

Kwa mujibu wa nyaraka za Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP) kiasi cha fedha zinazokadiriwa kuchangiwa katyika Programu hii kutokaMfuko wa Pamoja kunafikia Dola za Kimarekani 315.5 milioni. Hatahivyo makadirio haya HAYAJUISHI gharama za Mradi wa Maendeleo wa Umwagiliaji wa Taifa ambao ni kichocheo kikubwa cha kuongeza uzalishaji na manufaa pamoja na kutoa suluhu ya madhara yatokanayo na mabadiliko hasi ya Hali ya hewa. Kwa msingi huu gharama za maakadirio halisi ya kutekeleza Programu hii inatakiwa kuwa kiasi cha Dola za Kimarekani 2.1 bilioni kwa kipindi cha miaka saba.
UCHANGANUZI

Kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2010/2011 mpaka mwisho wa Awamu ya ASDP ya sasa ya mwaka 2012/2013 upungufu wa fedha kama unavyoonyeshwa na Jedwali hapo juu ambapo kuna upungufu wa Jumla ya Tshs 1,348.31 bilioni ambazo ni sawa na Dola za Kimarekani 1,037 milioni. Hii ni sawa na wastani wa Tshs 450 bilioni ambazo ni sawa na Dola za Kimarekani 348.6 bilioni kwa mwaka kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Hatahivyo, makadirio kuelekea mwaka wa fedha wa 2014/2015 yanaonyesha upungufu wa Bajeti wa kilimo kufikia Tshs 8,257 milioni (US$ 6.35 bilioni). Ifahamike kuwa Fedha hizi zinajumuisha Makadirio ya baadhi ya vipaumbele vinavyopendekezwa ndani ya mkakati wa vipaumbele vya uwekezaji vilivyo ndani ya Programu Kabambe ya Kuendeleza Kilimo Afrika (CAADP) kama vile umwagiliaji, matumizi ya machine katika kilimo, utafiti, huduma za ughani na uendelezwaji wa rasilimali watu.

MAENEO YANAYOHITAJI VIPAUMBELE KWA MAENDELEO YA SEKTA YA KILIMO TANZANIA

Ili kuchochea ukuaji katika sekta ya kilimo na kupu0nguza umasikini kwa jamii kubwa iliyo vijijini na mjini matumizi ya umma kwa maana ya Bajeti ya serikali lazima yaongezwe. Nguvu kubwa ielekezwe kwenye uzalishaji wa mahindi, mpunga, mazao ya mizizi ka vile nihogo, ufugaji na uvuvi kama vipaumbele. Uwekezaji katika kilimo cha umwagiliaji, zana bora za kilimo, utafiti na pembejeo za kilimo unahitajika kuongeza uzalishaji. Vilevile uwekezaji katika miundombinu vijijini, usindikaji wa mazao, na uhifadhi wake (ambavyo vinatajwa na nguzo ya Pili ya CAADP) vitahitajika kuongeza wigo la soko la mazao hasa kwa mazao yaliyotajwa hapo juu kama vipaumbele. Yafuatayo ni maeneo yanayohitaji vipaumbele yakihusianishwa na mapendekezo ndani ya CAADP:

Eneo la Kwanza: Uwekezaji muhimu ili Kuongeza Uzalishaji

I. Umwagiliaji ( Nguzi ya Pili ya CAADP)

Kilimo cha Umwagiliaji
Tanzania bara ina jumla ya eneo la hekta milioni 29.4 linaloweza kufanya uzalishaji kwa umwagiliaji, lakini ni karibu eneo la hekta laki 330,000 tu (sawa na 1.1% tu ya eneo linalofaa kwa umwagiliaji) ndilo kwa sasa linafanya uzalishaji kwa umwagiliaji. Kwa upande wa Zanzibar eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ni hekta 8,500 lakini ni hekta 700 tu (sawa na 8.2% ya eneo linalofaa kwa umwagiliaji) ndizo zinafanya uzalishaji.

Hivyo moja ya mapungufu ndani ya ASDP na ASP ambayo yanahitaji kutafutiwa suluhisho yanajumuisha upungufu wa zana na rasilimali watu, miundo mbinu ya umwagiliaji na mfumo mzuri wa usimamizi wa maji. Hivyo kama kutakuwa na ongezeko la bajeti ya kilimo na sehemu kubwa ya bajeti hiyo ikaelekezwa katika uwekezaji baadhi ya mapungufu haya yatatatuliwa na uzalishaji utaongezeka.

II. Zana za Kilimo (Nguzo ya Kwanza na ya Pili ya CAADP)


Wakulima wengi bado wanatumia Jembe la mkono

Wakulima wachache ndio wanatumia Jembe la kukokotwa na ng'ombe 
Kwa kuzingatia kuwa uzalishaji wa mazao yanayopewa kipaumbele unafanyika hasa kwa jembe la mkono, maendeleo katika sekta hii hayatakuwa rahisi pasipo jitahada za makusudi katika zana za kisasa za kilimo. Inakadiriwa kuwa zaidi ya 70% ya wakulima bado wanatumia jembe la mkono, 20% wanatumia jembe la kukokotwa na wanyama, na chini ya 10% ndio wanatumia trekta. Kimsingi matumizi ya zana duni kama jembe la mkono ndio hasa chanzo cha uzalishaji mdogo na usiokuwa na tija. Ni wazi kuwa maendeleo ya Taifa kupitia kilimo yahahitaji uwekezaji mkubwa katika zana za kisasa kwa wakulima na wafugaji wadogo lengo likiwa kutumia jembe la kukokotwa na wanyama na matrekta kama zana za kilimo. Pamoja na zana za kilimo ipo haja ya kuanzisha programu zitakazowawezesha wakulima wadogo kutumia teknolojia rahisi kupata nishati kama vile jua na upepo.

Kwa kuzingatia uwezo wa kiuchumi wa wakulima wadogo Tanzania, serikali lazima ichukue jukumu la kuchangia kwa asilimia kubwa au kutoa mikopo nafuu wa zana hizi kwa wakulima. Hili litawezekana endapo serikali itatenga fungu la kutosha katika bajeti ya Kilimo, na hivyo ongezeko la kufikia angalau 10% ya Bajeti ya jumla ni muhimu sana.

III. Utafiti, Maendeleo na huduma za Ughani (Nguzo ya Nne ya CAADP)

Utafiti ndio msingi wa uhakika na maamuzi sahihi, na huduma za ughani ndio dira ya kitaalamu kwa wakulima katika hatua zote za uzalishaji, uhifadhi na hata masoko. Kwa sasa kiasi cha bajeti kinachoelekezwa katika utafiti na maendeleo kwa seka ya kilimo ni 0.3% ya Bajeti ya jumla ya sekta ya kilimo. Ushahidi uliopo unaonyesha kuwa uwekezaji katika utafiti na ughani huleta matokeo mazuri katika ukuaji wa kilimo na kipato katika ngazi ya familia. Kwa mfano kwa kila shilingi milioni moja (1,000,000/-) iliyotumika katika utafiti kwa sekta ya kilimo, kipato kwa ngazi ya familia kimeongezeka kwa shilingi 12.5 milioni na idadi ya watu wapatao 40 wameondelewa katika umasikini.

Miundombinu isiyitosheleza kwa utafiti na ukosefu wa wataalamu wa kutosha ni moja ya mambo ambayo hayajatiliwa mkazo na kupewa bajeti ya kutosha katika ASDP na ASP. Hivyo hii ni moja ya sababu za msingi zinazolazimu serikali kuongeza bajeti ya sekta ya kilimo.

IV. Matumizi ya pembejeo bora za kilimo.

Ili kufanikisha, kile kinachoitwa, Mapinduzi ya Kijani, upatikanaji wa pembejeo za kilimo, kwa wakati ni suala muhimu sana. Hatahivyo matumizi ya pembejeo za kilimo nchini Tanzania bado yapo chini sana, kwa mfano, wakati Tanzania inatumia Kilogramu 26 za mbolea kwa hecta, wastani wa matumizi kwa nchi za kusini mwa Afrika (SADC) ni Kiligramu 16 za mbolea kwa hekta, na China ni Kiligramu 276 kwa hekta. Inakadiriwa kuwa miongoni mwa wakulima wa Tanzania ni asilimia 10 tu ndio wanatumia mbegu zilizoboreshwa.

Eneo la Pili: Uwekezaji kwa lengo la kuongeza Masoko

I. Miundo-mbinu vijijini (Barabara, Masoko, Huduma za Uhifadhi wa mazao(Maghala), Nishati, n.k) – Hii ni sawa na Mapendekezo katika Nguzo ya Pili ya CAADP

Uboreshwaji na ujenzi wa barabara vijijini na miundombinu ya masoko ni muhimu sana kwa masoko ya zinazoingia vijijini kusaidia shughuli za kilimo, na mazao ya kilimo na mifugo yanayotoka vijijini.

II. Usindikaji wa Mazao ya Kilimo na Ufugaji ili Kuongeza Thamani ya Mazao.

Usindikaji wa mazao ya kilimo na mifugo ili kuongeza thamani ni muhimu sana kwa maendeleo ya kilimo na kuondoa umasikini kwa wakulima. Shughuli hizi pia zitaongeza ajira kwa jamii za wakulima na kuunganisha shughuli za uzalishaji wa mazao na ufugaji, kwa mfano usindikaji wa mazao huweza kuzalisha chakula cha mifugo na hivyo kusaidia ukuaji wa sekta ya mifugo.

Hatua za ukuaji wa sekta ya usindikaji kwa nchi ya Tanzania bado ipo chini sana na imekuwa ikishuka mwaka hadi mwaka. Matokeo yake ni kuwa Tanzania imekuwa ikiuza mazao ghafi nchi za nje kwani sekta hii haitoshelezi mahitaji kulingana na uzalishaji. Takwimu zinaonesha kuwa kwa sasa kati ya asilimia 30 hadi asilimia 70 ya mazao ya nafaka, matunda na mbogamboga hupotea baada ya kuvunwa kutokana na kukosekana kwa huduma za usindikaji. Katika sekta ndogo ya uvuvi inakadiriwa kuwa asilimia 20 ya samaki wanaovuliwa hupotea kutokana na kukosekana kwa miundo mbinu ya usindikaji.

Hii inaonyesha ulazima wa serikali kuwekeza kikamilifu katika eneo hili hasa kwa maeneo ya vijijini, nah ii itawezekana endapo serikali itatenga bajeti ya kutosha kwa sekta ya kilimo na wizara nyingine zinazohusiana nayo, vilevile kutenga sehemu kubwa ya bajeti itakayotengwa kwa shighuli za maendeleo ikiwemo uanzishwaji wa viwanda vidogo maeneo ya vijijini kwa ajili kusindika mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Eneo la Tatu: Kuwajengea uwezo wakulima na wafugaji hasa wakulima na wafugaji wadogo. Ili kuhakikisha mipango ya maendeleo kwa sekta ya kilimo na uwekezaji unaopendekezwa, ni lazima suala la kuiwajengea uwezo wakulima lipewe kipaumbele pia. Kuna njia nyingu za kuwajengea uwezo wakulima zikiwemo, kutoa elimu ya kilimo na ufugaji bora kwa kutumia wataalamu wa kilimo na mifugo, kuoeleka maofisa wa kilimo maeneo ya vijijini na kuwawekea mazingira mazuri ya kufanya kazi, kuanzisha mashamba ya mfano, n.k

HITIMISHO

Tanzania inahitaji mchango wa sekta ya kilimo ili kujikwamua katika umasiki ikiwa ni sambamba na kufikia Malengo ya Millennia, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na Mpango wa Kukuza Uchumu na Kuondoa Umasikini Tanzania (MKUKUTA I & II). Pakoja na hayo Tanzania inao wajibu wa kutekeleza Maazimio ya Kimataifa ambayo imeingia yenye lengo la kukuza sekta ya Kilimo , ikiwa ni pamoja na Programu Kabambe ya Kuendeleza Kilimo Afrika ambayo pamoja na mambo mengine inaitaka serikali kuongeza bajeti ya kilimo hadi kufikia angalau asilimia 10 ya Bajeti ya Taifa, na kuelekeza sehemu kubwa ya Bajeti hiyo katika Miradi ya maendeleo, na kuiwezesha kukua sekta hii kwa asilimia 6. Hili litafanikiwa iwapo nguvu ya kirasilimali (Bajeti) itaongezwa katika shughuli za maendeleo ya kilimo na kuweka kipaumbele kwa wakulima na wafugaji wadogo.



MALALAMIKO YA WANANCHI WA MTAA WA YOMBO MAKANGARAWE JUU YA KERO ZITOKANAZO NA UJENZI WA BAA KATIKATI YA MAKAZI YA WATU

UTANGULIZI

Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira (LEAT) kilipokea malalamiko kupitia Barua ya TAREHE 29.09.2011 kutoka kwa wananchi wa Yombo MAKANGARAWE kuhusu kero zinatokana na uwepo wa Baa na nyumba ya kulala wageni “Guest House” ijulikanayo kama KB METRO PUP iliyotajwa kumilikiwa na Bwana Lugano Kikoti ambayo imejengwa katikati na makazi ya watu.

Kimsingi malalamiko haya yaligusia mambo makuu wawili;

i. Kelele zitokanazo na muziki unaopigwa na baa hiyo hasa wakati wa usiku na kuwa kero kubwa kwa wananchi wanaoishi jirani na baa hizo na kushindwa kupumzika. Vilevile wafanyakazi na wanafunzi kushindwa kusoma kutokana na kelele nyingi zinazotokana na muziki unaokuwa ukiendelea KB METRO PUB.

ii. Suala la uharibifu wa mazingira uliofanywa na Baa hiyo baada ya kuziba iliyokuwa njia kuu au mbondo wa maji jambo linalopelekea kutokea kwa mafuriko makubwa wakati wa masika. Suala hili pia lilitajwa kuharibu nyumba zilizopo karibu na mkondo huo wa maji kiasi cha kuhatarisha usalama wa waishio katika nyumba hizo kutokana na mmomonyoko unaosababishwa na maji yanayojaa wakati wa mvua ikiwa ni matokeo ya kuzibwa kwa mkondo wa maji. Vilevile kwa mujibu wa malalamiko suala hili limekuwa chanzo kikuu cha milipuko ya magonjwa yaa mara kwa mara kutokana na maji yaliyotuama kuwa mazalia ya mbu na mkusanyiko wa uchafu.

Wananchi hawa tayari walikwishafanya juhudi mbalimbali katika kutafuta suluhisho la tatizo hili, na kuripoti katika Mamlaka zfuatazo (LEAT ina nakala ya barua):-

1. Ofisi ya Serikali za Mitaa

2. Kituo cha Polisi Makangarawe

3. Kituo cha Polisi Chang’ombe

4. Baraza la Usuluhishi la Kata ya Makangarawe

5. Ofisi ya Mtendati Kata-Makangarawe

6. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam

Kwa upande wa mlalamikiwa ilielezwa kuwa alijibu malalamiko ya wananchi kwa kutoa NOTISI iliyopokelewa na wananchi tarehe 17.09.2011 kupitia Wakili wake ‘ALEX $ SAMWEL CORPORATE ADVISORY SERVICES’ abayo pamoja na mambo mengine inataja hasara ya Kiasi cha Shilingi Milioni 50 ilyotokana na kilichotajwa kuwa ni kuzuia uendeshaji mzuri wa biashara unaofanywa na wananchi HIVYO kuwataka wananchi hao kumlipa mmliki wa Baa hiyo kiasi cha Shilingi 50 MILIONI kama fidia la sivyo suala hilo litafikishwa katika vyombo vya sheria.

JUHUDI ZA ZILIZOFANYWA NA LEAT

Baada ya kupokea malalamiko hayo LEAT ikiwa taasisi isiyi ya kiserikali inayojishughulisha na usimamizi wa mazingira na haki za binadamu ilifanya mambo yafuatayo:

i.Baada ya LEAT kulipokea suala hili ililifikisha moja kwa moja katika Mamlaka ya serikali inayosimamia mazingira, Baraza la Usimamizi wa Mazingira Tanzania (NEMC) kwa Barua ya Tarehe 04.10.2011 ikiwa ni TAARIFA kwa mamlaka hiyo kama chombo chenye mamlaka na usimamizi wa mazingira Tanzania. Vilevile LEAT iliiomba NEMC kutoa mwakilishi ili kuambatana na timu ya Mwanasheria wa Mazingira pamoja na Waandishi wa Habari katika ziara ya kujiridhisha na malalamiko ya wananchi na kuona hali halisi.

ii. LEAT pamoja na timu ya waandishi wa habari wa magazeti ya MAJIRA na MWANANCHI walifanya ziara katika eneo husika Tarehe 07.10.2011 na kushudia hali halisi pamoja na kufanya mahojiano ya msingi na wawakilishi wa waathirika wa tatito lililo mezani. Ziara hii ilitoa picha halisi ya kilichoelezwa katika barua za malalamiko kwani kimazingira Baa hiyo ipo katikati ya makazi ya watu na kuwa suala la pili la mkondo wa maji ni kweli kabisa linajidhihirisha.

iii. LEAT baada ya kujiridhisha na malalamiko ililifikisha suala kwa jamii hilo kupitia magazeti la Majira Tarehe 09 na 10/10/2011 na kuripoti NEMC ambao hawakuweza kuwepo katika ziara ya kutembelea eneo husika. Hatahivyo NEMC walishauri wananchi wenyewe kulifikisha suala hilo NEMC ushauri ambao LEAT iliufikisha kwa walalamikaji.

TATIZO LA MSINGI NA MAPENDEKEZO

Pamoja na malalamiko mengi kuripotiwa LEAT imegundua matatizo makuu mawili na mapendekezo yake kama ifuatavyo:-

Kwanza, Baa ya KB METRO PUB imejengwa katikati ya makazi ya watu jambo lililoibua kero nyingine nyingi. Endapo Baa hii itaondolewa katika eneo husika kero nyingine nyingi zikiwemo za kelele za muziki, danguro linalosemekana kewepo, taka zinatupwa eneo hilo na mgomgano huu baina ya mmiliki na wananchi vitakwisha.

Pili, Suala la kuzua mkondo wa maji wa asili, hili pia litaweza kusuluhishwa na pendekezo lililotajwa hapo juu kwani uzibuaji wa mkondo asili wa maji utategemea kubomolewa kwa sehemu ya ukuta wa Baa hiyo. Kwa kuwa NEMC waliahidi kulifanyia kazi suala hili baada ya kupata malalamiko ya Wananchi tunategemea suala hili kulingana na mazingira yake litafanyiwa kazi.

Katika kutafuta suluhu LEAT imfanikiwa kufanya taratibu za awali ikiwemo kutoa Taarifa NEMC kikiwa ni chombo chenye Mamlaka kisheria kusimamia mazingia nchini. Vilevile LEAT imetumia vyombo vya habari kupaza sauti hizi za watanzania, Gazeti la Majira la Tarehe 9/10/2011 Ukurasa wa 5 linaripoti. LEAT pia ipo katika mchatako wa kuripoti suala hili kwa Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Jeshi la Polisi hasa kwa suala la kupiga kelele za muziki katikati ya makazi ya watu usiku kucha.

MENGINEYO

Katika utekelezaji wa shughuli hii yameibuka malalamiko mengi ya aina hiyo kutoka katika mitaa mbalimbali hapa jijini Dar es Salaam ikiwemo mtaa huo huo wa Makangarawe ambapo Baa ya BATOTOZI km Night Club imeripotiwa.

Mwisho LEAT itaendelea kuwa na wananchi katika harakati za kutetea haki zao za kimazingira ili wapate mazingira mazuri ya kuishi, ikiwa ni haki ya kisheria ‘Haki ya Kuishi’.